Ujana na Makuzi | Mapenzi na Ngono Salama

Vidonge vya kuzuia mimba vinasababisha vidonda vya tumbo?

Wanawake wengine wanapata vidonda vya tumbo, lakini haya hayana uhusiano na vidonge vya kuzuia mimba. Vyanzo vya vidonda vya tumbo mara nyingi ni maambukizi yatokanayo na msongo wa mawazo, kula vyakula vyenye mafuta mengi na viungo vingi, au kuwa na historia ya ugonjwa huu katika familia. Baadhi ya dawa huathiri tumbo kama vile asprini na ndiyo maana sio kila mtu anashauriwa kuzitumia. Vidonge vya kuzuia mimba havisababishi vidonda vya tumbo.

Umri wa kuanza kutumia njia za uzazi wa mpango

Muda unaofaa kutumia njia ya kupanga uzazi ni wakati unapojamiiana kwa mara ya kwanza. Huu ni wakati mzuri wa kutumia kondomu, kwa sababu kondomu inazuia kupata mimba isiyotarajiwa pamoja na magonjwa ya zinaa.
Huu pia ni muda mzuri wa kwenda kliniki ili kupata ufafanuzi kuhusu njia mbalimbali za kuzuia mimba. Daktari au muuguzi anaweza kuwasaidia mwanaume na mwanamke kuamua njia inayofaa kwa hali yao.
Mara nyingi, watu wanafikiri kwamba huduma ya uzazi wa mpango ni kwa wanawake ambao wameshaolewa, kwa mama wajawazito au wanawake waliozaa tu. Lakini si kweli. Hapa Tanzania, kisheria kila mtu aliyebalehe, iwe mvulana au msichana ana haki ya kupata huduma ya uzazi wa mpango.

Njia za Kuzuia Mimba

Njia za uzazi wa mpango zinatofautiana sana na zinaweza kugawanywa katika makundi mengi:

Vizuizi

(hizi huzuia mbegu kulifikia yai): Kuna mpira wa kiume (kondomu ya kiume), yaani mfuko wa mpira uliozibwa upande moja. Unavishwa kwenye uume uliosimama kabla ya kuingia ukeni. Pia kuna mpira wa kike (kondomu ya kike), yaani mpira unaoingizwa ukeni kabla ya kujamiiana.

Vidonge vya kuzuia mimba:

Lazima mwanamke anywe vidonge hivi kila siku hata kama hajamiiani.

Njia nyingine za kuzuia mimba kwa muda mrefu

. Njia hizi hazihitaji maandalizi maalum, ili kuzuia mimba, kabla ya kujamiiana na pia mwanamke hahitaji kukumbuka kufanya chochote kila siku. Kati ya njia hizi ni pamoja na sindano anazopewa mwanamke kila baada ya miezi mitatu. Pili, kuna vipandikizi, yaani vijiti vyembamba vya plastiki vinavyowekwa kwenye sehemu ya juu ya mkono wa mama kwa njia ya upasuaji mdogo. Vijiti vina kichocheo kinachozuia kupevuka kwa yai. Pia, kuna kitanzi ambacho ni kitu kidogo kilichotengenezwa kwa aina maalum ya plastiki. Kwa ufupi kinaitwa IUD. Huwekwa kwa utaalamu ndani ya mfuko wa uzazi. Sindano, vipandikizi na vitanzi lazima viwekwe na mtaalamu mwenye ujuzi kwenye kituo cha afya chenye vifaa vya kutosha. Kwa vile dawa za kuzuia mimba kwa muda mrefu zinaingiliana na mzunguko wa kawaida wa hedhi kwa kiasi, athari zake ni kubwa kuliko kutumia vidonge.

Kwa mwanaume na mwanamke kuna njia ya kudumu ya kufunga kizazi kwa njia ya upasuaji

. Kwa mwanaume mirija inayopitisha mbegu hukatwa na kufungwa, ili kuzuia mbegu zisitoke. Akijamiiana, anaweza kumwaga shahawa, lakini ndani ya shahawa hakuna mbegu. Kama mwanaume amefunga kizazi uume utadinda kama kawaida na kufikia mshindo atamwaga maji ya shahawa ambayo hayatakuwa na mbegu. Kwa mwanamke mirija ya kupitisha mayai hukatwa na kufungwa, ili kuzuia mayai kufika kwenye mfuko wa uzazi. Baada ya upasuaji huu, mama ataendelea na hedhi kama mwanzo, lakini yai halitaweza kukutana na mbegu za kiume tena.

Vilevile kuna njia nyingine mbalimbali ambazo hazina uhusiano na matumizi ya dawa au vizuizi vya mimba. Njia hizi hazina uhakika mkubwa wa kutopata mimba. Mara nyingine mama anatumia ishara mbalimbali, au tarehe kujua lini anaweza kupata mimba, ili kuepuka kujamiiana katika kipindi hicho. Kumwaga mbegu za kiume nje ya uke, au kutegemea kwamba mimba hazishiki wakati wa kunyonyesha ni njia nyingine za asili zinazotumiwa. Kumbuka kwamba njia hizi hutumika sana, lakini si njia salama sana za kuzuia mimba wala kuambukizwa na magonjwa ya zinaa.
Ni muhimu kukumbuka kwamba njia ya uzazi wa mpango inaweza kufaa kwa mtu huyu na isifae kwa mtu mwingine. Kwa hiyo, ni vizuri kila mtu aliyeamua kupanga uzazi apate ushauri kwenye kliniki kuhusu njia inayomfaa zaidi

Mapenzi salama ni yapi?

Mapenzi salama ni yale yanayofanyika bila wasiwasi wa kupata mimba zisizotarajiwa, magonjwa ya zinaa pamoja na maambukizi ya virusi vya UKIMWI. Mapenzi salama yanaweza kuwa ni vitendo vya kumaliza hamu bila uume kuingizwa ukeni. Ngono ya kuingiza uume ukeni inaweza kuwa ngono salama kama tahadhari husika zinatumika.
Vitendo vya kumaliza hamu bila kujamiiana ni kupiga busu, kukumbatia, kunyonyana ndimi, kushikana mikono na kupiga punyeto. Matendo haya yote ni salama kabisa kuhusiana na mimba zisizotarajiwa na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.
Ili kuhakikisha mnafanya mapenzi salama wakati mnahusisha mwingiliano kati ya uume na uke, lazima mchukue tahadhari. Tahadhari mojawapo ni uaminifu katika mapenzi, kwa maana wewe uwe mwaminifu na yeye awe mwaminifu. Lakini pia inabidi muwe na uhakika kwamba wote wawili hamjaambukizwa magonjwa wakati mnapojamiiana kwa mara ya kwanza. Tahadhari nyingine ni kutumia kondomu. Kondomu inazuia mimba pamoja na magonjwa ya zinaa. Kuwa mwaminifu pekee yake haitoshi kama mmoja wenu au wote wawili mliwahi kujihusisha na uhusiano wa kimapenzi ambao haukuwa salama. Kama kweli mnataka kuwa upande wa uhakika wote ni vyema kwenda kupima Virusi vya Ukimwi kwa hiari.

Je, kama mwanamke na mwanaume wanapata watoto wa jinsia moja tu, ni kosa la nani?

Hakuna mwenye kosa, kwa sababu jinsia ya mtoto i inategemea na bahati na hamna uwezekano wa kupanga kuzaa aina fulani ya mtoto. Tulivyoona juu ni mwanaume ndiye aliye na aina mbili za mbegu. Aina moja husababisha kutokea mtoto wa kike na aina nyingine mtoto wa kiume. Mwanaume hana uwezo wa kuhakikisha achangie aina ya mbegu gani. Kwa hiyo, hata kama ni mwanaume anayeyakinisha jinsia ya mtoto, hana kosa, kwa sababu hana uwezo wa kuamua achangie mbegu ya aina gani.

Shopping Cart