Ujana na Makuzi | Mapenzi na Ngono Salama

Msaada juu ya ukeketaji

Unaweza ukajaribu kuzungumza na wazazi wako kwamba
ukeketaji ni desturi mbaya, na pia unaweza ukamtafuta mtu
wa kukusaidia ambaye ni mwaminifu. Msaidizi anaweza akawa
rafiki, mlezi, mzazi au mtu mzima katika familia ambaye
unaweza kumwamini. Katika jamii yako unaweza kumtafuta
mwalimu anayeaminika, kiongozi wa dini au muuguzi ambaye
anaunga mkono mawazo yako na mwenye msimamo wa kumaliza
tatizo la ukeketaji.

Kama hakuna mashirika yanayopinga ukeketaji katika sehemu
yako, unaweza kufikiria watu wanaofanya katika shirika la
vijana, vituo vya vijana, jumuia za wanawake, makanisa na
mashirika ya uzazi wa mpango. Unaweza kutoa habari hii katika
kituo cha afya kilicho karibu nawe. Kumbuka vijana chini ya
miaka 18 ukeketaji ni kosa la jinai na unaweza kuripoti katika
kituo cha polisi kilicho karibu nawe.

Sheria gani zimetungwa kuhusu ukeketaji?

Serikali zote na mashirika ya kimataifa wameweka mdhamana
na kukubali kulinda haki za binadamu. Tanzania imetia saini ya
mapatano na mikataba ya kimataifa inayohakikisha kuwa kila
mtu ana haki kwa afya na haki ya kuwa huru kutokunyanyaswa
kwa mfano katika Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za
Binadamu.
Maazimio mengine yaliyoboreshwa ili kulinda haki za wanawake na
watoto,15 ni kama lile Azimio la Kuondoa Ubaguzi kwa Wanawake
na Azimio la Haki za Mtoto. Maazimio haya yanaeleza wazi kuwa
ukeketaji ni desturi mbaya na ni kinyume na haki za binadamu,
kinyume cha haki za mtoto na kinyume cha haki za afya kwa
wanawake. Na zaidi nchi nyingi za kiafrika wamepitisha sheria
kupiga marufuku ukeketaji.16 Hapa Tanzania, Bunge limepitisha
sheria maalumu ya Makosa ya Kujamiiana ya mwaka 1998 ambayo
inakataza ukeketaji kwa wasichana na wanawake vijana chini ya
miaka 18. Pia kuna sera17 ambayo inaelezea jamii kuondoa mila na
desturi kama vile ukeketaji kwa kuwa zina madhara kwa vijana.
Hivyo kama wewe ni msichana chini ya miaka 18 ni kosa la jinai
kufanyiwa tohara na pia ni kosa kwa mangariba kujishughulisha
na ukeketaji wa wanawake.

Madhara yatokanayo na ukeketaji

Ukeketaji au tohara ya wanawake ni hatari sana kwa msichana
anayetahiriwa. Wasichana hufa kutokana na madhara yake
makubwa zaidi kwa vile:

  • Hutokwa na damu nyingi.
  • Uambukizo unatokea iwapo vifaa vilivyotumiwa
  • havikuwa safi. Uambukizo unaweza kuenea mpaka katika

viungo vya ndani vya uzazi na kusababisha ugumba na
hata vifo.

  • Hatari ya kuambukizwa Virusi vya UKIMWI wakati wa

ukeketaji.

  • Kuziba kwa mkojo na damu ya mwezi (hedhi) ndani ya

mwili wa mwanamke na kusababisha uambukizo.

  • Matatizo na maumivu makali wakati wa kujamiiana na

wakati wa kujifungua kutokana na kupungua ukubwa wa
uke. Ukeketaji wa wanawake mara nyingi una madhara
ya kisaikologia ambapo wasichana hupoteza tumaini
na imani kwa walezi au wazazi na wanaweza wakapata
mateso ya kujisikia waoga, kufadhaika, kutojiweza na
kutokuwa kamilifu kimwili.

Zaidi ya hayo, ukeketaji unampunguzia mwanamke hamu ya
kujamiiana. Kufanikisha hamu ya ngono inategemea kwa kiasi
kikubwa viungo vya uzazi vya nje. Ukeketaji hata hivyo unaharibu
umbile na kazi za viungo vya uzazi vya nje vya mwanamke.
Ina madhara kimwili na kisaikologia ambapo mara nyingi
huleta matatizo ya mahusiano ya kimwili kati ya mwanamume
na mwanamke. Kisimi ni sehemu ya mwili wa msichana chenye
ashiki na hisia kali ya viungo vya uzazi. Kinasisimua ashiki kwa
mwanamke anaposhikwa. Sehemu ya ndani ya mashavu na kisimi
kwa kiasi kikubwa vinahusika na hali kiwango cha raha ya na
kufikia mshindo wakati wa kujamiiana. Wakati kisimi na viungo
vingine vya uzazi vimeondolewa, ashiki na raha hupungua kwa
kiasi kikubwa. Endapo mwanamke amekatwa vibaya sana au uke
umeshonwa, kuna uwezekano wa kupata maumivu na matatizo
wakati wa kujamiiana na wa kujifungua.

Sababu za ukeketaji

Hakuna hata mmoja anayejua hasa kwa nini, na lini desturi
imeanza. Jamii inatoa maelezo tofauti kwa nini wasichana
wanatakiwa watahiriwe. Sababu zifuatazo zimetolewa kufanya
desturi hii: mila na utamaduni, dini, usafi, kulinda ubikira, kukaa
bila kuzini.
Kila mara sababu zinazotolewa za kuondoa au kukata kisimi
ni kupunguza nyege au starehe kwa mwanamke. Kwa makosa,
baadhi ya watu huamini kuwa kwa njia hii wanawake watakuwa
waaminifu kwa waume zao.
Kiafya hakuna sababu ya kumtahiri msichana, kinyume chake
inaweza kusababisha idadi ya matatizo ya afya. Ukeketaji
hautakiwi na dini yoyote. Hatakiwi na Koran wala Biblia.
Ukeketaji ni desturi na mila ambayo imepitishwa toka kizazi
kimoja hadi kizazi kingine.

Ndoa ya kulazimishwa

Ndoa ya kulazimishwa ni ile ambayo mwanamume au mwanamke
anaozwa bila yeye mwenyewe kukubali kufunga ndoa kwa
hiari yake. Katika mazingira hayo wasichana au wavulana
wanalazimishwa kufunga ndoa. Wakati mwingine wazazi wanafikiri
wanajua nini kizuri kwa watoto waona hivyo kuwachagulia mume
au mke.

Mara nyingi wazazi wanafikiria mambo ya uchumi na
kijamii katika kumchagulia
msichana au mvulana nani
amwoe.
Wanaweza kujaribu kumwoza
mtoto wao katika familia
ya kitajiri. Sababu nyingine
inayolazimisha mtu kuoa
ni mimba. Iwapo binti,
amepata mimba yeye na
mvulana aliyempa mimba
wanalazimishwa kufunga
ndoa kwa sababu baadhi ya
jamii hazikubali watoto wa
nje ya ndoa. Mara nyingine vijana wanalazimishwa kuoa kwa sababu
wamefikia umri ambao jamii inawategemea kuoa. Mara nyingi kuna
utii wa amri ya kuoa kwa vile mvulana au msichana anaogopa
kutengwa na kufukuzwa na mara nyingine anatishiwa, mateso
na unyanyasaji wa kimwili.

Shopping Cart