Ujana na Makuzi | Mapenzi na Ngono Salama

Nikitafuta rafiki kwa nia ya kuoana (mchumba), je ni sifa gani niangalie kwa msichana/mvulana?

Kuchagua mchumba ni moja ya maamuzi ambayo kijana anahitaji kuyafanya kwa uangalifu mkubwa sana. Kwa sababu huyo ndiye atakayekuwa mwenzi wake wa maisha. Katika kuchagua mchumba kila mtu ana mawazo yake kuhusiana na kilicho muhimu kuzingatiwa. Mara nyingi mhemuko una nguvu zaidi kuliko uamuzi wa kimantiki

Hata hivyo, vifuatavyo ni kati ya vigezo ambavyo vinaweza kuangaliwa:

• Chagua mtu anayekuheshimu wewe na wengine; Chagua mtu unayemwamini;
• Chagua mtu ambaye unaweza kuongea, kujadiliana, na kuhojiana naye kwa uwazi bila kugombana;
• Chagua mtu mwenye umri unaokaribiana na wa kwako;
• Chagua mtu anayependelea vile unavyopendelea;
• Chagua mtu ambaye ataelewa matatizo yako na yuko tayari kukusaidia kuyatatua; na
• Chagua mtu mwenye afya nzuri.

Hii inamaanisha pia kumpata mtu ambaye kabla ya kuanza kujaamiana naye, atakuwa tayari kwenda kupima kwa hiari kujua hali yake ya VVU na pia kuwa tayari kutumia kinga kwa maana ya kondomu hadi hapo mtakapojua hali zenu.

Wafahamishe wazazi wako mtu uliyemchagua kama mchumba na mtambulishe kwao i ili wamfahamu na yeye awafahamu wazazi wako. Wakati huohuo na wewe jaribu kuwafahamu wazazi wake. Usifanye uchumba wa haraka. Pata muda wa kutosha kumwelewa rafiki yako.

Kufahamu tabia ya rafiki yako wa kike/kiume kabla ya kuoana hata kama anaishi mbali

Unaweza kufanya uchunguzi wa kutosha kuhusu tabia, muono na imani ya rafiki yako hata kama mnaishi mbalimbali. Unaweza kumuuliza maswali kuhusu mahali anapoishi na familia yake kwa ujumla. Jaribu kufanya mawasiliano ya karibu zaidi ili uweze kumdadisi, na yeye aweze kujieleza mwenyewe kwa undani zaidi kuhusu yeye mwenyewe.

Njia nyingine ni kutumia watu wengine walio karibu naye. Unapomchunguza mtu ambaye unafikiri anaweza kuwa mchumba wako inakubidi uwe na vigezo ulivyojiwekea ambavyo ungependa awe navyo.

Uchunguzi wa namna hiyo unaweza kukusaidia kujua tabia ya rafiki yako. Hata hivyo kufanya uchunguzi hakuna maana kwamba huhitaji kuwa naye kabisa. Bado unahitaji muda zaidi wa kuwa naye ili kumjua na kujenga uhusiano.

Jambo la kukumbuka ni kwamba tabia, siyo rahisi kufahamika na kuelezeka waziwazi, na hasa kama watu wako kwenye mapenzi. Mara nyingi katika mazingira haya siyo rahisi kuona kasoro. Vilevile tabia ya mtu huenda ikabadilika kulingana na umri.

Nifanye nini ili kuepuka kubakwa na mpenzi/ rafiki?

Kuna baadhi ya vidokezo ambavyo vinaweza kukusaidia:
1. Usikae faragha na mwenzi wako kabla hujawa tayari na kumwamini. Ongozana na marafiki wengine hasa mwanzoni mwa urafiki wenu. Msitoke tu nyie wawili hadi hapo utakapojisikia kuwa umemjua kiasi cha kumwelewa na kumwamini. Pia jiepushe kukaa sehemu za faragha naye.

2. Kama utatoka naye, hakikisha kuwa kuna mtu anayejua mnakokwenda na ni muda gani unakusudia kurudi nyumbani. Ikiwezekana kuwa na namba ya simu ya mmoja kati ya rafiki zako. Hii itakusaidia kama ikijitokeza hali ya kutaka msaada.
3. Usikubali yeye alipe gharama zote. Ni vizuri kugawa gharama hizo kati yenu. Kama mtakwenda kwenye tamasha au kupata kinywaji hakikisha kulipia nusu ya hizo gharama. Ukifanya hivyo utamzuia mwenzio mawazo ya kukufikiria “kuwa anakudai ngono“ kama malipo ya pesa yake aliyotumia.
4. Ni vizuri kutafakari na kuweka kichwani kabla ya kwenda naye popote juu ya nini unachotaka na kile usichotaka kitokee.
5. Onyesha wazi kuwa unaposema “hapana“ unamaanisha “hapana“ usimpe nafasi ya kuchukulia hiyo “hapana“ kuwa ndiyo.
6. Amini hisia zako. Kama unaona unalazimishwa usisite kueleza maoni yako / unavyojisikia. Ikibidi ondoka sehemu hiyo.

Kulambana sehemu za siri ni salama kiafya? Je, tendo hili ni la kawaida?

Si rahisi kusema ni kitendo kipi kilicho cha kawaida na kisicho cha kawaida. Kulamba ni jambo linalofanyika

na kama wahusika wote wanalipenda ni sawa. Inashauriwa kuosha sehemu za siri kabla ya kufanya hivyo. Kwa kufanya hivyo, yaani kunawa kunafanya tendo hili kufanyika katika hali ya usalama kiafya. KAMA wote mtakuwa wazima bila kuwa na maambukizi ya magonjwa ya zinaa hasa kisonono (gono).

Je, kuna matatizo yoyote kama mdomo wa msichana utagusana na shahawa?

Kama mpenzi wako hatakuwa na maambukizi ya magonjwa ya zinaa hakuna madhara ya kiafya. kama shahawa i itagusana na mdomo wa msichana. Lakini, wasichana wengi hawapendi kupokea shahawa mdomoni na wanasikia kukerwa kufanya hivyo.

Wapenzi wajadiliane kati yao na kuamua kama tendo la kumwaga mbegu mdomoni wanalipenda au hawalipendi. Huu ni msingi mmojawapo wa kuonyesha kujaliana.

Hata hivyo, kama mwanaume ameambukizwa na magonjwa ya zinaa ni rahisi sana kwa mwanamke kuambukizwa magonjwa hayo wakati anapokea majimaji na shahawa mdomoni. Kwa hiyo, kutumia kondomu katika mtindo huu ni salama zaidi.

Shopping Cart