Author name: DIN - Melkisedeck Leon Shine

Usipite bila kusoma kisa hiki cha kusisimua

Siku moja jioni katika mji flani, kulikuwa na basi likisafiri kutoka mji huo kuelekea mji mwingine. Lilikuwa ni basi kubwa na limejaa abiria. Wakati wakiendelea na safari, ghafla, mvua kubwa iliyoambatana na radi ikaanza kunyesha. Dereva hakuogopa, wala abiria, wakaendelea na safari. Mara wakati wanaenda, radi ikaanza kufuatilia gari. Kila wakienda, radi inapiga karibu na basi kana kwamba inalifuata basi. Likisimama, radi inapiga pembezoni mwa basi.

Dereva kuona hivyo, akasimamisha gari mita 5 kutoka kwenye mti… Akawaambia abiria, “Humu ndani ya basi, kuna mtu ambaye leo ni siku yake ya kufa, tena kufa kwa radi. Ili tusife wote, nataka kila abiria ashuke akaguse mti ili anayepigwa na radi, apigwe wengine wasife kwa ajili yake. “Abiria wakitetemeka, wakaanza kushuka mmoja mmoja. Unaenda unagusa mti , kisha unarudi kwenye basi. Abiria wote pamoja na dereva mmoja mmoja, wakaenda, wakagusa mti na kurudi bila dhara lolote! Akawa kabaki abiria mmoja tu, ambaye alikuwa hajagusa mti. Abiria wote kwa macho ya hasira wakamwambia akaguse mti. Akawa anaogopa kufa. Akagoma. Wakamlazimisha kwa nguvu sana na kumtoa nje……. …….. Yule abiria akiwa amefumba macho, akaenda akagusa mti. Hamadi bin Vuu! Radi kali sana ikalipiga basi, abiria na wote waliokuwamo, wakafa palepale. Kumbe uwepo wake ndio ulikuwa unazuia abiria wengine wasidhurike na radi.

MAFUNZO

1. Unapofanikiwa, huwezi jua uwepo wa nani umefanikisha mafanikio yako, usichukue sifa zote peke yako. Wapatie na wengine bila kumsahau MUNGU.
2. Unaweza kujiona huna thamani sehemu ulipo, iwe kwenye kundi la WhatsApp, darasani, kazini, kwenye basi, barabarani bila kujua kama uwepo wako ni wa muhimu sana kwa ustawi wa wengine.
3. Usimtenge wala kumnyanyasa mtu au jirani yako, huwezi jua uwepo wake ni kwa ajili gani.

Maana halisi ya kuolewa au ya kuwa mke

NDOA sio kichaka cha kujificha kukimbia matatizo. NDOA sio mahali pa kutolea mkosi. Wala sio mahali pa kupunguzia shida. Ndoa sio mbadala wa elimu na michakato ya kimaisha. Huolewi ili kupunguza adha za maisha. NDOA ni jukumu zito kuliko hata kusoma masters degree ya Neuro-surgeon. Wengi hamjaweza kumudu maisha yenu binafsi na bado mnalilia Mungu kuwaongezea jukumu la kumeneji maisha ya mtu mwingine.

Kama huwezi hata kujitafutia hela ya kusuka nywele zako utawezaje kuendesha maisha ya familia. Maana unaweza kuolewa na mwanaume mwenye pesa lakini akapitia mithihani pesa zikatoweka utafanyaje kama huna akili ya kujiongeza? Ndio maana wengi mnawakataa watu wenye Ndoto lakini hawanapesa kwa sasa kwa sababu ya akili ya utegemezi. Unataka mwanaume mwenye kila kitu, sababu kubwa ni uvivu na uzembe. Hutaki kujitafutia vya kwako.
Ukisoma MITHALI 31 inaeleza habari za MKE MWEMA.

Hapo ndio pa kujipima je unakidhi hivyo viwango? Mke mwema sio tegemezi ila ni mwanamke mwenye uhuru wa kifedha (Financial Freedom). JIULIZE TU KAMA IKITOKEA HUJAOLEWA MIAKA MITANO IJAYO UTAKUWAJE? MAISHA YAKO YATAKUWAJE? UTAKUWA NA HALI GANI? Maswali kama haya yatakusaidia kujiongeza. Tafuta kitu cha kufanya hata kama Ndoa isipotokea leo isiwe mwisho wa maisha, Ndoto na maono yako. Siku hizi wanaume hawaulizi ukoo wanauliza UNAFANYA NINI?

Mtu anapiga hesabu akikuoa mkaunganisha nguvu mtafanya nini kwenye maisha. Sasa wewe kalia kubandika kope na kuchora kucha kutwa nzima huna shughuli ya kufanya huku ukingoja kuombewa upate Mume. Watu hawaoi mapambo wanataka Wake watakao tengeneza nao hatma zao. Pambo ni kwaajili ya Starehe lakini MKE ni kwaajili ya maisha. Sikupondi wala sio nia yangu kukuvunja moyo, nataka utoke hapo ulipo ujiongeze ili hata ukiingia kwenye Ndoa isijae visa na kuonewa. Pesa itakupa heshima, pesa inakupa sauti, hata Wakwe zako hawawezi kukunyanyasa ukiwa na pesa kwani wanajua watakosa vitenge.

Nataka nikwambie kweli, ukiwa na hela utachagua mwanaume wa kukuoa kwani wapo wengi ila kama umefulia, tegemezi kweli utaona wanaume ni wachache. Pata kitu cha kufanya, tengeneza milango ya kipato. Badala ya kukesha unaomba Mungu akupe Mume anza kuomba Mungu akupe uhuru wa kifedha, kama itakubidi kurudi shule rudi tu. Jiongeze usibaki hapo ulipo. Ni Yesu peke yake asiyebadilika (Hebrania 13) Lakini wanadamu wote lazima tubadilike kila kukicha tukihama hatua moja kwenda nyingine.

Mungu akufungue macho kuona kiini cha ujumbe huu na lengoF lake na wala usichukuliwe na upepo wa adui upindishao maana katika jumbe zenye kubadilisha maisha kama hii.

Kuolewa sio mwisho wa maisha, Mungu kwanza achukue nafasi kwenye maisha yako na akupe utoshelevu katika moyo wako kiasi kwamba uone hata bila Mume unaweza kuishi.

Uelewa wa namba katika Biblia

Biblia imeandikwa na Mungu kupitia waandishi wanadamu kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu. Hivyo Biblia ni Neno la Mungu. Hivyo mwandishi wa Biblia ni Mungu kupitia wanadamu (God is the primary author of the Bible while human authors are secondary authors). Mungu aliwavuvia (inspiration by the Holy Spirit) waandishi wanadamu ili waweze kuandika kile tu ambacho Yeye (Mungu) alitaka kiandikwe kwa ajili ya wokovu wa wanadamu. Kusema kuwa Biblia imeandikwa na Mungu kupitia wanadamu haina maana ya kuandikwa kwa njia ya imla (dictation), kana kwamba Mungu anataja sentensi au neno na wao wanaandika. Hapana, pamoja na kuwavuvia Roho Mtakatifu, waandishi wanadamu walikuwa huru kutumia vipawa mbalimbali vya uandishi na mazingira yao ili kufikisha ujumbe ambao Mungu amewavuvia. Hivyo walikuwa “active writers of the Bible, and not passive writers.” Walitumia akili (reason), utashi (will), ujengaji picha (imagination) na vipawa vingine. Lakini vipawa hivi vyote vilikuwa chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu ili kuwawezesha waandishi wa Biblia kufikisha ujumbe kwa ufasaha bila makosa.

Hivyo kuelewa kifungu au ujumbe wa Biblia ni lazima kujua yafuatayo:
Maana aliyokusudia mwandishi (the meaning of the human author)
Kusudi/malengo ya Roho Mtakatifu

Na kwa kuwa kwa mara ya kwanza Biblia waliandikiwa Wayahudi na waandishi wengi walikuwa Wayahudi, hivyo tunapaswa kujua yafuatayo ili kufasiri Biblia vizuri:

Tamaduni za Wayahudi
Historia ya Wayahudi
Mambo ya Kijografia
Namna yao ya uandishi n.k

Jambo muhimu kuelewa
Namba, wanyama, rangi, vitu, watu, maeneo, shughuli mbalimbali n.k vilikuwa na maana sana kwa Wayahudi na kwa Wakristo wa kwanza. Hivyo si ajabu kuona vimetajwa au kutumika katika Biblia.

ISHARA NYINGINE TOFAUTI NA NAMBA

Kabla ya kuzungumzia namba tuzungumzie baadhi ya vitu, rangi, watu au mahali kama vinavyoongelewa kwenye kitabu cha Ufunuo na sehemu nyingine za Biblia:

Mwanamke:

kwenye Ufu.12:1+ anamaanisha taifa au mji, na siyo mwanamke kama tunavyojua

Pembe:

neno pembe kwenye Ufu. 5:6; 12:3 linamaanisha “mamlaka”. Hata kwenye kiswahili mtu akiambiwa kuwa “ameota pembe” maana yake anajifanya kuwa ana mamlaka fulani na hivyo ana kiburi.

Mabawa:

kwenye Ufu. 4:8; 12:14 linamaanisha uwezo wa kufika mahali pote (mobility).

Upanga mkali:

kwenye Ufu. 1:16; 2:12,16) linamaanisha Neno la Mungu, ambalo lina hukumu na kuadhibu.

Matawi ya mtende:

kwenye Ufu. 7:9 ni ishara ya ushindi.

Taji:

kwenye Ufu. 2:10; 3:11 ni ishara ya utawala na ufalme.

Bahari:

kama lilivyotumika kwenye Ufu. 13:1; 21:1 linamaanisha sehemu ya uovu, chanzo cha machafuko na kifo.

Nyeupe:

rangi nyeupe inamaanisha furaha ya ushindi (Ufu. 1:14; 2:17)

Zambarau:

rangi ya zambarau huashiria anasa, utajiri na ufalme (Ufu. 17:4; 18:12,16). Kwenye Yohane 19:2,5; Mk. 15:17 vazi la zambarau huashiria “ufalme”. Kwenye Lk. 16:19 vazi la zambarau la yule tajiri liliashiria “maisha ya anasa”.

Nyeusi:

rangi nyeusi iliashiria kifo (Ufu. 6:5,12).

NAMBA KATIKA BIBLIA

Namba zilikuwa na maana sana kwa Wayahudi kwa sababu za kimazingira, kiuandishi na kilugha. Kila namba ilikuwa na maana. Hebu tutazame baadhi tu ya namba hizo:

Namba 3 na7

Namba hizi kwa Wayahudi (kwenye Biblia) zinamaanisha ukamilifu au utimilifu wa jambo (perfection or completion). Kwa mfano katika Kiebrania (lugha ya Wayahudi) hakuna “superlative” (kulinganisha kwa kutumia sifa ya juu kabisa) mfano “the tallest, the youngest, the holiest” kama kwenye Kiingereza. Hivyo Myahudi kwa upande wake atatamka neno husika mara tatu kuonesha ukamilifu: God is holy, holy, holy (ambapo kwenye Kiingereza tungesema tu “God is the holiest”). Kwa hiyo akitaja neno mara tatu alimaanisha ukamilifu wa jambo(perfection). Anaposema Mungu ni Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu ana maana kwamba Mungu ana ukamilifu wa utakatifu, yaani ni Mtakatifu kupita viumbe au vitu vyote. Mfano mwingine: Myahudi akisema kwamba nilipigwa viboko vitatu haina maana kuwa lazima vilikuwa vitatu tu. Hapa ina maana kwamba alipigwa katika ukamilifu wake yaani alipigwa barabara, sawia, alipigwa mno,
alipigwa mpaka basi. Hata kwenye Biblia ni vivyo hivyo. Yesu alimuuliza Petro mara tatu kama anampenda (Yohane 21:15-19). Hapa Yesu alitaka kujua kama Petro alimpenda katika ukamilifu wa upendo. Namba 7 imetumika mara 42 kwenye kitabu cha Daniel na Ufunuo: mfano “roho saba” ilimaanisha “ukamilifu wa roho” yaani Roho Mtakatifu. Kwa hiyo namba 3 na7 ni namba za ukamilifu. Yesu anapomwambia Petro asamehe “saba mara sabini” (Mt. 18:21-22) anamaanisha kuwa Petro asamehe “kwa ukamilifu, pasipo kukoma”.

Namba 4

Namba 4 kwenye Biblia inamaanisha “ulimwengu mzima” (universality of the visible world). Kwa hiyo aya isemayo “malaika wanne waliokuwa wamesimama katika pembe nne za dunia” (Ufu.7:1; 21:16; Rejea pia Is.11:12) ulimaanisha malaika walikuwa wameenea katika ulimwengu mzima. Pia aya hiyo hiyo inamaanisha kuwa jukumu lao lilikuwa ni kwa ulimwengu mzima.

Namba 6

Hii namba inasimama kumaanisha “mapungufu, isiyo kamilifu”. Namba hii ilihusianishwa na maadui wa Mungu kwenye Biblia. Kitendo cha mtu kuwa adui wa Mungu kilimaanisha mtu huyo si mkamilifu na ana mapungufu (Rejea 1 Nyakati 20:6; Daniel 3:1; Ufu.13:18).

Namba 12, 24

Hizi mara nyingi kwenye Biblia zinawakilisha kabila kumi na mbili za Israeli. Wapo wataalam wa Maandiko wanaosema kuwa Mitume 12 waliwakilisha makabila 12 ya Israel, yaani kila mmoja alitoka miongoni mwa makabila 12 ya Israel. Pia namba 12 inawakilisha Kanisa zima. Lakini pia 12 ni namba ya ukamilifu. Kwa hiyo Mitume 12 walikamilisha taifa zima la Israeli.

Namba 40, 175

Namba hizi kwenye Biblia zinamaanisha “urefu wa jambo” (longevity). Mfano wakisema fulani amekuwa mgonjwa kwa siku 40 ina maana amekuwa mgonjwa kwa kipindi kirefu, haina maana kuwa ni lazima zilikuwa 40 (huenda hata zilizidi). Kusema kuwa gharika ilidumu siku 40 mchana na usiku, ni kusema kuwa gharika ilidumu kwa kipindi kirefu; kusema kuwa Yesu alifunga siku 40 ni kumaanisha kuwa alifunga kwa muda au kipindi kirefu, yawezekana hata zaidi ya siku hizo 40. Kusema kuwa Waisraeli walikaa jangwani miaka 40 ni kusema kuwa walikaa jangwani kwa kipindi kirefu. Kusema kuwa Ibrahimu aliishi miaka 175 ina maana aliishi miaka mingi au kipindi kirefu, si lazima kwamba alifikisha miaka 175 lakini kwamba aliishi miaka ya kutosha, aliishi kipindi kirefu. Haya yote Wayahudi walielewa vizuri, hawakuhitaji kuuliza.

Kuanzia maelfu

Kwenye Biblia ikitajwa namba ya maelfu inamaanisha “umati mkubwa” wa watu. Yohane anaposema “…na watu mia na arobaini na nne elfu pamoja naye..” (Ufunuo 14: 1) anamaanisha kuwa aliona umati mkubwa wa watu wasio na idadi. Hivyo Ufunuo 14:1 haimaanishi watu 144,000 tu bali umati mkubwa wa watu wasio na idadi. Hata kwa Kiswahili kuna wakati tunasema “akihubutia maelfu ya watu” tukiwa na maana kwamba alihutubia umati mkubwa wa watu.

N.B. Hapa nimeeleza baadhi ya namba tu. Zipo nyingine nyingi sana na zina maana yake. Hivyo tusitafsiri Biblia kwa maana sisisi tu (Literal interpretation), yaani kile kilichoandikwa tu. Twende zaidi ya hapo.

UFAFANUZI WA NAMBA 666 (Ufu.13:11-18)

Kuelewa maana ya namba hii ni lazima kuelewa mazingira na sababu za kuandikwa kitabu cha Ufunuo. Kitabu cha Ufunuo kiliandikwa karne ya kwanza (kati ya 90-96 AD) ambapo dini ya Ukristo ilianza kuenea kwa kasi. Hivyo tawala za Warumi na Wayahudi ziliona Ukristo kama dini mpya na tishio kwa imani, siasa na tamaduni zao. Ili kuifutilia mbali Warumi na hata Wayahudi waliendesha madhulumu (persecutions) dhidi ya Wakristo: kuwaua, kuwafunga, kuwatesa na kuwalazimisha wakane Ukristo. Yohane mwenyewe anaandika kitabu cha Ufunuo akiwa gerezani (uhamishoni) katika kisiwa cha Patmos kama matokeo ya madhulumu. Yohane anaandika kitabu cha Ufunuo kuwatia moyo Wakristo katika madhulumu wanayopata, wasikate tamaa, wasikane imani kwa kuwa baada ya madhulumu watapata utukufu katika Yerusalem mpya (mbinguni) na damu watakayomwaga katika madhulumu ndiyo itawatakasa (Ufu. 7:14).

Kwa kuwa madhulumu yalikuwepo ilikuwa ni vigumu Wakristo kuwasiliana kwa lugha ya wazi ili kuepuka kuuawa au kufungwa. Hivyo Wakristo walitumia lugha ya namba na mafumbo kufikishiana ujumbe kwa waandishi (they used coded language). Kumtaja mfalme wa dola ya Kirumi kwa jina ilikuwa ni dharau na hivyo sababu tosha ya kuuawa. Yohane anatumia lugha ya namba kumtaja mmoja wa wafalme wakatili wa dola ya Kirumi aitwaye NERO kwa kutumia namba 666. Wakristo na wataalamu wa Maandiko Matakatifu walijuaje kuwa 666 inamwakilisha mfalme NERO? Mpaka leo kwa Warumi na Wagiriki kila herufi imepewa thamani ya namba. Walipojumlisha herufi zinazounda jina “NERO” walipata jumla ya 666. Kwa Warumi jina la NERO liliandikwa NERON (likiwa na “N” mwishoni). Walijumlisha herufi za jina NERON na kupata 666 na hivyo kugundua kuwa mnyama aliyetajwa kwenye Ufu. 13:11-18 alikuwa NERO. Kwa nini amezungumziwa mnyama halafu sisi tunazungumzia mtu? Ni kwa sababu Yohane mwenyewe anasema: “Hapa ndipo penye hekima. Yeye aliye na akili, na aihesabu hesabu ya mnyama huyo; maana ni hesabu ya kibinadamu [for it is man’s number]. Na hesabu yake ni mia sita, sitini na sita” (Ufu. 13:18).

Utaalamu wa kuzipa herufi thamani ya namba unaitwa “gematria”. Mfumo wa kuzipa herufi thamani ya namba unafanana na kutofautiana kwa kiasi fulani kwa Warumi na Wagiriki. Utaratibu wa kuthaminisha herufi na namba upo bado. Ndiyo maana tukiwa shule ya msingi tulifundishwa “Namba za Kirumi”. Tunajuaje kuwa MM ni 2000 au MMIX ni 2009. Ni kwa sababu kwa Warumi kila herufi ina thamani ya namba: M ni 1000, hivyo M+M ni sawa na kusema 1000+1000, na hivyo 2000. Tuone sasa kwa jina NERO na thamani ya kila herufi.

Gematria kwa Kirumi: NERON
N = 50
E = 6
R = 500
O = 60
N = 50
neron (50 + 6 + 500 + 60 + 50) = 666

Gematria kwa Wayunani (Waebrania): KAISER NERON

Wayunani walitamka jina ya mfalme kwa kuanza na jina la heshima “title” yaani Kaisari (Ceaser). Hivyo NERO aliitwa qsr nrwn (Kaiser Neron, kwa Kigiriki). Mwanzoni Kiebrania (Kiyunani) hakikuwa na irabu (vowels). Herufi zilizounda neno qsr nrwn (Kaiser Neron) zilipewa thamani ya namba kama ifuatavyo:
q = 60
s = 100
r = 200
n = 50
w = 6
Hivyo basi neno qsr nrwn (60 + 100 + 200 + 50 + 200 + 6 + 50) = 666.

Na Fr. Kelvin O. Mkama

Uzinzi na Uasherati ndio mtego wa kizazi hiki

Uzinzi na uasherati wakati huu umekuwa ndio sumaku kuu ya kuwanasa watu ili waende jehanamu.

Sumaki hii imewanasa hata ambao hawakutegemewa wala kutarajiwa.

Uzinzi uzinzi uzinzi umekuwa kama perfume ya kujipulizia kila Mara mtu akipenda.

Uasherati umekuwa kama heshima ya kibinadamu kwa vijana wengi.

Mbingu zimenyamaza kwa sababu iko jehanamu inawangoja wazinzi na waasherati.

Dhambi hii imekuwa sumaku kubwa ya shetani ya kukamata wanadamu ili waende jehanamu.

Wanadamu wa Leo ukimwambia kwamba aache uzinifu maana wazinzi na waasherati hawataenda uzima wa milele, mtu huyo anakuambia unamhukumu.

Ni Neno la MUNGU ndile limesema katika maandiko mengi tu kwamba wazinzi na waasherati sehemu yako itakuwa katika ziwa la moto.

Hata makanisani baadhi ya watu wamenasa kwenye sumaku hii.

Dada mmoja ambaye kila wiki anasimama na kushika mic kanisani kwao siku moja aliniambia kwamba hawezi kumaliza wiki bila kufanya ngono, na hajaolewa. Niliumia sana rohoni nikamwambia aache kutumika madhabahuni, yeye akasema itakuaje maana yeye ndiye tegemeo.

Mama mmoja alisema yeye ana mume mema sana na mume wake ni mwaminifu sana katika ndoa yao lakini yeye huyo mama ndio hutoka nje ya ndoa Mara kwa Mara, ni hatari inayohitaji neema ya MUNGU tu ili kutubu na kuacha.

Mama mmoja yeye ana watoto zaidi ya wawili na yuko katika ndoa lakini hana uhakika kama watoto wale ni wa mume wake wa ndoa, ni hatari sana.

Baba mmoja akiwa ndani ya ndoa amezaa watoto zaidi ya watatu nje ya ndoa tena wanawake zaidi ya wanne(4) tofauti tofauti.

Mwanaume moja ambaye husimama madhabahuni yeye kila Mara humdanganya mkewe kwamba anaenda safari kumbe ana mahawara karibia kila mkoa, ni hatari sana.

Watu wengi sasa wanaona uzinzi na uasherati ndio fashion nzuri ya wakati kuu.

Kila kijana ana girlfriend kwa lengo la ngono tu na sio vinginevyo.

Kila binti ana boyfriend kwa ajili ya uasherati.

Ukitaka watu wakuchukie basi kemea uzinzi na uasherati.

Watu wengi wamekuwa vipofu wa kiroho kwa sababu ya uzinzi na uasherati.

Lakini upo mwisho mmoja kwa watenda dhambi wote ambayo ni jehanamu.

Ndugu unahitaji kutubu Leo na kuacha dhambi.

Ndugu mmoja akasema yeye anaishi maisha matakatifu ila dhambi moja tu yaani uzinifu ndio imemshinda, hiyo ni hatari.

Leo hata ndoa takatifu zimeadimika maana wahusika huanza kwanza uzinzi na uasherati ndio baadae ndoa, ndugu mnahitaji kutubu.

Ndugu yangu unayenisikiliza kwa njia ya ujumbe huu nakuomba tubu na acha dhambi hiyo.

Amua kuiacha.

Mwisho wa uzinzi na uasherati ni kifo(Mauti) na baada ya kifo ni hukumu(Waebrania 10:27)

Nimekuonya wewe Leo ili ukishupasa shingo usije ukalaumu siku ile ukiwa katikati ya bahari ya moto huku kifo kimezuiliwa ili uteseke milele.

Mimi naamini utatengeneza ndugu baada ya kuusoma ujumbe huu.

Mimi naamini utaachana na mahawara na kuanza kuiheshimu ndoa yako.

Mimi naamini hutamsaliti tena mkeo/Mumeo.

Mimi naamini utaachana na huyo girlfriend/Boyfriend, wengine wanao zaidi ya mmoja, nakuomba ndugu achana nao.

Kijana au binti kaa tulia hadi wakati wako wa ndoa.

Uliyenisikia na utatubu na kuacha dhambi hiyo, MUNGU akubariki sana.“`

ALIYE NA AKILI AWEKE MOYONI MANENO HAYA. AMINA

Shopping Cart