Upishi na Maandalizi ya Milo yenye Afya

Mapishi ya Wali Wa Nyanya Wa Kukaanga

Vipimo

Mchele basmati, pishori – 3 vikombe

Vitunguu katakata – 2

Nyanya/tungule katakata – 5 takriban

Viazi/mbatata menya katakata – 3 kiasi

Thomu (saumu/garlic) ilosagwa – 1 kijiko cha supu

Bizari mchanganyiko – 1 kijiko cha kulia

Hiliki ya unga – ½ kijiko cha chai

Kidonge cha supu – 2

Chumvi – kisia

Mafuta – ½ kikombe

Maji ya moto au supu – 5 takriban

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha na roweka mchele
Katika sufuria weka mafuta yashike moto, tia viazi, vitunguu ukaange.
Vikianza tu kugeuka rangi tia thomu na bizari, hiliki, endelea kukaanga kidogo.
Tia nyanya kaanga lakini usiache zikavurugika sana.
Tia mchele ukaange chini ya dakika moja.
Tia maji ya moto, na kidonge cha supu au supu yoyote kiasi cha kufunika mchele yazidi kidogo.
Koroga vichanganyike vitu, kisha funika upike kama pilau.
Pakua ikiwa tayari, tolea kwa samaki wa kukaanga au kitoweo chochote kile

Mapishi ya Wali Wa Kichina Wa Kuku Na Mboga Mchanganyiko

Vipimo

Mchele wa basmati/pishori – 4 vikombe vikubwa (mugs)

Kuku – 2

Vitnguu vya kijani (sprin onions) katakata – 5 miche

Maharage machanga (spring beans) katakata – kiasi kujaza mug moja

Pilipili boga la (capsicum) katakata – 1

Karoti katakata vipande virefu – 1

Kitunguu thomu (garlic) kuna (grate) – 1 kubwa

Tangawizi mbichi kuna (grate) – 1 kubwa

Sosi ya soya (soy sauce) – 2 vijiko vya supu

Kidonge cha supu – 1

Mafuta ya kupikia – ¼ kikombe cha chai

Chumvi – kiasi

Pilipili manga – 1 kijiko cha supu

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha kuku vizuri, katakata vipande, weka katika sufuria, tia chumvi, pilipili manga, mfunike, umkaushe motoni huku ukimgeuza geuza.

Roweka mchele kisha uchemshe uive nusu. Chuja maji, tia siagi kidogo ili usigandane.

Weka karai ya kupika mboga (wok) au sufuria kisha tia mafuta yashite moto.

Tia kitunguu thomu, tangawizi, kaanga kidogo.

Tia mboga zote, ulizokatakata.

kaanga kidogo, kisha tia sosi ya soya na kidonge cha supu. Usizipike sana mboga mpaka zikalainika mno. Sababu zitaiva katika mchele

Changanya kuku na mboga kisha changanya vyote katika mchele, urudishe katika moto.

Funika upike hadi uive kamilifu.

Pakua kwenye sahani.

Jinsi ya kupika Mseto Kwa Mchuzi Wa Samaki Wa Nazi

Vipimo vya mseto

Tanbihi: Kiasi ya vipimo inategemea wingi wa watu, unaweza kupunguza au kuongeza. Hiki ni kiasi cha watu 6 takriban.

Chooko – 3 Vikombe

Mchele – 2 Vikombe

Samli – 2 vijiko Vya supu

Chumvi – kiasi

NAMNA YA KUTAYARISHA NA KUPIKA

Safisha na kosha chooko utoe taka taka zote.
Osha mchele kisha roweka pamoja na chooko kwa muda wa saa au zaidi.
Pika chooko na mchele ukiongeza maji inapohitajika, tia chumvi, funika pika moto mdogo mdogo huku unakoroga kwa mwiko kila baada ya muda huku unaponda ponda.
Karibu na kuwiva na kupondeka tia samli endelea kupika hadi karibu na kukauka. Epua.

Samaki

Vipande vya samaki (nguru) – 6 – 7 (4LB)

Kitunguu saumu na tangawizi iliyosagwa – 2 vijiko vya supu

Pilipili ya unga nyekundu – 1 kijiko cha supu

Pilipili mbichi iliyosagwa ukipenda – 1 kijiko cha chai

Bizari ya samaki – 1 kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Ndimu – kiasi

Mafuta ya kukaangia – kiasi

Namna Ya Kutaysha Na Kupika

Changanya thomu/tangawizi, pilipili, bizari, chumvi pamoja na ndimu iwe masala nzito.
Paka vipande vya nguru kwa masala hayo weka akolee dakika kumi hivi.
Kaanga vipande vya nguru katika mafuta madogo kwenye kikaango (fyring pan) uweke upande.

Mchuzi Wa Nazi

Vitunguu maji – katakata vidogodogo – 4

Nyanya zilizosagwa (crushed) – 3- 4

Nyanya kopo – 1 kijiko cha chai

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Bizari ya mchuzi – 1 kijiko cha chai

Bamia zilizokatwa ndogo ndogo – 2 vikombe

Chumvi – kiasi

Ndimu – 2 vijiko vya supu

Tui la nazi – 3 Vikombe au 800 ml

Namna Ya Kupika

Katika karai au sufuria, tia mafuta ukaange vitunguu hadi vianze kugeuka rangi.
Tia nyanya zilizosagwa, nyanya kopo, uendelee kukaanga, kisha tia bizari, chumvi.
Tia nazi na mwisho tia bamia uache ziwive kidogo tu.
Tia vipande vya samaki vilivyokwisha kaangwa.
Tayari kuliwa na mseto upendavyo.

Vidokezo:

Bizari nzuri kutumia ni ya ‘Simba Mbili’ inaleta ladha nzuri katika mchuzi.
Ni bora kupika mchuzi kwanza kabla ya mseto kwani mseto ukikaa kwa muda unazidi kukauka.

Jinsi ya kupika Biriani ya Nyama Ng’ombe Na Mtindi

Mahitaji

Mchele wa biriani – 5 gilasi

Nyama ya ngombe ya mifupa – 1 ½ kilo na nusu

Vitunguu – 2 kilo

Tangawizi mbichi – ¼ kikombe

Thomu (saumu/garlic) – 3 vijiko vya supu

Mtindi – 2 vikombe

Nyanya ilokatwakatwa (chopped) – 3

Nyanya kopo – 1 kikombe

Masala ya biriani – 2 vijiko vya supu

Hiliki ya unga – 2 vijiko vya chai

Pilipili mbichi ilosagwa – 3 kiasi

Kotmiri ilokatwakatwa – 1 msongo (bunch)

Rangi ya biriani ya manjano – ½ kijiko cha chai

Zaafarani au zaafarani flavour – 1 kijiko cha supu

Mafuta ya kukaangia

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Katakata vitunguu ukaangae katika mafuta mpaka vigeuke rangi ya brown ilokoza.
Weka nyama iwe ilokatwakatwa katika treya au bakuli kubwa la oveni.
Chaganya pamoja na tangawizi, thomu, nyanya, nyanya kopo, mtindi, masala ya biriani, chumvi, pilipili.
Acha irowanike kwa muda wa masaa mawili takriban.
Funika kwa karatasi ya jalbosi (foil paper) utie katika oveni upike muda wa dakika 45 takriban mpaka nyama iwive na huku unachanganya changanya sosi. Ikiwa ina maji ongezea nyanya kopo iwe nzito.
Epua funua, kisha vuruga vitungu umwagie pamoja na kotmiri na umwagie mafuta ya moto kiasi.
Ongezea kutia masala ya biriani na hiliki ya unga.
Chemsha mchele nusu kiini, mwaga maji chuja, umwagie juu ya sosi ya nyama ukipenda kuchanganya au chemsha wali pekee.
Nyunyizia rangi ya biriani pamoja na zaafarani flavour au zaafarani yenyewe ukipenda.
Mimina mchele juu ya masala ya nyama, funika urudishe ndani ya oven upike muda wa kiasi ya dakika ishirini.
Epua upake kwa kuchota wali kwanza kisha masala uwekee juu yake, kiwa tayari.

Jinsi ya kuandaa Ndizi Mbichi Za Supu Ya Nyama Ng’ombe

Mahitaji

Ndizi mbichi – Kisia

Nyama ng’ombe – ½ kilo

Pilipili ya kusaga – 1 kijiko cha chai

Tangawizi ya kusaga – 2 vijiko vya supu

Thomu (garlic/saumu) – 1 kijiko cha supu

Bizari mchuzi – 1 kijiko cha chai

Nazi ya unga (ukipenda kuongezea) – 2 vijiko cha supu

Chumvi – Kiasi

Ndimu – 1 kamua

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Weka nyama ng’ombe katika sufuria, tia tangawizi, thomu, pilipili mbichi, bizari, chumvi. Roweka kidogo ukipenda kisha ikaushe yenyewe kwa maji yake
Ongezea maji ya kiasi yasizidi mno, kisha funika na chemsha.
Menya ndizi, ukatekate.
Nyama ikikaribia kuiva, weka ndizi uendelee kupika mpaka viive vyote.
Tia nazi ya unga kidogo tu ukipenda. Koleza kwa bizari mchuzi, pilipili, na ndimu
Epua mimina katika chombo cha kupakulia zikiwa tayari.

Shopping Cart