Mafundisho Kuhusu Bikira Maria

DOGMA ZA KANISA KATOLIKI KUHUSU BIKIRA MARIA.

Kuna mafundisho makuu manne
kumhusu Bikira Maria ambayo ni lazima
kila Mkatoliki ayasadiki kutokana na
ufunuo wa Mungu: 1. B. Maria
mkingiwa dhambi ya asili 2. B. Maria
Mama wa Mungu 3. B. Maria Bikira
daima 4. B. Maria kupalizwa mbinguni
mwili na roho

MKINGIWA DHAMBI YA ASILI

Malaika alimsalimia Maria “umejaa
neema” (Lk 1:28) maana ndiye tunda
bora la ukombozi ulioletwa na Yesu. Ni
imani ya Wakatoliki kwamba kwa stahili
za Mwanae alikingiwa asirithi kwa wazazi
dhambi ya asili na madonda
yanayotokana nayo, wala asitende
dhambi maisha yake yote. Kwa maneno
mengine, Bikira Maria tangu atungwe
mimba Mungu alimkinga na kila doa la
dhambi kwa kutazamia stahili za Yesu
Kristo aliye Mkombozi wa binadamu
wote. Ndiye aliyekombolewa kwa namna
bora kushinda viungo vyote vya Kanisa.
Maisha yake yote hakutenda dhambi
hata moja. Mapokeo ya mashariki
yanamuita “A Panagia” = “Mtakatifu tu”.
Dogma hiyo ilitangazwa na papa Pius IX
mwaka 1854, halafu mwaka 1858 Bikira
Maria alijitambulisha kama Mkingiwa
kwa Bernadeta Soubirous huko Lurdi
( Ufaransa ). Tena mwaka 1917 huko
Fatima ( Ureno ) aliwafunulia Lusia,
Fransisko na Yasinta Marto moyo wake
safi usio na doa.

MAMA WA MUNGU

Injili ya Yohane inaanza kwa kishindo,
“Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye
Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno
alikuwa Mungu” (Yoh 1:1). Huyo Mungu
Mwana alitwaa ubinadamu katika Bikira
Maria akazaliwa mtoto, jina lake Yesu,
maana yake Mungu Mwokozi. Huyo ni
binadamu kama sisi katika yote
isipokuwa dhambi. Ubinadamu wa Yesu
unategemea Nafsi yake ya Kimungu:
akisema, ‘Mimi’, ni kwa Nafsi yake hiyo.
Ndiyo maana aliwaambia Wayahudi,
“Kweli nawaambia, kabla Abrahamu
hajazaliwa, nalikuwepo” (Yoh 8:50).
“Kama vile Baba alivyo asili ya uhai,
ndivyo alivyomjalia Mwanae kuwa asili
ya uhai” (Yoh 5:26).
Mtume Paulo akaeleza, “Wakati
maalumu ulipotimia Mungu alimtuma
Mwanae aliyezaliwa na mwanamke” (Gal
4:4). Bikira Maria ni Mama wa Mungu
kwanzia wakati huo: tangu Bikira Maria
alipojaliwa kumchukua mimba, kumzaa,
kumnyonyesha na kumlea mtu ambaye
kwa asili ni Mungu. Cheo hicho
kimemuinua juu kuliko hata malaika.
“Malaika alimwambia, ‘Hicho
kitakachozaliwa kitaitwa Kitakatifu,
Mwana wa Mungu’” (Lk 1:35).
Dogma ilitangazwa mwaka 431 kwenye
Mtaguso wa Efeso uliomuita “Mzazi wa
Mungu”, ukisema Maria anastahili
kuitwa hivyo kwa sababu Mwana wa
milele wa Mungu, ambaye ni Mungu
sawa na Baba, alifanyika mtu toka
kwake. Akiwa mja mzito alishangiliwa:
“Umebarikiwa wewe katika wanawake,
naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa.
Limenitokeaje neno hili, hata mama wa
Bwana wangu anijilie mimi?” (Lk
1:42-43). Ungamo hilo la Elizabeti
likakamilishwa na Mtume Thoma
aliyemuambia Yesu mfufuka: “Bwana
wangu na Mungu wangu!” (Yoh 20:28).

BIKIRA NA MAMA

Wakristo na Waislamu wote wanakiri
kuwa Yesu alitungwa bila ya mchango
wa mwanamume. La ajabu zaidi katika
imani hiyo ni kwamba hata uzazi
wenyewe haukuondoa ubikira wake, bali
uliutakasa: ni Bikira daima. Ingawa akili
inasita, ni lazima kukiri na malaika,
“Hakuna lisilowezekana kwa Mungu” (Lk
1:38). Yosefu , ingawa kisheria alikuwa
mume wake, hakutenda naye tendo la
ndoa.
Ni imani ya Wakatoliki na Waorthodoksi
kuwa Mama wa Yesu anastahili kuitwa
“Bikira daima” kwa sababu alimchukua
mimba akiwa bikira, akamzaa bila ya
kupotewa na ubikira, akabaki bikira hadi
mwisho wa maisha yake. Hamu yake ya
kuwa bikira hata kisha kuchumbiwa
inajitokeza katika jibu alilompa malaika
aliyemtabiria mimba: “Litakuwaje neno
hili, maana sijui mume?” (Lk 1:35). Ni
kielelezo cha Wakristo ambao Mtume
Paulo aliwaandikia: “Nawaonea wivu,
wivu wa Mungu; kwa kuwa naliwaposea
mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira
safi” (2Kor 11:2), “mpate kumhudumia
Bwana pasipo kuvutwa na mambo
mengine” (1Kor 7:35).
Wanaosemwa katika Injili “ndugu zake
Yesu” si watoto wa Bikira Maria, bali
ndugu wa ukoo waliokuwa jirani sana
na familia hiyo takatifu. Kama Bikira
Maria angekuwa na watoto wengine,
Yesu angekuwa amefanya kosa la
kuwanyang’anya Mama yao na
kumfanya awe Mama wa mtume
Yohane alipomkabidhi msalabani,
“‘Mwana, tazama Mama yako’. Na tangu
saa ile huyo mwanafunzi alimchukua
akae nyumbani kwake” (Yoh 19:27).
Katika Agano Jipya yupo Yakobo
anayeitwa na mtume Paulo “ndugu yake
Bwana” (Gal 1:19): Yakobo huyo alikuwa
maarufu katika Kanisa la Yerusalemu
(Mdo 12:7; 15:13-21; 21:18-20; Gal
2:9). Yakobo huyo si mtume Yakobo
kaka yake Yohane (Lk 6:12-16), bali ni
Yakobo ndugu yake Yose na mama yao
kwenye Injili anaitwa “Maria mwingine”,
si Maria Mama wa Yesu. “Walikuwepo
pia wanawake waliotazama kwa mbali.
Miongoni mwao akiwa Maria
Magdalena , Salome na Maria mama wa
akina Yakobo mdogo na Yose” (Mk
15:40). Maria lilikuwa jina la kawaida
kwa Wayahudi: akina Maria wakiwa
wengi hivyo, tujue kuwatofautisha
kwenye Injili, ambazo zinamtaja Bikira
Maria kama “Mama wa Mungu”

KUPALIZWA MBINGUNI MWILI NA ROHO

Baada ya maisha haya ya duniani Bikira
Maria alipalizwa mbinguni mwili na
roho, ishara ya mwanamke mshindi.
“Ishara kubwa ikaonekana mbinguni,
ambapo mwanamke aliyevikwa jua , pia
na mwezi chini ya miguu yake, na taji la
nyota kumi na mbili juu ya kichwa
chake” (Ufu 12:1). Maneno ya shangilio
lake yametimia: Mungu “amewaangusha
wakuu katika viti vyao vya enzi; na
wanyonge amewakweza” (Lk 1:52).
Imani hiyo ya mapokeo ya kale,
yanavyoshuhudiwa na Mababu wa
Kanisa, ilitangazwa rasmi na Papa Pius
XII kwa niaba ya ma askofu wote mwaka
1950.

Je, Bikira Maria ni Bikira Daima au alizaa watoto wengine?

Jibu fupi ni kwamba Bikira Maria hakuzaa watoto wengine na hakuwa na watoto wengine zaidi ya Yesu
Hapo zamani hakuna mkristu au dehebu lolote lililokuwa linapinga kuwa Bikira Maria sio Bikira Daima hata Waprotestanti/walokole waliamini Bikira Maria ni Bikira Hata Baada ya Kumzaa Yesu. Kwenye Miaka ya 1400-1600 Watu wote wakwanza waliopinga Kanisa Katoliki walikubali kuwa Bikira Maria ni Bikira daima wakiwemo Martin Lutha aliyeanzisha kanisa la Lutheran, John Calvin aliyeanzisha Ulokole/Protestanti, Mchungaji Ulrich Zwingli, Heinrich Bullinger, and Thomas Cranmer. Kwa miaka zaidi ya 350 Waprotestant/walokole waliendelea kuamini kuwa Bikira Maria ni Bikira Daima.
Lakini baadae wakristo wengi walianza kupinga kuwa Bikira Maria ni Bikira Daima.

Tunaweza kuthibitisha kuwa Bikira Maria hakuzaa watoto wengine kwa kunukuu Biblia Kama ifuatavyo;

1. Bikira Maria Alikuwa Bikira Kabla ya kumzaa Yesu

Biblia inatuambia wazi kwamba Bikira Maria alikuwa Bikira Kabla ya kumzaa Yesu Kama tunavyosoma katika Luka 1:26-35
26 Mnamo mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu aende kwenye mji uitwao Nazareti huko Galilaya, 27 kwa msichana mmoja aitwaye Maria, mchumba wa mtu mmoja jina lake Yosefu, wa ukoo wa Daudi. 28 Malaika akamwendea, akamwambia, “Salamu Maria! Umejaliwa neema nyingi! Bwana yu pamoja nawe.” 29 Maria aliposikia maneno hayo alifadhaika sana, akawaza: maneno haya yanamaanisha nini? 30 Malaika akamwambia, “Usiogope Maria, kwa maana Mungu amekujalia neema. 31 Utachukua mimba, utamzaa mtoto wa kiume na utampa jina Yesu. 32 Yeye atakuwa mkuu na ataitwa Mwana wa Mungu Mkuu. Bwana Mungu atampa kiti cha mfalme Daudi, babu yake. 33 Kwa hivyo atautawala ukoo wa Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.” 34 Maria akamjibu, “Yatawezekanaje hayo, hali mimi ni bikira?” 35 Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakushukia, na uwezo wake Mungu Mkuu utakujia kama kivuli; kwa sababu hiyo, mtoto atakayezaliwa ataitwa Mtakatifu, Mwana wa Mungu. (Luka 1:26-35)

2. Biblia Haiwataji ndugu wa Yesu wakati Yosefu na Maria walipokimbilia Misri kumficha Yesu na wakati waliporudi

19 Baada ya kifo cha Herode, malaika wa Bwana alimtokea Yosefu katika ndoto kule Misri, 20 akamwambia, “Amka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake, urudi tena katika nchi ya Israeli, maana wale waliotaka kumwua mtoto huyo wamekwisha kufa.” 21 Basi, Yosefu aliamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake, akarejea katika nchi ya Israeli. 22 Lakini Yosefu aliposikia kwamba Arkelao mwanawe Herode alikuwa mfalme wa Yudea mahali pa baba yake, aliogopa kwenda huko. Naye baada ya kuonywa katika ndoto, alikwenda katika mkoa wa Galilaya, 23 akahamia katika mji uitwao Nazareti. Ndivyo yalivyotimia maneno yaliyonenwa kwa njia ya manabii: “Ataitwa Mnazare.” Matayo 2:19-23
Kama wangekuwepo wadogo zake Yesu Biblia ingetuambia kwamba walikuwa wapi wakati huo na walikuwa na Yesu au la.

3. Biblia haituambii kuwa Yesu alikua na wadogo zake alipokuwa na miaka 12

Wakati wa Maria, Yoseph na Yesu walipoenda Yerusalemu Yesu akiwa na miaka 12 Biblia haituambii kuwa Yesu alikuwa na wadogo zake na walikuwa wapi. Kumbuka walikuwa na Desturi ya kwenda Yerusalemu kila mwaka kwa ajili ya Pasaka familia nzima kama familia. Je hao watoto wengine walikuwa wapi. Kwa nini walikuwa na Yesu Mwenyewe? Maana yake ni kwamba Yesu hakuwa na Wadogo zake.
41 Wazazi wa Yesu walikuwa na desturi ya kwenda Yerusalemu kila mwaka wakati wa sikukuu ya Pasaka. 42 Mtoto alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili, wote walikwenda kwenye sikukuu hiyo kama ilivyokuwa desturi. 43 Baada ya sikukuu, walianza safari ya kurudi makwao, lakini Yesu alibaki Yerusalemu bila wazazi wake kuwa na habari. 44 Walidhani alikuwa pamoja na kundi la wasafiri, wakaenda mwendo wa kutwa, halafu wakaanza kumtafuta miongoni mwa jamaa na marafiki. 45 Kwa kuwa hawakumwona, walirudi Yerusalemu wakimtafuta. 46 Siku ya tatu walimkuta Hekaluni kati ya walimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. 47 Wote waliosikia maneno yake walistaajabia akili yake na majibu yake ya hekima. 48 Wazazi wake walipomwona walishangaa. Maria, mama yake, akamwuliza, “Mwanangu, kwa nini umetutenda hivyo? Baba yako na mimi tumekuwa tukikutafuta kwa huzuni.” 49 Yeye akawajibu, “Kwa nini mlinitafuta? Hamkujua kwamba inanipasa kuwa katika nyumba ya Baba yangu?” 50 Lakini wazazi wake hawakuelewa maana ya maneno aliyowaambia. 51 Basi, akarudi pamoja nao hadi Nazareti, akawa anawatii. Mama yake akaweka mambo hayo yote moyoni mwake. 52 Naye Yesu akaendelea kukua katika hekima na kimo; akazidi kupendwa na Mungu na watu. (Luka 2:41-52).
Kwa hiyo Biblia haionyeshi kuwa Yesu alikuwa na kaka na dada wakati akiwa na miaka 12. Kama wangekuwepo wangetajwa hapa kuwa walikuwa pamoja na Wazazi wao kama Yesu au walikuwa na Yesu wakati anapotea. Biblia haituambii chochote kwa hiyo wakati huo hapakuwa na wadogo zake Yesu.

4. Kukosekana kwa neneo “Binamu” kwenye lugha ya Yesu

Wakristu wa kwanza pamoja na Yesu aliongea Kiaramaiki au Kiebrania. Katika lugha zote hizo hakuna neno “Binamu” kwa hiyo mabinamu walijulikana kama dada na kaka wa mtu. Kwenye Agano jipya Neno kaka na Dada lilitumika pia kuwakilisha binamu.
Biblia inapotuambia kuwa Kaka na dada zake Yesu haimaanishi kaka wa kuzaliwa bali ndugu au Binamu
55 Je, huyu si yule mwana wa seremala? Je, mama yake si anaitwa Maria, na ndugu zake si kina Yakobo, Yosefu, Simoni na Yuda? 56 Na dada zake je, si wote wako hapa pamoja nasi? Basi amepata wapi haya yote?” (Mathayo 13:55-56)
Kwa hiyo wanaotajwa hapa ni ndugu wa Yesu kwa maana maneno kama; ndugu, kaka au dada lilitumika badala ya Binamu yaani mtoto wa shangazi au mjomba. Hapa juu Yosefu ametajwa kama kaka yake Yesu lakini tunajua kuwa Yosefu ni Baba yake Yesu. Baba na mwana hawawezi kuwa na jina sawa.

5. Biblia haitumii neno Ndugu, kaka au dada ikimaanisha ndugu wa kuzaliwa mama mmoja na baba mmoja

Sio mara zote Biblia imetumia neno Ndugu kumaanisha ndugu (Dada na Kaka) wa kuzaliwa yaani kaka na dada kwa mfano
Kwa kuangalia lugha ya Kiswahili na Kiingereza 1 Wakorintho 15:6 tunaona tafsiri tofauti.
KISWAHILI 6 Kisha aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano kwa mara moja; wengi wao wanaishi bado, lakini baadhi yao wamekwisha kufa.
ENGLISH 6 After that, he appeared to more than five hundred of the brothers and sisters at the same time, most of whom are still living, though some have fallen asleep.
Kwa hiyo hapa neno kaka dada na ndugu linaonekana wazi halikumaanisha ndugu au kaka wa damu.

6. Undugu wa Yakobo, Simoni, Yosefu na Yuda kwa Yesu Sio wa mtu na kaka zake

Wasemao kuwa Bikira maria alikuwa na wana zaidi ya Yesu wananukuu kifungu hiki;
55 Je, huyu si yule mwana wa seremala? Je, mama yake si anaitwa Maria, na ndugu zake si kina Yakobo, Yosefu, Simoni na Yuda? 56 Na dada zake je, si wote wako hapa pamoja nasi? Basi amepata wapi haya yote?” (Mathayo 13:55-56)
Kumbuka kulikuwa na Yakobo wawili wakati wa Yesu, Vifungu vifuatavyo yunaweza kuona kuwa kulikuwa na yakobo wawili ambao walikuwa ndugu za Yesu lakini sio kaka wa kuzaliwa kwa mama.
35 Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, walimwendea Yesu wakamwambia, “Mwalimu, tunataka utufanyie kitu tutakachokuomba.” (Marko 10:35)
55 Mahali hapo walikuwapo wanawake wengi wakitazama kwa mbali. Hao ndio wale waliomfuata Yesu kutoka Galilaya wakimtumikia. 56 Miongoni mwao walikuwa Maria Magdalene, Maria mama yao Yakobo na Yosefu, pamoja na mama yao wana wa Zebedayo. (Matayo 27:55-56)
Tunaweza kuona Undugu huu na Yesu kwa kusoma;
19 Lakini sikuwaona mitume wengine isipokuwa Yakobo, ndugu yake Bwana. (Wagalatia 1:19)
Lakini Yuda anasema;
1 Mimi Yuda, mtumishi wa Yesu Kristo, ndugu yake Yakobo, nawaandikia ninyi mlioitwa na Mungu na ambao mnaishi katika upendo wa Mungu Baba, na katika ulinzi wa Yesu Kristo. (Yuda 1:1)
Kwa hiyo Yakobo na Yohane walikuwa watoto wa Mama mwingine ambao baba yao ni Zebedayo. Na Yakobo na Yosefu walikuwa watoto wa Maria Mwingine. Kwa hiyo ni Yakobo wa wili wa Mama wengine Tofauti na Maria. Yuda alikuwa ni ndugu yake Yakobo. Yakobo vilevile alikuwa ndugu yake Yesu.
Kuthibitisha kuwa Hawa kina Mama ndio waliokuwa Mama zao kina Yakobo wote hao wawili na wengine tunaweza kusoma;
25 Karibu na msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mama yake, na dada ya mama yake, Maria mke wa Kleopa, na Maria Magdalene. (Yohana 19:25)
Kwa hiyo kwenye (Yohana 19:25) tunaona Kuwa ni kwenye Msalaba wa Yesu alikuwepo Mama yake Yesu (Bikira Maria), Dada yake Bikira Maria, Mke wa Cleopa na Maria Magdalena. Na kwenye (Matayo 27:55-56) wamwtajwa ni Mama za kina nani kama inavyoonekana kwenye kifungu kifuatachi;.
55 Mahali hapo walikuwapo wanawake wengi wakitazama kwa mbali. Hao ndio wale waliomfuata Yesu kutoka Galilaya wakimtumikia. 56 Miongoni mwao walikuwa Maria Magdalene, Maria mama yao Yakobo na Yosefu, pamoja na mama yao wana wa Zebedayo. (Matayo 27:55-56).
Kwa hiyo hii ina maanisha kulikua na wanawake watatu wenye majina sawa ya Maria waliokuwa chini ya Msalaba. Yakobo na Yuda walikuwa watoto wa Maria Mke wa Cleofasi, na sio Mama wa Yesu, na hivyo sio kaka za Yesu.

7. Yesu alimwacha Mama yake kwa Yohane kwa kuwa hakuwa na Kaka na dada wakumwachia mamaye

26 Yesu alipomwona mama yake, na karibu naye amesimama yule mwanafunzi aliyempenda, akamwambia mama yake: “Mama! Tazama, huyo ndiye mwanao.” 27 Halafu akamwambia yule mwanafunzi: “Tazama, huyo ndiye mama yako.” Na tangu saa ile huyo mwanafunzi alimchukua akae nyumbani kwake.
Ndiyo maana Bikira Maria tangu siku ile alihamia kwa Yohani kwa kuwa hakuwa na watoto wengine.
Melkisedeck Leon Shine

Editor: Melkisedeck Leon Shine. About Me | Contact Me | LinkedIn | TikTok | WhatsApp

Read and Write Comments
Shopping Cart