Author name: SW - Melkisedeck Shine

Mapishi ya Pilau Ya Adesi Za Brown Karoti Na Mchicha Kwa Samaki Wa Salmon

Vipimo

Mchele vikombe 3

Karoti 1 ikune (grate)

Mchicha katakata kiasi

Adesi za brown

Kitunguu katakata (chopped)

Supu ya kitoweo chochote upendayo au vidonge vya supu 2

Garama masala (bizari mchanganyiko) kijiko 1 cha kulia

Samli ¼ kikombe

Chumvi kiasi

Vipimo Vya Samaki Wa Salmon

Samaki wa Salmon vipande 4 vikubwa

Tangawizi mbichi ilosagwa kijiko 1 cha kulia

Thomu (garlic/saumu) kijiko 1 cha kulia

Chumvi kiasi

Bizari ya mchuzi kijiko 1 cha kulia

Ndimu 1 kamua

Nyanya 2 kata slice kubwa kubwa

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika Samaki wa Salmon

Changanya viungo vyote upake katika samaki.
Weka katika treya na panga slice za nyanya juu yake.
Oka (grill/choma) katika oven umgeuze samaki upande wa pili.
Akiwa tayari epua.

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika Wali

Roweka mchele kiasi kutegemea aina ya mchele. Tumia basmati (pishori)
Roweka adesi kisha zichemshe katika maji ya kiasi. Chuja maji adesi na maji yatakayobakia tumia katika kupikia pilau hii.
Kaanga vitunguu katika samli iliyoshika moto kwenye sufuria ya kupikia.
Vikianza kugeuka rangi tia karoti, mchicha, adesi, bizari mchanganyiko kisha kaanga kidogo.
Tia mchele ukaange kidogo kisha tia supu au maji pamoja na kidonge cha supu.
Tia chumvi ukoroge funika upike kama pilau.
Epua upakue katika sahani utolee kwa samaki wa salmon

Mapishi ya Boga La Nazi

Vipimo

Boga la kiasi – nusu yake

Tui zito la nazi 1 ½ gilasi

Sukari ½ kikombe

Hiliki ½ kijiko cha chai

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Menya boga kisha katakata vipande vya kiasi.
Weka katika sufuri tia maji kiasi ya kuchemshia na kuwiva bila ya kubakia maji mengi.
Changanya tui na sukari na hiliki kisha mimina juu ya boga wacha katika moto dakika chache tu bila ya kufunika.
Epua mimina katika chombo likiwa tayari.

Jinsi ya kupika Magimbi Kwa Nyama Ya Ng’ombe

Vipimo

Majimbi (Eddoes) kiasi 6 au 7

Nyama ng’ombe ½ kilos

Tangawizi ilosagwa 1 kijiko cha kulia

Haldi (bizari manjano/turmeric) ½ kijiko cha chai

Tui zito la nazi vikombe 2

Chumvi kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Safisha nyama kisha weka chumvi, bizari ya manjano, tangawizi mbichi, ukaushe kwanza katika sufuria kwa kukaanga kaanga.
Ikianza kukauka, weka maji funika uchemshe iwive.
Menya majimbi ukate kate na uweke katika sufuria nyengine.
Mimina supu na nyama katika majimbi uchemshe yawive majimbi.
Mwisho weka tui zito la nazi uchanganye vizuri kisha weka katika moto kidogo tu bila kufunika yakiwa tayari.

Mapishi ya Wali Mweupe Kwa Mchuzi Wa Kuku Wa Balti

Vipimo

Kuku 1 mkate vipande vipande

Vitunguu 3 katakata (chopped)

Nyanya 5 zikatekate (chopped)

Tangawizi mbichi ilokunwa au ilosagwa 1 kijiko cha kulia

Thomu (kitunguu saumu) kilosagwa kijiko 1 cha kulia

Bizari mchanganyiko (garam masala) kijiko 1 cha chai

Jira/bizari ya pilau (cummin powder) kijiko 1 cha chai

Dania/gilgilani ilosagwa (coriander powder) kijiko 1 cha chai

Mtindi/maziwa lala (yoghurt) vijiko vya kulia 4 mjazo au paketi moja ndogo.

Malai ya kupikia (cooking cream) kikombe 1

Kasuri methi (majani makavu ya uwatu/dried fenugreek leaves) 1 kijiko cha kulia

Mafuta ya kupikia ½ kikombe

Chumvi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha kuku vizuri mwache achuje maji.
Weka mafuta katika sufuria kaanga vitunguu mpaka vianze kugeuka rangi ya brown hafifu. Kisha tia tangawizi na thomu ukaange.
Tia kuku ukaange mpaka ageuke mweupe kisha tia nyanya endelea kukaanga ziwive.
Piga mtindi vizuri katika kibakuli uwe nyororo.
Epua sufuria weka kando kisha tia mtindi uchanganye vizuri pamoja na kuku.
Rudisha katika moto acha uchanganyike na kuku kidogo kisha mwagia malai ya kupikia (cooking cream)
Tia kasuri methi/majani makavu ya uwatu yaliyovurugwa. Acha katika moto dakika 1 tu.
Epua umimine katika chombo na nyunyizia ikiwa tayari kuliwa na wali mweupe.

Mapishi ya Ugali Mchuzi Wa Samaki Nguru Wa Nazi Na Bamia Za Kukaanga

Vipimo Vya Ugali:

Unga wa mahindi/sembe – 4

Maji – 6 takriban

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Chota unga kidogo katika kibakuli uchanganye na maji kidogo .
Weka maji mengineyo katika sufuria kwenye moto.
Changanya na mchanganyiko mdogo ufanya kama uji.
Kisha kidogo kidogo unaongeza sembe huku unakoroga na kuusonga ugali hadi uive.

Vipimo Vya Mchuzi Wa Samaki Wa Nazi

Samaki nguru – 5 vipande

Pilipili mbichi ilosagwa

Kitunguu maji kilosagwa – 1 kimoja

Nyanya ilosagwa – 2

Haldi/tumeric/bizari ya manjano – ¼ kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Ndimu – 2 kamua

Tui la nazi zito – 2 vikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Baada ya kumuosha samaki, weka katika sufuria.
Tia chumvi, ndimu, pilipili mbichi ilosagwa.
Tia vitunguu na nyanya zilosagwa
Mkaushe kwa hivyo viungo, akianza kukauka tia tui la nazi.
Acha kidogo tu katika moto tui liwive mchuzi ukiwa tayari.

Vipimo Vya Bamia

Bamia – ½ kilo takriban

Nyanya kopo – 1 kijiko cha chai

Methi/uwatu/fenugreek seeds ilosagwa – 1 kijiko cha chai

Dania/corriander ilosagwa – ½ kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Mafuta – 1 kikombe cha kahawa

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Katakata bamia kwa urefu.
Weka mafuta katika karai, kisha tia bizari zote na nyanya kopo, kaanga kidogo.
Tia bamia endelea kukaanga, kisha acha katika moto mdogomdogo ufunike.
Kila baada ya muda funua karai ukaange bamia hadi ziwive zikiwa tayari.

Shopping Cart