Ujana na Makuzi | Mapenzi na Ngono Salama

Jinsi ya kutumia kondomu ya kike

Kondomu ya kike inafahamika kwa jina la „care“ na “Lady Peteta”. Hapa Tanzania hazipatikani sehemu zote na bei yake ni kubwa kidogo.
Kondomu ya kike huingizwa ukeni kabla ya kujamiiana. Kama unatumia kondomu ya kike, chana kwa uangalifu pembezoni mwa pakiti. Kondomu ina pete mbili za plastiki na uwazi upande wa juu. Pete moja imelegea ni ndogo na iko kwa ndani, upande usio na uwazi. Pete ya pili ni kubwa zaidi, imeshikiliwa na iko upande wa tundu. Shikilia kondomu upande uliozibwa na minya pete ya ndani kwa dole gumba na kidole cha pili na cha kati. Mara nyingine inaweza ikakuponyoka, (kuteleza) lakini endelea kujaribu hadi umeiminya vizuri. Tafuta mkao mzuri na ingiza kondomu ya kike. Huku bado unaminya kwa vidole vyako iongoze kondomu ndani ya uke wako. Ukiiachia pete ya ndani itashikilia kondomu ndani ya uke. Sasa ingiza kidole chako kwenye kondomu, sukuma pete mpaka inapogota kwenye mlango wa uzazi.
Kondomu ya kike inaweza kuvaliwa saa kadhaa kabla ya kufanya ngono na pia inaweza kuvuliwa baada ya muda wa kufanyika ngono kupita. Ili kuhakikisha kuwa uume umeingia sehemu husika, msaidie mwenzi wako kuongoza uume kuingia kwenye uke ili usipenye pembeni.
Baada ya kujamiiana, vua kondomu kwa uangalifu. Tupa kondomu iliyotumika kwenye choo cha shimo au uichome. Usitupe kondomu iliyotumika ovyo.
Kama ilivyo kwa kondomu ya kiume, kondomu ya kike itatumika kwa mafanikio zaidi pale ambapo wahusikia wanakuwa na makubaliano na maelewano juu ya matumizi yake.

Jinsi ya kutumia Kondomu

Wakati wa kutumia kondomu ya kiume ni muhimu kufuata hatua zifuatazo. Hakikisha kwamba pakiti inayoihifadhi haijapasuka na kwamba tarehe ya kuisha muda wake haijafika.
Uume ukishadinda, fungua pakiti kwa uangalifu. Minya sehemu ya juu kutoa hewa ndani ya kondomu wakati wa kuvalisha uume, ili kuzuia kupasuka kwa kondomu wakati wa kujamiiana. Visha uume kondomu taratibu mpaka uufunike wote. Ukiwa na uhakika kwamba kondomu imevishwa inavyotakiwa, unaweza kukutana kimwili na mwanamke.
Wakati wa kutoa uume kutoka ukeni, uwe mwangalifu kwamba kondomu bado ipo sehemu inayopaswa kuwa. Baada ya kutoa uume kutoka ukeni, vua kondomu kwa uangalifu uume ukiwa bado umedinda, ili kuepuka shahawa zisimwagikie ukeni. Tupa kondomu iliyotumika kwenye choo cha shimo au uichome. Usitupe kondomu iliyotumika ovyo. Pia usitupe kondomu iliyotumika kwenye vyoo vya kisasa yaani vya kuflashi na maji.
Ukinunua “salama kondomu“ ndani ya pakiti, kuna maelekezo kuhusu matumizi ya kondom. Unapotaka kutumia kondom wakati wa kujamiiana, ni vizuri ukajaribisha kwanza ukiwa peke yako ili kuzoea jinsi ya kuitumia.

Njia ya kuzuia mimba inayofaa kwa kijana anayeanza kujamiiana

Kila njia ya kuzuia mimba ina faida na hasara zake. Kwa mfano faida ya vidonge ni kwamba kama mwanamke atavimeza kila siku, hakuna haja ya kufanya chochote wakati wa kujamiiana. Matatizo ya vidonge ni kwamba mwanamke anahitaji kufikiria kuvinywa kila siku. Kondomu, kwa mfano ina faida kwamba pamoja na mimba inazuia magonjwa ya zinaa, lakini kasoro yake ni kwamba unahitaji kuivaa wakati wa kujamiiana.
Hakika, ushauri wa sasa ni kuwa kondomu ndiyo njia bora zaidi kwani ni njia pekee inayozuia kwa pamoja mimba zisizotarajiwa na maambukizi ya magonjwa yatokananyo na kujamiiana.

Je, ni lazima kumeza vidonge vya kuzuia mimba siku zote, hata zile siku nisipojamiiana?

Ndiyo, vidonge vya kuzuia mimba ni lazima vimezwe kila siku hata kama hufanyi ngono siku hiyo. Kuna aina ya vidonge vya kuzuia mimba inayokuja katika pakiti yenye vidonge 21 na kuna inayokuja katika pakiti ya vidonge 28. Iwapo utapewa ile ya vidonge 21 utapumzika kunywa siku 7 katika mwezi. Iwapo utapewa ile ya vidonge 28, itabidi kumeza kidonge kimoja kila siku, hata siku za hedhi. Ili kuhakikisha vidonge vya kuzuia mimba vinafanya kazi sawasawa, mwulize yule aliyekushauri kutumia vidonge hivyo jinsi ya kuvimeza.
Kama mwanamke akisahau kunywa kidonge hata kama ni siku moja kuna uwezekano wa kupata mimba. Anaposahau kumeza vidonge, ni vizuri zaidi watumie kondom wakati wa kujamiiana kwa kuhakikisha kutopata mimba. Hii inahusika vilevile kama mwanamke ameharisha au ametapika katika kipindi cha saa 4 tangu ameze vidonge. Kama mwanamke anashindwa kukumbuka kunywa vidonge mara kwa mara, ni vizuri zaidi apate ushauri kutoka kwenye kliniki ya uzazi wa mpango kutumia njia nyingine ya kuzuia mimba.

Je, baada ya kutumia vidonge au sindano kwa muda mrefu, mwamamke akiacha kuzitumia hizo njia ataweza kupata mimba tena?

Vidonge na sindano zinazuia mimba kwa kuzuia yai lisipevuke. Akitumia njia hizi za kuzuia mimba, mwanamke anaona hedhi yake kama kawaida, lakini hakuna yai linalokuwa limepevuka kwa ajili ya kurutubishwa.
Mara mwanamke akiacha kutumia vidonge, mayai hupevuka tena ndani ya kokwa na mwanamke huweza kupata mimba. Mwanamke aliyetumia sindano, anaweza akachukua muda kiasi kurudia hali yake ya uzazi. Kwa wanawake wengine inachukua miezi 12.
Muhimu ni kukumbuka kwamba sindano na vidonge siyo njia za kudumu za kuzuia mimba, hata kama itachukua muda fulani kurudia hali ya kawaida ya uzazi

Shopping Cart