Upishi na Maandalizi ya Milo yenye Afya

Mapishi ya Chicken Curry

Leo wapendwa nitaenda kuzungumzia mapishi ya mchuzi wa kuku (chicken curry).

Mahitaji

Kuku mzima
Nyanya kubwa 3
Karoti mbili
Pilipili hoho
Kotmiri
Tangawizi
Kitunguu maji
Kitunguu saumu kidogo
Ndimu
Mafuta ya kupikia
Chumvi (pilipili ukipenda)

Matayarisho

1. Menya vitunguu saumu na tangawizi na uvitwange pamoja.
2. Katakata kuku vipande vidogo kisha ukamulie ndimu na kupaka mchanganyiko wa tangawizi na vitunguu saumu (kiasi tu).
3. Katakata vitunguu maji na pilipili hoho uweke pembeni.
4. Grind (Kwangua) kwenye grater nyanya na karoti pia uweke pembeni.
5.Katakata kotmiri vipande vidogo uweke pembeni.
6. Andaa kikaango na jiko.

Mapishi

1. Bandika kikaango jikoni na mafuta kiasi, yakishachemka weka vitunguu maji na kaanga hadi vimelainika na kuiva (hakikisha haviungui).
2. Weka pilipili hoho na karoti na endelea kukoroga hadi vyote viive na kulainika, Kisha weka chumvi.
3. Sasa weka vipande vya nyama koroga na funikia kwa dakika 3, kisha weka nyanya zako ulizo grind na koroga ili zichanganyike vizuri, vikishachanganyika weka kotmiri na pilipili kama utapenda. Acha vichemke kwa dakika 5. Hakikisha moto sio mkali sana.
4. Angalia kama nyama zimeiva vizuri kisha epua mchuzi wako.
5. Pakua kwenye bakuli na katakata kotmiri uweke kwa juu.
Unaweza kula kwa ugali, wali, ndizi rost au chipsi.

Mapishi – Fish Finger

Leo tunaangalia mapishi ya fish finger ( sijui kama unaweza kusema kidole cha samaki)!, Ni mlo mzuri hasa kuliwa kama kitafunio au mboga ya pembeni.

Mahitaji

500g Fileti ya samaki
120g Chenga za mkate
100g Unga wa ngano
Mayai 2
Ndimu 1
Kitunguu saumu 1
Kotmiri
Mafuta ya kupikia

Matayarisho

Menya vitunguu saumu kisha visage

Katakata fileti kwa muundo wa mraba (kama vidole) kisha paka mchanganyiko wa vitunguu saumu

Kata ndimu na kamulia kwenye fillet yako

Weka chenga za mkate kwenye bakuli kisha uchanganye chumvi kiasi na kata kata kotmiri majani 3 na uchanganye pamoja.

Kwenye bakuli lingine weka mayai na uyapigepige yawe kama uji mzito

Weka unga kwenye bakuli jingine.

Chukua kipande cha fillet kiweke unga kidogo kisha kizamishe kwenye yai na baada ya hapo kizamishe kwenye mchanganyiko wa chenga za mkate. Fanya hivyo kwa vipande vyote.

Weka mafuta kwenye kikaago na subiri yachemke kisha weka fillet zako vizuri na zikaange pande zote hadi zimekuwa rangi ya brown ( hakikisha moto sio mkali sana).

Epua na weka pembeni mafuta yote yakauke

Weka kwenye sahani tayari kwa kula.

Mapishi – Mayai Mchanganyiko, Tosti na Soseji

Karibu tena jikoni, leo tunaandaa vitafunwa kwa ajili ya kifungua kinywa asubuhi.

Mahitaji

Mayai 3
Soseji 2
Mkate slesi 2
Mafuta ya kupikia vijiko 2
Chumvi

Matayarisho

Piga piga mayai vizuri kwenye bakuli na weka chumvi kidogo kisha weka kikaango kwenye moto na mafuta kidogo.

Kikisha pata moto miminia mchanganyiko wa mayai na uanze kukorogo pale tu unapomiminia, endelea kukoroga hadi uone yanakuwa magumu na kuanza kuiva. Pika kwa kiwango unachopendelea na kusha epua na weka kwenye sahani.

Weka mafuta kijiko kimoja kwenye kikaango na kisha weka soseji zako na uzipike kiasi pande zote kisha epua na weka pembeni.

Weka slesi za mikate kwenye toster na zikiwa tayari unaweza weka siagi ili kuongeza ladha na mvuto.
Andaa mlo wako pamoja na juice, maziwa au chai.

Mapishi – Saladi ya Matunda

Matunda ni mojawapo wa kundi la vyakula, ni muhimu sana kwa afya bora. Matunda yakitengenezwa vizuri yanavutia sana na yanakuwa ni chakula kizuri sana.

Mahitaji

Embe iliyoiva kiasi
Nanasi
Tango
Tikiti maji
Zabibu
Papai

Matayarisho

1. Ondoa maganda kwenye embe, nanasi, tango, papai na tikiti maji kisha kata kata vipande vidogo vidogo vya mraba

2. Changanya vipande vya matunda kwenye bakuli safikisha weka na zabibu zilizotolewa kwenye kikonyo chake.

3. Weka kwenye friji yapate ubaridi kidogo

4. Saladi yako tayari kwa kuliwa

Waweza kula saladi hii kama mlo wa kati au kama mlo kamili wa usiku.

Mapishi – Kisamvu cha Karanga

Mapishi yetu leo ni kisamvu cha kuchanganya na karanga. Karibu.

Mahitaji

Majani ya kisamvu
Karanga nusu kikombe
kitunguu kimoja
nyanya mbili
karoti moja
mafuta na chumvi kiasi

Matayarisho

1. Osha kisamvu chako vizuri kisha katakata vipande vidogo vidogo

2. Unaweza kutwanga kwa kutumia kinu au kuchemsha kidogo na kisha kusaga kwa kutumia mashine. Ukitumia mashine uwe makini usije ukasaga sana ukaharibu.

3. Kaanga karanga kidogo na kisha zisage ziwe unga unga.

4. Chemsha kisamvu chako hadi kiive.

5. Katakata kitunguu, karoti na na nyanya

6. Anza kuunga kisamvu kwa kukaanga vitunguu, weka karoti na kisha nyanya na vikishaiva weka kisamvu na koroga pamoja kisha weka karanga. Acha vichemke kwa muda na unaweza pia weka na nazi tui la kwanza.

7. Baada ya muda mfupi epua na kitakiwa tayari. Waweza kula kwa ugali, wali, chapati, makande n.k

Shopping Cart