Author name: DIN - Melkisedeck Leon Shine

MASOMO YA MISA, MARCHI 16, 2022: JUMATANO, JUMA LA 2 LA KWARESIMA

SOMO 1

Yer. 18-18-20

Waliposema, Njoni na tufanye mashauri juu ya Yeremia; maana sheria haitampotea kuhani, wala shauri halitampotea mwenye hekima, wala neno halitampotea nabii. Njoni, na tumpige kwa ndimi zetu, wala tusiyaangalie maneno yake yoyote.

Niangalie, Ee Bwana, ukasikilize sauti ya wanaoshindana nami. Je! Mabaya yalipwe badala ya mema? Maana wameichimbia nafsi yangu shimo. Kumbuka jinsi nilivyosimama mbele zako, ili nisema mema kwa ajili yao, nikaigeuze ghadhabu yako isiwapate.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 31:4-5, 13-15 (K) 16

(K) Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako, Ee Bwana.

Utanitoa katika wavu walionitegea kwa siri,

Maana Wewe ndiwe ngome yangu.

Mikononi mwako naiweka roho yangu;

Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli. (K)

Maana nimesikia masingizio ya wengi;

Hofu ziko pande zote.

Waliposhauriana juu yangu,

Walifanya hila wauondoe uhai wangu. (K)

Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana,

Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu.

Nyakati zangu zimo mikononi mwako;

Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia. (K)

SHANGILIO

Lk. 8:15

Heri wale walishikao neno la Mungu katika moyo wao mwema na unyofu, na wazaao matunda katika uvumilivu.

INJILI

Mt. 20:17-28

Yesu alipokuwa akipanda kwenda Yerusalemu aliwachukua wale wanafunzi kumi na wawili faraghani; na njiani akawaambia, Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu; na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa wakuu wa makuhani na waandishi nao watamhukumu afe; kisha watampeleka kwa Mataifa wapate kumdhihaki, na kumpiga mijeledi na kumsulibisha; na siku ya tatu atafufuka.

Ndipo mama yao wana wa Zebedayo akamwendea pamoja na wanawe, akamsujudia, na kumwomba neno. Akamwambia, Wataka nini? Akamwambia, agiza kwamba hawa wanangu wawili waketi mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika ufalme wako. Yesu akajibu akasema, Hamjui mnaloliomba. Je! Mwaweza kunywea kikombe nitakachonywea mimi? Wakamwambia, Twaweza. Akawaambia, Hakika mtakinywa kikombe change; lakini kuketi mkono wangu wa kuume na mkono wangu wa kushoto, sina amri kuwapa, bali watapewa waliowekewa tayari na Baba yangu.

Na wale kumi waliposikia, waliwakasirikia wale ndugu wawili. Lakini Yesu akawaita, akasema, Mwajua ya kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu yeyote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu; na mtu yeyote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumikia na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

Vile unavyoweza kuwa DARAJA au KIKWAZO kwa wengine

Kwa namna unayoishi unaweza ukawa daraja au kikwazo cha wengine kuishi maisha ya Amani raha na fanaka.
Unaweza ukawa daraja kwa maana kwamba wewe unaweza kuwa sababu ya wengine kupata Baraka na neema za Mungu.
Unaweza kuwa kikwazo kwa maana kwamba unaweza kuwa wewe ni sababu ya wengine kutokupata Baraka na Neema za Mungu.

Kwa jinsi unavyoishi unaweza ukawa chanzo cha Baraka kwa wengine au chanzo cha matatizo na vikwazo kwa wengine.

Vile unavyoweza kuwa Daraja kwa Wengine

Unaweza kuwa daraja au njia ya wengine kupata neema na Baraka katika maisha yao kulingana na matendo yako mema na Ibada yako kwa Mungu.

Kwa ucha Mungu wako, watu wako unaowapenda sana wanaweza kubarikiwa na kupata neema za Mungu Pamoja na wewe. Wale watu unaochangamana nao watabarikiwa kwa sababu na wewe umebarikiwa.
Kwa mfano wewe kama ni mzazi mcha Mungu unaweza ukawa chanzo cha Baraka na neema kwa watoto wako na kwa mwenzi wako wa ndoa. Vivyo hivyo na kwa watoto, mtoto anaweza kuwa chanzo cha Baraka kwa wazazi wake.

Inawezekana kuna Amani katika familia yako kwa sababu tuu wewe ni miongoni mwa wanafamilia hiyo na hivyo Mungu ameachilia Amani katika familia yako kwa sababu tuu wewe upo pale na wewe ni mcha Mungu.

Unaweza kuona sasa wewe ni chanzo cha Baraka kwa wale watu wako wa karibu. Kwa sababu tuu wewe ni mcha Mungu, na wao wanabarikiwa pamoja na wewe. Mungu anapobariki familia yako na wao pia wanabarikiwa.

Kwa hiyo basi, unapolegalega katika ucha Mungu wako unaweza pia kusababisha kulegalega au kikwazo cha Baraka za wengine.

Vile unavyoweza kuwa Kikwazo kwa Wengine

Unaweza kuwa kikwazo au kizuizi cha wengine kupata neema na Baraka katika maisha yao kulingana na matendo yako mabaya na kukosa kwako kumcha Mungu.

Kwa kuacha kumcha Mungu, watu wako unaowapenda sana wanaweza kukosa kubarikiwa na kukosa neema za Mungu kwa sababu wewe unazuia Baraka hizo. Wale watu unaochangamana nao watakosa Baraka kwa sababu umeandikiwa kutokubarikiwa na wanachanganyikana na asiyestahili kubarikiwa.

Kwa mfano wewe kama ni mzazi asiyemcha Mungu unaweza ukasababisha watoto wako wakashindwa kubarikiwa kwa sababu tuu kwa udhambi wako unazuia Baraka kwa familia yako yote wakiwemo watoto wako. Vivyo hivyo na wazazi wanaweza wakashindwa kubarikiwa kwa sababu watoto wao wanawazuilia Baraka zao.

Inawezekana hakuna Amani katika familia yako kwa sababu tuu wewe ni miongoni mwa wanafamilia hiyo. Kunakosekana Amani katika familia yako kwa sababu tuu wewe upo pale na wewe ni mdhambi/ mtu asiyemcha Mungu.

Unaweza kuona sasa wewe ni chanzo cha kukosekana Baraka kwa wale watu wako wa karibu. Kwa sababu tuu wewe ni mtu asiye mcha Mungu, na wao wanazuiliwa baraka pamoja na wewe. Mungu anapoacha kuibariki familia yako na wao pia wanakosa baraka. Kwa mfano unapokosa Amani na Mafanikio ukae ukijua kuwa wale unaowapenda na wanaokutegemea nao watakosa Amani na hawatanufaika kwa sababu hauna mafanikio.

Mwisho

Wewe ni kama Kiungo cha myororo wa Baraka au laana kwa wale uwapendao hasa familia yako. Ukibarikiwa unabarikiwa pamoja nao, ukilaaniwa unalaaniwa pamoja nao.

Kwa sababu hiyo, mara zote chagua kuishi kwa kumcha Mungu kwa sababu huwezi jua ni wangapi walioko nyuma yako na wanaobarikiwa kwa sababu ya ucha Mungu wako.

Mche Mungu kwa juhudi zote kwa sababu hujui ni wangapi wanaonufaika na ucha Mungu wako. Vilevile jitahidi usiwe mdhambi sana kwa sababu huwezi kujua ni wangapi wanaokosa Baraka za Mungu kwa udhambi wako.

Kumcha Mungu kuna faida kwako na kwa wengine, hasa unaowapenda. Kuto kumcha Mungu ni hasara kwako na kwa wale unaowapenda hasa familia yako

MASOMO YA MISA, JULAI 26, 2021 JUMATATU, JUMA LA 17 LA MWAKA

SOMO 1

Kut. 32:15-24, 30-34

Musa aligeuka akashuka katika mlima, na zile mbao mbili za mawe mikononi mwake; mbao ziliandikwa pande zote mbili, upande huu na upande huu ziliandikwa. Na zile mbao zilikuwa kazi ya Mungu, nayo maandiko yalikuwa maandiko ya Mungu, yaliyochorwa katika zile mbao.

Na Yoshua aliposikia kelele za watu walipokuwa wakipiga kelele, akamwambia Musa, Kuna kelele ya vita maragoni. Akasema, Hiyo si sauti ya watu wapigao kelele kwa sababu ya kushinda vitani, wala si sauti ya watu wapigao kelele kwa sababu ya kushindwa; bali kelele za watu waimbao nizo ninazozisikia mimi.

Hata alipyakaribia marago akaiona ile ndama, na ile michezo. Hasira ya Musa ikawaka, akazitupa zile mbao mikononi mwake, akazivunja chini ya mlima. Akaitwaa ile ndama walioifanya, akaichoma moto, akaisaga hata ikawa mavumbi, akainyunyiza juu ya maji, akawanywesha wana wa Israeli. Musa akamwambia Haruni; Watu hawa wamekufanyani hata ukaleta dhambi hii kuu juu yao? Haruni akasema, Hasira ya bwana wangu isiwake; wewe unawajua watu hawa, ya kuwa wamejielekeza kwa mabaya. Maana waliniambia, Katufanyie miungu itakayokwenda mbele yetu, kwa maana mtu huyo Musa, aliyetutoa katika nchi ya Misri, hatujui yaliyompata. Nikawaambia, Mtu yeyote aliye na dhahabu na aivunje; basi wakanipa, nami nikaitupa ndani ya moto, akatoka ndama huyu.

Basi asubuhi yake Musa akawaambia watu, Mmetenda dhambi kuu; na sasa nitakwenda juu kwa Bwana, labda nitafanya upatanisho kwa ajili ya dhambi yenu. Musa akarejea kwa Bwana akasema, Aa! Watu hawa wametenda dhambi kuu, wamejifanyia miungu ya dhahabu. Walakini sasa ikiwa utawasamehe dhambi yao – na kama sivyo, unifute, nakusihi, katika kitabu chako ulichokiandika. Bwana akamwambia Musa, Mtu yoyote aliyenitenda dhambi, ndiye nitakayemfuta katika kitabu changu. Basi sasa uende ukawaongoze watu hawa mpaka mahali pale ambapo nimekuambia habari zake; tazama, malaika wangu atakutangulia; pamoja na hayo siku nitakayowajilia nitawapatiliza kwa ajili ya dhambi yao.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 106:19-23 (K) 1

(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema.

Walifanya ndama huko Horebu,

Wakaisujudia sanamu ya kuyeyuka.

Wakaubadili utukufu wao,

Kuwa mfano wa ng’ombe mla majani. (K)

Wakamsahau Mungu, mwokozi wao,

Aliyetenda makuu katika Misri.

Matendo ya ajabu katika nchi ya Hamu,

Mambo ya kutisha penye bahari ya Shamu. (K)

Akasema ya kuwa atawaangamiza,

Kama Musa, mteule wake, asingalisimama,

Mbele zake kama mahali palipobomoka,

Ili aigeuze hasira yake asije akawaharibu. (K)

SHANGILIO

Efe. 1:17, 18

Aleluya, aleluya,

Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristu, awape roho ya hekima mjue tumaini la mwito wake.

Aleluya.

INJILI

Mt. 13:31 – 35

Yesu aliwatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na punje ya haradali, aliyoitwaa mtu akaipanda katika shamba lake; nayo ni ndogo kuliko mbegu zote; lakini ikiisha kumea, huwa kubwa kuliko mboga zote, ikawa mti, hata nyuni wa angani huja na kukaa katika matawi yake.

Akawaambia mfano mwingine; Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu aliyoitwaa mwanamke, akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachachwa wote pia.

Hayo yote Yesu aliwaambia makutano kwa mifano; wala pasipo mfano hakuwaambia neno; ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema, Nitafumbua kinywa changu kwa mifano, Nitayatamka yaliyositirika tangu awali.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, JUMAPILI JULAI 25 2021: DOMINIKA YA 17 YA MWAKA B WA KANISA

SOMO 1

2 Wafalme:4.42

Alikuja mtu kutoka Baal-shalisha, akamletea mtu wa Mungu chakula cha malimbuko, mikate ishirini ya shayiri, na masuke mabichi ya ngano guniani. Akasema, Uwape watu, ili wale. Na mtumishi wake akasema, Je! Niwaandikie hiki watu mia? Lakini akasema, Uwape watu, ili wale; kwa kuwa Bwana asema hivi, Watakula na kusaza. Basi akawaandikia, nao wakala, wakasaza, sawasawa na neno la Bwana.

WIMBO WA KATIKATI

1. Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru, Na wacha Mungu wako watakuhimidi. Wataunena utukufu wa ufalme wako, Na kuuhadithia uweza wako. (K)

Waufumbua mkono wako, wakishibisha kila kilicho hai matakwa yake.

2. Macho ya watu yakuelekea Wewe, Nawe huwapa chakula chao wakati wake. Waufumbua mkono wako, Wakishibisha kila kilicho hai matakwa yake. (K)

3. Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote, Na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote. Bwana yu karibu na wote wamwitao, Wote wamwitao kwa uaminifu.

SOMO 2

Waefeso:4.1 – 6

Nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani. Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu. Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja. Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote.

SHANGILIO

Yohana:14.6

Aleluya Aleluya!

Mimi ndimi njia, na ukweli, na uzima, asema Bwana; Mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. Aleluya

INJILI

Yn. 6:1-15

Yesu alikwenda zake ng’ambo ya Bahari ya Galilaya, nayo ndiyo ya Tiberia. Na mkutano mkuu wakamfuata, kwa sababu waliziona ishara alizowafanyia wagonjwa. Naye Yesu akakwea mlimani, akaketi huko pamoja na wanafunzi wake. Na Pasaka, sikukuu ya Wayahudi, ilikuwa karibu. Basi Yesu alipoinua macho yake akaona mkutano mkuu wanakuja kwake, alimwambia Filipo, Tununue wapi mikate, ili hawa wapate kula? Na hilo alilinena ili kumjaribu; kwa maana alijua mwenyewe atakalotenda. Filipo akamjibu, Mikate ya dinari mia mbili haiwatoshi, kila mmoja apate kidogo tu. Wanafunzi wake mmojawapo, Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia, Yupo hapa mtoto, yuna mikate mitano ya shayiri na samaki wawili, lakini hivi ni nini kwa watu wengi kama hawa? Yesu akasema, Waketisheni watu. Na mahali pale palikuwa na majani tele. Basi watu waume wakaketi, wapata elfu tano jumla yao. Basi Yesu akaitwaa ile mikate, akashukuru, akawagawia walioketi; na kadhalika katika wale samaki kwa kadiri walivyotaka. Nao waliposhiba, aliwaambia wanafunzi wake, Kusanyeni vipande vilivyobaki, kisipotee cho chote. Basi wakavikusanya, wakajaza vikapu kumi na viwili, vipande vya mikate mitano ya shayiri vilivyowabakia wale waliokula. Basi watu wale, walipoiona ishara aliyoifanya, walisema, Hakika huyu ni nabii yule ajaye ulimwenguni. Kisha Yesu, hali akitambua ya kuwa walitaka kuja kumshika ili wamfanye mfalme, akajitenga, akaenda tena mlimani yeye peke yake.

Neno la Bwana….. Sifa Kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, JULAI 24, 2021: JUMAMOSI, JUMA LA 16 LA MWAKA

SOMO 1

Kut. 24:3-8

Musa aliwambia watu maneno yote ya Bwana, na hukumu zake zote; watu wote wakajibu kwa sauti moja, wakasema, Maneno yote aliyoyanena Bwana tutayatenda. Basi Musa akayaandika maneno yote ya Bwana, akaondoka asubuhi na mapema, akajenga madhabahu chini ya mlima, na nguzo kumi na mbili, kwa hesabu ya kabila kumi na mbili za Israeli, akapeleka vijana wa wana wa Israeli, waliotoa sadaka za kuteketezwa, wakamchinjia Bwana sadaka za amani za ng’ombe. Musa akatwaa nusu ya ile damu, akaitia katika mabakuli; na nusu ya ile damu akainyunyiza juu ya madhabahu. Kisha akakitwaa kitabu cha agano akakisoma masikioni mwa watu; wakasema, Hayo yote aliyoyanena Bwana tutayatenda, nasi tutatii. Musa akaitwaa ile damu, akawanyunyizia watu, akasema, Hii ndiyo damu ya agano alilolifanya Bwana pamoja nanyi katika maneno haya yote.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 50:1-2, 5-6, 14-15 (K) 14 (K)

Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru. Mungu, Mungu Bwana, amenena, ameiita nchi, Toka maawio ya jua hata machweo yake. Tokea Sayuni,, ukamilifu wa uzuri, Mungu amemulika. (K)

Nikusanyieni wacha Mungu wangu, Waliofanya agano nami kwa dhabihu. Na mbingu zitatangaza haki yake, Kwa maana Mungu ndiye aliye hakimu. (K)

Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru; Mtimizie Aliye juu nadhiri zako. Ukaniite siku ya mateso; Nitakuokoa, na wewe utanitukuza. (K)

SHANGILIO

Zab. 8:15

Aleluya, aleluya,

Wanabarikiwa wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao, hulisikia neno la Mungu na kulishika.

Aleluya.

INJILI

Mt. 13:24 – 30

Yesu aliwatolea makutano mfano akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake; lakini watu walipolala akaja adui yake akapanda magugu katikati ya agano, akaenda zake. Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu. Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu? Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye? Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa ngano pamoja nayo. Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

Shopping Cart