Ujana na Makuzi | Mapenzi na Ngono Salama

Lengo na sababu ya kujamiiana

Lengo kuu la kujamiiana ni kutafuta watoto. Lakini si sababu pekee. Sababu hizo ni pamoja na;

  1. kupata starehe,
  2. kujiburudisha,
  3. kupoteza mawazo,
  4. kujenga na kudumisha uhusiano na hisia za kupendana,
  5. kuhitajiana,

Hata hivyo ni muhimu sana kuzingatia uzazi wa mpango. Ili kuleta raha katika tendo la kujamiiana na kuzuia mimba isiyotakiwa na kuzaa mtoto ambaye mtashindwa kumlea ni lazima kutumia uzazi wa mpango.

Tumia njia za kupanga uzazi kama hamtaki kupata mimba! Au kwa usalama zaidi tumia kondomu ambayo ni kinga ya mimba na maambukizi mengine yanayosababishwa na ngono.

Mahusiano ya kimapenzi kati ya msichana mwenye umri mdogo na watu wazima

Inawezekana kwa msichana mdogo kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanaume mwenye umri mkubwa. Hata hivyo uzoefu umeonyesha kwamba uhusiano kama huo mara nyingi unakuwa mgumu. Kwanza kabisa ni suala la upevu wa akili na uwiano wa jinsi ya kufurahia maisha.

Kwa mfano, vijana ambao hawajapishana sana umri (miaka ishirini na zaidi) wanaweza kuongea, kujadiliana na kuelimishana kuhusu mambo yao. Lakini inapotokea umri umepishana sana, mvuto wao wa maisha unakuwa tofauti vilevile. Kwa kuongezea, mzunguko wao wa watu wa rika utakuwa wa umri tofauti na watakuwa na mambo machache sana ambayo yatawafurahisha wote wawili kwa pamoja. Mara nyingi, hili linaweza kuleta mtafaruku kati ya msichana na mume wake na kusababisha kuwa na uhusiano wa juujuu.

Pili, kuna shaka kidogo kuhusu kulea watoto. Kumlea mtoto mpaka afikie umri mkubwa wa kuweza kujitegemea na kufanya maamuzi yake mwenyewe, kunahitaji nguvu nyingi. Sasa iwapo mume naye amezeeka na anahitaji kutunzwa itamuwia vigumu sana mwanamke kutekeleza majukumu yote mawili kwa ufanisi, ili kuhakikisha kuwepo kwa maendeleo mazuri ya familia.

Kwa kuongezea mwanaume mzee anaweza kupungua nguvu na hamu ya kutaka kujamiiana wakati msichana hamu yake iko juu. Hili linaweza kuleta ugomvi mkubwa kati yao.

Pia ni muhimu kukumbuka kuwa wanaume wenye umri mkubwa tayari watakuwa wamekuwa na wapenzi wengi kabla yako. Kwa hiyo ni muhimu kwako kumtaka aende kupima virusi vya UKIMWI kabla ya kuanza uhusiano wa kimwili.

Unapofikiria uhusiano na mwanaume mwenye umri unaozidi umri wako sana, fikiria hoja zilizoandikwa hapo juu na angalia hali yako. Mara nyingi ni rahisi kudumisha uhusiano, ukiolewa na mtu ambaye mnalingana umri.

Umri unaofaa kuoa

Kuoana maana yake ni kuwajibika kwa maisha yako na mke au mume wako. Mara nyingi kuoana kunaambatana na kuzaa watoto. Ni vigumu sana kutambua umri sahihi wa mtu kuoa au kuolewa, kwa sababu watu wanatofautiana katika kuamua ni lini yuko tayari kujitegemea na kuwajibika kumtunza mtu mwingine. Wengine wanakuwa tayari katika umri wa miaka 20 na wengine katika umri mkubwa zaidi.

Kwa vile kuoa au kuolewa mara nyingi kunahusishwa na mtu kuwa mzazi, kuna vipengele vya kiafya vinavyofaa kuzingatia. Kwa mfano siyo vema msichana kuzaa kabla hajafikisha umri wa miaka 18, kwa sababu mwili wake hauko tayari kuzaa mtoto. Nyonga i nakuwa bado ni nyembamba, viungo vya uzazi ni vidogo na havijakomaa kiasi ambacho vinaweza kuharibika wakati wa kuzaa mtoto.
Kwa hiyo basi unashauriwa kusubiri i kuoana mpaka hapo utakapokuwa umejenga msingi i mzuri i wa maisha yako. Kabla hujawa tayari kuoa au kuolewa unaweza kuwa na urafiki na yule aliye mtarajiwa wake ili taratibu muweze kuelewana tabia, yale anayoyapenda na asiyoyapenda na kujenga msingi mzuri wa uhusiano.

Jinsi ya kumfanya mpenzi au rafiki yako asiwe na mwingine

Jambo la muhimu ni kuwasiliana kwa karibu i ili kuelewa mawazo na matatizo ya rafiki yako. Hakikisha unakuwa muwazi na mkweli. Mkielewana vizuri mnaweza kufurahia mazungumzo yenu vizuri. Vilevile mnaweza kusaidiana katika kutatua matatizo yanayoweza kumkabili mmoja wenu. Kwa kufanya hivyo mtajenga moyo wa kuaminiana.

Ili kudumisha urafiki wenu unashauriwa kuonyesha upendo wa hali ya juu. Jitahidi usiwe na marafiki wengine na mthibitishie kwamba yeye pekee ndiye unayempenda na uko mwaminifu kwake.

Utamfahamu vizuri rafiki yako iwapo mtazungumza mara kwa mara juu ya maisha yenu. Kwa mfano mnaweza kuzungumzia mipango ya uhusiano wenu, vitu anavyopendelea kufanya baada ya saa za kazi au masomo, watu anaowasiliana na kuandikiana nao. Iwapo mawasiliano yenu yatakuwa mazuri na iwapo utachunguza uhusiano wake na watu wengine utahisi kama kweli mnaaminiana.

Hata hivyo, iwapo hutaweza kumwamini rafiki yako na kama unahisi kwamba hata yeye hakuamini, jiulize kwamba kwa nini iwe hivyo. Je, inawezekana huyu mtu hanifai? Au, inaweza kuwa mapenzi yako ni kidogo kiasi ambacho siwezi kuzuia vishawishi vingine?

Jinsi ya kufanya wazazi wamkubali mchumba

Uhusiano mzuri na wazazi ni muhimu sana siyo katika masuala ya uchaguzi wa mchumba tu, bali katika masuala yote ya msingi maishani. Kwa hiyo, hatua ya kwanza ni kujaribu kuelewana nao.
Mara nyingi vijana hufikiri wazazi hawaelewi maisha ya vijana wa kisasa. Mara nyingine hufikiri kwamba mila na desturi zinamzuia kijana kufanya uamuzi ambao unafaa. Pia wengine hufikiri kwamba tofauti ya malengo kati ya vijana na wazazi huleta mgongano.

Hali kama hii ikijitokeza, ni vizuri kuwasiliana na wazazi kwa nia ya kuelewana. Usisahau kwamba wazazi wakati wote wanajaribu kujena maisha bora ya baadaye ya watoto wao. Unapowasiliana na wazazi jaribu kuwaeleza kwa heshima na upole kwa nini hukubaliani na mawazo yao na kwa nini unaona uamuzi wako unafaa. Inawezekana kwa kufanya hivi unaweza kupata ridhaa ya wazazi wako.
Kama hujawahi kuzungumza na wazazi wako kwa karibu, mara nyingi i i inakuwa vigumu kuanzisha mazungumzo. Jaribu kuanza kwa mazungumzo rahisi. Tafuta muda mzuri wa kuanzisha mazungumzo. Usianzishe mazungumzo na wazazi wakati wamechoka au wakati wametingwa na kazi nyingi; hawatakusikiliza. Jaribu kuwa wazi na mkweli, na waonyeshe wazazi wako kwamba unayajali mawazo yao. Kwa kufanya hivyo wazazi wako wanaweza kukuamini na kuafikiana na wewe katika maswali mazito zaidi. Vilevile onyesha kwamba unawaheshimu. Inachukua muda mrefu kufanikisha mawasiliano mazuri na wazazi, lakini ni vema kuyaanzisha mapema kwa ajili ya kufanikisha lengo la mawasiliano mazuri na wazazi.

Shopping Cart