Mafundisho ya Msingi ya Kanisa Katoliki: Makala za Katoliki

Mambo yanayoweza kusababisha sala au maombi yako yasijibiwe

Mara nyingi tumekua tukiomba lakini hatupati, sababu zinaweza zikawa hizi ;

1. Mawazo na matarajio yetu

Mara nyingi tunajifunga kwenye maombi yetu pale tunapoomba na kisha kuanza kuwaza “hivi Mungu atanipa kikubwa au kidogo au atanisaidia sana au kidogo” Au tunaomba halafu tunakua na matarajio tofauti na kile tunachoomba. Aidha tunatarajia kupata kidogo au kikubwa.
Hali hii ni sawa na kumuwekea Mungu kizuizi kwenye maombi yako. Yaani kumuongoza Mungu afanye kwa kiasi kile unachofikiri.

2. Kulenga kutizamwa na watu.

Hii ni kuomba kwa majivuno yaani kuomba ili ukishapata watu waone kuwa umepata.
Jambo hili linamchukiza Mungu ndio maana unapoomba kupewa kitu au kusaidiwa kitu Mungu hafanyi /hakupi. Na Mara nyingine hata vile ulivyonavyo unanyan’ganywa kwa kuwa hauombi kwa utukufu wa Mungu bali kwa utukufu wako.
Hali hii ni sawa na kumuwekea Mungu ukuta kwenye maisha yako.

Namna njema ya kuomba ni hii

1. Kutokuomba mambo makuu sana ambayo huna haja nayo na hayana maana katika maisha yako.
2. Kutokuomba mambo madogo kwa mawazo labda nikiomba makubwa Mungu hataweza
3. Kutokuomba kwa ajili ya kutaka kuonekana na watu.

Maana ya Kumuamini Mungu

Kumuamini Mungu ni kuwa na uhakika na uwepo na uwezo wa Mungu. Ni kutambua na kukubali kwa uhakika kuwa Mungu yupo na anaweza kutenda. Unaweza kuwa na Imani lakini ukakosa kuamini yaani unaamini kwa Mungu lakini huamini kama atakutendea.

Kuamini kunakua na sifa zifuatazo

1. Kutokuwa na mashaka kama Mungu atatenda au hatatenda

2. Kuwa na subira. Kusubiri Mungu atende wakati unaofaa

3. Kuwa na matumaini hata kama hujatendewa.

Mara nyingi watu wanakuwa na imani lakini hawaamini ndio maana wanashindwa kuelewa mapenzi ya Mungu, mipango na matendo yake.

Kuwa na Imani tuu bila Kuamini huwezi kuendelea mbele kiroho. Kukosa Kuamini ndiyo sababu inayokwamisha maendeleo ya kiroho kwa watu wenye imani.

Dalili za kukosa au kupungukiwa Kuamini ni kama ifuatavyo

1. Kutokuwa na uhakika kama sala zako zitajibiwa.

2. Kukosa subira na matumaini.

3. Kuwa na maswali kama, Hivi Mungu yupo na mimi au hayupo na mimi??. Kujiuliza Hivi Mungu amenisikia?, Ananikumbuka?, Atafanya kweli??

Kukosa Kuamini kukizidi kunaleta hali ya kuhisi kuwa Mungu yupo na anaweza kutenda chochote lakini hatendi. Utakua sasa unaanza Kujiuliza kwa nini. Mtu akifika katika hali hii, Imani huporomoka na kupotea Mara nyingine mtu hufikia Kukosa imani kabisa na Mungu japokuwa anajua yupo na anaweza.

Ili kuondokana na hali hii ya kuwa na Imani lakini unakua na Kukosa kuamini, jitahidi kusali /kuomba neema ya kuamini, Jitahidi kusoma Biblia itakujengea kuamini na pia omba ushauri kwa watu wenye imani na wanaoamini.

AHADI 15 ZA ROZARI TAKATIFU

Mama Bikira Maria alitoa ahadi 15 kwa yule au wale watakaosali Rozari takatifu kila siku. Ahadi hizi aliwapa Mtakatifu Dominic na mwenye heri Alan de la Roche.

1. Yeyote yule atakayesali kwa imani rozari hii takatifu atapokea neema kuu zenye nguvu
2. Naahidi ulinzi wa kipekee na neema za kipekee kwa yule atakayesali rozari hii
3. Rozari itakuwa silaha kubwa dhidi ya nguvu za kuzimu, itaharibu maovu, itapunguza dhambi na kushinda kutofautiana
4. Itafanya fadhila kukua, kazi nzuri kuongezeka, itapatia roho huruma tele toka kwa MUNGU, itaondoa hamu ya wanadamu kupenda mambo ya dunia na majivuno yake na kufanya wapende zaidi mambo ya mbinguni. Ooh, ni kwa namna gani roho hizo zitajifurahisha na kubarikiwa kwa namna hii.
5. Roho zitakazojikabidhi kwangu kwa njia ya kusali rozari, kamwe hazitapotea.
6. Yeyote atakayesali rozari kwa uaminifu huku akiyatafakari matendo makuu ya rozari, kamwe hatashindwa na ubaya. MUNGU hatamwadhibu katika hukumu yake, hatapotea katika kifo asichopangiwa na atabaki katika neema za MUNGU na kustahili kupata uzima wa milele.
7. Yeyote atakayekuwa mwaminifu katika kusali rozari, kamwe hatakufa bila ya kupokea Sakramenti takatifu za Kanisa.
8. Wote watakaokuwa waaminifu katika kusali rozari watadumu katika mwanga wa MUNGU katika maisha yao na saa yao ya kufa na kupata neema zake tele; katika saa yao ya kufa watashiriki fadhila za watakatifu waliopo peponi
9. Nitawatoa toharani wale wote waliokuwa waaminifu katika kusali rozari
10. Watoto wangu waaminifu katika kusali rozari watapata fadhila kuu ya utukufu Mbinguni.
11. Utapata yale yote unayoniomba kwa kusali rozari
12. Wote wale wanaoeneza rozari hii takatifu nitawasaidia katika mahitaji yao
13. Nimepata toka kwa mwanangu Mtukufu kuwa mawakili wote wa rozari takatifu watapata
waombezi toka baraza lote kuu la Mbinguni wakati wa maisha yao na wakati wa saa yao ya kufa.
14. Wote wanaosali rozari hii takatifu ni wanangu, na kaka na dada wa mwanangu wa pekee YESU KRISTO
15. Ibada kwa rozari takatifu ni ishara kuu ya kuelekea ukombozi

JE,SHERIA YA MAPADRE KUTOOA NA KUISHI USEJA IMEANDIKWA WAPI KATIKA BIBLIA AU IMETUNGWA TU NA PAPA?

Pengine umewahi kuulizwa swali hili wakati fulani.Na jibu lake ni kama ifuayavyo:
Mtu anapouliza kila kitu kimeandikwa wapi katika Biblia ni kudhihirisha kutokuijua au kuielewa vizuri Biblia Takatifu na historia yake.Mtu anapong’ang’ania “nionyeshe kitu fulani kimeandikwa wapi kwenye Biblia”ni kutaka kujiona ya kwamba yeye anaielewa sana Biblia na ameisoma yote kwa hiyo kila kitu kilichopo kwenye Biblia anakifahamu kumbe haijui Biblia bali anakariri Biblia!
Na hili suala la kushupalia swala la kuoa linadhihirisha jinsi gani tulivyo kizazi cha zinaa,ni kama tunadhani kuwa UZIMA upo katika kujamiiana!La hasha.
Paulo anasema “Kwasababu ya zinaa ni bora kuoa na kuolewa”(1Wakorintho 7:2.9) haya sio maneno ya kufurahia na kuchekelea tu maana “YANAWALENGA WALE WALIOSHINDIKANA KATIKA YALE YAPENDEZAYO”(1Wakorintho 7:1.8)sasa ni lazima tujiulize je tumeshindikana kiasi hicho?,hiyo sio sifa!
1Wakorintho 7:1.8
“Basi kwa habari ya mambo yale mliyoandika,ni heri mwanaume asimguse mwanamke,8.Lakini nawaambia wale wasiooa bado na wajane heri wakae kama mimi nilivyo”
Na Paulo Mtume anasema “Ni bora kuoa au kuolewa” lakini hakusema “Ni LAZIMA kuoa au kuolewa”
Suala la kutooa kwa mapadre kadiri ya historia lilianza tangu zamani kabisa mwanzoni mwa milenia ya pili katika mtagusi wa pili wa Laterani mwaka wa 1139 ili waweze kumtumikia Mungu kwa uhuru na bila mawaa wala pasipo vikwazo(1wakorintho 7:32-35)
1wakorintho 7:32-35
“32Lakini nataka msiwe na masumbufu.Yeye asiyeoa hujishughulisha zaidi na mambo ya Bwana ampendezeje Bwana;33.bali yeye aliyeoa hujishughulisha zaidi na mambo ya dunia hii,jinsi atakavyompendeza mkewe.34-Tena iko tofauti kati ya mke na mwanamwali.Yeye asiyeolewa hujishughulisha na mambo ya Bwana ili apate kuwa mtakatifu mwili na Roho.Lakini yeye aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya dunia hii,jinsi atakavyompendezesha mumewe.,35.Nasema hayo niwafaidie ninyi,si kwamba niwategee tanzi,bali kwaajili ya vile vipendezavyo,tena mpate kumhudumia Bwana pasipo kuvutwa na mambo mengine”
Maandiko hayo hapo juu yanajieleza wala sidhani kama yanahitaji kufafanuliwa zaidi ya yanavyojifafanua yenyewe.
Watu wengine wanafikiri kwamba kutooa ni dhambi,kama ni hivyo basi hata Yesu mwenyewe alikosa maana hata yeye mwenyewe hakuoa.
Yesu mwenyewe anafundisha kuhusu ubikira(Mathayo 19:10-12)
Mathayo 19:10-12,
“Wanafunzi wake wakamwambia,kama mambo ya mme na mke yakiwa hivyo ni afadhali kutuooa kabisa.Lakini Yeye akawaambia ‘SI WOTE WAWEZAO KULIPOKEA NENO HILO,ILA TU WALE WALIOJALIWA,maana wako MATOWASHI waliozaliwa katika hali hiyo toka matumboni mwa mama zao;tena wako matowashi waliofanywa na watu kuwa matowashi,tena wako Matowashi WALIOJIFANYA WENYEWE KUWA MATOWASHI KWAAJILI YA UFALME WA MBINGUNI’,awezaye kulipokea neno hili na alipokee”
Yesu mwenyewe analifafanua jambo hili kwa mapana,katika orodha ya matowashi Yesu aliowataja,Mapadre ni Matowashi waliojifanya hivyo kwaajili ya huduma ya kanisa na ufalme wa Mungu.
Tena Yesu anatuambia waziwazi kwamba”sio wote wawezao kulipokea neno hilo”yaani sasa sio wote wawezao kuwa Matowashi(Mapadre)bali ni wale tu waliojaliwa na Mungu neema hiyo.wale wasioweza kuishi upadre huoa na kuwa na familia.Tena Yesu anamalizia kwa kusema “Awezaye kulipokea fundisho hili na alipokee”,kwa maana nyingine ni kusema “Fundisho au Utowashi huu sio wa lazima”anayeweza kuishi maisha hayo basi na ayapokee na yule asiyeweza basi aache!
Vilevile Mitume ili kumfuata Yesu kikamilifu waliyaacha yote waliokuwa nayo ikiwepo familia zao ili wamtumikie Bwana(Mathayo 19:27.29)
Mathayo 19:27.29:
“Ndipo Petro akajibu akamwambia ‘Tazama sisi tumeacha vyote tukakufuata wewe,tutapata nini basi?29.Amini nawaambia,kila mtu aliyeacha nyumba au ndugu wa kiume au wakike,au baba au mama au watoto au mashamba KWAAJILI YA JINA LANGU,atapokea mara mia zaidi na kuurithi uzima wa milele”
katika injili hiyo,Yesu anadhihirisha kwamba aliyeacha hayo yaliotajwa si kwasababu hawezi kuyapata la hasha,bali ameyaacha hayo yote KWAAJILI YA JINA LA YESU atapokea mengi hapa duniani halafu tena ataurithi ufalme wa mbinguni.
Mapadre wameyaacha hayo yote,wameacha nyumba,familia zao na kila kitu SIO KWASABABU HAWANA UWEZO AU HAWAWEZI KUPATA MAMBO HAYO bali WAMEACHA KWASABABU YA KUMTUMIKIA MUNGU KWA KADIRI YA MAANDIKO MATAKATIFU na kwakutaka kwao kuyaishi kimamilifu MASHAURI YA INJILI ikiwepo USEJA.
Maneno ya Paulo na yale ya Yesu mwenyewe kuhusu kumtumikia Mungu bila kuoa sio ya bahati mbaya bali ndiyo njia bora na inayofaa sana na kukubalika mbele ya Mungu.
Kwahiyo unapowaona mapadre hawaoi ujue sababu yake ni hiyo kwamba “Wamejitoa kwaajili ya kulihudumia kanisa”
(Na pia huwa nawashangaa mno watu wanaowapiga vita Mapadre kwamba kwanini hawaoi,najiuliza je,hao Mapadre wamewakataza wao kwamba wasioe?.)..na kama jibu ni hapana,sasa Je,”Pilipili ya shamba usiyoila inakuwashia nini?”
TUMSIFU YESU KRISTO!

Majivuno na Kujikweza Mbele ya Mungu

Rejea Luka 14:7-24 na Luka 18 :9-18
Mungu anakawaida ya kumkweza yoyote ajishushaye na kumshusha yule ajikwezaye. Vile unavyojiona bora mbele ya Mungu na mbele ya watu ndivyo na Mungu anatakavyokuonyesha kuwa wewe sio bora au wewe sio zaidi ya wengine.

Madhara ya Kujikweza au majivuno

1. Sala zako hazitajibiwa kwa kuwa mara zote nia ya sala zako zitakua ni za kujitakia makuu.
2. Kusahau nafasi ya Mungu katika maisha yako na kuhisi unajitosheleza kwa yote.
3.Kusahau nafasi na umuhimu wa wengine kwa kuhisi kuwa hawana thamani kama wewe.

Dalili za Kujikweza au majivuno

1.Kutaka au kupenda kuwa na nafasi ya kwanza kwenye kila kitu.
2. Kukosa uvumilivu
3. Kuwa na hofu ya kushindwa na kufedheheshwa
4.Kukosa upendo na kujali kwa wengine
5. Kupungua imani kwa Mungu. Yani kuhisi kama Mungu anaweza kufanya au hawezi.
6. Kupungua ukaribu wako kwa Mungu.
7.Kutokupenda kusali /kuomba Mungu.

Dawa ya majivuno au jinsi ya kujishusha

1.Kujifunza unyenyekevu.
2.Kujifunza upendo wa kweli kwa Mungu na wengine.
3. Jifunze kuwaombea wengine. Hii itasaidia kujenga unyenyekevu.
4. Kujifunza kuridhika
5. Jifunze kufurahia mafanikio ya wengine.
6. Usiwe muongeaji sana na mchunguzi wa mambo ya watu sana.

Shopping Cart