Sidebar with Floating Button
AckySHINE SMS💌💕
AckyShine

Novena ya Siku tisa kwa Mtakatifu Agustino wa Hippo: Sala zote na Litania

Featured Image

Anza Novena hii tarehe 19 Agosti ili kumalizia tarehe 27 Agosti na kusheherekea tarehe 28 Agosti, Sikukuu ya Mtk. Augustino wa Hippo.





SIKU YA KWANZA – kutafuta ukweli – kweli ni nini?





Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, Amina





Tafakari
Pamoja na Mtakatifu Augustino tunasema “ Umetuumba kwa ajili yako ee Bwana, kwani ni wewe peke yako ndie Mungu wetu, na nyoyo zetu hazitapumzika, hadi tupumzike ndani mwako.”





Tunapoanza Novena yetu kwa Mtakatifu Augustino tunamwomba Mungu neema ya kuwa na roho kama yake katika safari yetu katika kuzitambua nafsi zetu. Tunatafakari sisi ni nani na tunaelekea wapi kama wafuasi wa Mtakatifu Augustino katika dunia ya leo. Kama Mt Augustino alivyoutafuta ukweli bila kuchoka, nasi tutulie na kuruhusu maswali haya yaguse ufahamu wetu. Ni nini kinachonisababisha niendelee kumtafuta Mungu? Baada ya kumpata Mungu, ninamfanyaje awe hai kwa watu wale ninaoishi nao?





Kama kuna jambo moja Mt Augustino anasisitiza tena na tena kuhusu kumtafuta Mungu, ni kuwa lazima tuanze kumtafuta ndani mwetu. Huko ndiko tutakuta ukweli, mwanga na furaha katika Kristu mwenyewe. Ndani ya nafsi zetu ndiko tutasikilizwa tunaposali, katika nafsi zetu ndiko tutampenda Mungu na kumwabudu.





Litania kwa heshima ya Mtakatifu Augustino





Bwana utuhurumie Bwana utuhurumie





Kristu utuhurumie Kristu utuhurumie





Bwana utuhurumie Bwana utuhurumie





Kristu utusikie Kristu utusikilize





Baba wa mbinguni Mungu utuhurumie





Mwana Mkombozi wa dunia Mungu utuhurumie





Roho Mtakatifu Mungu utuhurumie





Utatu Mtakatifu Mungu mmoja utuhurumie





Maria Mama wa Yesu utuombee





Maria Mama wa faraja utuombee





Maria Mama wa shauri jema utuombee





Mt. Augustimo nyota angavu ya Kanisa utuombee





Mt Augustino uliyejawa bidii kwa ajili ya kuutafuta utukufu wa Mungu utuombee





Mt. Augustino mtetezi jasiri wa Ukweli utuombee





Mt Augustino ushindi wa neema ya Mungu utuombee





Mt Augustino uliyewaka mapendo kwa Mungu utuombee





Mt Augustino mkuu sana na mnyenyekevu sana utuombee





Mt Augustino mfalme wa maaskofu na wanateolojia utuombee





Mt Augustino baba wa maisha ya kitawa utuombee





Mt Augustino mtakatifu kati ya wenye hekima na mwenye hekima kati ya watakatifu utuombee





Utuombee Mtakatifu Augustino – ili tustahili maagano ya Kristu.





Tuombe: Umetuumba kwa ajili yako ee Bwana, na nyoyo zetu hazitapumzika kamwe, hadi tutakapopumzika ndani mwako. Tunakuomba utubariki katika mahangaiko yetu ya kukutafuta wewe na utusaidie tunapokutana na makwazo. Tunapokupata, tunaomba utujalie neema ya kuwa waaminifu kwako ee Mungu wa historia, tuwe waaminifu kwa Yesu Kristu Mkombozi wetu, kwa Kanisa letu na mafundisho yake, na tuwe waaminifu katika wito wetu tuliouchagua katika kukutumikia wewe. Tunaomba hayo kwako wewe Baba mwema, kwa njia ya Kristu Bwana wetu na kwa maombezi ya Mtakatifu Augustino Msimamizi wa Jumuiya yetu, Amina.





Baba yetu……, Salamu Maria….., Atukuzwe Baba……





Siku ya pili - Utulivu





Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, Amina





Tafakari





“Ingia sasa, ndani ya moyo wako (Isaya 46:8) na uwe na imani, utamkuta Kristu humo. Humo anaongea na wewe, mimi, mwalimu, napaaza tu sauti yake lakini Yeye ndiye anayekufunza wewe kwa ufanisi zaidi katika utulivu wako”





Je tunapenda maisha ya utulivu ambapo tunapata muda wa kumtafakari Mungu na mambo anayotutendea katika maisha yetu? Kwa vile Yesu anaongea nasi katika utulivu, inatupasa tujifunze namna ya kuutunza utulivu ndani ya nafsi zetu licha ya mahangaiko na misukosuko ya maisha. Tutenge muda katika siku yetu ambapo tunaweza kutulia na Kristu na kumsikiliza, na wala sio sisi kuongea nae tu bila kumsikiliza naye pia. Soma Neno la Mungu kwa utulivu na kwa tafakari, na uone kama kuna kitu gani Mungu anakuaombia leo. Lazima tusafishe macho ya nyoyo zetu, ili tuweze kumwona Mungu ndani mwetu. Tunafanya hivyo kwa njia ya toba na maungamo. Kusafishwa vizuri ni jambo linaloweza kuambatana na maumivu, lakini tunahitaji usafi wa nafsi ili tuweze kuwa wasikivu zaidi kwa sauti ya Mungu ndani mwetu.





Litania kwa heshima ya Mtakatifu Augustino





(Angalia siku ya kwanza)





Tuombe: Ee Baba mwema, tunataka kumfuata Mwanao Yesu kwa ukaribu zaidi. Utuwezeshe kuumbika upya nawe kwa mfano wa Mtakatifu Augustino katika maisha yake ya utulivu. Utusaidie kuacha mambo ya dunia hii yanayopita ili tupate hamu kubwa zaidi ya kukufuata. Imarisha imani yetu ili tusikie sauti yako katika maandiko: ili tuweze kukuona Wewe katika matukio ya maisha yetu. Tunaomba haya kwa njia ya Kristu Bwana wetu, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu mmoja milele na milele. Amina.





Baba yetu……, Salamu Maria….., Atukuzwe Baba……





Siku ya tatu – matendo-tafakari na matendo





Katika wito wetu uwao wote wa maisha yetu, tunaalikwa na Yesu tutafakari jinsi Martha alivyolalamika kuwa dada yake Maria alitumia muda wote katika kumsikiliza Yesu badala ya kusaidia kazi. Mt. Augustino akiwa kama mtawa aliuchukua mfano wa Martha na Maria kwa kushiriki kwa ukamilifu pia katika ujenzi wa uhai wa Kanisa kwa njia ya maandishi na kazi zake njema. Je mimi ninaoanishaje kati ya kutenda, kusali na tafakari takatifu?





Mt. Augustino anatufundisha kuwa tuwe tayari kuwatumikia wengine. Asiwepo mtu anayedhani kuwa anaweza kusali tu muda wote bila matendo, na wala asiwepo anayedhani atafaidika kwa matendo mengi yasiyosindikizwa na wingi wa sala. Tunapozigundua karama zetu Mungu alizotupa, tuwe tayari kuzishirikisha kwa wengine, kwani siku ya mwisho tutahukumiwa kwa namna ambavyo tuliwajali wengine. Kwa hiyo baada ya kumpata Mungu ndani mwako, usibaki humo, bali mgeukia yeye aliyekuumba. “Tupande mlimani lakini tusijenge vibanda, tushuke tuwatumikie wengine”





Litania kwa heshima ya Mtakatifu Augustino





(Angalia siku ya kwanza)





Tuombe: Mungu Baba yetu, tunakutukuza na kukushukuru kwa kulijalia Kanisa lako mtakatifu mkuu namna hii. Tunapojitahidi kuishi roho na karama zake, utujalie neema za kukua katika utumishi wetu kwa wengine kwa njia ya matendo mema na pia katika maisha yetu ya sala, kwa mfano wa Mt. Augustino. Tunaomba hayo kwa Jina la Mwanao, Bwana na Mwokozi wetu. Amina.





Baba yetu……, Salamu Maria….., Atukuzwe Baba……





Siku ya nne – umaskini wa kiinjili – maisha ya kujitoa





Kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, Amina.





Kuna wakati Mt. Augustino alikosa kitu chochote cha kuwapatia wasiojiweza, kwa sababu alikuwa anagawa kila alichoweza kwa wenye shida. Alipoishiwa kabisa, aliuza baadhi ya vitu alivyokuwa navyo ili kupata pesa iliyohitajika kwa ajili ya wenye shida.





Je, mimi pamoja na karama zote alizonijalia Mungu na vipaji vyote nilivyo navyo, ninajitahidi kuiga mfano wa Mt. Augustino katika kujitoa kwa wengine?





Umaskini wa kiinjili ni tofauti na umaskini wa kukosa mali au pesa. Ni namna moyo wa mtu anavyopenda kujitoa hata nje ya Jumuiya yake. Yesu Kristu alijitoa kabisa kwetu kwa kuuacha Umungu wake na kujitwalia ufukara wetu ili aweze kututajirisha. Hii ni changamoto kwetu kuwa tuwe tayari kujitoa kwa ajili ya wale wanaotuhitaji na Augustino ni mfano katika hilo. Tujitolee kufanya kazi za huruma, kwani mtu hataishi kwa mkate tu. Je tunawasaidiaje maskini walioko katika eneo letu? Ufalme wa Mungu utawafikiaje wengine kupitia kwetu. Mt Augustino anatupa changamoto leo kuwa tukubali kwa moyo mmoja kutoa vitu tulivyo navyo kwa ajili ya wengine, na tumfuate Kristu kwa moyo mpya na wa dhati.





Litania kwa heshima ya Mtakatifu Augustino





(Angalia siku ya kwanza)





Tuombe: Tunakutukuza ee Bwana kwa kila unatupowezesha kushirikisha vile ulivyotujalia kwa ajili ya wahitaji, na kushikama katika upendo wako. Tunakuomba utujalie neema ya kudumu katika kushirikiana na kupendana ili tuwe mashahidi wa ukarimu wako mkuu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristu, anayeishi na kutawala pamoja nawe na Roho Mtakatifu, Mungu mmoja daima na milele, Amina.





Baba yetu……, Salamu Maria….., Atukuzwe Baba……





Siku ya tano – urafiki katika jumuiya yetu





Kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, Amina.





Mt. Augustino anashuhudia kuwa kitu kilichomweka karibu na marafiki zake kaka na dada zake ni kulekuongea na kucheka pamoja, kusaidiana, kusoma vitabu vinavyofanana vyenye mambo ya kujenga, kutaniana, kutofautiana mara kwa mara bila kukasirikiana, na alama za urafiki wetu zilijionyesha katika nyuso zetu, sauti zetu, macho yetu, na namna nyingi nyingine”. Je mimi nafurahia mahusiano yaliyoko katika Jumuiya yetu? Kuna jambo gani naweza kufanya ili kuboresha mahusiano na wanajumuiya wenzangu?





Ushahidi wa mapendo ya kweli unakuja pale tunapokuwa tayari kubebeana mizigo yetu. Tunapojitahidi kuboresha mambo yanayohusu Jumuiya, ukweli ni kuwa tunaboresha mambo yetu binafsi pia. Tumwombe Mungu ili tuweze kuona namna ambavyo Jumuiya yetu inatutegema katika hali na namna mbalimbali na tuweze kuboresha mahusiano ili kukuza urafiki kati yetu kama anavyotufundisha Kristu.





Litania kwa heshima ya Mtakatifu Augustino





(Angalia siku ya kwanza)





Tuombe: Bwana Mungu wetu, ulimfunulia Mt. Augustino uzuri ulioko katika urafiki uliojengwa katika misingi yako. Utujalie sisi tunaosimamiwa naye hapa duniani, tukue katika urafiki mtakatifu wa kijumuiya. Utujalie tufikie ukamilifu wa urafiki huo katika makao yetu ya mbinguni unakoishi na kutawala daima na milele, Amina.





Baba yetu……, Salamu Maria….., Atukuzwe Baba……





Siku ya sita – augustino mfano wa unyenyekevu





Kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, Amina.





Unyenyekevu unapatikana tu katika vita vya kiroho. Umuhimu wa majaribu katika maisha yako ya kiroho ni kuwa ni kwa kupitia tu majaribu hayo unajipatia unyenyekevu. Hapo ndio unauona umuhimu wa kumpokea yesu kuwa Mwokozi wako. Ukiwa na kiburi itakuwa ni kikwazo kikubwa kumpokea Mwokozi.





Kwa Augustino, unyenyekevu sio kujidharau, bali ni kujitahidi kufahamu karama alizotujalia Mungu na kuziendeleza. Ili kuwa mtu mnyenyekevu, jifahamu kuwa u mdhambi, na kuwa Mungu ndie anayeweza kukuweka huru. Fanya maungamo ya dhambi zako ili uwe wa kundi lake Mungu. Je, kama unyenyekevu ndio ukweli, ninajitahidije kuushirikisha ukweli huu kwa wengine katika Jumuiya yetu?





Litania kwa heshima ya Mtakatifu Augustino





(Angalia siku ya kwanza)





Tuombe: Tuelekezee nyoyo zetu katika wema wako ee bwana, na geuza macho yetu mbali na kiburi na puuzi za dunia ili tuwe wafuasi wa maneno yako: Jifunzeni kwangu kwani mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo. Utujalie tukue kila siku katika unyenyekevu ambao unampendeza sana moyo wa Msimamizi wetu mt. Augustino. Amina.





Baba yetu……, Salamu Maria….., Atukuzwe Baba……





Siku ya saba – uangalizi wa imani yetu





Kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, Amina.





Na tumpende Bwana wetu, tulipende kanisa lake. Tunampokea Roho Mtakatifu kadri tunavyolipenda Kanisa lake, kama tukiunganika pamoja kwa upendo, kama tukilifurahia jina katoliki na Imani yake. Tuamini kuwa tutakuwa na Roho Mtakatifu kwa kipimo cha upendo wetu kwa Kanisa lake. Tunalipenda Kanisa kama tulisimama imara katika ushirika na upendo.





Je ninalipenda Kanisa Katoliki? Ninajitahidi kujifunza imani hii na kuwashirikisha wengine au ninafuata mkumbo tu? Tunaalikwa kuishi kwa mfano wa Mt. Augustino ambaye alijielimisha kuhusu imani ya Kanisa Katoliki na kuikumbatia, kuitetea na kuishirikisha kwa wengine. Tusisite kujitoa katika dunia yetu ya leo pale tunapohitajika katika kueneza imani yetu. Tumwombe Mungu atujalie kwa mfano wa Mt. Augustino, moyo wa kusukumwa kuwashirikisha wengine imani iliyo hai kwa njia ya maneno, na matendo yetu, na hivyo kulitetea Kanisa la Bwana wetu Yesu Kristu kila wakati kwa injili iliyo hai.





Litania kwa heshima ya Mtakatifu Augustino





(Angalia siku ya kwanza)





Tuombe: Baba mwenye upendo, tunakushukuru kwa zawadi ya Mt. Augustino uliyolipatia Kanisa lako. Kwa maombezi yake, sisi tunakuomba mwanga na ujasiri wa kujitoa bila masharti kwa unyenyekevu na daima katika huduma kwa wengine hasa wenye shida mbalimbali katika mahitaji ya mwili na ya roho. Tunaomba hayo, kwa njia ya Kristu Bwana wetu, Amina.





Baba yetu……, Salamu Maria….., Atukuzwe Baba……





Siku ya nane – utayari katika kulisaidia kanisa letu





Kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, Amina.





Jumuiya ni kiini cha Kanisa la leo, kama ilivyokuwa wakati wa mitume, wakifundishwa na mitume. Kama Jumuiya za kwanza za wakristu, tunaalikwa nasi leo tuwe na utayari katika kulisaidia Kanisa letu kwa njia mbalimbali hasa kwa kutoa zaka kwa wakati. Wakati huohuo pia tuelewe kuwa Roho Mtakatifu anatupatia vipaji na karama kuendana na mahitaji ya Kanisa lake, na hivyo tusisahau kushirikisha karama na vipaji hivyo kanisani kwetu ili kuujenga mwili wa Kristu. Kwa njia hiyohiyo, kazi zetu za kitume ziendane na mahitaji ya Kanisa letu leo hii kwani yote tunapewa na Roho wa Mungu kwa ajili ya utumishi kwa wengine. Je, shughuli zetu kama Jumuiya zinaendana na mahitaji ya Kanisa la Mungu kwa wakati huu? Ni mabadiliko gani tunaitwa kuyafanya kama Jumuiya na kama mtu mmoja mmoja ili kuboresha Kanisa kupitia Jumuiya yetu?





Litania kwa heshima ya Mtakatifu Augustino





(Angalia siku ya kwanza)





Tuombe: Baba mwema, tunakuheshimu na kukutukuza kwa kutupatia Mt. Augustino. Tukiwa tumejiweka chini ya mafundisho yake, tunaomba neema na maongozi yako ili tuweze daima kuwa na utayari wa kulisaidia Kanisa letu kwa njia ya zaka na majitoleo kadri ya mahitaji, na utujalie neema tunazokuomba kwa njia ya Yesu Kristu, Bwana na Mwokozi wetu. Amina.





Baba yetu……, Salamu Maria….., Atukuzwe Baba……





Siku ya tisa – utayari wa kuwasaidia wenzetu





Kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, Amina.





Mt. Augustine daima alikuwa tayari kuwasaidia wahitaji. Alitoa kila alichoweza vikiwemo vile vitu alivyotengewa kwa ajili ya matumizi yake yeye mwenyewe, na alipokosa kitu zaidi cha kutoa, aliyeyusha baadhi ya vyombo vya dhahabu vilivyokuwa vimewekwa wakfu kwa ajili ya kuuza na kisha aliwagawia maskini pesa iliyopatikana. Nasi mara nyingine inawezekana hatuna pesa mfukoni za kuwapa wale wanaohitaji tuwasaidie, lakini bila shaka tuna vitu. Mazao ya mashambani, mifugo, na vitu aina mbalimbali alivyotujalia Mungu. Kwa hiyo kila mmoja wetu ana kitu anachoweza kumpa mwenzake, pengine kama sina chochote zaidi angalau nina muda wa kusali na kuwaombea wengine kuendana na mahitaji ya Jumuiya yetu, au kuwatembelea wapweke, wenye majonzi na kuwafariji wengine. Cha msingi ni kumtazama Kristu, ambaye ana njaa na anateseka, ndani ya wenzetu.





Tunafanya vyema kushikamana na maskini. Sio maskini wa mali na pesa tu tunazungumzia hapa, bali pia maskini wa kiroho, wale wanaohitaji kuelekezwa, wenye mashaka, wapweke, wagonjwa, na wanaoteseka na dhambi. Tumwombe Mungu ili tuimarike kiroho, maana tutaweza kuwasaidia hao maskini tu pale ambapo sisi wenyewe tuna utajiri wa kiroho, yaani tunaye Kristu ndani mwetu.





Tunapomalizia Novena yetu ya siku tisa, tutafakari kuwa, kama Mt. Augustino angekuwa hai leo, angewajibika namna gani, angewasaidiaje maskini walioko katika Jumuiya yetu, mahali petu pa kazi na hata katika familia zetu?





Litania kwa heshima ya Mtakatifu Augustino





(Angalia siku ya kwanza)





Tuombe: Bwana, tunakuomba urejeshe upya katika Kanisa lako roho kama ile uliyompa Mt. Augustino. Kwa mfano wake, tujazwe na kiu ya kukupata wewe peke yako kama chemchem ya hekima na chanzo cha upendo wa milele ili tuwe na utayari wa kuwasaidia wenzetu wote wenye shida za aina mbalimbali. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu. Amina.





Baba yetu……, Salamu Maria….., Atukuzwe Baba……


AckySHINE Solutions

Comments

Please Join AckySHINE to Participate in Discussion.

James Kimani (Guest) on June 9, 2024

Nguvu hutoka kwa Bwana

Betty Akinyi (Guest) on May 14, 2024

🙏❤️💖 Bwana akujalie baraka

Daniel Obura (Guest) on May 11, 2024

🙏✨ Neema ya Mungu iwe nawe

Thomas Mwakalindile (Guest) on April 17, 2024

Kuna tumaini kwa ajili ya siku zijazo, maana Mungu anajua mipango aliyokupangia

Lucy Wangui (Guest) on March 30, 2024

Imani ni kuwa na uhakika wa kile tunachotarajia na kujua kwa hakika kile ambacho hatuoni

Sarah Karani (Guest) on March 9, 2024

🙏🙏🙏

Elizabeth Mrope (Guest) on January 28, 2024

Mungu akubariki!

James Kawawa (Guest) on December 12, 2023

Rehema za Mungu ni kubwa kuliko kosa lolote

Hellen Nduta (Guest) on December 5, 2023

Ahadi za Mungu ni za kweli daima

Grace Wairimu (Guest) on November 27, 2023

Wakati wa Mungu ni kamilifu

Joseph Kiwanga (Guest) on November 27, 2023

Nakuombea 🙏

Sarah Achieng (Guest) on October 5, 2023

🙏❤️💖 Tumshukuru Mungu kwa yote

Grace Mligo (Guest) on August 27, 2023

Katika rehema zake, Mungu husamehe na kurejesha

Samuel Were (Guest) on July 10, 2023

🙏💖✨ Neema yako ni ya kutosha

Lucy Wangui (Guest) on April 14, 2023

Wacha nuru yako iangaze mbele ya wengine

John Lissu (Guest) on February 25, 2023

🙏🙏🙏

Rose Kiwanga (Guest) on February 16, 2023

Mwamini Bwana kwa moyo wako wote, na usitegemee ufahamu wako mwenyewe

Grace Wairimu (Guest) on February 5, 2023

Mungu ni mwema, wakati wote!

Nancy Kabura (Guest) on December 25, 2022

Kwa Mungu, yote yanawezekana

Rose Mwinuka (Guest) on November 9, 2022

🙏✨❤️ Neema za Mungu zikufunike

Victor Mwalimu (Guest) on August 30, 2022

Anaponya mioyo iliyovunjika na kufunga majeraha yao

Rose Kiwanga (Guest) on August 28, 2022

Rehema hushinda hukumu

Ann Awino (Guest) on August 25, 2022

Sifa kwa Bwana!

Joyce Mussa (Guest) on August 7, 2022

🙏💖 Nakusihi Mungu

Ann Awino (Guest) on July 6, 2022

Hauko peke yako; Mungu yuko nawe

Charles Mchome (Guest) on July 1, 2022

🙏🌟 Mungu alete amani

Wilson Ombati (Guest) on May 19, 2022

🙏❤️✨ Asante Mungu kwa kila kitu

Samson Tibaijuka (Guest) on April 6, 2022

Katika giza, nuru yake inaangaza zaidi

Joyce Aoko (Guest) on November 23, 2021

🙏💖🙏 Mungu akufunike na upendo

Patrick Mutua (Guest) on October 1, 2021

Mungu ni kimbilio letu na nguvu zetu, siku zote tayari kusaidia wakati wa shida

Stephen Mushi (Guest) on June 3, 2021

Wacha imani yako iwe kubwa kuliko hofu yako

Victor Mwalimu (Guest) on June 3, 2021

Rehema zake hudumu milele

Susan Wangari (Guest) on May 24, 2021

🙏💖 Nakushukuru Mungu

John Mwangi (Guest) on May 9, 2021

Mungu ni mwaminifu; hatakuacha kamwe wala hatakupungukia

Lydia Mzindakaya (Guest) on March 30, 2021

Kupitia Kristo, tunapokea rehema za Mungu kwa wingi

Robert Ndunguru (Guest) on March 15, 2021

🙏✨ Mungu atupe nguvu

Elizabeth Mrema (Guest) on February 24, 2021

🙏✨💖 Mungu atajibu maombi yako

Henry Mollel (Guest) on November 25, 2020

Mungu ana kusudi hata katika maumivu yako

Ruth Kibona (Guest) on October 22, 2020

🙏🌟❤️ Nakuombea heri

David Nyerere (Guest) on September 5, 2020

Upendo wa Mungu na rehema zake havikosei kamwe

Anna Mchome (Guest) on July 6, 2020

🙏❤️ Mungu akubariki

Frank Macha (Guest) on July 6, 2020

Bwana atapigana kwa ajili yako; wewe unahitaji tu kutulia

Grace Mligo (Guest) on May 11, 2020

🙏💖 Mungu wetu asifiwe

Paul Kamau (Guest) on October 6, 2019

Dumu katika Bwana.

Anthony Kariuki (Guest) on September 15, 2019

🙏❤️ Mungu ni mwaminifu

Charles Mchome (Guest) on July 18, 2019

Hadithi yako haijaisha; Mungu bado anaandika

Kevin Maina (Guest) on May 26, 2019

Katika udhaifu wetu, rehema za Mungu zinatupa nguvu

John Kamande (Guest) on April 18, 2019

Endelea kuamini, hata ikiwa ni vigumu kuona njia

Susan Wangari (Guest) on March 22, 2019

Endelea kuwa na imani!

David Nyerere (Guest) on December 31, 2018

🙏🌟 Mungu akujalie amani

Henry Mollel (Guest) on December 17, 2018

Tumaini ni nanga ya roho

Irene Akoth (Guest) on October 29, 2018

🙏🌟 Namuomba Mungu akupiganie

Charles Mrope (Guest) on October 1, 2018

Katika imani, yote yanawezekana

Emily Chepngeno (Guest) on July 7, 2018

🙏❤️✨ Mungu akujalie furaha

Joseph Mallya (Guest) on June 9, 2018

Mwamini katika mpango wake.

Paul Ndomba (Guest) on May 11, 2018

🙏❤️🌟 Asante Mungu kwa uhai

Diana Mumbua (Guest) on April 28, 2018

Tumeokolewa kwa rehema zake, si kwa matendo yetu

Mary Njeri (Guest) on February 23, 2018

🙏💖 Asante kwa neema zako Mungu

Thomas Mwakalindile (Guest) on January 12, 2018

Katika uwepo wake, kuna ukamilifu wa furaha

Charles Mrope (Guest) on November 8, 2017

Imani inakua imara zaidi wakati wa majaribu

Related Posts

SALA KWA MAMA WA UCHUNGU KUOMBA NEEMA YA PEKEE

SALA KWA MAMA WA UCHUNGU KUOMBA NEEMA YA PEKEE

Ee Mama mbarikiwa na Bikira mwenye uchungu, Malkia wa Mashahidi, uliyesimama chini ya msalaba na ... Read More

SALA MUHIMU ZA MKRISTO ZA KILA SIKU ASUBUHI

SALA MUHIMU ZA MKRISTO ZA KILA SIKU ASUBUHI

SALA YA ASUBUHI

Tuusifu Utatu Mtakatifu wa Mungu Mwenyezi, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu,... Read More

SALA WAKATI WA KUJIBARIKI NA MAJI YA BARAKA

SALA WAKATI WA KUJIBARIKI NA MAJI YA BARAKA

Kwa njia ya Maji haya ya Baraka,

na kwa njia ya Damu yako azizi,

na kwa maombezi ya M... Read More

SALA KWA MT. YOSEFU KUOMBA KUFAHAMU WITO WAKO

SALA KWA MT. YOSEFU KUOMBA KUFAHAMU WITO WAKO

Ee uliye Mkuu, Mt. Yosefu, uliyatii kabisa maongozi ya Roho Mt. Unijalie neema ya kufahamu aina y... Read More

Majitoleo kwa Bikira Maria

Majitoleo kwa Bikira Maria

(Sala iliyotungwa na Mtk. Aloisi)
Bibi yangu mtukufu Maria, nakuwekea amana ya roho yangu na... Read More

Sala ya Usiku kabla ya kulala

Sala ya Usiku kabla ya kulala

Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.

SALA YA KUSHUKURU

Tunakus... Read More

Novena ya Noeli

Novena ya Noeli

Novena ya Noeli (maarufu kama novena ya Mt. Andrea)

Husaliwa kuanzia tar 30 Nov hadi usiku ... Read More

SALA YA MATUMAINI

SALA YA MATUMAINI

Mungu wangu,

natumaini kwako nitapewa kwa njia ya Yesu Kristu,

neema zako duniani na ... Read More

SALA YA KUMWOMBA MTAKATIFU TERESIA WA MTOTO YESU

SALA YA KUMWOMBA MTAKATIFU TERESIA WA MTOTO YESU

Ee Mtakatifu Teresia wa mtoto Yesu, ulistahili kuitwa Msimamizi wa misioni katoliki za dunia yote... Read More

SALA YA UHAI KWA MT. YOSEFU

SALA YA UHAI KWA MT. YOSEFU

(Sala hii inafaa sana kwa ajili ya kutetea uhai wa watoto wachanga wakiwa tumboni mwa mama za... Read More

Sala ya Malaika wa Bwana

Sala ya Malaika wa Bwana

Malaika wa Bwana alimpasha habari Maria, naye akapata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Salamu M... Read More

SALA YA MAJITOLEO KWA MAMA WA HUZUNI

SALA YA MAJITOLEO KWA MAMA WA HUZUNI

Mama Mtakatifu, Mama wa Mungu na Malkia wa Mashahidi, leo nakuchagua Wewe uwe mfano wangu, mkinga... Read More