Dondoo za Mapishi na Lishe

Mapishi ya Wali Wa Karoti Na Kuku Wa Kukaanga

Vipimo Vya Wali

Mchele wa Basmati/Pishori – 1 kilo moja

Vitunguu maji – 3

Karoti – 2

Siagi – 3 vijiko vya supu

Kidonge cha supu (stock) – 1 kimoja

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Ósha mchele uroweke kama saa moja au mbili
Katakata vitunguu vipande vidogodogo (chopped) weka kando.
Kwaruza karoti (grate) weka kando.
Tia siagi katika sufuria ya kupikia wali, weka katika moto iyayuke
Kaanga vitunguu hadi vigeuke rangi kiasi tu.
Tia maji kiasi ya kupikia wali, changanya na kidonge cha supu.
Yakichemka tia mchele, koroga, funika uweke moto mdogo mdogo.
Kabla ya maji kukauka tia karoti changanya wali kisha funika uive kama unavyopika pilau.

Vipimo Vya Kuku Wa Kukaanga

Kuku alokatwakatwa – 1

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi ilosagwa – 2 vijiko vya supu

Bizari ya mchanganyiko/garam masala – kijiko cha supu

Mtindi/Yoghurt – 1 kijiko cha supu

Ndimu – 1

Chumvi – kiasi

Mafuta ya kukaangia – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Ukishamuosha kuku, mchuje atoke maji yote.
Changanya viungo vyote katika kibakuli kidogo.
Changanya pamoja na kuku kisha acha akolee viungo (marinate) kwa muda wa masaa mawili takriban.
Weka mafuta katika karai na kaanga kuku, akiwiva yu tayari kuliwa na wali.

Mapishi ya Wali Wa Nazi Wa Adesi, Bamia Na Mchuzi Wa Kamba

Mahitaji

Mchele – 2 vikombe

Adesi -1 ½ vikombe

Nazi ya unga – 1 Kikombe

Maji (inategemea mchele) – 3

Chumvi – Kiasi

Vipimo Vya Bamia:

Bamia – ½ kilo

Vitunguu maji – 2 vya kiasi

Nyanya iliyosagwa – 1 kubwa

Nyanya ya kopo – 2 vijiko vya chai

Pilipili manga – ½ kijiko cha chai

Mafuta – 3 vijiko vya chai

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika:

Wali wa adesi

Osha na roweka mchele na adesi .
Chuja nazi kwa vikombe 3 vya maji tia chumvi kisha weka jikoni.
Tui la nazi likishachemka tia mchele na adesi pamoja. Punguza moto, funika wali upikike kwa moto mdogo mpaka ukauke vizuri.

Bamia

Katakata bamia vipande vya kiasi/ Katakakata vitunguu weka kando.
Katika sufuria tia mafuta na kaanga vitunguu hadi viwe rangi ya hudhurungi.
Tia nyanya ilosagwa na nyanya ya kopo na pilipili manga na chumvi.
Kisha Tia bamia punguza moto mdogo mdogo mpaka ziwive.

Vipimo: Mchuzi Wa Kamba

Kamba – 1Lb

Vitunguu vilokatwa katwa – 2

Nyanya ilokatwa katwa – 2

Pilipili mbichi iliyosagwa – 1 Kijiko cha chai

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 1 Kijiko cha chai

Bizari ya mchuzi (curry powder) – ½ Kijiko cha chai

Haldi – bizari ya manajano – ½ kijiko cha chai

Nyanya ya kopo – ½ Kijiko cha chai

Ndimu – 1

Chumvi – Kiasi

Mafuta ya kukaangia – 2 Vijiko vya supu

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Kaanga vitunguu kidogo hadi vilainike,
Tia nyanya, thomu na piilipili mbichi. Endelea kukaanga, tia nyanya ya kopo, chumvi, bizari zote.
Tia tia kamba na huku unakoroga mpaka wabadilike rangi na kuwiva. Kamulia ndimu na mchuzi uko tayari.

Jinsi ya kupika Pilau ya Mpunga Na Nyama Ya Ng’ombe

Mahitaji

Mpunga – 4 vikombe

Nyama – 1 kilo moja

Kitunguu maji – 3

Mbatata/viazi – 7 vidogodogo

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi ilosagwa 3 vijiko cha supu

Bizari nzima/ya pilau/uzile/cumin – 3 vijiko vya supu

Mdalasini – 3 vipande

Hiliki – 7 punje

Pilipili manga nzima – 1 kijiko cha supu

Chumvi kiasi

Mafuta – ½ kikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha mchele weka kando
Katakataka vitunguu slice ndogo ndogo.
Weka mafuta katika sufuria kisha ukaange vitunguu pamoja na mdalasini, hiliki pilipilimanga.
Vitunguu vikigeuka rangi unatia kitunguu thomu na tangawizi.
Tia supu kidogo na nyama, kisha tia bizari ya pilau/uzile, na viazi/mbatata.
Maliza kutia supu yote, na ikiwa ni kidogo ongeze maji kiasi cha kuivisha mchele. kisha tia mchele ufunike hadi wali uwe tayari.
Ikiwa unatumia mkaa palia juu yake, ikiwa hutumii uache uive kwa moto mdogo mdogo.

Mapishi ya Ndizi na Nyama Ya Ng’ombe

Mahitaji

Ndizi mbichi – 10-12

Nyama ng’ombe – 1 kilo moja

Kitunguu maji – 2

Nyanya/tungule – 2

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 7

Tangawizi mbichi – 1 kipande

Ndimu – 2 kamua

Chumvi – kiasi

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Tui la nazi – 3 vikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Saga kitunguu thomu na tangawiz mbichi.
Weka nyama katika sufuria tia kijiko kimoja cha kitunguu thomu na tangawizi, chumvi na ndimu kisha chemsha hadi iive.
Menya ndizi ukatekate
Weka mafuta katika sufuria tia kitunguu maji kilokatwakatwa ukaange kidogo tu kisha tia nyanya/tungule uendelea kukaanga.
Tia tangawizi na thomu ilobakia.
Tia ndizi, kaanga kidogo kisha tia supu ya nyama na nyama yake.
Ziache ndizi ziive zikiwa tayari tia tui la nazi zikiwa tayari.

Jinsi ya kuandaa Biriani Na Sosi Ya Nyama Ya Mbuzi

Mahitaji

Nyama Ya Mbuzi – 1 Kilo

Mchele – 4 Magi

Vitunguu – 3

Nyanya – 2

Nyanya kopo – 3 vijiko vya chai

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi iliyosagwa – 2 vijiko vya supu

Pilipili mbichi iliyosagwa – 1 kijiko cha supu

Garam Masala (mchanganyiko wa bizari) – 2 vijiko vya supu

Hiliki – 1 kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Mafuta – ½ kikombe

Zaafarani au rangi za biriani za kijani na manjano/orenji

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika Sosi Ya Nyama

Changanya nyama na thomu, pilipili, chumvi na nusu ya garam masala. Tia katika treya ya oveni uipike nyama (Bake) hadi iwive. Au iwivishe kwa kuichemsha.
Katika kisufuria kingine, tia mafuta (bakisha kidogo ya wali) kaanga vitunguu hadi vigeuke rangi, kisha tia nyanya, nyanya kopo, bizari zote nyingine zilizobakia.

Namna Ya Kupika Wali

Mchele – 4 magi

Mdalasini – 1 kijiti

Hiliki – 3 chembe

Kidonge cha supu – 1

Chumvi

Osha na roweka mchele wa basmati.
Tia maji katika sufuria uweke jikoni. Tia kidonge cha supu, mdalasini, hiliki na chumvi .
Yakichemka maji tia mchele, funika upike hadi nusu kiini kisha uchuje kwa kumwaga maji.
Tia mafuta kidogo katika mchele na zaafarani iliyorowekwa au rangi za biriani kisha rudisha mchele katika sufuria ufunike na upike hadi uwive.
Pakua wali katika sahani kisha mwagia sosi ya nyama juu yake, pambia kwa kukatika nyanya, pilipili mboga na figili mwitu (Celery) au mboga yoyote upendayo.

Shopping Cart