Ujana na Makuzi | Mapenzi na Ngono Salama

Kama sitaki kujamiiana kabla ya ndoa, nifanye nini ili kuondokana na adha ya vishawishi vya hao ambao ameshaanza kujamiiana?

Kama umeamua kutojamiiana kabla ya ndoa, huo ni uamuzi mzuri na ni haki yako. Kutojamiiana kabla ya ndoa ni uamuzi wako binafsi kama ambavyo watu wengine walivyo na haki ya kuamua kuhusu maisha yao.

Hakuna haja ya kujisikia vibaya unaposikia vijana wenzako wanapoelezea jinsi wanavyojamiiana na raha wanayoipata. Unayo haki ya kujisifu kwamba mpaka sasa hivi umeweza kuvumilia kutojamiiana.

Kumbuka kwamba vijana wengi wanaozungumzia kujamiiana wanatia chumvi tu. Iwapo marafiki zako watazidi kukunyanyasa, jaribu kuwaeleza kwa nini umeamua kutojamiiana kabla ya ndoa. Wape ufafanuzi kuhusu madhara ya kujamiiana katika umri mdogo. Kama wataendelea basi hatua sahihi za kuchukua ni kutafuta marafiki wengine mtakaoelewana nao vizuri.

Nifanyeje kuepuka vishawishi vya kujamiiana kutoka kwa watu wengine, hasa wakubwa?

Vijana wengi wanajikuta wanatumbukia katika matatizo mazito kama kupata mimba mapema, utoaji wa mimba, magonjwa ya zinaa pamoja na maambikizi ya virusi vya UKIMWI na UKIMWI, kwa sababu wanapokea zawadi bila ya kujiuliza lengo la zawadi hizo.

Wanaume wengi wanatumia fedha kuwahadaa wasichana na wasichana wengine wamezoea kupata fedha hizo kukidhi mahitaji yao ya maisha. Jambo hili linaweza pia kuwapata wavulana kwani kwa maana kwamba wanawake watu wazima hujaribu kuwatongoza wavulana wadogo. Hivyo basi ni muhimu kwa wasichana na wavulana wote kwa pamoja kuwa waangalifu sana na zawadi zinazotolewa. Ni vema wakati wote ujiulize nini lengo la zawadi hiyo.

Pia fikiria kuhusu faida na hasara ya kujamiiana kila unapokutana na vishawishi mbalimbali. Ukikumbuka madhara ambayo unaweza kuyapata itakupa nguvu na msimamo wa kusema “hapana” na kujiepusha na vishawishi.

Nifanye nini nikipata hamu ya kujamiiana au kufanya mapenzi?

Unapofikia ujana unaanza kuwa na hisia za upendo na kujisikia kupata mvuto au msisimko ambao sio wa kawaida. Jambo hili ni la kawaida kwa kijana yeyote anayekua. Ni dalili zinazoonyesha kwamba sasa unaingia utu uzima.

Unapopata hisia za namna hiyo jaribu kutafuta shughuli zitakazokusahaulisha, kama vile, michezo, kujisomea, kuwasaidia wazazi kazi za nyumbani au kujihusisha katika shughuli za vikundi katika jamii. Vijana wengine wanasema kwamba wanaoga maji baridi ili kuondoa hamu na msisimko wa kutaka kujamiiana.
Unapojisikia kutaka kujamiiana au uume kudinda haimaanishi lazima ujamiiane. Kujamiiana ni njia mojawapo tu ya kuonyesha mapenzi. Kuna njia nyingine ambazo zinaweza kutumika kama vile kuongea, kushikana, mikono, kukumbatiana, kubusu na kushikanashikana.
Njia nyingine ni kupiga punyeto. Kupiga punyeto ni wakati msichana anajishika au anasuguasugua kinembe mpaka anapofikia mshindo, au wakati mvulana anasugua sugua uume wake mpaka anaposhusha. Watu wengi wanaopiga punyeto hufanya hivyo wakiwa peke yao. Kupiga punyeto hakuna madhara yoyote kiafya wala kiakili na ni aina moja ya kuwa na „mapenzi salama“.

Je, kuna madhara gani kama mtu anakaa muda mrefu bila kujamiiana au kufanya mapenzi?

Ukweli ni kwamba hakuna madhara yoyote ya kiafya iwapo utakaa muda mrefu bila ya kujamiiana. Viungo vya uzazi havidhuriki wala sehemu nyingine yoyote katika mwili wako. Mwanamke na mwanaume wakianza kujamiiana baada ya kukaa muda mrefu watapata raha na starehe kama kawaida.

Kuna uvumi potofu kwamba kutofanya mapenzi kunasababisha kuwa na chunusi usoni au sehemu za siri, au hata kuchanganyikiwa kiakili. Siyo kweli kwamba hali hiyo inasababishwa na kutojamiiana bali husababishwa na mambo mengine kabisa.

Elewa kwamba kutojamiiana kabisa hakuna madhara yoyote. Lakini kama tulivyosema awali kujamiiana kunaweza kuleta matatizo mengi kama mimba isiyotarajiwa, magonjwa ya zinaa ikiwa pamoja maambukizi ya virusi vya UKIMWI na UKIMWI wenyewe.

Kwa nini vijana wanakatazwa kujamiiana?

Ujana ni kipindi cha mabadiliko kutoka utotoni kuelekea utu uzima, wakati wa kipindi hiki kijana hupata mabadiliko ya kimwili, kiakili na kimtazamo. Mwili na akili hupevuka. Ni kipindi muhimu cha kuweka msingi wa maisha ya baadaye. Vijana wanakatazwa kujamiiana kwa sababu matatizo mengi yanaweza kutokea kutokana na tendo hilo.

Kwanza kabisa kwa kujihusisha na kitendo cha kujamiiana vijana wanapoteza nguvu na muda ambao wangeweza kutumia kwa shughuli za maendeleo. Kwa mfano, kusoma, kufanya kazi, kushiriki katika shughuli za vikundi katika jamii au kucheza michezo.
Pili, matatizo ya mimba katika umri mdogo ni mengi. Mojawapo ni msichana kufukuzwa shule, au hata jamii kumtenga. Matatizo mengine ni ya kiafya kutokana na mwili wa msichana bado kuwa haujakomaa vyema.
Tatu, vijana wanakuwa bado hawajajiandaa kwa uzazi au kujitegemea. Sababu nyingine ya kuwakataza vijana kujamiiana ni ile ya hatari ya kuambukizana magonjwa ya zinaa ikiwa ni pamoja na Virusi vya UKIMWI. Magonjwa haya ni mabaya sana yanaweza kusababisha maumivu makali, ugumba au hata kifo.
Unapofikiria sababu zote hizo utaona kwamba kujamiiana katika umri mdogo kunaweza kuleta madhara mengi kwa afya yako na malengo yako maishani. Hivyo basi unapokatazwa kujamiiana ni kwa sababu ya matatizo haya. Hata hivyo, kama kwa vyovyote huwezi kuacha kujamiiana, hakikisha kwamba unajikinga wewe na mpenzi wako kwa kutumia kondomu.

Shopping Cart