Masomo ya Misa ya Kanisa Katoliki

MASOMO YA MISA, MACHI 19, 2022: JUMAMOSI, JUMA LA 3 LA KWARESIMA

SHEREHE YA MT. YOSEFU, MUME WA BIKIRA MARIA

SOMO 1

2Sam. 7: 4 – 5, 12 – 14, 16

Ikawa usiku uo huo, neno la Bwana likamfikia Nathani kusema, Enenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, Bwana asema hivi, siku zako zitakapo timia, ukalala na Baba zako, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayetoka viunoni mwako, nami nitaufanya imara ufalme wake.

Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu, nacho kiti cha enzi cha ufalme wake nitakifanya imara milele. Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu, akitenda maovu nitamwadhibu kwa fimbo yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 89:1 – 4, 26, 28 (K) 36(K)

Wazao wake watadumu milele.

Fadhili za Bwana nitaziimba milele;Kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako.

Maana nimesema, Fadhili zitajengwa milele;Katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako. (K)

Nimefanya agano na mteule wangu,Nimemwapia Daudi, mtumishi wangu.Wazao wako nitawafanya imara milele,Nitakijenga kiti chako cha enzi hata milele. (K)

Yeye ataniita, Wewe baba yangu,Mungu wangu na mwamba wa wokovu wangu.

Hata milele nitamwekea fadhili zangu,Na agano langu litafanyika amini kwake. (K)

SOMO 2

Rum. 4:13, 16 – 18, 22

Ahadi ile ya kwamba atakuwa mrithi wa ulimwengu alipewa Ibrahimu na uzao wake, si kwa sheria bali kwa haki aliyohesabiwa kwa Imani. Kwa hiyo ilitoka katika Imani, iwe njia ya neema, ili kwamba ile ahadi iwe imara kwa wazao wote; si kwa wale wa torati tu, ila kwa wale wa Imani ya Ibrahimu; aliye baba yetu sisi sote; (kama ilivyoandikwa, Nimekuweka kuwa baba wa mataifa mengi); mbele zake yeye aliyemwamini, yaani Mungu, mwenye kuwahuisha wafu, ayatajaye yale yasiyokuwako kana kwamba yamekuwako.Naye aliamini kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa, ilia pate kuwa baba wa mataifa mengi, kama ilivyonenwa, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako. Kwa hiyo ilihesabiwa kwake kuwa ni haki.Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

SHANGILIO

Zab. 84:5

Heri wakaao nyumbani mwako, Ee Bwana.

INJILI

Mt. 1:16, 18 – 21, 24

Yakobo alimzaa Yusufu mumewe Mariamu aliyemzaa yesu aitwaye Kristo.Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akimchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.Naye Yusufu alipoamka katika usingizi, alifanya kama malaika wa Bwana alivyomwagiza; akamchukua mkewe.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, MACHI 18, 2022: IJUMAA, JUMA LA 2 LA KWARESIMA

SOMO 1

Mwa. 37:3-4, 12-13, 17-28

 

Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, na hawakuweza kusema naye kwa amani.

Ndugu zake wakaenda kuchunga kondoo za baba yao huko Shekemu. Israeli akamwambia Yusufu, Je! Ndugu zako hawachungi kondoo katika Shekemu? Njoo, nikutume kwao.

Basi Yusufu akawafuata ndugu zake akawakuta huko Dothani. Wakamwona toka mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya shuri juu yake ili wamwue. Wakasemezana wao kwa wao, Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja. Haya, twende, tukamwue na kumtupa katika birika mojawapo, nasi tutasema, Mnyama mkali amemla; kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake. Reubeni akasikia akamwokoa katika mikono yao, akasema, Tusimwue. Reubeni akawaambia, Msimwage damu; mtupeni katika birika iliyopo nyikani, wala msimguse; ili apate kumwokoa katika mikono yao, akamrudishe kwa baba yake. Ikawa Yusufu alipofika kwa ndugu zake, wakamvua Yusufu kanzu yake, kanzu ile ndefu aliyoivaa, wakamtwaa wakamtupa katika birika; na hiyo birika ilikuwa tupu, hamna maji. Nao wakakaa kitako kula chakula.

Wakainua macho yao, wakaona, msafara wa Waishmaeli wanakuja wakitoka Gileadi na ngamia zao, wakichukua ubani na zeri na manemane, wakisafiri kuvichukua mpaka Misri. Yuda akawaambia ndugu zake, Kwafaa nini kumwua ndugu yetu, na kuificha damu yake? haya, na tumwuze kwa hawa Waishmaeli, wala mikono yenu isimdhuru, maana yeye ni ndugu yetu, na damu yetu. Ndugu zake wakakubali.

Wakapita wafanyabiashara Wamidiani; basi wakamtoa Yusufu, wakampandisha kumtoa katika birika wakamwuza Yusufu kwa Waishmaeli kwa vipande vya fedha ishirini; nao wakamchukua Yusufu mpaka Misri.

 

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

 

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 105:16-21 (K) 5

 

(K) Zikumbukeni ajabu zake Bwana alizozifanya.

 

Akaiita njaa iijilie nchi,

Akakiharibu chakula chote walichokitegemea.

Alimpeleka mtu mbele yao,

Yusufu utumwani. (K)

 

Walimwumiza miguu yake kwa pingu,

Akatiwa katika minyororo ya chuma.

Hata wakati wa kuwadia neno lake,

Ahadi ya Bwana ilimjaribu. (K)

 

Mfalme alituma watu akamfungua,

Mkuu wa watu akamwachia.

Akamweka kuwa bwana wa nyumba yake,

Na mwenye amri juu ya mali zake zote. (K)

 

SHANGILIO

Yn. 3:16

 

Jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee; Kila mtu amwaminiye huwa na uzima wa milele.

 

INJILI

Mt. 21:33-43; 45-46

 

Yesu aliwaambia wakuu wa makuhani na wazee wa watu, Sikilizeni mfano mwingine. Kulikuwa na mtu mwenye nyumba, naye alipanda shamba la mizabibu, akalizungusha ugo, akachimba shimo la shinikizo ndani yake, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. Wakati wa matunda ulipokuwa karibu, akawatuma watumwa wake kwa wale wakulima, wapokee matunda yake. Wale wakulima wakawakamata watumwa wake, huyu wakampiga, na huyu wakamwua, na huyu wakampiga kwa mawe. Akawatuma tena watumwa wengine wengi kuliko wa kwanza, wakawatenda vile vile.

Mwishowe akamtuma mwanawe kwao, akisema, Watamstahi mwanangu. Lakini wale wakulima walipomwona yule mwana, wakasemezana wao kwa wao, Huyu ni mrithi; haya na tumwue, tuutwae urithi wake. Wakamkamata, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua. Basi atakapokuja yule bwana wa shamba la mizabibu, atawatendaje wale wakulima? Wakamwambia, Ataangamiza vibaya wale wabaya; na shamba la mizabibu atawapangisha wakulima wengine, watakaomlipa matunda kwa wakati wake.

Yesu akawaambia, Hamkupata kusoma katika maandiko, Jiwe walilolikataa waashi, hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni; neno hili limetoka kwa Bwana, nalo ni ajabu machoni petu? Kwa sababu hiyo nawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa, linguine lenye kuzaa matunda yake.

Wakuu wa makuhani na Mafarisayo, waliposikia mifano yake, walitambua ya kuwa anawanenea wao. Nao walipotafuta kumkamata waliogopa makutano, kwa maana wao walimwona kuwa nabii.

 

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

 

MASOMO YA MISA, MACHI 17, 2022: ALHAMISI, JUMA LA 2 LA KWARESIMA

SOMO 1

Yer. 17:5-10

Bwana asema hivi: Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake, na moyoni mwake amemwacha Bwana. Maana atakuwa kama fukara nyikani, hataona yatakapotokea mema; bali atakaa jangwani palipo na ukame, katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu.

Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, ambaye Bwana ni tumaini lake. Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, uenezao mizizi yake karibu na mto; hautaona hofu wakati wa hari ujapo, bali jani lake litakuwa bichi; wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, wala hautaacha kuzaa matunda.

Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua? Mimi, Bwana, nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya matendo yake.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 1:1-4, 6 (K) 40:4

(K) Heri aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake.

Heri mtu yule asiyekwenda

Katika shauri la wasio haki;

Wala hakusimama katika njia ya wakosaji;

Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.

Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo,

Na sheria yake huitafakari mchana na usiku. (K)

Naye atakuwa kama mti uliopandwa

Kandokando ya vijito vya maji,

Uzaao matunda yake kwa majira yake,

Wala jani lake halinyauki;

Na kila alitendalo litafanikiwa. (K)

Sivyo walivyo wasio haki;

Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.

Kw akuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki,

Bali njia ya wasio haki itapotea. (K)

SHANGILIO

Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako.

INJILI

Lk. 16:19-31

Yesu aliwaambia Mafarisayo: Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, na kula sikuzote kwa anasa. Na maskini mmoja, jina lake Lazaro, huwekwa mlangoni pake, ana vidonda vingi, naye alikuwa akitamani kushibishwa kwa makombo yaliyoanguka katika meza ya yule tajiri; hata mbwa wakaja wakamramba vidonda vyake. Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa.

Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake. Akalia, akasema, Ee baba Ibrahimu, nihurumie, umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake majini, auburudishe ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto huu. Ibrahimu akasema, Mwanangu, kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe unaumizwa. Na zaidi ya hayo, kati yetu sisi na ninyi kumewekwa shimo kubwa, ili wale watakao kutoka huku kwenda kwenu wasiweze; wala watu wa kwenu wasivuke kuja kwetu.

Akasema, Basi, baba, nakuomba, umtume nyumbani kwa baba yangu, kwa kuwaninao ndugu watano, ili awashuhudie, wasije wao piawakafika mahali hapa pa mateso. Ibrahimu akasema, Wanao Musa na manabii; na wawasikilize wao. Akasema, La, baba Ibrahimu, lakini kama akiwaendea atokaye kwa wafu, watatubu. Akamwambia wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishwa hata mtu akifufuka katika wafu.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, MARCHI 16, 2022: JUMATANO, JUMA LA 2 LA KWARESIMA

SOMO 1

Yer. 18-18-20

Waliposema, Njoni na tufanye mashauri juu ya Yeremia; maana sheria haitampotea kuhani, wala shauri halitampotea mwenye hekima, wala neno halitampotea nabii. Njoni, na tumpige kwa ndimi zetu, wala tusiyaangalie maneno yake yoyote.

Niangalie, Ee Bwana, ukasikilize sauti ya wanaoshindana nami. Je! Mabaya yalipwe badala ya mema? Maana wameichimbia nafsi yangu shimo. Kumbuka jinsi nilivyosimama mbele zako, ili nisema mema kwa ajili yao, nikaigeuze ghadhabu yako isiwapate.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 31:4-5, 13-15 (K) 16

(K) Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako, Ee Bwana.

Utanitoa katika wavu walionitegea kwa siri,

Maana Wewe ndiwe ngome yangu.

Mikononi mwako naiweka roho yangu;

Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli. (K)

Maana nimesikia masingizio ya wengi;

Hofu ziko pande zote.

Waliposhauriana juu yangu,

Walifanya hila wauondoe uhai wangu. (K)

Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana,

Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu.

Nyakati zangu zimo mikononi mwako;

Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia. (K)

SHANGILIO

Lk. 8:15

Heri wale walishikao neno la Mungu katika moyo wao mwema na unyofu, na wazaao matunda katika uvumilivu.

INJILI

Mt. 20:17-28

Yesu alipokuwa akipanda kwenda Yerusalemu aliwachukua wale wanafunzi kumi na wawili faraghani; na njiani akawaambia, Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu; na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa wakuu wa makuhani na waandishi nao watamhukumu afe; kisha watampeleka kwa Mataifa wapate kumdhihaki, na kumpiga mijeledi na kumsulibisha; na siku ya tatu atafufuka.

Ndipo mama yao wana wa Zebedayo akamwendea pamoja na wanawe, akamsujudia, na kumwomba neno. Akamwambia, Wataka nini? Akamwambia, agiza kwamba hawa wanangu wawili waketi mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika ufalme wako. Yesu akajibu akasema, Hamjui mnaloliomba. Je! Mwaweza kunywea kikombe nitakachonywea mimi? Wakamwambia, Twaweza. Akawaambia, Hakika mtakinywa kikombe change; lakini kuketi mkono wangu wa kuume na mkono wangu wa kushoto, sina amri kuwapa, bali watapewa waliowekewa tayari na Baba yangu.

Na wale kumi waliposikia, waliwakasirikia wale ndugu wawili. Lakini Yesu akawaita, akasema, Mwajua ya kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu yeyote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu; na mtu yeyote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumikia na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, JULAI 26, 2021 JUMATATU, JUMA LA 17 LA MWAKA

SOMO 1

Kut. 32:15-24, 30-34

Musa aligeuka akashuka katika mlima, na zile mbao mbili za mawe mikononi mwake; mbao ziliandikwa pande zote mbili, upande huu na upande huu ziliandikwa. Na zile mbao zilikuwa kazi ya Mungu, nayo maandiko yalikuwa maandiko ya Mungu, yaliyochorwa katika zile mbao.

Na Yoshua aliposikia kelele za watu walipokuwa wakipiga kelele, akamwambia Musa, Kuna kelele ya vita maragoni. Akasema, Hiyo si sauti ya watu wapigao kelele kwa sababu ya kushinda vitani, wala si sauti ya watu wapigao kelele kwa sababu ya kushindwa; bali kelele za watu waimbao nizo ninazozisikia mimi.

Hata alipyakaribia marago akaiona ile ndama, na ile michezo. Hasira ya Musa ikawaka, akazitupa zile mbao mikononi mwake, akazivunja chini ya mlima. Akaitwaa ile ndama walioifanya, akaichoma moto, akaisaga hata ikawa mavumbi, akainyunyiza juu ya maji, akawanywesha wana wa Israeli. Musa akamwambia Haruni; Watu hawa wamekufanyani hata ukaleta dhambi hii kuu juu yao? Haruni akasema, Hasira ya bwana wangu isiwake; wewe unawajua watu hawa, ya kuwa wamejielekeza kwa mabaya. Maana waliniambia, Katufanyie miungu itakayokwenda mbele yetu, kwa maana mtu huyo Musa, aliyetutoa katika nchi ya Misri, hatujui yaliyompata. Nikawaambia, Mtu yeyote aliye na dhahabu na aivunje; basi wakanipa, nami nikaitupa ndani ya moto, akatoka ndama huyu.

Basi asubuhi yake Musa akawaambia watu, Mmetenda dhambi kuu; na sasa nitakwenda juu kwa Bwana, labda nitafanya upatanisho kwa ajili ya dhambi yenu. Musa akarejea kwa Bwana akasema, Aa! Watu hawa wametenda dhambi kuu, wamejifanyia miungu ya dhahabu. Walakini sasa ikiwa utawasamehe dhambi yao – na kama sivyo, unifute, nakusihi, katika kitabu chako ulichokiandika. Bwana akamwambia Musa, Mtu yoyote aliyenitenda dhambi, ndiye nitakayemfuta katika kitabu changu. Basi sasa uende ukawaongoze watu hawa mpaka mahali pale ambapo nimekuambia habari zake; tazama, malaika wangu atakutangulia; pamoja na hayo siku nitakayowajilia nitawapatiliza kwa ajili ya dhambi yao.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 106:19-23 (K) 1

(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema.

Walifanya ndama huko Horebu,

Wakaisujudia sanamu ya kuyeyuka.

Wakaubadili utukufu wao,

Kuwa mfano wa ng’ombe mla majani. (K)

Wakamsahau Mungu, mwokozi wao,

Aliyetenda makuu katika Misri.

Matendo ya ajabu katika nchi ya Hamu,

Mambo ya kutisha penye bahari ya Shamu. (K)

Akasema ya kuwa atawaangamiza,

Kama Musa, mteule wake, asingalisimama,

Mbele zake kama mahali palipobomoka,

Ili aigeuze hasira yake asije akawaharibu. (K)

SHANGILIO

Efe. 1:17, 18

Aleluya, aleluya,

Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristu, awape roho ya hekima mjue tumaini la mwito wake.

Aleluya.

INJILI

Mt. 13:31 – 35

Yesu aliwatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na punje ya haradali, aliyoitwaa mtu akaipanda katika shamba lake; nayo ni ndogo kuliko mbegu zote; lakini ikiisha kumea, huwa kubwa kuliko mboga zote, ikawa mti, hata nyuni wa angani huja na kukaa katika matawi yake.

Akawaambia mfano mwingine; Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu aliyoitwaa mwanamke, akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachachwa wote pia.

Hayo yote Yesu aliwaambia makutano kwa mifano; wala pasipo mfano hakuwaambia neno; ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema, Nitafumbua kinywa changu kwa mifano, Nitayatamka yaliyositirika tangu awali.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

Shopping Cart