MATATIZO YANAYORUDISHA UIMBAJI WA KWAYA KATOLIKI NYUMA

1.Kuwaimbia binadamu.Yaani tupo kwa ajili ya kuimba ili tusifiwe na watu.
2.Kuimba bila tafakari.Mara nyingi tunaimba tu bila kuzingatia ujumbe Wa ule wimbo
3.Kuimba bila kusali!Yasemekana Kuimba ni kusali Mara mbili.Waimbaji wengi hukariri wimbo na nyimbo nyingi zimetungwa kwa njia ya sala lakini wanakwaya wengi huimba tu wala hali ya sala haimo ndani yao!
4.Walimu wenye hasira na ubinafsi.Mkufunzi Wa kwaya ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya uimbaji.Iwapo choirmaster ni mwenye vurugu, mchochezi na mpenda fitina, bila shaka itakuwa vigumu kwa kwaya kupiga hatua kiuimbaji!
5.Sheria Kali zisizoenda na maadili ya kanisa.Kila jamii INA sheria zake na sheria ni nzuri.lakini tukiwa na sheria zinazowakandamiza wengine, tutapoteza kondoo wengi badala ya kuwaleta kwa Mungu!
6.Utoaji Wa albamu au kurekodi nyimbo kwa nia ya kutafuta pesa au kigezo kwa kwaya.Kwaya nyingi zimeanguka pindi tu wanapotoa albamu ya kwanza!Maana tunakosa kufahamu kuwa sisi ni wainjilisiti na tunawasaidia mapadri wetu kuhubiri injili.
7.Kutotii viongozi Wa kanisa.Wanakwaya wanaokosa kufahamu kuwa wapo chini ya viongozi na kanisa husika Mara nyingi hujipata wakiwa kwa makosa bila kunuia!
8.Kutoishi kwa hali ya sakramenti!Kama kuna jambo kubwa ambalo ibilisi hufurahia, ni yule MTU anayeishi katika maisha ya ndoa isiyo halali mbele za Mungu.Yaani Maana yake unaishi na mke au Mme bila ndoa ya kanisa na huna kizuizi chochote kinachokufanya usipate sakramenti hiyo.
9.Kitubio.Wengi tunapokea sakramenti ya ekaristi katika hali ya dhambi na hatushughuliki kabisaa kwenda kitubio.Hii inachochea zaidi kuwepo kwa dhambi za mazoea katika maisha yetu!
10.Kutosali kila siku.Inakuwa rahisi kwetu sisi kujaribiwa tukiwa hatusali.Kuimba kwako kunawasha hasira za shetani kwa hivo usiposali, bila shaka atarudi kulipiza kisasi.

Nifunge nini Kwaresma? Mambo ya kufunga kipindi cha Kwaresima

NIFUNGE NINI?
Funga huzuni upate furaha,
Funga ulabu upate siha,
Funga majivuno upata utukufu,
Funga uzinzi upate wongofu,
Funga kisirani upate utakatifu,
Funga umbea upate fanaka,
Funga wivu upata baraka,
Funga unafiki upate uchaji,
Funga kinyongo upate faraja,
Funga kwaresima wakati ni huu
Funga kiburi ujazwe hekima,
Funga jeuri ujawe rehema,
Funga hofu ujazwe imani,
Funga kinywani ujazwe moyoni,
Funga kisirani ujazwe rohoni,
Funga dharau ujazwe heshima,
Funga majungu, ujazwe neema,
Funga usiri ujawe wafuasi,
Funga tamaa ujazwe kiasi,
Funga kwaresima wakati ni huu.

Maana kamili ya Kwaresma

Neno kwaresma ni neno la kilatini liitwalo Quadragesima maana yake ni arobaini(40). Mpenzi msomaji, katika maisha ya kikristo kuna kipindi cha siku 40.majira haya ya kwaresma huanza siku ya jumatano ya majivu na kuishia jumapili ya pasaka siku ambayo wakristo wanakumbuka kufufuka kwa yesu kristo kutoka katika wafu.
Kwaresma ni kipindi maalum ambacho wakristo wanakumbuka maisha ya Yesu kristo hapa duniani hususan mateso, kufa na kufufuka kwake.
Ni kipindi cha kutafakari maana na umuhimu wa dhabihu ya YESU kristo katika ukombozi wa dunia na kumrudia Mungu. Aidha ni kipindi ambacho wakristo wanakumbushwa kufanya toba na kumrudia Mungu kwa mujibu wa maandiko matakatifu.
Ingawa kipindi cha kwaresma ni kipindi cha mafungo kwa wakristo, watu wengi na hasa wa dini nyingine hushindwa kutambua funga inayofanywa na wakristo katika kipindi hiki na hasa kwa sababu wakristo wengi huonekana wakiendelea kula na kunywa wakati wa kwaresma. Wakristo walio wengi pamoja na kufuata kielelezo cha Yesu kristo ambae alifunga siku arobaini (usiku na mchana) huzingatia maagizo ya YESU mwenyewe na nabii Isaya ambao kwa kiasi kikubwa hufafanua aina ya funga ambayo wakristo wanapaswa kuizingatia.
Mwenyezi Mungu alitoa maagizo ya namna ya kufunga kupitia kwa nabii isaya akisema hivi
“Walakini wanitafuta kila siku, hupenda kujua njia zangu ; kama vile taifa waliotenda haki, wasioacha sheria ya Mungu wao. Hutaka kwangu sheria za haki, humkaribia Mungu. Husema, mbona tumefunga lakini huoni? Mbona tumejitaabisha nafsi zetu lakini huangalii? Fahamuni siku ya kufunga kwenu mnatafuta anasa zenu wenyewe, na kuwalemea wote watendao kazi kwenu. Tazama, ninyi mwafunga mpate kushindana na kugombana na kupiga kwa ngumi ya uovu. Hamfungi siku hii ya leo hata kuisikizisha sauti yenu juu. Je, kufunga namna hii ni saumu niliyoichagua mimi? Je, ni siku ya mtu kujitabisha nafsi yake? je ni kuinamisha kichwa kama unyasi na kutanda nguo za magunia na majivu chini yake? je utasema ni siku ya kufunga na ya kukubaliwa na BWANA? Je, saumu niliyoichagua sio ya namna hii? Kufunguo vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaachia huru walio onewa, na kwamba mvunje kila nira? Je, sio kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? umwonapo mtu aliye uchi umvike nguo, wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe? Ndipo nuru yako itakapo pambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia, utukufu wa BWANA (Mungu) utakufuata nyuma ukulinde. Ndipo utaita na BWANA ataitika, utalia nae atasema mimi hapa…” (Isaya 58: 2-9).
Mwenyezi Mungu alitoa maagizo haya baada ya kuona watu wengi wakipoteza muda mwingi na kujitabisha kuacha kula na kujitesa miili yao ili kumpendeza Mungu, huku wakisahau mambo muhimu zaidi ambayo Mungu anawataka wafanye ili kumpendeza. (Katika kipindi hicho wayahudi walikuwa wakifunga kwa kujitesa sana ikiwa ni pamoja na kuacha kula, kuvua nguo zao za thamani na kuvaa magunia, kujipaka majivu na wengine kujipiga na kujikata miili yao ili waone maumivu zaidi.
Aidha, watu walikuwa wakitumia kipindi cha kufunga kuuonesha umma jinsi walivyo wacha Mungu na hivyo kupewa heshima mtaani. Mtu asiyefunga alionekana mjinga, mtenda dhambi na asiyefaa katika jamii. Kufunga ilikuwa sehemu ya maisha na si suala la uhusiano binafsi kati ya mtu na Mungu).

Kwa vile Mwenyezi Mungu wetu ni wa upendo na huruma, alimtuma nabii isaya kuwaambia watu hao kuachana na funga hiyo isiyo na maana na badala yake kuelekeza nguvu zao katika mambo muhimu ambayo Mungu anaangalia katika kutathimini utu wa mtu. Mambo hayo ni upendo, huruma na kujitoa kama ilivyoelezwa hapo juu na kuachana uovu wa aina zote.. Kwa msingi huo, mtu mwenye upendo na anaejitoa kusaidia wengine ana thamani kubwa mbele za Mungu kuliko mtu anaeshinda njaa siku 300 za mwaka pasipo kuonesha upendo wa kweli kwa wengine.
Yesu kristo alipokuja ulimwenguni, alisisitiza maneno ya nabii Isaya kwa kutaka watu waache tabia ya funga za kujionesha kwa watu, na badala yake wajitahidi kumpendeza Mugu.
Yesu alisema “Tena mfungapo msiwe kama wanafiki wenye nyuso za kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao ili waonekane na watu kuwa wanafunga. Amini nawaambia, wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso; ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na baba yako (Mungu) aliye sirini; na baba yako aonae sirini atakujazi” (Mathayo 6:16)
Kumbe tabia ya kujionesha mbele za watu kwamba tumefunga inamuudhi Mungu na kutufanya tukose thawabu. Mtu anaejionesha au kujisifu kwamba anafunga huambulia kusifiwa na watu wa kidunia ambao wanadhani mtu huyo ni mtakatifu sana, lakini kwa mujibu wa maandiko matakatifu mtu huyo anajisumbua na kupoteza muda wake bure kwani hakuna thawabu anayo pata kwa Mwenyezi Mungu.
Tumuombe Mungu sana atuongoze na kutusaidia katika kipindi hiki cha Kwaresma na baada ya hapo.Ni wajibu wetu kujitahidi kuachana na maovu yote, kufanya toba ya kweli na kumpokea Yesu katika mioyo yetu badala ya kumuabudu kwa midomo tu. Tunapaswa kukumbuka kuwa Mungu wetu ni yule yule kabla, wakati na baada ya kipindi cha Kwaresma na hivyo kipindi hiki kiwe kipindi cha kutukumbusha na kutuandaa kwa ajili ya wakati mrefu ujao baada ya Kwaresma.

Ijue Ishara ya Msalaba

Ishara ya Msalaba ni tendo la mtu kugusa paji la uso, kifua na mabega kwa kutumia mkono wa kulia na kutamka ‘Kwa Jina la Baba, na la Mwana na la Roho Mtakatifu, Amina’.
Kugusa paji la uso tuna maana kukubali kwa akili, kugusa kifua maana yake ni kupokea na kuupenda msalaba moyoni na kugusa Mabega maana yake ni kuwa tayari kuubeba Msalaba kwa nguvu zetu zote.
Tunafanya njia ya Msalaba kwa nia ya kumkiri Mungu Mmoja katika Nafsi tatu. Pia Msalaba ni Ishara ya Ukombozi wetu.
Ishara ya Msalaba Juu ya Paji la uso, mdomo na kifua kabla ya injili:
Hii ina maana kwamba Niko tayari kulifahamu Neno la Mungu Kwa Akili yangu,
Nitalitangaza kishujaa kwa midomo yangu, na Nitalipenda na kulishika kwa Moyo wangu Wote.

Maana ya siku ya Jumatano ya Majivu

Utangulizi

Wakati umetimia na ufalme wa Mungu umekaribia, tubuni na kuiamini Injili, (Mk 1:15), haya ndiyo maneno ya kwanza ya Yesu ambayo kadri ya Mwinjili Marko yanafungua kazi ya hadhara ya Yesu, kwa maana hiyo kazi ya Yesu inaanza kwa kuwaandaa watu katika toba ili hatimaye, wapate kuukaribia au kuingia katika ufalme wa Mungu.
Na wakati ndiyo sasa. Wakati ni sasa, Yesu anatuhubiria na Kwaresima imewadia, na ndiyo maana siku ya Jumatano ya majivu, kwa kuitikia mwito wa maneno ya Yesu kanisa linatualika kuingia katika kipindi cha Kwaresma, ambacho ni kipindi cha kujikusanya, kujitayarisha, kijitengeneza na kujikarabati hasa kwa toba, kufunga, kusali na kujitoa sadaka zaidi mambo yanayorutubishwa kwa tafakari ya kina ya Neno la Mungu.

Nini maana ya Jumatano ya majivu?

Jumatano ya majivu ni mwanzo wa kipindi cha kwaresima katika kanisa, Ni mwanzo wa siku arobaini za kutafakari kwa undani fumbo kuu la upendo wa Mungu linalofunuliwa kwa kujitoa kwake na kufa msalabani, kifo cha aibu cha Msalaba ili kuichukua aibu yetu au dhambi zetu.

Kwaresma ni nini?

Kwaresma ni kipindi cha siku 40 cha kujiandaa kuadhimisha Sherehe kuu ya PASAKA yaani kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Tunajiandaa kwa Kufunga Kusali, Kutubu, na Matendo mema.
Mama kanisa anatupatia kipindi hiki ili tuweze kutafakari njia na mienendo yetu na kubadilika kama haimpendezi Mungu
Tunapofunga tunatakiwa kuzuia vilema vyetu na kuviacha kabisa, tunaomba kujaliwa moyo wa toba, tunainua mioyo yetu na tunaomba Mungu atujalie nguvu na tuzo. Haitoshi tu kukiri makosa yetu bali tunahimizwa kuungama na kutubu hayo makosa na kuwa tayari kuanza upya. Kipindi cha Kwaresima huanza tangu Jumatano ya majivu. Mwanzoni mwa kazi yake ya kuhubiri Habari njema Yesu anaanza kwa kusema tubuni na kuiamini Injili – Mk 1,15. Maneno haya haya tunayasikia/tumeyasikia kila tunapopakwa majivu. Mwaliko huu wa Yesu unatuingiza katika kipindi cha toba – tubuni na kuiamini Injili. Huu ni mwaliko wa uzima. Ni mwaliko ili tuongoke, tuanze maisha mapya, maisha ya sala, kufunga na kutoa sadaka.

Kwa nini ikaitwa Jumatano ya majivu?

Jina linatokana na desturi ya kumpaka mtu majivu kichwani pamoja na kumtamkia maneno ya kumhimiza afanye toba inavyotakiwa na kipindi hicho cha liturujia kinachoandaa Pasaka.
Kwa kawaida siku ya Jumatano ya majivu unaanza mfungo unaofuata kielelezo cha Yesu kufunga chakula siku arubaini jangwani baada ya kubatizwa na Yohane Mbatizaji na kabla ya kuanza utume wake mwenyewe.

Nini maana ya majivu tunayopaka?

Majivu ni ishara ya majuto, nayo hufanywa visakramenti kwa kubarikiwa na kanisa. Tunapopakwa majivu katika paji la uso hutusaidia kutafakari na kutukumbusha kuwa wanadamu sisi tu mavumbi na mavumbini tutarudi. Hutukumbusha zaidi kuwa maisha ya hapa duniani tunapita na safari yetu itakamilika pale tutakapoungana na Bwana na mwokozi wetu katika ufalme wako.
Angalia; Isaya 61:3, Ester 4:1-3, Yeremia 6:26, Ezekieli 27:30, Mathayo 11:21 na Luka 10:13.

Kwa nini majivu yanapakwa kwenye paji la uso na si vinginevyo?

Ishara yoyote iwekwayo katika paji la uso huonesha umiliki (soma Ufunuo 7:3, Ufunuo 9:4, Ufunuo 14:1, Ezekieli 9:4-6, ). Tunapochorwa ishara ya msalaba katika paji la uso ni ishara kwamba sisi tupo chini yake yeye aliyekufa msalabani kwa ajili yetu.
Hali kadhalika hutukumbusha ishara ya msalaba tuliyochorwa na mafuta matakatifu siku ya ubatizo wetu, hutukumbusha ahadi tuliyoiweka siku hiyo ya ubatizo na kutuita tuishi maisha ya utakatifu

Padri hutamka maneno gani wakati anapaka majivu?

Tunapopakwa majivu Padre husema; Mwanadamu kumbuka u mavumbi na mavumbini utarudi AU Tubuni na kuiamini Injili.

Maneno anayosema padre yana maana gani?

Maneno haya kwa upande mmoja hutukumbusha tunapoelekea, tusisikitike kwamba siku moja tutarudi mavumbini bali tuwe na furaha kwani wakati miili yetu unarudi mavumbini roho zetu zitakwenda kuungana na Mungu Baba mbinguni.
Hivyo maandalizi tunayoalikwa kuyafanaya si maandalizi ya kuelekea mavumbini bali maandalizi ya kuelekeza roho zetu mbinguni. Ndio maana pia twaambiwa tubuni na kuiamini Injili.

Majivu tunayopakwa yanatoka wapi?

Majivu tunayopakwa hutoka katika matawi yaliyotumika katika jumapili ya matawi ya mwaka jana. Majivu haya hubarikiwa na kuwa visakramenti. Hivyo majivu yanapoashiria toba na majuto pia hutukumbusha wema wa Mungu na utayari wake wa kutusamehe.

Kwa nini unatumia matawi ya Jumapili ya Matawi?

Matawi haya yalimkaribisha Yesu Yerusalemu akiwa tayari kufa kwa ajili ya dhambi zetu, yalimpokea mfalme kwa furaha na shangwe kuu. Matawi haya yanapochomwa na sisi kupakwa majivu yetu yanatukumbusha kuwa ni kwa ajili ya dhambi zetu Mungu alimtoa mwanae wa pekee kufa msalabani kwa ajili ya dhambi zetu sisi wanaadamu. Hivyo hututafakarisha kuacha dhambi.

Kanisa limekataza nini siku ya Jumatano ya majivu?

Tumekatazwa kula chakula siku ya Jumatano ya Majivu na kula nyama siku ya Ijumaa Kuu katika Amri ya Pili ya Kanisa.

Nani analazima kufunga siku ya Jumatano ya majivu na Kwaresma?

Kila Mkristo aliyetimiza miaka 14 na zaidi anapaswa kufunga kula nyama (Ijumaa kuu) na mwenye miaka zaidi ya 21 kufunga chakula Jumatano ya Majivu

Tunaposema kujinyima wakati wa Kwaresma tunamaana gani?

Kujinyima ni kujikatalia kitu ukipendacho mfano nyama, pombe, sigara, muziki, safari, maongezi n.k.

Mwisho

Wakati wa Kwaresma Waamini wanapaswa kujitakasa zaidi kwa kusali, kufunga, toba na matendo mema
Kipindi cha Kwaresima ni fursa makini ya kumkimbilia Mwenyezi Mungu, kwani kwa njia ya dhambi wamejikuta wakiwa mbali na Uso wa huruma ya Mungu, kiasi hata cha kupoteza imani na matumaini kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni changamoto ya kumpenda Mungu na jirani badala ya kukumbatia malimwengu yanayoendelea kuwatumbukiza katika utupu wa maisha ya kiroho. Kwaresima ni kipindi cha waamini kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu inayoganga na kuponya dhambi. Ni wakati wa sala, upendo na kufunga.
Shopping Cart