Ujana na Makuzi | Mapenzi na Ngono Salama

Mafuta kwenye kondomu

Mafuta yanayowekwa kwenye pakiti ya kondomu ni mafuta maalum na yana kazi ya kuhifadhi kondomu mpaka siku yake ya kutumiwa. Bila mafuta haya kondomu isingekuwa imara, ingekauka na isingekuwa nyumbufu vya kutosha. Vilevile mafuta hayo yanalainisha mpira ili kurahisisha uvaaji na matumizi yake. Kwa watu wengi, mafuta haya hayawaletei matatizo yoyote. Watu wachache sana ambao ngozi yao ni nyepesi kuathirika wanapata matatizo ya kuwasha baada ya kutumia kondomu.

Muwasho huwa sio wa kudumu. Watu wa namna hii wanashauriwa kunawa na sabuni ya kawaida baada ya kujamiiana.
Kuna uvumi kwamba mafuta haya yaliyomo ndani ya pakiti ya kondomu yana virusi vya UKIMWI. Hii siyo kweli, mafuta hayo yanawekwa kwa ajili ya kuhakikisha uimara wa kondomu tu.

Je, mbegu za kiume zinaweza kupita kwenye kondomu?

Hapana, mbegu za kiume haziwezi kupita kwenye kondomu. Kondomu zimetengenezwa ili kuzuia mbegu za kiume kufikia ukeni wakati wa kujamiiana. Kwa sababu shahawa haziwezi kupita kwenye kondomu, kondomu ni njia nzuri ya kuzuia mimba pamoja na maambukizi ya magonjwa ya zinaa pamoja na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.

Watu wengine wanasema kwamba kuna mashimo madogo kwenye kondomu yanayorahisisha mbegu pamoja na vijidudu vya magonjwa ya zinaa kupita. Huu ni uongo. Ukitaka kuwa na uhakika kwamba kondomu mpya haina mashimo, chukua kondomu moja na ijaze maji ya kawaida. Utaona kwamba maji hayapiti kwenye kondomu kabisa. Baada ya kujaribisha itupe kondomu ndani ya choo cha shimo au ichome moto, lakini usiitumie wakati wa kujamiiana

Kupasuka kwa kondomu

Kupasuka kwa kondomu mara nyingi kunasababishwa na kondomu kutowekwa vizuri uumeni. Ni muhimu sana kutoa hewa ndani ya kondomu wakati wa kuvalisha uume. Kwa sababu ile hewa ndani ya kondomu inaweza ikasababisha kondomu kupasuka wakati wa kujamiiana.
Vilevile siyo vizuri kupaka mafuta kama vaselini juu ya kondomu ili kurahisisha kitendo cha kuingiliana. Mafuta kama vaseline yanadhoofisha uimara wa kondomu na yanarahisisha kondomu kupasuka. Mafuta haya yanayowekwa kwenye pakiti ya kondomu yanahifadhi uimara wa kondomu, na ni aina maalumu ya mafuta.
Ni muhimu kukumbuka kwamba mwanaume akivaa kondomu vizuri jinsi tulivyoeleza awali, uwezekano wa kondomu kupasuka ni mdogo sana.

Ukubwa wa kondomu

Kuna aina kondomu za ukubwa mbalimbali. Kwa wastani ukubwa wa kondomu unafaa kwa wanaume watu wazima karibu wote na vijana balehe waliokomaa. Mara chache sana, kondomu ni ndogo kwa wanaume fulani, lakini wakati mwingine wanaume wanaringa tu kuwa na uume mkubwa au wanatumia kisingizio tu kwa sababu hawataki kutumia kondomu.
Kwa upande wa vijana, balehe kondomu zinaweza kuwa ndogo ukilinganisha na ukubwa wa uume wao. Kwa vijana, ambao uume bado mdogo, ni vizuri zaidi wangeacha kujamiiana badala yake watumie njia nyingine za kumaliza hamu ya kutaka kujamiiana kama vile kukumbatiana na kubusu.

Shopping Cart