Dondoo za Mapishi na Lishe

Jinsi ya kupika Pilau Ya Nyama Ya Ng’ombe Na Nyanya

Viambaupishi

Mchele (Basmati) 3 vikombe

Nyama ya ngo’mbe 1 kg

Pilipili boga 1 kubwa

Nyanya 2 kubwa

Vitunguu maji 2 vikubwa

Kitunguu saumu(thomu/galic) iliyosagwa 1 kijiko cha supu

Tangawizi 1 kijiko cha chai

Ndimu 1

Mafuta ya kupikia ½ kikombe

Mdalasini ½ kijiko cha chai

Binzari nyembamba 1 kijiko cha chai

Pilipili manga ½ Kijiko cha chai

Hiliki ½ Kijiko cha chai

Jinsi ya kuandaa na kupika

Loweka mchele wako katika chombo

Chukuwa nyama na ioshe vizuri na itie thomu, tangawizi, ndimu, pilipili manga na chumvi kiasi

Iweke jikoni hadi ikauke maji na kuwa imewiva huku ukiikaanga kaanga kwa hayo hayo mafuta yake hadi kuwa rangi ya hudhurungi

katakata Vitunguu na nyanya weka pembeni

Chukua pilipili boga, thomu, tangawizi na visage katika mashine ya kusagia

Weka sufuria pembeni na utie mafuta, subiri yapate moto

Kisha tia vitunguu na vikaange hadi kuwa hudhurungi na tia nyanya

Kisha mimina mchanganyiko wako ulio usaga wa pilipili boga, thomu na tangawizi

Koroga kwa dakika kadhaa Kisha mininia nyama uliyokuwa tayari, maji kiasi na chumvi wastani na subiri maji hayo yachemke

Weka mchele humo na koroga kiasi na onja chumvi kama ipo sawa au kama ndogo unaweza kuongeza

Funika na punguza moto na uache uive taratibu

Baada ya kukauka maji kabisa basi ugeuze na subiri tena kwa dakika kama mbili na tayari kuliwa.

Jinsi ya kutengeneza Wali Wa Dengu Kwa Samaki Wa Kukaanga

Mahitaji

Mchele wa basmati – 3 Vikombe

Dengu – 2 vikombe

Viazi – 3 vikubwa

Kitunguu – 2 kubwa

Nyanya – 2

Pilipili mbichi kubwa – 3

Pilipilimanga – ½ kijiko cha chai

Garama Masala (bizari mchanganyiko) -1 kijiko cha chai

Supu ya vidonge (stock cubes) – 2 vidonge

Chumvi – kiasi

Mafuta – ¼ kikombe

Zaafarani – 1 kijiko cha chai

Samaki wa kukaanga

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Dengu kama sio za tayari kwenye kopo, roweka na zichemshe hadi ziwive

Maandalizi ya Masala Ya Dengu:

Zaafarani – iroweke katika maji ya dafu dafu (warm) ya chini ya robo kikombe weka kando.
Osha mchele, roweka.
Menya viazi na vitunguu, katakata vitunguu, na nyanya , weka kando.
Katakata viazi vipande vidogo vidogo kwa umbo la mchemraba (cubes).
Katika sufuria tia mafuta yakipata moto, tia viazi ukaange kidogo kwa moto mdogo mdogo hadi kukaribia kuwiva, toa weka kando.
Kaanga vitunguu hadi vigeuka rangi ya hudhurungi isiyokoza (light brown) kisha tia nyanya ukaange kidogo.
Tia vidonge vya supu (stock cubes) uvivuruge katika mchanganyiko, katakata pilipili mbichi kwa urefu tia, uendelee kukakaanga. Tia bizari, chumvi.
Zima moto, changanya dengu na viazi katika mchanganyiko huo.

Mapishi ya Wali:

Chemsha mchele kama kawaida ya kupika wali mweupe, kiini kiwe kimewiva nusu yake.
Chuja maji kisha changanya katika mchanganyiko wa dengu.
Nyunyizia zaafarani, uchanganye wali na mchanganyiko kidogo tu.
Funika acha uive katika mtoto mdogo mdogo au tia katika oveni hadi uive kama kawaida ya kupika wali.
Pakua katiha sahani na tolea na samaki yoyote wa kukaanga.

Mapishi ya Biriani Ya Kuku Wa Kuchoma Wa Tanduri

Mahitaji

Mchele – 4 vikombe

Kuku – 1

Vitunguu – 3

Nyanya/tungule – 4

Zabibu kavu – ½ kikombe

Tangawizi na kitunguu (thomu/galic) – 2 vijiko cha supu

Pilipili mbichi iliyosagwa – 1 kijiko cha supu

Mtindi (yoghurt) – 2 kijiko cha supu

Masala ya tanduri – 2 vijiko vya supu

Pilipili manga – 1 kijiko cha chai

Hiliki – ½ kijiko cha chai

Mdalasini – kijiti kimoja

Ndimu – 3 vijiko vya supu

Chumvi – kiasi

Zaafarani (saffron) – 1 kijiko cha chai

Mafuta – ½ kikombe

Namna Ya Kutayarisha Kuku:

Baada ya kumsafisha kuku, mkate vipande vikubwa vikubwa kiasi upendavyo, muoshe mchuje atoke maji.
Katika bakuli, tia tangawizi, kitunguu thomu ilosagawa, pilipili mbichi ilosagwa, chumvi, ndimu, mtindi, masala ya tanduri na uchanganye vizuri, kisha mtie kuku na uchanganye tena na acha arowanike kwa muda wa kiasi saa au zaidi.
Panga kuku katika sinia ya kuchoma ndani ya oveni. Kisha mchome (grill) hadi awive, mtoe acha kando. Mwagia juu yake masala yatakayobakia katika sinia baada ya kumchoma.

Namna Ya Kutayarisha Masala Ya Nyanya:

Weka mafuta katika karai, tia vitunguu ulivyokatakata, kaanga hadi vianze kugeuka rangi.
Tia nyanya ulizokatakata, tia pilipili manga, hiliki, mdalasini, chumvi, na zabibu. Kaanga kidogo tu yakiwa tayari.

Namna Ya Kutayarisha Wali:

Osha na roweka mchele wa basmati.
Roweka zaafarani kwa maji ya moto kiasi robo kikombe weka kando.
Chemsha maji, tia chumvi, kisha tia mchele uive nusu kiini.
Mwaga maji uchuje mchele kisha rudisha katika sufuria au sinia ya foil. Nyunyizia zaafarini, na rudisha katika moto upike hadi uive kamili.
Epua, kisha pakua wali katika sahani au chombo upendacho, mwagia juu yake masala ya nyanya. Kisha weka vipande vya kuku ulivyochoma, biriani ikiwa tayari

Mapishi ya Ugali Kwa Mchuzi Wa Samaki Wa Kuchoma

Vipimo Vya Ugali

Unga wa mahindi – 4 vikombe

Maji – 6 kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Tia maji kiasi katika sufuria wacha yachemke hasa

Tia unga kidogo kidogo huku ukikoroga mpaka ukamatane

Punguza moto huku ukiendelea kuusonga

Endelea kusonga kwa dakika kadhaa mpaka uanze kuchambuka

Kisha mimina kwenye bakuli au sahani na itakuwa tayari

Vipimo Ya Upishi Wa Mchuzi Wa Samaki Wa Kuchoma Wa Nazi

Samaki:

Samaki wa Nguru – kiasi vipande 5 – 6

Pilipili mbichi – 3

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 5 chembe

Tangawizi mbichi – 1 kipande

Bizari ya samaki – 1 kijiko cha supu

Pilipili nyekundu ya unga – 1 kijiko cha chai

Ndimu – 3 kamua

Chumvi – kiasi

Ukipenda mkate samaki vipande kiasi.
Saga vipimo vyote vinginevyo katika mashine. Mchanganyiko ukiwa mzito ongezea ndimu
Changanya pamoja na samaki upake vizuri vipande vya samaki
Acha kwa muda wa nusu saa vikolee mchanganyiko
Panga samaki katika treya ya kupikia ndani ya oveni, kisha mchome (grill) samaki huku ukigeuza hadi viwive.
Epua weka kando.

Kuandaa Mchuzi:

Nyanya/tungule – 3

Kitunguu – 2

Bizari ya manjano/haldi – ¼ kijiko cha chai

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Tui la nazi zito – 3 vikombe

Chumvi – kiasi

Katakata vitunguu na nyanya vidogodogo (chopped) weka kando

Weka mafuta katika karai au sufuria, kaanga vitunguu hadi vianze kugeuka rangi

Tia nyanya kaanga pamoja na tia bizari ya njano/haldi .

Tia tui la nazi, chumvi koroga .

Mwishowe tia vipande vya samaki na rojo lake litakalobakia katika treya, mchuzi uko tayari

Shopping Cart