Author name: DIN - Melkisedeck Leon Shine

Amri za Kanisa: Mambo ya Muhimu kujua na Kuzingatia

Amri za Kanisa ni zipi?

Amri za kanisa ni;
1. Hudhuria Misa Takatifu Dominika na sikukuu zilizoamriwa.
2. Funga siku ya Jumatano ya Majivu; usile nyama siku ya Ijumaa Kuu
3.Ungama dhambi zako walau mara moja kila mwaka.
4. Pokea Ekaristi Takatifu hasa wakati wa Pasaka
5. Saidia Kanisa Katoliki kwa zaka
6. Shika sheria Katoliki za ndoa.


Katika Amri ya kwanza ya Kanisa tumeamriwa nini?

Tumeamriwa tusikilize Misa kila siku ya Mungu na Sikukuu zilizoamriwa.


Sikukuu zilizoamriwa ni zipi?

Ndizo:

1. Kuzaliwa kwa Yesu – Noeli tarehe 25/12
2. Pasaka –
 Ufufuko wa Bwana Yesu
3. Kupaa Yesu —- Siku 40 baada ya Pasaka.
4. Kupalizwa Mbinguni Bikira Maria 15/8
5. Sikukuu ya Watakatifu Wote 1/11


Katika Amri ya Kwanza ya kanisa tumekatazwa nini?

Tumekatazwa;
1. Kukosa Misa
2. Kufanya kazi nzito siku hizo


Kujinyima ni nini?

Kujinyima ni kujikatalia kitu ukipendacho mfano nyama, pombe, sigara, muziki, safari, maongezi n.k.


Nani ana lazima ya kufunga?

Kila Mkristo aliyetimiza miaka 14 na zaidi anapaswa kufunga kula nyama (Ijumaa kuu) na mwenye miaka zaidi ya 21 kufunga chakula. (Jumatano ya Majivu)


Siku za kufunga ni zipi? Na siku gani tumekatazwa kula nyama?

Siku za kufunga ni Jumatano ya majivu, siku za Kwaresima isipokuwa Dominika zake, na siku iliyokatazwa kula nyama ni siku ya Ijumaa kuu.


Katika Amri ya Tatu ya Kanisa tumeamriwa nini?

Katika Amri ya Tatu ya Kanisa tumeamriwa kuungama mara kwa mara walau mara moja kila mwaka


Katika Amri ya Nne ya Kanisa tumeamriwa nini?

Katika Amri ya Nne ya Kanisa tumeamriwa tupokee Ekaristi Takatifu walau mara moja kwa mwaka wakati wa pasaka.


Katika Amri ya Tano ya Kanisa tumeamriwa nini?

Katika Amri ya Tano ya Kanisa tumeamriwa kufahamu kuwa gharama za dini na za mapadre zatupasa. Yaanai wakristo walitegemeze Kanisa na wahudumu wake na hasa katika kazi ya kueneza injili.


Zaka ni nini?

Zaka ni asilimia kumi (10%) ya pato la mtu kwa mwaka ambalo anapaswa kulitoa kwa Kanisa.


Asiyelipa Zaka na michango mingine ya Kanisa ya lazima atenda dhambi gani?

Atenda dhambi kubwa: Yampasa kulipa na kuungama.


Amri ya Sita ya Kanisa Inadai nini?

Inadai kushika Sheria Takatifu Za ndoa

Amri ya nne ya Mungu: Kuheshimu Wazazi

Katika Amri ya nne ya Mungu tumeamriwa nini?

Tumeamriwa tuwaheshimu wazazi wetu na wakubwa wetu wote, tuwapende, tuwatii na tuwaombee. (Kut 20:12, Kol 3:20)


Amri ya Nne ya Mungu tumeamriwa nini?

Tumeamriwa tuwaheshimu wazazi wetu na wakubwa wote, tuwapende, tuwatii na tuwaombee. (Kut 20:12), Kol 3:20


Kwa sababu gani yatupasa kuwaheshimu Baba na Mama?

Yatupasa kuwaheshimu Baba na Mama kwa sababu;

1. Wameshirikiana na Mungu kutuleta duniani walipotuzaa
2. Wamewekwa na Mungu ili watulee na kutuongoza Mbinguni
3. Mungu ameamuru tuwapende wazazi mara baada ya Yeye. (Ayu 3:1-9)


Wazazi na wakubwa wameamriwa nini?

Wazazi na wakubwa wameamriwa watutunze na kutulea


Tuwaheshimu Baba na Mama kwa matendo gani?

Tuwaheshimu Baba na Mama kwa matendo ya adabu, heshima, utii na mapendo (Ayu 3:12)


Twawakosea Heshima Baba na Mama kwa kufanya nini?

Twawakosea Heshima Baba na Mama kwa;

1. Tukiwakasirisha na kuwatukana
2. Tukiwakaidi na kuwapiga
3. Tukiacha kuwaombea
4. Tukiacha kuwasaidia katika shida na uzee. (Kut 21:15-17)


Wazazi wawaleeje watoto wao katika imani ya Kikristo?

Wawalee hasa kwa mfano wao, kwa sala, kwa katekesi ya kifamilia na kushiriki maisha ya Kanisa


Lini tunakatazwa kuwatii watu?

Tunakatazwa kuwatii watu wanaotuamuru jambo lililokatazwa na Mungu (Mdo 5:29)


Katika Amri ya Nne ya Mungu tumekatazwa nini?

Tumekatazwa haya;

1. Kukaidi wazazi na wakubwa wetu
2. Kuwakasirisha.
3. Kuwadharau.


Wakubwa tunaopaswa kuwaheshimu ni kina nani?

Wakubwa hao ni;

1. Viongozi wa Kanisa
2. Viongozi wa Serikali
3. Walimu na walezi
4. Wakubwa wa kazi (War 13:1)
5. Viongozi wa Jumuiya

Amri ya Tano ya Mungu: Kutunza uhai wetu na wa watu wengine

Katika Amri ya Tano ya Mungu tumeamriwa nini?

Tumeamriwa tutunze uhai wetu na wa watu wengine tangu mwanzo hadi mwisho. (Mwa 4:10-11)


Kwa nini ni lazima kutunza uhai wetu na wa wenzetu?

Kwa sababu uhai wa watu wote umetoka kwa Mungu


Haki gani ya Binadamu ni ya msingi kupita zote?

Haki ya binadamu iliyo ya msingi kupita zote ni uhai wake ambao ni lazima uheshimiwe na kulindwa tangu siku ya kutungwa mimba


Nani anatenda dhambi dhidi ya amri ya tano ya Mungu? Mambo yanayovunja Amri ya Tano ya Mungu

Anayetemda dhambi dhidi ya amri ya tano ya Mungu ni yule;-

1. Anayemuua mtu au anayejiua mwenyewe
2. Anayemdhuru mwingine kwa namna yoyote ile
3. Anayeua Mimba na kuharibu nguvu za uzazi
4. Anayesaidia kuua, kumdhuru mtu au anayesaidia kutoa/kuharibu mimba
5. Anayeharibu mazingira yaliyomuhimu kwa uhai
6. Anayetetea au kuendeleza mifumo ya ya dhuluma, uhasama na vita.

Amri ya Nane ya Mungu: Makatazo na Amri

Amri ya Nane ya Mungu inatukataza nini?

Inakataza haya:

1. Ushahidi wa uongo, kiapo cha uongo na uongo wowote.
2. Hukumu isiyo ya haki, usengenyaji, uchafuzi wa jina na usingiziaji.
3. Kusifu watu uongo, kujisifu mwenyewe au ulaghai.


Katika Amri ya Nane Mungu anaamuru nini?

Katika Amri ya Nane Mungu anaamuru tuseme ukweli na tulinde heshima ya wengine. (Mt 5:37, Yak 5:12).


Twaharibu heshima ya wengine kwa namna gani?

Twaharibu Kwa

1. Kuwadhania vibaya
2. Kuwasengenya (Mith 12:22)
3. Kuwasingizia na kuleta uzushi. (Mdo 5:1-11; Law 19:11)


Aliyeharibu heshima ya mwingine yampasa afanye nini?

Aliyeharibu heshima ya mwingine yampasa kuirudisha kadiri awezavyo.


Tunalinda heshima ya wengine kwa namna gani?

Tunalinda heshima ya wengine kwa kuwaza na kusema mema juu yao. (1Kor 13:6)

Shopping Cart