Ujana na Makuzi | Mapenzi na Ngono Salama

Haki za ujinsia na afya ya uzazi zinamhusu pia mtu anayeishi na ualbino?

Haki za msingi; hasa zile zinazohusiana na kuthaminiwa na
kuheshimiwa kama binadamu zinawahusu binadamu wote
kuanzia siku unayozaliwa. Mataifa yote Ulimwenguni yameridhia
mikataba ya Kimataifa inayokubaliana na matamko haya ya
haki. Haki hizi ziko dhahiri katika sheria za nchi husika. Haki
muhimu za ujinsia na afya ya uzazi ni hizi:
• Kupata habari juu ya ujinsia na mada zinazohusu afya ya
uzazi.
• Mwanamke au mwanaume kuamua kwa uhuru na kuwajibika,
kama anataka kujamiiana lini na mtu gani.

• Kuamua idadi ya watoto anaotaka kuzaa na hao watoto
wapishane miaka mingapi.
• Kupata huduma za afya ya uzazi.
• Kuamua bila kulazimishwa nani wa kufunga naye ndoa.
• Kulindwa dhidi ya mila zenye madhara kama vile ukeketaji
wa wanawake.
Watu wote wakiwemo wale wanaoishi na ualbino au ulemavu
wa aina yoyote wanalindwa na haki za binadamu. Changamoto
iliyopo ni kwa wale watu wanaoishi na ualbino kutoa sauti katika
kutetea na kuhamasisha jamii juu ya haki zao.

Je, mimi ni msichana Albino ninaweza kupata mimba kama nikijamiiana mara moja tu?

Ndiyo msichana anaweza kupata mimba kwa kujamiiana mara
moja tu bila kujali ana rangi gani ya ngozi. Wasichana weupe,
weusi na wanaoishi na ualbino au wasio na ulemavu wa ngozi
wanafanana wote inapokuja kwenye suala la uwezekano wa
kupata mimba. Kinachobainisha/ kinachosababisha upatikanaji
wa mimba ni wakati tendo la kujamiiana linapofanywa na hatua
ya mzunguko wa hedhi. Kama yai lililopevuka kwa ajili ya
kurutubishwa litakuwa tayari basi ujauzito utatokea mara tu
baada ya mbegu ya mwanaume kuingia, (wakati wa kujamiiana).
Ujauzito unaweza kutokea hata kama msichana alikuwa bado
bikira na ni mara yake ya kwanza kujamiiana.

Je, wazazi ambao wote ni Albino wanaweza kupata mtoto ambaye siyo Albino?

Kwa kawaida, wazazi wote wakiwa Albino watazaa mtoto
Albino. Kwa maana hiyo basi, iwapo watu wawili wanaoishi na
ualbino wataamua kuunda familia itakuwa vizuri wafikirie kwa
makini kama wangependa kuzaa pamoja wakizingatia matatizo
ambayo wamewahi kupitia wao wenyewe kama Albino ndani ya
jamii. Ualbino ni hali ya kurithi na inabidi mtoto Albino abebe
vinasaba kutoka kwa wazazi pande zote ili aweze kuonyesha
ualbino. Hata hivyo, kuna aina zaidi ya moja ya ualbino na
pia aina tofauti za vinasaba, kama wazazi watakuwa na aina
tofauti ya ualbino na aina tofauti katika vinasaba, uwezekano
wa kupata mtoto asiyekuwa na ulemavu wa ngozi unakuwepo.
Lakini matukio kama haya yamejitokeza mara chache sana
ulimwenguni.

Je, ni kweli kuwa ulemavu unaweza kugundulika mara tu mtoto anapozaliwa?

Ni kweli kuwa daktari anaweza kufanya vipimo vya kugundua
kama mtoto aliye tumboni ni mwenye ulemavu au la. Baadhi ya
vipimo hivi ni “ultra sound” ambacho kinawezesha kuona picha ya
umbo la mtoto akiwa bado tumboni. Vipimo vingine vinaangalia
damu. Lakini ualbino hauwezi kugundulika kwa vipimo hivi.
Pia baada ya kuzaliwa daktari ana uwezo wa kutambua kama
mtoto ana ulemavu / hitilafu kama vile moyo, kwenye damu
kama vile “sickle cell”. Ualbino unaweza kugundulika mara tu
mtoto anapozaliwa au baada ya wiki chache.

Je, mtu anaweza kuzuia kupata mimba baada yakujamiiana bila kinga (kufanya ngono zembe) kwa mfano amebakwa?

Kama umebakwa au kulazimishwa kujamiiana unaweza kupata
huduma katika hospitali, kituo cha afya , zahanati au kutoka
kwa mhudumu wa afya ambaye atakupatia vidonge vya dharura
vya kuzuia mimba. Hivi ni vidonge ambavyo vinatumika ili
kupunguza uwezekano wa kupata mimba kama ulijamiiana bila
kinga, au umesahau kutumia njia yako ya uzazi wa mpango au
ulilazimishwa kujamiiana.

Ili ufanye kazi, njia hii ya dharura ya kuzuia mimba inatakiwa
itumiwe ndani ya saa 120 (ndani ya siku tano) baada ya tukio.
Inakuwa vizuri zaidi kama njia hii ya dharura itatumika punde
bila kusubiri kwani kwa kufanya hivyo, ufanisi wake unakuwa
wa kuaminika zaidi.

Hii njia ya dharura inazuia tu mimba kutungwa, haiwezi kusababisha
kutoka kwa mimba pindi mimba ikishatunga. Utakapotafuta
msaada wa kupata huduma ya vidonge vya dharura
vya kuzuia mimba hasa kwa wale waliobakwa au kulazimishwa ,
mwombe mhudumu akusaidie kupata huduma ya kuzuia maambukizo
ya UKIMWI. (Post exposure prophylasis). Unaweza
kupata taarifa zaidi kwa mtoa huduma wa uzazi wa mpango
kwenye kliniki za serikali, kliniki za UMATI, kliniki za Marie
Stopes au sehemu yoyote wanapotoa njia za kisasa za uzazi
wa mpango.

Shopping Cart