Upishi na Maandalizi ya Milo yenye Afya

Jinsi ya kupika Magimbi Kwa Nyama Ya Ng’ombe

Vipimo

Majimbi (Eddoes) kiasi 6 au 7

Nyama ng’ombe ½ kilos

Tangawizi ilosagwa 1 kijiko cha kulia

Haldi (bizari manjano/turmeric) ½ kijiko cha chai

Tui zito la nazi vikombe 2

Chumvi kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Safisha nyama kisha weka chumvi, bizari ya manjano, tangawizi mbichi, ukaushe kwanza katika sufuria kwa kukaanga kaanga.
Ikianza kukauka, weka maji funika uchemshe iwive.
Menya majimbi ukate kate na uweke katika sufuria nyengine.
Mimina supu na nyama katika majimbi uchemshe yawive majimbi.
Mwisho weka tui zito la nazi uchanganye vizuri kisha weka katika moto kidogo tu bila kufunika yakiwa tayari.

Mapishi ya Wali Mweupe Kwa Mchuzi Wa Kuku Wa Balti

Vipimo

Kuku 1 mkate vipande vipande

Vitunguu 3 katakata (chopped)

Nyanya 5 zikatekate (chopped)

Tangawizi mbichi ilokunwa au ilosagwa 1 kijiko cha kulia

Thomu (kitunguu saumu) kilosagwa kijiko 1 cha kulia

Bizari mchanganyiko (garam masala) kijiko 1 cha chai

Jira/bizari ya pilau (cummin powder) kijiko 1 cha chai

Dania/gilgilani ilosagwa (coriander powder) kijiko 1 cha chai

Mtindi/maziwa lala (yoghurt) vijiko vya kulia 4 mjazo au paketi moja ndogo.

Malai ya kupikia (cooking cream) kikombe 1

Kasuri methi (majani makavu ya uwatu/dried fenugreek leaves) 1 kijiko cha kulia

Mafuta ya kupikia ½ kikombe

Chumvi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha kuku vizuri mwache achuje maji.
Weka mafuta katika sufuria kaanga vitunguu mpaka vianze kugeuka rangi ya brown hafifu. Kisha tia tangawizi na thomu ukaange.
Tia kuku ukaange mpaka ageuke mweupe kisha tia nyanya endelea kukaanga ziwive.
Piga mtindi vizuri katika kibakuli uwe nyororo.
Epua sufuria weka kando kisha tia mtindi uchanganye vizuri pamoja na kuku.
Rudisha katika moto acha uchanganyike na kuku kidogo kisha mwagia malai ya kupikia (cooking cream)
Tia kasuri methi/majani makavu ya uwatu yaliyovurugwa. Acha katika moto dakika 1 tu.
Epua umimine katika chombo na nyunyizia ikiwa tayari kuliwa na wali mweupe.

Mapishi ya Ugali Mchuzi Wa Samaki Nguru Wa Nazi Na Bamia Za Kukaanga

Vipimo Vya Ugali:

Unga wa mahindi/sembe – 4

Maji – 6 takriban

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Chota unga kidogo katika kibakuli uchanganye na maji kidogo .
Weka maji mengineyo katika sufuria kwenye moto.
Changanya na mchanganyiko mdogo ufanya kama uji.
Kisha kidogo kidogo unaongeza sembe huku unakoroga na kuusonga ugali hadi uive.

Vipimo Vya Mchuzi Wa Samaki Wa Nazi

Samaki nguru – 5 vipande

Pilipili mbichi ilosagwa

Kitunguu maji kilosagwa – 1 kimoja

Nyanya ilosagwa – 2

Haldi/tumeric/bizari ya manjano – ¼ kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Ndimu – 2 kamua

Tui la nazi zito – 2 vikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Baada ya kumuosha samaki, weka katika sufuria.
Tia chumvi, ndimu, pilipili mbichi ilosagwa.
Tia vitunguu na nyanya zilosagwa
Mkaushe kwa hivyo viungo, akianza kukauka tia tui la nazi.
Acha kidogo tu katika moto tui liwive mchuzi ukiwa tayari.

Vipimo Vya Bamia

Bamia – ½ kilo takriban

Nyanya kopo – 1 kijiko cha chai

Methi/uwatu/fenugreek seeds ilosagwa – 1 kijiko cha chai

Dania/corriander ilosagwa – ½ kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Mafuta – 1 kikombe cha kahawa

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Katakata bamia kwa urefu.
Weka mafuta katika karai, kisha tia bizari zote na nyanya kopo, kaanga kidogo.
Tia bamia endelea kukaanga, kisha acha katika moto mdogomdogo ufunike.
Kila baada ya muda funua karai ukaange bamia hadi ziwive zikiwa tayari.

Mapishi ya Biriani Nyepesi Kupika Ya Samaki

Vipimo

Mchele wa pishori (basmati) – 4

Vitunguu katakata – 3

Nyanya (tungule) katakata vipande vikubwa – 3 -5

Pilipili boga la kijani (capsicum) katakata

Supu ya kitoweo au vidonge vya supu – 1

Bizari mchanganyiko Garama masala – 5-7

Pilipili mbichi ya kusaga – Kiasi

Zaafarani ya maji (flavor) – 1 kijiko cha chakula

Mafuta ya kupikia – ¼ kikombe

Samaki wa kukaanga

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Roweka mchele kiasi nusu saa kisha chemsha mchele kwa supu uive nusu kiini. Mwaga maji chuja.
Wakati mchele unapikika, weka mafuta katika sufuria kubwa ya kupikia wali, kaanga vitunguu mpaka vigeuke rangi ya hudhurungi.
Tia nyanya na vitu vinginevyo vyote kaanga kidogo tu.
Mwaga wali katika sufuria na nyunyizia zaafarani kisha changanya na masala vizuri.
Funika upike katika oven (bake) au juu ya stovu moto mdogo mdogo kiasi dakika 15- 20.
Epua ikiwa tayari, pakua kwenye sahani kisha tolea kwa samaki wa kukaanga.

Mapishi ya Pilau Ya Nyama Ya Ng’ombe Na Nyanya

Vipimo

Mchele (Basmati) – 3 vikombe

Nyama ya ngo’mbe – 1 kg

Pilipili boga – 1 kubwa

Nyanya – 2 kubwa

Vitunguu maji – 2 vikubwa

Kitunguu saumu(thomu/galic) iliyosagwa – 1 kijiko cha supu

Tangawizi – 1 kijiko cha chai

Ndimu – 1

Mafuta ya kupikia – ½ kikombe

Mdalasini – ½ kijiko cha chai

Binzari nyembamba – 1 kijiko cha chai

Pilipili manga – ½ Kijiko cha chai

Hiliki – ½ Kijiko cha chai

Namna ya kutayarisha na Kupika

Roweka mchele wako katika chombo

Chukuwa nyama na ioshe vizuri na itie thomu, tangawizi, ndimu, pilipili manga na chumvi kiasi

Iweke jikoni hadi ikauke maji na kuwa imewiva huku ukiikaanga kaanga kwa hayo hayo mafuta yake hadi kuwa rangi ya hudhurungi

Katakata Vitunguu na nyanya weka pembeni

Chukua pilipili boga, thomu, tangawizi na visage katika mashine ya kusagia

Weka sufuria pembeni na utie mafuta, subiri yapate moto

Kisha tia vitunguu na vikaange hadi kuwa hudhurungi na tia nyanya

Kisha mimina mchanganyiko wako ulio usaga wa pilipili boga, thomu na tangawizi

Koroga kwa dakika kadhaa Kisha mininia nyama uliyokuwa tayari, maji kiasi na chumvi wastani na subiri maji hayo yachemke

Weka mchele humo na koroga kiasi na onja chumvi kama ipo sawa au kama ndogo unaweza kuongeza

Funika na punguza moto na uache uive taratibu

Baada ya kukauka maji kabisa basi ugeuze na subiri tena kwa dakika kama mbili na tayari kuliwa.

Shopping Cart