Pengine umewahi kuulizwa swali hili wakati fulani.Na jibu lake ni kama ifuayavyo:
Mtu anapouliza kila kitu kimeandikwa wapi katika Biblia ni kudhihirisha kutokuijua au kuielewa vizuri Biblia Takatifu na historia yake.Mtu anapong’ang’ania “nionyeshe kitu fulani kimeandikwa wapi kwenye Biblia”ni kutaka kujiona ya kwamba yeye anaielewa sana Biblia na ameisoma yote kwa hiyo kila kitu kilichopo kwenye Biblia anakifahamu kumbe haijui Biblia bali anakariri Biblia!
Na hili suala la kushupalia swala la kuoa linadhihirisha jinsi gani tulivyo kizazi cha zinaa,ni kama tunadhani kuwa UZIMA upo katika kujamiiana!La hasha.
Paulo anasema “Kwasababu ya zinaa ni bora kuoa na kuolewa”(1Wakorintho 7:2.9) haya sio maneno ya kufurahia na kuchekelea tu maana “YANAWALENGA WALE WALIOSHINDIKANA KATIKA YALE YAPENDEZAYO”(1Wakorintho 7:1.8)sasa ni lazima tujiulize je tumeshindikana kiasi hicho?,hiyo sio sifa!
1Wakorintho 7:1.8
“Basi kwa habari ya mambo yale mliyoandika,ni heri mwanaume asimguse mwanamke,8.Lakini nawaambia wale wasiooa bado na wajane heri wakae kama mimi nilivyo”
Na Paulo Mtume anasema “Ni bora kuoa au kuolewa” lakini hakusema “Ni LAZIMA kuoa au kuolewa”
Suala la kutooa kwa mapadre kadiri ya historia lilianza tangu zamani kabisa mwanzoni mwa milenia ya pili katika mtagusi wa pili wa Laterani mwaka wa 1139 ili waweze kumtumikia Mungu kwa uhuru na bila mawaa wala pasipo vikwazo(1wakorintho 7:32-35)
1wakorintho 7:32-35
“32Lakini nataka msiwe na masumbufu.Yeye asiyeoa hujishughulisha zaidi na mambo ya Bwana ampendezeje Bwana;33.bali yeye aliyeoa hujishughulisha zaidi na mambo ya dunia hii,jinsi atakavyompendeza mkewe.34-Tena iko tofauti kati ya mke na mwanamwali.Yeye asiyeolewa hujishughulisha na mambo ya Bwana ili apate kuwa mtakatifu mwili na Roho.Lakini yeye aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya dunia hii,jinsi atakavyompendezesha mumewe.,35.Nasema hayo niwafaidie ninyi,si kwamba niwategee tanzi,bali kwaajili ya vile vipendezavyo,tena mpate kumhudumia Bwana pasipo kuvutwa na mambo mengine”
Maandiko hayo hapo juu yanajieleza wala sidhani kama yanahitaji kufafanuliwa zaidi ya yanavyojifafanua yenyewe.
Watu wengine wanafikiri kwamba kutooa ni dhambi,kama ni hivyo basi hata Yesu mwenyewe alikosa maana hata yeye mwenyewe hakuoa.
Yesu mwenyewe anafundisha kuhusu ubikira(Mathayo 19:10-12)
Mathayo 19:10-12,
“Wanafunzi wake wakamwambia,kama mambo ya mme na mke yakiwa hivyo ni afadhali kutuooa kabisa.Lakini Yeye akawaambia ‘SI WOTE WAWEZAO KULIPOKEA NENO HILO,ILA TU WALE WALIOJALIWA,maana wako MATOWASHI waliozaliwa katika hali hiyo toka matumboni mwa mama zao;tena wako matowashi waliofanywa na watu kuwa matowashi,tena wako Matowashi WALIOJIFANYA WENYEWE KUWA MATOWASHI KWAAJILI YA UFALME WA MBINGUNI’,awezaye kulipokea neno hili na alipokee”
Yesu mwenyewe analifafanua jambo hili kwa mapana,katika orodha ya matowashi Yesu aliowataja,Mapadre ni Matowashi waliojifanya hivyo kwaajili ya huduma ya kanisa na ufalme wa Mungu.
Tena Yesu anatuambia waziwazi kwamba”sio wote wawezao kulipokea neno hilo”yaani sasa sio wote wawezao kuwa Matowashi(Mapadre)bali ni wale tu waliojaliwa na Mungu neema hiyo.wale wasioweza kuishi upadre huoa na kuwa na familia.Tena Yesu anamalizia kwa kusema “Awezaye kulipokea fundisho hili na alipokee”,kwa maana nyingine ni kusema “Fundisho au Utowashi huu sio wa lazima”anayeweza kuishi maisha hayo basi na ayapokee na yule asiyeweza basi aache!
Vilevile Mitume ili kumfuata Yesu kikamilifu waliyaacha yote waliokuwa nayo ikiwepo familia zao ili wamtumikie Bwana(Mathayo 19:27.29)
Mathayo 19:27.29:
“Ndipo Petro akajibu akamwambia ‘Tazama sisi tumeacha vyote tukakufuata wewe,tutapata nini basi?29.Amini nawaambia,kila mtu aliyeacha nyumba au ndugu wa kiume au wakike,au baba au mama au watoto au mashamba KWAAJILI YA JINA LANGU,atapokea mara mia zaidi na kuurithi uzima wa milele”
katika injili hiyo,Yesu anadhihirisha kwamba aliyeacha hayo yaliotajwa si kwasababu hawezi kuyapata la hasha,bali ameyaacha hayo yote KWAAJILI YA JINA LA YESU atapokea mengi hapa duniani halafu tena ataurithi ufalme wa mbinguni.
Mapadre wameyaacha hayo yote,wameacha nyumba,familia zao na kila kitu SIO KWASABABU HAWANA UWEZO AU HAWAWEZI KUPATA MAMBO HAYO bali WAMEACHA KWASABABU YA KUMTUMIKIA MUNGU KWA KADIRI YA MAANDIKO MATAKATIFU na kwakutaka kwao kuyaishi kimamilifu MASHAURI YA INJILI ikiwepo USEJA.
Maneno ya Paulo na yale ya Yesu mwenyewe kuhusu kumtumikia Mungu bila kuoa sio ya bahati mbaya bali ndiyo njia bora na inayofaa sana na kukubalika mbele ya Mungu.
Kwahiyo unapowaona mapadre hawaoi ujue sababu yake ni hiyo kwamba “Wamejitoa kwaajili ya kulihudumia kanisa”
(Na pia huwa nawashangaa mno watu wanaowapiga vita Mapadre kwamba kwanini hawaoi,najiuliza je,hao Mapadre wamewakataza wao kwamba wasioe?.)..na kama jibu ni hapana,sasa Je,”Pilipili ya shamba usiyoila inakuwashia nini?”
TUMSIFU YESU KRISTO!
Read and Write Comments