Upishi na Maandalizi ya Milo yenye Afya

Mapishi ya Wali Wa Kichina Wa Kamba Na Kuku

MAHITAJI

Mchele wa pishori (basmati) – 4

Nyama ya kuku bila mafupa – 1 Lb

Kamba saizi kubwa – 1Lb

Mchanganyiko wa mboga – njegere, karoti,

mahindi, maharage ya kijani (spring beans) – 2 vikombe

Figili mwitu (Cellery) – 2 mche

Vitunguu vya majani (spring onions) – 4-5 miche

Kebeji – 2 vikombe

Pilipili ya unga nyekundu – 1 kijiko cha chai

Pilipili manga ya unga – 1 kijiko cha chai

Sosi ya soya – 3 vijiko vya supu

Mafuta – 1/4 kikombe

Chumvi – kiasi

MAPISHI

Osha na roweka mchele.
Tia kamba chumvi na pilipili nyekundu ya unga. Tia mafuta vijiko viwili katika kikaango (frying pan), kaanga kamba kidogo tu, weka kando.
Katakata kuku vipande vidogo vidogo, tia chumvi na pilipili manga. Kaanga kaTika kikaango (ongeza mafuta kidogo) Weka kando.
Katika karai, tia mafuta kidogo kama vijiko vitatu vya supu, tia kamba na kuku, tia mboga za mchanganyiko, sosi ya soya na chumvi, kaanga kidogo. (Kama mboga sio za barafu) itabidi uchemshe kidogo.
Katakata kebeji, figili mwitu (cellery) na vitunguu vya majani (spring onions) utie katika mchaganyiko. acha kwa muda wa chini ya dakika moja katika moto.
Chemsha mchele, tia mafuta kidogo au siagi, chumvi upikie uive nusu kiini, mwaga maji uchuje.
Changanya vyote na wali rudisha katika sufuria au bakuli la oveni, funika na upike kwa moto wa kiasi kwa muda wa dakika 15-20 takriban.
Epua na upakue katika sahani ukiwa tayari kuliwa.

Mapishi ya Pilau Ya Bilingani Na Kuku

Viambaupishi

Mchele wa basmati – 3 vikombe

Kuku – Β½

Bilingani – 2 ya kiasi

Viazi – 4

Vitunguu – 2

Kitunguu (thomu/galic) iliyosagwa – 2 vijiko vya supu

Pilipili mbichi iliyosagwa – 2

Chumvi – kiasi

Garama masala (mchanganyiko wa bizari) – 1 kijiko cha chai

Hiliki ya unga – ΒΌ kijiko cha chai

Mafuta ya kupikia wali – ΒΌ kikombe

Mafuta ya kukaangia viazi na bilingani – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika:

Osha mchele na roweka kwa muda kutegemea na aina ya mchele.
Kata kuku vipande upendavyo safisha
Kisha mchemshe kwa chumvi, pilipili iliyosagwa, thomu, na bizari mchanganyiko (garama masala).
Akiwiva kuku, mtoe weka kando, bakisha supu katika sufuria.
Menya na kata viazi kaanga weka kando.
Kata kata bilingani slesi nene kaanga, chuja mafuta weka kando.
Katika sufuria, kaanga vitunguu hadi vigeuke rangu ya hudhurungi. Tia vipande vya kuku, ukaange kidogo.
Tia supu ya kuku, mchele, tia hiliki, ufunike hadi karibu na kuwiva kabisa.
Tia viazi na bilingani uchanganye kidogo, kisha tia katika oven imalizike kupikika pilau humo au unaweza kuendelea kufunika juu ya jiko hadi pilau iwive.
Pakua katika sahani ikiwa tayari kuliwa kwa saladi ya mtindi.

Mapishi ya wali kuku wa Kisomali

Mahitaji ya wali

Mchele – 3 vikombe

Vitunguu (viliokatwa vidogo vidogo) – 2

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi iliyosagwa – 1 kijiko cha chai

Bizari ya pilau – 1 kijiko cha supu

Mdalasini – 1 kijiti

Hiliki – 3 chembe

Pilipili manga nzima – chembe chache

Siagi – Vijiko 2 vya supu

Chumvi – kiasi

Mahitaji kwa kuku

Kuku kidari (Breast) kata vipande vipande – 2 LB

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi iliyosagwa – 1 kijiko cha supu

Pilipili mbichi iliyosagwa – 1 kijiko cha supu

Kotmiri iliyokatwa ndogo ndogo – kiasi

Bizari ya pilau (cummin au jiyrah) – 1 kijiko cha chai

Pilipili kubwa tamu la kijani – 1

Pilipili kubwa tamu nyekundu – 1

(zikate vipande vipande)

Karoti iliyokunwa – 1 – 2

Chumvi – Kiasi

Mapishi ya Wali:

Roweka mchele kwa muda fulani kutegemea mchele
Katika sufuria tia mafuta na kaanga vitunguu hadi vibadilike rangi kidogo.
Tia thomu iliyosagwa, mdalasini, bizari ya pilau, hiliki, pilipili manga na chumvi, kaanga kidogo.
Tia mchele kaanga kidogo, kisha tia maji ya moto kiasi kutegemea na aina ya mchele kama kawaida ya kupika wali kama pilau.
Tia sigai, funika upikike wali hadi uwive.

Mapishi ya Kuku:

Mchanganye kuku pamoja na thomu/tangawizi iliyosagwa, chumvi, pilipili mbichi.
Katika karai tia mafuta yapate moto vizuri.
Mtie kuku, bizari ya pilau (jiyrah) na ukaange, karibu na kuiva tia vitunguu.
Tia mapilipili makubwa, kotmiri, na kaanga kwa dakika moja tu uzime moto na epua weka kando.

Mapishi ya Biriani Ya Samaki Nguru, Njegere Na Snuwbar (UAE)

Mahitaji

Mchele wa basmati – 4 cups

Samaki nguru (king fish) – 7 vipande au zaidi

Kitunguu – 5

Nyanya/tungule – 3

Njegere – 1 kikombe

Snuwbar (njugu za pine) – 1 kikombe

Viazi – 2 kata kata mapande makubwa

Tangawizi mbichi – 1 kijiko cha supu

Kitunguu saumu – 1 kijiko cha supu

Pilipili nyekundu – 1 kijiko cha chai

Bizari ya biriani/garama masala – 1 kijiko cha supu

Namna Ya Kupika:

Kaanga samaki mbali kwa viungo upendavyo umkoleze vizuri. Au choma (bake/grill) katika oveni ukipenda.
Weka mafuta katika sufuria, tia vitunguu kaanga hadi vigeuka rangi. Gawa sehemu mbili.
Sehemu moja bakisha katika sufuria kisha tia tangawizi mbichi na kitunguu thomu ukaange.
Tia nyanya kaanga kisha tia bizari zote endelea kukaanga, tia njegere, njugu za snuwbar na ndimu kavu.
Tia viazi ulivyokwishakaanga, na vitunguu vilobakia.
Tia mapande ya samaki, changanya na masala bila ya kumvuruga samaki.
Chemsha wali kisha mwagia juu yake, funika upike ndani ya oveni au mkaa hadi wali uive kama unavyopika kawaida ya biriani.
Epua pakua huku ukichanganya na masala ya samaki.

Jinsi ya kupika Pilau ya Nyama ya Kusaga Na Mboga Mchanganyiko

Mahitaji

Mchele – 2 Mugs

Viazi – 3

Nyama ya Kusaga – 1 Pound

Mboga mchanganyiko za barafu – 1 Mug

(Frozen vegetable)

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi – 2 vijiko vya supu

Garam masala – 1 kijiko cha supu

Nyanya – 1

Kitungu maji – 1

Mdalasini nzima – 1 vijiti

Karafuu – 3 chembe

Pilipili mbichi – 1

Chumvi – kiasi

Maji – 2 Β½ Mugs

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha mchele na uroweke kiasi kutegemea aina ya mchele.
Katakata viazi kaanga katika mafuta, toa weka kando.
Tia mafuta katika sufuria, kaanga kitunguu maji mpaka kigeuke rangi ya hudhurungi (brown).
Tia nyama ya kusaga, thomu na tangawizi, pilipili, bizari zote na chumvi. Kaanga hadi nyama iwive.
Katakata nyanya uliyokatakata itie katika mchanganyiko wa nyama na endelea kukaanga kidogo tu.
Tia mboga ya barafu (frozen vegetables)
Tia maji, kidonge cha supu.
Yatakapochemka tia mchele.
Punguza moto uwe mdogo funika kwa muda wa Β½ saa hadi wali ukauke na uwive. Utakuwa tayari kuliwa.

Shopping Cart