Mafundisho ya Msingi ya Kanisa Katoliki: Makala za Katoliki

Jinsi Bikira Maria anavyoelezwa Katika dini ya Kiislamu

Kurani inamtaja mwanamke mmoja tu, tena mara 34: ni Mariamu, mama wa nabii Isa. Akichanganywa na dada wa Haruni na Musa, aliyekuwa na jina hilohilo, anatajwa kama binti Imrani. Pia habari nyingine kadhaa zinapishana na zile za Injili.
Hata hivyo anapewa heshima ya pekee, kama inavyoonekana katika sura ya 3:43: “Na kumbukeni malaika waliposema, ‘Ewe Mariamu, kwa hakika Mwenyezi Mungu amekuchagua na kukutakasa na kukutukuza kuliko wanawake wa walimwengu”. Tena katika aya 3:46: “Na kumbukeni waliposema malaika: ‘Ewe Mariamu, bila shaka Mwenyezi Mungu anakupa habari njema za Neno litokalo kwake, jina lake Masihi Isa mwana wa Mariamu, mwenye heshima katika dunia na ahera, na yu miongoni mwa waliokaribishwa’”.
Aliambiwa amefanywa “ishara” pamoja na mwanae, ingawa haisemwi ni ishara ya nini. Sura ya 19, yenye jina lake, inaeleza kwamba Malaika Jibrili (Gabrieli) akimpasha habari ya mimba alisema, ‘Hakika mimi ni mjumbe wa Mola wako ili nikupe mwana mtakatifu’. Akasema, ‘Ninawezaje kupata mtoto hali hajanigusa mwanamume yeyote, wala mimi si mwasherati?’ Akasema, ‘Ni kama hivyo; Mola wako amesema: Haya ni rahisi kwangu, na ili tukufanya ishara kwa mwanadamu na rehema itokayo kwetu, na ni jambo lililokwisha hukumiwa’ ” (19:19-21). “Na mwanamke yule aliyejilinda tupu yake na tukampulizia roho yetu na tukamfanya yeye na mwanawe ishara kwa walimwengu” (21:91).
Pamoja na kusifiwa kwa usafi wake, anaongezewa sifa za imani na unyenyekevu: “Na Mariamu binti Imrani aliyejilinda uchi wake, na tukampulizia humo Roho yetu na kayasadikisha maneno ya Mola wake, na vitabu vyake; na alikuwa miongoni mwa wanyenyekevu” (66:12).

Namna Biblia inavyomueleza Bikira Maria

Biblia inashuhudia kuwa watu wanatofautiana

Maandiko matakatifu yanawasifu watu mbalimbali kutokana na jinsi walivyomuamini Mungu na kutenda makuu kwa ajili ya taifa lake.
Abrahamu alimuamini Mungu akawa tayari kumtolea sadaka mwanae Isaka, tukio lililomfanya apate baraka ya pekee ya kuwa baba wa waamini (Mwa 22:15-18).
Yosefu, mwana mpenzi wa Yakobo, alikuwa mwaminifu hata akaliokoa taifa lisiangamie kwa njaa (Mwa 50:20).
Musa ndiye mkombozi wa taifa la Mungu katika Agano la Kale: aliongoza Israeli kutoka [[utumwani Misri akalipatia sheria kutoka kwa Mungu katika mlima Sinai. Maandiko ya Agano la Kale yanakiri, “Wala hajainuka kiongozi kama alivyokuwa Musa” (Kumb 34:10-12).
Waliofuata ni Yoshua, Debora, Gideoni, Ruthu, Samweli, wafalme Daudi na Solomoni, manabii Eliya, Isaya, Yeremia, Ezekieli na wengineo.
Mwishoni Yesu Kristo akamsifu Yohane Mbatizaji akisema, “Ni mkuu kati ya uzao wa wanawake” (Lk 7:24-28).
Elizabeti, mama wa Yohane, alijiona hastahili kutembelewa na Bikira Maria, Mama wa Yesu, akamuita, “Mama wa Bwana wangu” (Lk 1:43).
Bikira Maria si mtu wa ziada katika mpango wa Mungu bali ni mshiriki mkuu wa ukombozi wa binadamu. Maria amechangia wokovu kwa kukubali mpango wote wa Mungu aliyetaka amzae Mwanae, amlee na kumfuata kiaminifu hadi msalabani, aliposhiriki kumtoa kama sadaka ya kutuokoa. Msimamo wake ulikuwa mmoja tu: “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema” (Lk 1:38).
Tukichunguza nafasi yake katika fumbo hilo, tunaweza kukiri pamoja naye kuwa ni Mwenyezi Mungu aliyemtendea makuu (Lk 1:49), kwa kuwa, “Mtu hawezi kuwa na kitu asipopewa na Mungu” (Yoh 3:27).
Yale yote ambayo Wakristo wengi wanayasadiki kuhusu Bikira Maria, hakujipatia bali alijaliwa na Mwenyezi Mungu huku akiitikia kwa hiari fumbo la mpango wake.

Utabiri kuhusu Bikira Maria kwenye Biblia

Biblia inatupatia utabiri uliotolewa na Mungu mwanzoni mwa historia kuhusu mwanamke atakayemshinda nyoka wa kale (Shetani): “Nitaweka uadui kati yako na huyu mwanamke, kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa chako” (Mwa 3:15). Juu ya [[Eva wa kale, ambaye alidanganywa na kuangushwa na Shetani atende dhambi, imesemwa: “Adamu akamwita mkewe jina lake Hawa, kwa kuwa ndiye aliye Mama wa walio hai” (Mwa 3:20). Hata hivyo Adamu na Eva wa kale wametuletea kifo (Rom 5:12). Mababu wa Kanisa wanamtazama Bikira Maria kama Eva mpya aliyemshinda Ibilisi na kuwa mama wa wote walio hai. Yesu, aliye Adamu mpya, alipokuwa anakamilisha sadaka ya ukombozi pale msalabani alimfanya Mama yake awe Mama wa waliokombolewa kwa kumkabidhi mwanafunzi, tena yule aliyempenda zaidi. “Penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na umbu la mamaye, Mariamu wa Kleopa, na Mariamu Magdalene. Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, “Mama, tazama, mwanao”. Kisha akamwambia yule mwanafunzi, “Tazama, mama yako”. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake. (Yoh 19:26-27).
Utabiri mwingine ulisema, “Tazama Bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamuita jina lake Emanueli, yaani Mungu pamoja nasi” (Isa 7:14). Dondoo hilo linalinganishwa na Lk 1:34-35, “Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu akakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli. Kwa sababu hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu”. “Imba, ee binti Sion, piga kelele, ee Israeli, furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, ee binti Yerusalemu. Mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana yu katikati yako” (Sef 3:14-15). Dondoo hilo linalinganishwa na Lk 1:28: “Malaika akaingia nyumbani mwake akamwambia, ‘Furahi Maria, umejaliwa neema kubwa, Bwana yu pamoja nawe’”. “Umebarikiwa wewe katika kila hema la Yuda na katika kila taifa, nao wanaposikia jina lako watafadhaika. Imani yako haitatoka mioyoni mwa watu wanaoukumbuka uweza wa Mungu milele” (Yudithi 14:7; 15:9). Dondoo hilo linalinganishwa na Lk 1:42, “Akapaza sauti kwa nguvu akasema, ‘Umebarikiwa wewe kuliko wanawake wote, na yeye utakayemzaa amebarikiwa’”.
Bikira Maria ni fumbo la ajabu alilolifanya Mungu katika mpango wa wokovu kwa ajili yake na kwa ajili yetu. Jamaa yake Elizabeti alimpongeza tena akiongozwa na Roho Mtakatifu, “Heri yako wewe uliyesadiki kwamba yatatimia yale uliyoambiwa na Bwana” (Lk 1:45).
Hivyo manabii mbalimbali kwa mwanga wa Roho Mtakatifu walimuagua Maria kwa heshima. Mambo yaliyotabiriwa katika Agano la Kale yalitimia katika Agano Jipya: ukombozi ulianza Bikira Maria alipokubali kwa imani fumbo la umwilisho wa Mwana wa Mungu. Bikira Maria hakuwa “chombo” tu kilichotumika bila ya kuelewa, bali alikuwa mshiriki huru wa kazi ya ukombozi ya Mwanae, kwa kuwa alipopashwa habari na malaika alikubali kwa hiari mpango wa Mungu akisema, “Mimi ni mtumishi wa Bwana, na iwe kwangu kama ulivyonena” (Lk 1:38).

Bikira Maria katika maisha ya Yesu

Yesu, kama mtu yeyote mcha Mungu, aliwaheshimu na kuwatii wazee wake: “Basi, akarudi pamoja nao Nazareti, akawa anawatii” (Lk 2:51).
Ishara ya kwanza kwenye maisha ya hadhara ya Yesu iliongozwa na Bikira Maria katika arusi ya Kana ya Galilaya, akisukumwa na huruma kwa wenye shida: kwa ombi lake Yesu aligeuza maji kuwa divai, na wanafunzi wake wakamwamini. Yohane alisimulia hivi, “Siku ya tatu palikuwa na arusi huko Kana, mji wa Galilaya; naye mama yake Yesu alikuwapo. Yesu naye alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake. Hata divai ilipowatindikia, mamaye Yesu akamwambia, ‘Hawana divai’. Yesu akamwambia, ‘Mama tuna nini mimi nawe? Saa yangu haijawadia’. Mamaye akawaambia watumishi, ‘Lo lote atakalowaambia, fanyeni’. Basi kulikuwako huko mabalasi sita ya mawe, nayo yamewekwa huko kwa desturi ya Wayahudi ya kutawadha, kila moja lapata kadiri ya nzio mbili tatu. Yesu akawaambia, ‘Jalizeni mabalasi maji’. Nao wakayajaliza hata juu. Akawaambia, ‘Sasa tekeni, mkampelekee mkuu wa meza’. Wakapelekea. Naye mkuu wa meza alipoyaonja yale maji yaliyopata kuwa divai, (wala asijue ilikotoka, lakini watumishi walijua, wale walioyateka yale maj), yule mkuu wa meza alimwita bwana arusi, akamwambia, ‘Kila mtu kwanza huandaa divai iliyo njema; hata watu wakiisha kunywa sana ndipo huleta iliyo dhaifu; wewe umeiweka divai iliyo njema hata sasa’. Mwanzo huo wa ishara Yesu aliufanya huko Kana ya Galilaya, akaudhihirisha utukufu wake, nao wanafunzi wake wakamwamini. (Yoh 2:1-12).
Bikira Maria anasifiwa kwanza kwa imani yake kuu kabisa, kuliko kwa kumchukua Yesu tumboni tu. Yesu alitaka kuwainua wasikilizaji wake wafuate mambo ya roho kuliko ya mwili. “Basi, mtu mmoja akamwambia, ‘Mama yako na ndugu zako wako nje, wataka kusema nawe’. Lakini Yesu akamjibu huyo mtu aliyemwambia hivyo, ‘Mama yangu ni nani, na ndugu zangu ni akina nani?’ Kisha akanyosha mkono wake juu ya wanafunzi wake akasema, ‘Hawa ndio Mama yangu na ndugu zangu, maana yeyote anayefanya anavyotaka Baba yangu aliye mbinguni, huyo ndiye kaka yangu na dada yangu na mama yangu’” (Math 12:46-50). Vilevile, wakati wa utume wake, alimsikia “mwanamke mmoja katika lile kundi la watu akisema, ‘Hongera kwa mwanamke aliyekuzaa na kukunyonyesha’. Yesu akamjibu, ‘Barabara, lakini heri yake zaidi yule anayelisikia Neno la Mungu na kulishika’” (Mk 11:27-28).

Bikira Maria alivyoshiriki Mateso ya Yesu

Katika kumfuata Mwanae Bikira Maria alitabiriwa wazi na mzee Simeoni uchungu kama upanga utakaopenya moyo wake, “Tazama huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe uchungu ulio kama upanga utauchoma moyo wako” (Lk 2:34-35).
Bikira Maria alishiriki kwanza mateso ya ukimbizi huko Misri kwa lengo la kumficha Mwanae asiuawe na Herode Mkuu, “Hivyo Yosefu aliamka akamchukua mtoto pamoja na Mama yake akaondoka usiku akaenda Misri akakaa huko mpaka Herode alipokufa” (Math 2:14-15).
Bikira Maria alishuhudia hatua kwa hatua kuteswa kwa Yesu; wanafunzi walipokimbia au kumtazama kwa mbali, yeye alikuwa karibu akaona vema kila teso lililompata Mwanae. Kutokana na fungamano la upendo wa ajabu lililokuwepo kati ya Yesu na Mamaye, alipoyashuhudia yote aliteseka sana katika moyo wake safi, kiasi kwamba Bernardo wa Klervoo akasema, “Msalaba wa Yesu uliwasulubisha wote wawili, Yesu mwilini na Mama yake moyoni”. Uaguzi wa mzee Simeoni ulitimia hivyo.
Kadiri ya mtume Paulo kuteseka ni kutimiliza yaliyopungua katika mateso ya Kristo kwa ajili ya Kanisa, “Na sasa nafurahi kuteseka kwa ajili yenu, maana kwa mateso yangu hapa duniani nasaidia kukamilisha kile kilichopungua bado katika mateso ya Kristo” (Kol 1:24). “… maana tukiyashiriki mateso yake Kristo, tutaushiriki pia utukufu wake” (Rom 8:17b).
Pale msalabani Bikira Maria, kwa njia ya mtume Yohane alifanywa Mama wa wote wanaompenda Mwanae; kisha kumzaa pasipo uchungu Bwana wa uzima, pale alituzaa sisi kwa uchungu wa kutisha uliotokana na kumuona Mwanae akifa msalabani. Hata hivyo Bikira Maria aliendelea kumuamini Mwanae aliyeonekana ameshindwa.

Bikira Maria baada ya kifo cha Yesu

Bikira Maria alikuwepo hapo mwanzo wa Kanisa, akilivutia zaidi Roho Mtakatifu kwa sala yake. “Hao wote walikusanyika pamoja kusali, pamoja na wanawake kadha wa kadha, na Maria Mama yake Yesu na ndugu zake” (Mdo 1:14).
Yesu alisema, “Ninayo bado mengi ya kuwaambieni, ila kwa sasa hamwezi kuyastahimili, lakini atakapokuja huyo Roho wa ukweli atawaongoza kwenye ukweli wote” (Yoh 16:12-13). Kwa msaada wa Roho Mtakatifu heshima kwa Bikira Maria ilienea katika Kanisa lote tangu zamani kabisa kadiri ya utabiri wake kuwa ataheshimiwa na vizazi vyote, “Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma mtumishi wake mdogo, hivyo tangu sasa vizazi vyote wataniita mwenye heri” (Lk 1:48).

Biblia inavyothibitisha kuwa Bikira Maria Mama wa Yesu ni Mama wa Wakristu Wote

Ufunuo 12:17
17Kisha lile joka likapatwa na hasira kali kwa ajili ya huyo mwanamke, likaondoka ili kupigana vita na watoto waliosalia wa huyo mwanamke, yaani, wale wanaozitii amri za Mungu na kuushika ushuhuda wa Yesu Kristo.
Kwa hiyo Bikira Maria ni Mama wa Wakritu wote yaani, wale wanaozitii amri za Mungu na kuushika ushuhuda wa Yesu Kristo

Ukisoma kwa urefu inasomeka hivi

Ufunuo 12:1-18

1 Kukaonekana ishara kuu mbinguni: Palikuwa na mwanamke aliyevikwa jua na mwezi ukiwa chini ya miguu yake na taji ya nyota kumi na mbili ilikuwa kichwani mwake. 2Alikuwa na mimba naye akilia kwa uchungu kwa kuwa alikuwa anakaribia kuzaa. 3Kisha ishara nyingine ikaonekana mbinguni: Likaonekana joka kubwa jekundu lenye vichwa saba na pembe kumi na taji saba katika vichwa vyake. 4Mkia wake ukakokota theluthi ya nyota zote angani na kuziangusha katika nchi. Ndipo lile joka likasimama mbele ya yule mwanamke aliyekuwa karibu kuzaa ili lipate kumla huyo mtoto mara tu atakapozaliwa. 5Yule mwanamke akazaa mtoto mwanamume, atakayeyatawala mataifa yote kwa fimbo yake ya utawala ya chuma. Lakini huyo mtoto akanyakuliwa na kupelekwa kwa Mungu kwenye kiti Chake cha enzi. 6Yule mwanamke akakimbilia nyikani, ambako Mungu alikuwa amemtayarishia mahali ili apate kutunzwa huko kwa muda wa siku 1,260. 7 Basi palikuwa na vita mbinguni: Mikaeli na malaika zake wakapigana na hilo joka, nalo joka pamoja na malaika zake likapigana nao. 8Lakini joka na malaika zake wakashindwa na hapakuwa tena na nafasi kwa ajili yao mbinguni. 9Lile joka kuu likatupwa chini, yule nyoka wa zamani aitwaye Ibilisi au Shetani, aupotoshaye ulimwenguni wote. Akatupwa chini duniani, yeye pamoja na malaika zake. Ushindi 10Kisha nikasikia sauti kuu mbinguni ikisema, “Sasa Wokovu na uweza na Ufalme wa Mungu wetu umekuja na mamlaka ya Kristo wake. Kwa kuwa ametupwa chini mshtaki wa ndugu zetu, anayewashtaki mbele za Mungu usiku na mchana. 11Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo na kwa neno la ushuhuda wao. Wala wao hawakuyapenda maisha yao hata kufa. 12Kwa hiyo, furahini ninyi mbingu na wote wakaao humo! Lakini ole wenu nchi na bahari, kwa maana huyo Shetani ameshuka kwenu, akiwa amejaa ghadhabu, kwa sababu anajua ya kuwa muda wake ni mfupi!’ 13Lile joka lilipoona kuwa limetupwa chini duniani, lilimfuatilia yule mwanamke aliyekuwa amezaa mtoto mwanamume. 14Lakini huyo mwanamke akapewa mabawa mawili ya tai mkubwa, kusudi aweze kuruka mpaka mahali palipotayarishwa kwa ajili yake huko nyikani, ambako atatunzwa kwa wakati na nyakati na nusu wakatia ambako yule joka hawezi kufika. 15Ndipo lile joka likamwaga maji kama mto kutoka kinywani mwake, ili kumfikia huyo mwanamke na kumkumba kama mafuriko. 16Lakini nchi ikamsaidia huyo mwanamke kwa kufungua kinywa na kuumeza huo mto ambao huyo joka alikuwa ameutoa kinywani mwake. 17Kisha lile joka likapatwa na hasira kali kwa ajili ya huyo mwanamke, likaondoka ili kupigana vita na watoto waliosalia wa huyo mwanamke, yaani, wale wanaozitii amri za Mungu na kuushika ushuhuda wa Yesu Kristo. Lile joka likasimama kwenye mchanga wa bahari. 18Yule joka akajikita katika mchanga ulioko ufuoni mwa bahari.

Tunajifunza nini

Mwanamke ni Bikira Maria

Mwanamke aliyetukuzwa Uf 12:1

1 Kukaonekana ishara kuu mbinguni: Palikuwa na mwanamke aliyevikwa jua na mwezi ukiwa chini ya miguu yake na taji ya nyota kumi na mbili ilikuwa kichwani mwake.

Anamzaa mtoto

Analindwa nyoka asimdhuru

Nyoka anapambana na wanawe

IShara ya joka kama Shetani

Akisubiri kuzaliwa kwa mtoto ili amdhuru kisha alishindwa na kutupwa duniani na kutaka kupambana na yule mwanamke Akashindwa na kuishia kupambana na watoto wa Yule mwanamke yaani, wale wanaozitii amri za Mungu na kuushika ushuhuda wa Yesu Kristo Uf 12:17

Mtoto Aliyezaliwa mwenye mamlaka

Ambaye ndiye Yesu Kristu

Kwa hiyo, Bikira Maria Aliwezeshwa kumshinda Shetani na ni Mama wa Wakristu wote

Mambo manne ya mwisho katika maisha

Mambo manne ambayo ni ya mwisho katika maisha ni;
  1. Kifo
  2. Hukumu
  3. Mbinguni
  4. Motoni
Mambo haya yote yanaweza kutokea wakati wowote bila kujua wala kutarajia

Kifo

Kifo ni kitu ambacho kinaweza kumpata mtu yeyote wa umri wowote awe mtoto kijana au mzee na kwa wakati wowote.
Maranyingi watu hawapendi kuongelea kuhusu kifo kwakua ni kitu ambacho kinampata kila mtu na hakipingiki wala hakina mjadala.

Hukumu

Baada ya kifo, inafuata hukumu, kila mtu atahukumiwa kulingana na matendo yake kama ulitenda mema utaenda mbinguni, na kama umetenda mabaya utaenda motoni.

Mbingu

Kama mtu akifa akiwa katika hali usafi wa moyo anaelekea mbinguni. Haijalishi ni kwa kipindi gani aliishi hivyo. Ila ni kwa hali gani kifo kilimkuta. Kwa sababu hii kila mtu anatakiwa aishi katika hali ya usafi wa moyo kwani hajui ni wakati gani atakutwa na kifo.

Motoni

Kama mtu akifa katika hali ya dhambi anaenda motoni. Kwa hiyo inatupasa tutumie vyema msamaa na huruma ya Mungu katika maisha yetu ili mwishi wetu uwe mzuri wakati bado tukiwa na muda.
Kila unapoishi ni lazima ufikirie mambo haya ukizingatia hujui wakati yanaweza kukupata. Kwa hiyo, nilazima uishi ukiwa unatafakari haya
ili uwe na mwisho mzuri.

Kwa nini Wakatoliki wanaungama dhambi kwa Padri?

KWANINI NYIE WAKATOLIKI MNAUNGAMA DHAMBI KWA PADRE AMBAYE NI MWANADAMU NA MDHAMBI BADALA YA KUUNGAMA MOJA KWA MOJA KWA MUNGU?
Pengine umewahi kuulizwa swali hili au umewahi kujiuliza: hapa ni maelezo yatayokusaidia kuelewa sababu (japo sio zote) na uhalali wa jambo hilo.
Hapa tunaongozwa na maneno ya Bwana Yesu mwenyewe alipotoa amri hiyo kwa mitume wake akisema;
“Pokeeni Roho Mtakatifu.wowote mtakaowaondolea dhambi wameondolewa na wowote mtakaowafungiwa dhambi wamefungiwa”(Yohane 20:22-23).
Na huo ndio utaratibu wetu tangu mwanzo wa kanisa wa mitume.
“Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi na kuombeana mpate kuponywa”(Yakobo 5:16a)
Ni miongoni mwa maagizo msingi kabisa ambayo hatuna mamlaka kuyabadili labda Yesu mwenyewe aliyeagiza hivyo aje mwenyewe kuyabadilisha.
Mungu anayesamehe dhambi ndiye aliyechagua njia ya kutoa msamaha huo,sisi tu nani tumpangie njia ya kutoa msamaha huo na kujipangia njia zetu?je tunamfundisha Mungu kazi?
Inashangaza siku hizi kusikia kwamba hata baadhi ya wakatoliki wameanguka katika mtego huu wa kutaka kubadilisha agizo hili la Yesu na inashangaza ni kwanini wanataka kurahisisha mambo kiasi hicho.
Mungu hafanyi kazi zake hewani bali huzifanya kupitia kwa watu wake.
Tunapoomba msamaha tunategemea kusikia maneno kama vile “nimekusamehe”,hutaka kuamini kwamba mtu akinyamaza au akiongea kimoyomoyo basi amekusamehe.
Yesu kwa kujua umuhimu na kazi ya neno hilo,alilitumia yeye mwenyewe akiwa binadamu(Luka 7:48).
Luka 7:48
“Naye Yesu akamwambia yule mwanamke,umesamehewa dhambi zako”
na alitaka aendelee kulitumia hata utimilifu wa dahari katika hali ya kibinadamu,ndio maana aliwaachia binadamu baada ya kifo chake ili waendeleze kazi hiyo.
Kuondolea watu dhambi ni moja ya utume wa Yesu(Marko 2:10),ni pamoja na kazi hiyo aliwaachia mitume wake(Yohane 20:23).
Tukilinganisha na mfano wa mtume Petro baada ya kumkana Bwana,tunaweza kujifunza kwamba tunapoongea na Mungu peke yetu ni katika hali ya toba na majuto(Luka 22:61-62).
Luka 22:61-62
“Bwana akageuka na kumtazama Petro,naye Petro akakumbuka yale aliyokuwa ameambiwa na Bwana ‘leo kabla jogoo hajawika utanikana mara tatu’ hapo akatoka nje,akalia sana.”
Hivyo bado tunadaiwa kuungama iki kuondolewa dhambi zetu(Yohane 21:15-17)
Chakushangaza ni kwamba,Wakristo wote tunaamini kwamba Sakramenti ya ubatizo inatuondolea kabisa dhambi ya asili na dhambi zote zikizowahi kutendwa na yule anayebatizwa na kwa kawaida huwa hatujibatizi wenyewe wala hatubatizwi moja kwa moja na Mungu moja bali hubatizwa na wanadamu wenzetu.
Sasa kama huyu mwanadamu mwenzetu anatubatiza na anatuondolea dhambi ya asili na wote tunasadiki hivyo iweje tukija kwenye kitubio tunapinga ushiriki wa binadamu mwenzetu na wakati matokeo yanayotarajiwa katika sakramenti hizo ni yaleyale kama ya ubatizo.
Iweje aliyekubatiza na kukuondolea dhambi ya asili na ukaamini kwamba amekuondolea ashindwe au ushindwe kusadiki ushiriki wake katika kitubio?
Iweje akisema “Nakubatiza kwa JINA LA BABA NA LA MWANA NA LA ROHO MTAKATIFU” hiyo iwe sahihi lakini akisema “Nakuondolea dhambi zako KWA JINA LA BABA NA LA MWANA NA LA ROHO MTAKATIFU” iwe sio sahihi?
Sasa huoni kama unajipinga na kujichanganya mwenyewe hapo?
Wapendwa,tuache kutafuta visingizio visivyo na ukweli kwaajili ya kutaka kupindisha ukweli.
Anayekuondolea dhambi ni Mungu mwenyewe kupitia kwa wapakwa mafuta wake yaani mapadre ambao amewaweka mwenyewe kwaajili ya huduma ya kanisa lake.
Wengine hudai pia kwamba ni watu wote waliopewa jukumu hilo na sio mapadre pekee,lakini ni vizuri kwanza kabla hujajitetea kwa msimamo huo dhaifu uchunguze tofauti iliyopo kati ya “Wanafunzi” na “wafuasi” kisha usome Biblia yako na kuona je jukumu hilo Yesu aliwatamkia wanafunzi wake au aliwatamkia wafuasi wake.
Wanafunzi wa Yesu ni wale kumi na wawili walioandamana naye.
Wafuasi ni wale makutano wengi waliokuwa wakimfuata kwaajili ya kusikiliza mafundisho yake.
Ikumbukwe kwamba Yesu hakusema mambo yote hadharani mbele ya makutano,baadhi ya maagizo msingi kama haya aliwachagua watu maalum kwaajili ya kuwapa kazi hizo na Biblia inasema aliwaita faragha peke yao na kuwapa maagizo hayo.
Shopping Cart