Ujana na Makuzi | Mapenzi na Ngono Salama

Je, kuna madhara gani yatokanayo na uvutaji sigara kwa vijana hasa kijana Albino?

Kuna madhara mengi ambayo hutokana na uvutaji sigara.
Madhara mengi yanampata mvutaji kwani moshi unaingia
kwenye mapafu na kuendelea kuleta madhara mengine sehemu
nyingine za mwili.

Unaweza pia kupata madhara kwa kukaa karibu na mtu
anayevuta (hii inaitwa mvutaji baki). Uvutaji unafanya mwili
wako kunyonya sumu ijulikanayo kama nikotini. Nikotini ndio
chanzo kikubwa cha matatizo yatokanayo na uvutaji.
Uvutaji sigara unahusishwa na magonjwa mengi. Kiungo cha
mwili kinachoathirika kwanza ni mapafu. Uvutaji husababisha
kukohoakohoa, vichomi na kulipuka kwa kifua kikuu (TB) na
hatimaye saratani ya mapafu. Uvutaji pia unaathiri ngozi.
Ngozi ya mvutaji inakuwa nyepesi kwani inaathiri mishipa ya
damu iliyopo karibu chini ya ngozi. Hali hii inaifanya ngozi
kushindwa kujitengeneza upya (regenerate). Kwa vile Albino
tayari wana matatizo ya ngozi ni vizuri kama hawatavuta na
kwa wale wanaovuta basi waache kuvuta.

Je, kuna madhara gani ya kunywa pombe kwa vijana hasa kijana Albino?

Athari za pombe kwa mtu anayeishi na ualbino ni sawa na zile
zinazowapata watu wengine.
Mtu akiwa katika hali ya ulevi anaweza kuzembea katika
kufanya uamuzi sahihi kwa mfano kuhatarisha maisha yake
kwa kuendesha baiskeli yake kimchoromchoro, kujamiiana
bila kuvaa kondomu na kadhalika. Mbali na hayo, watu wenye
matatizo ya kunywa pombe husahau kujiweka katika hali nzuri
kwa maana hawajali kula chakula. Tabia hii inamuweka katika
hatari ya kuandamwa na maradhi.
Pombe zinaweza pia kuingiliana na maisha/uhusiano wa kimwili.
Mwanzo kabisa pombe inaweza kukusisimua na kukufanya
mchangamfu (kutoona aibu), lakini kadiri unavyoendelea
kunywa unaanza kusinzia na kwa upande wa wanaume wengine,
uume kukosa nguvu. Unaweza kushawishika kutoa aibu uliyo
nayo kwa kunywa pombe lakini mara nyingi hii haileti mvuto
kutoka kwa wenzi wako.

Kunywa pombe pia kunaleta uharibifu wa kudumu kwenye ubongo
ambao unamfanya mtu kupata matatizo ya kumbukumbu.
Pombe imewekwa kwenye kundi la vilevi tegemezi. Mwili
ukishazoea pombe, ni rahisi sana watu kutumia pesa zote
kwa ajili ya pombe na kusahau kufanya mambo mengine
yatakayomletea maendeleo katika maisha yake.

Watu wanaoishi na ulemavu wanapewa huduma za upasuaji hasa wakati wa kujifungua?

Upasuaji unafanyika kwa wanawake wote ambao wamegundulika
kuwa na tatizo la kujifungua kwa njia ya kawaida. Hii inafanyika
bila kujali hali yao kwa maana kwa watu wenye ulemavu na
wasio na ulemavu. Kila mwanamke atapata huduma hiyo kama
itakuwepo sehemu anapoishi.
Tatizo lililopo hapa Tanzania kwa sasa hivi hasa sehemu
zilizojitenga ni umbali wa kufikia huduma hii. Umbali huu
unamfanya mama aliyeanza uchungu wa kujifungua kushindwa
kuweza kufika kwa muda unaotakiwa.

Shopping Cart