Author name: DIN - Melkisedeck Leon Shine

SALA KWA MT. YOSEFU KUOMBA KUFAHAMU WITO WAKO

Ee uliye Mkuu, Mt. Yosefu, uliyatii kabisa maongozi ya Roho Mt. Unijalie neema ya kufahamu aina ya maisha ambayo Mungu anapenda mimi niishi. Usiniache nidanganyike katika jambo muhimu kama hili, ambalo furaha yangu hapa duniani inalitegemea, na hata pia wokovu wa roho yangu.

Unijalie, nikiangazwa na matakwa matakatifu na nikiwa mwaminifu katika kuyatimiza, nikumbatie aina ya maisha ambayo Mungu ameniandalia na yatakayoniongoza kwenye furaha ya milele.
Amina.

SALA KWA MAMA WA UCHUNGU KUOMBA NEEMA YA PEKEE

Ee Mama mbarikiwa na Bikira mwenye uchungu, Malkia wa Mashahidi, uliyesimama chini ya msalaba na uliyemtazama Mwana wako akifa, unitazame kwa huruma ya kimama ninayekusikitikia. Kwa sababu ya upanga uliochoma moyo wako, kwa mateso ya maisha yako nakuomba uniangalie kwa wema ukasikilize maombi yangu. Nakuomba, ee Mama, uniombee daima kwa Mwana wako, najua hawezi kukuvyima wewe kitu chochote. Basi, ufanye, Moyo wa Mwanao ukubali kunijalia ombi langu hili …………………(taja ombi lako).
Maana nitamkimbilia nani katika mahitaji na misiba yangu isipokuwa kwako, ee Mama wa huruma? Wewe hasa unaweza kutusaidia sisi tulio bado katika bonde la machozi kwa sababu ulishiriki mateso ya Mwanao kutukomboa. Umtolee Yesu tone moja la Damu yake takatifu. Umkumbushe ya kuwa wewe ni matumaini, furaha na maisha yetu ukanipatie jambo ninalokuomba kwa Yesu Kristo, bwana wetu. Amina.

SALA KWA MT. YOSEFU KWA WASIO NA AJIRA WAPATE AJIRA

Ee Mt. Yosefu, tunakuomba kwa ajili ya wale asio na ajira, kwa ajili ya wale wanaotaka kujipatia kipato chao na kulisha familia zao.
Wewe u Msimamizi wa wafanyakazi, tujalie kwamba pasiwepo kati yetu mtu asiye na ajira, na kwamba wale wote ambao wako tayari kufanya kazi waweze kuelekeza nguvu zao na uwezo wao katika kuwatumikia wanadamu wenzao na kujipatia kipato halali.

Wewe u Msimamizi wa familia, usiwaache wale wenye watoto wa kuwatunza na kuwalea wakose namna ya kufanya hivyo. Uwahurumie ndugu zetu waliokosa ajira na kugubikwa na umasikini kwa sababu ya magonjwa au mipango mibaya ya kijamii. Wasaidie viongozi wetu wa kisiasa na walioshika usukani katika nyanja mbalimbali za kiuzalishaji wavumbue suluhu mpya na za haki za jambo hili. Utujalie ili kila mmoja wetu apate kujipatia kipato halali na kufurahia fursa ya kushiriki kadri ya uwezo wake, katika maisha bora zaidi kwa wote. Utujalie ili wote tushiriki pamoja katika raslimali alizotujalia Mungu, na pia utujalie tuwe tayari daima kuwasaidia wale walio wahitaji kuliko sisi.
Amina.

Shopping Cart