Dondoo za Mapishi na Lishe

Mapishi ya Pilau Ya Nyama Ng’ombe Karoti Na Zabibu

Vipimo – Nyama

Nyama ng’ombe ya mifupa ilokatwa vipande – 1 kilo

Tangawizi na thomu (somu/garlic) ilosagwa – 2 vijiko vya supu

Bizari mchanganyiko/garama masala – 1 kijiko cha chai

Chumvi – Kiasi

Vipimo – Wali

Mchele – 4 glass

Mbatata/viazi menya katakata – 3 kubwa

Vitunguu katakata – 5

Kitunguu thomu kilosagwa (garlic/somu) – 1 kijiko cha supu

Hiliki ya unga – 1 kijiko cha chai

Bizari nzima ya pilau/cumin – 1 mti

Samli au mafuta – 2 Vijiko vya supu

Karoti zilokatwakatwa nyembamba – 6-7

Zabibu – Kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Katika sufuria weka mafuta kijiko kimoja cha supu tia nyama na viungo vyake.
kaushe katika moto hadi ikaribie kukauka kisha tia maji kiasi cha kuivisha na kubakisha supu ya mchele.
Katika sufuria ya kupikia weka samli au mafuta ishike moto.
Tia mbatata/viazi kaanga, tia vitunguu kaanga kidogo.
Tia kitunguu thomu, hiliki, bizari ya pilau endelea kukaanga hadi viwe rangi ya brown kidogo.
Tia mchele kaanga kidogo, kisha mimina nyama na supu yake. Funika wali uwive.
Weka kikaangio katika moto, tia samli kijiko kimoja kisha tia karoti na zabibu, kaanga kwa sekunde chache tu kwa ajili ya kulainisha karoti na zabibu.
Utakapopakuwa wali, pambia juu karoti na zabibu.

Mapishi ya Muhogo Na Mbatata Za Nazi Kwa Nyama Ngombe

Vipimo – Mahitaji Ya Nyama

Nyama ya n’gombe ya mifupa – 3 lb

Tangawizi mbichi ilosagwa – 1 kijiko cha supu

Kitunguu thomu – 1 kijiko cha supu

Bizari ya pilau/jira/uzile (cumin) – 1 kijiko cha supu

Ndimu – 1

Kitunguu kilokatwakatwa (chopped) – 1 cha wastan

Pilipili mbichi – 3 Zilizosagwa

Chumvi – Kiasi

Vipimo – Muhogo Na Mbatata/Viazi

Muhogo menya na ukate vipande pande – 2

Mbatata/Viazi menya ukate vipande vikubwa kiasi – 5 kiasi

Tui la nazi zito – 1 gilasi

Nyanya ilokatwakatwa au kusagwa – 1

Kitunguu kilokatwakatwa (chopped) – 1 kiasi

Bizari ya mchuzi – kiasi

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha nyama kisha weka katika pressure cooker au sufuria.
Tia viungo vyote vya nyama uchanganye vizuri, kisha ikorogekoroge mpaka maji yake yakaribie kukauka. Usifunike.
Tia maji kiasi ya kuivisha nyama na kubakisha supu yake kiasi ya kuivisha muhogo na mbatata. Muda wa kuivisha nyama inategemea nyama yenyewe na kama unatumia pressure cooker ni takriban dakika 35-40. Ikiwa sufuria ya kawaida utakuwa unaikoroga.
Mimina ndani ya supu, muhogo, mbatata, nyanya, kitunguu, bizari ya mchuzi, chumvi.
Acha ichemke uive muhogo na viazi.
Tia tui la nazi, changanya vizuri acha kwenye moto dakika chache tu.
Epua ikiwa tayari. Tolea na achari.

Mapishi ya Ugali Kwa Mchuzi Wa Kamba Wa Nazi, Kisamvu Na Kachumbari Ya Papa Mkavu

Vipimo – Ugali

Maji – 4 vikombe kiasi inategemea na unga wenyewe.

Unga wa sembe – 2 vikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Tia maji kiasi katika sufuria, weka motoni, yakipata moto korogea unga wa sembe kiasi na ufanye uji mzito uache uchemke vizuri huku ukikoroga.
Chota kibakuli kimoja cha uji huo weka pembeni kisha mimina unga wote uliobaki upigepige uchanganyike vizuri kwenye uji huo mpaka ushikamane
Punguza moto anza kuusonga taratibu huku ukiongeza ule uji ulioweka pembeni kidogo kidogo mpaka uone sasa umeshikamana vizuri.
Endelea kusonga mpaka ulainike kisha mimina kwenye bakuli au sahani iliyolowanishwa na maji kisha upete pete huku ukiugeuza geuza mpaka ukae shepu nzuri ya duara.Weka tayari kwa kuliwa.

Vipimo – Mchuzi wa kamba wa nazi

Kitunguu – 1

Nyanya – 2

Kamba waliomenywa – 1 Kilo

Pilipili mbichi iliyosagwa – ½ kijiko cha chai

Kitunguu saumu na tangawizi ilivyosagwa – 1 kijiko cha supu

Nazi nzito iliyochujwa – 1 kikombe

Bizari ya mchuzi – ½ kijiko cha chai

Chumvi – Kiasi

Ndimu – Nusu

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Safisha na osha kamba vizuri kisha mtie katika sufuria. Katia kitunguu, nyanya, tia chumvi, pilipili mbichi ya kusaga, thomu na tangawizi, bizari ya mchuzi na ndimu. Tia maji kidogo kiasi acha ichemke.
Watakapoiva na karibu kukauka, mimina tui la nazi taratibu koroga kiasi
Punguza moto aacha ichemke kidogo ukiwa mchuzi tayari.

Vipimo – Kisamvu

Kisamvu – 2 vikombe

Kunde mbichi zilizochemshwa – 1 kikombe

Kitunguu – 1

Nazi nzito iliyochujwa – 1 vikombe

Chumvi – Kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Weka kisamvu katika sufuria, katia kitunguu, tia chumvi, maji kidogo acha kichemke.
Huku ikichemka mimina kunde mbichi zilizochemshwa acha zipikikie kidogo mpaka kisamvu kikaribie kukauka na kunde kuiva.
Mimina nazi nzito punguza moto acha ichemke kidogo, mimina kwenye bakuli tayari kwa kuliwa.

Vipimo – Kachumbari Ya Papa

Papa mkavu (au nguru) – kipande

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Muoshe papa vizuri atoke mchanga kisha mchome kwenye jiko la mkaa au unaweza kumtia kwenye treya kisha kwenye oven kwa moto wa 350 kwa dakika 15 mpaka 20.
Akikauka mchambue chambue weka kando.
Tengeneza kachumbari, kwa kukata kitunguu, nyanya na pilipili mbichi, tia ndimu na chumvi.
Changanya na papa mkavu uliyemchambu ikiwa tayari.

Mapishi ya Wali Wa Nazi Kwa Mchuzi Wa Samaki Na Rojo La Bilingani Na Viazi/Mbatata

Wali Wa Nazi

Mpunga – 4 vikombe

Tui la nazi – 6 vikombe

Chumvi – Kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha mchele kisha
Bandika tui jikoni likichemka tia mchele na chumvi.
Funika uchemke, tui likikauka wacha moto mdogomdogo hadi wali uive ukiwa tayari. Ikiwa unatumia mkaa unapalia juu yake.

Mchuzi Wa Samaki Nguru

Samaki – 4

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi – 2 viijiko vya supu

Kitunguu maji kilokatwakawa – 2 slice ndogo

Nyanya/tungule – 4

Nyanya kopo – 3 vijiko vya supu

Pilipili mbichi – 2

Kotmiri ilokatwakatwa – 3 msongo (bunches)

Bizari ya mchuzi (simba 2) – I kijiko cha chai

Ndimu – 1 kamua

Mafuta – ¼ kikombe

Chumvi kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Katakata samaki mkaange kwa kumtia viungo.
Weka mafuta katika sufuria, kaanga kitunguu. Vinapogeuka rangi thomu na tangawizi mbichi, nyanya, nyanya kopo, kitunguu na bizari ya mchuzi endelea kukaanga.
Tia maji kiasi na ndimu, pilipili mbichi ilosagwa kisha tia kotmiri.
Mwisho tia nusu ya samaki alokaangwa ukiwa tayari

Bilingani Za Kukaanga Na Viazi

Bilingani – 4 madogodogo

Viazi/mbatata – 3

Nyanya – 3

Majani ya mchuzi/mvuje/curry leaves – kiasi 6-7

Nnyanya kopo – 2 vijiko vya supu

Methi/uwatu ulosagwa – 1 kijiko cha chia

Rai/mustard seeds – 1 kijiko cha supu

Bizari ya manjano/haldi/turmeric – 1 kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Mafuta ya kukaangia – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

1. Weka mafuta ya kukaangia katika karai

2. Katakakata bilingani vipande vipande vya mraba (cubes) kaanga katika mafuta ya moto hadi yageuke rangi. Eupa weka kando.

3. Katakataka viazi/mbatata vipande vidogodogo vya mraba (cubes) Kaanga hadi viive epua weka kando.

4. Ondosha mafuta yote katika karai bakisha kidogo tu kiasi ya vijiko 2 vya supu.

5. Kaanga rai kisha majani ya mchuzi, na methi/uwatu kisha kaanga nyanya.

6. Tia nyanya ya kopo kisha changanya pamoja bilingani na viazi ikiwa tayari.

Jinsi ya kutengeneza Pilau Ya Kuku

Mahitaji

Mchele wa basmati – 3 vikombe

Kuku – ½

Viazi – 4

Vitunguu – 2

Kitunguu saumu(thomu/galic) iliyosagwa – 2 vijiko vya supu

Binzari ya pilau nzima – 1 Kijiko cha chakula

Binzari ya pilau – ½ kijiko cha chai

Pilipili manga nzima – ½ kijiko cha chai

Karafuu nzima – 8

Iliki nzima – 6

Mdalasini nzima – 5 vijiti

Pilipili mbichi iliyosagwa – 2

Chumvi – kiasi

Mafuta ya kupikia – ¼ kikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika:

Osha mchele na roweka kwa muda kutegemea na aina ya mchele.
Kata kuku vipande upendavyo, safisha kisha mchemshe kwa chumvi, pilipili iliyosagwa, thomu na tangawizi.
Akiwiva kuku, mtoe weka kando, bakisha supu katika sufuria.
Katika sufuria, kaanga vitunguu hadi vigeuke rangu ya hudhurungi.
Tia thomu na tangawizi na binzari zote kaanga kidogo
Kisha tia viazi kanga kidogo kisha tia kisha tia vipande vyako vya kuku na supu acha ichemke kidogo kisha tia maji ukisie kutokana na mchele unaotumia.
Mwisho tia mchele koroga uchanganye na vitu vyote acha ichemke kiasi kisha funika na punguza moto mpaka uive (huku ukiugeuzageuza)
Ukishakuwa tayari pakua kwenye sahani tayari kwa kula na salad na pilipili.

Shopping Cart