Makala za Tafakari za Melkisedeck Leon Shine

Vile unavyoweza kuwa DARAJA au KIKWAZO kwa wengine

Kwa namna unayoishi unaweza ukawa daraja au kikwazo cha wengine kuishi maisha ya Amani raha na fanaka.
Unaweza ukawa daraja kwa maana kwamba wewe unaweza kuwa sababu ya wengine kupata Baraka na neema za Mungu.
Unaweza kuwa kikwazo kwa maana kwamba unaweza kuwa wewe ni sababu ya wengine kutokupata Baraka na Neema za Mungu.

Kwa jinsi unavyoishi unaweza ukawa chanzo cha Baraka kwa wengine au chanzo cha matatizo na vikwazo kwa wengine.

Vile unavyoweza kuwa Daraja kwa Wengine

Unaweza kuwa daraja au njia ya wengine kupata neema na Baraka katika maisha yao kulingana na matendo yako mema na Ibada yako kwa Mungu.

Kwa ucha Mungu wako, watu wako unaowapenda sana wanaweza kubarikiwa na kupata neema za Mungu Pamoja na wewe. Wale watu unaochangamana nao watabarikiwa kwa sababu na wewe umebarikiwa.
Kwa mfano wewe kama ni mzazi mcha Mungu unaweza ukawa chanzo cha Baraka na neema kwa watoto wako na kwa mwenzi wako wa ndoa. Vivyo hivyo na kwa watoto, mtoto anaweza kuwa chanzo cha Baraka kwa wazazi wake.

Inawezekana kuna Amani katika familia yako kwa sababu tuu wewe ni miongoni mwa wanafamilia hiyo na hivyo Mungu ameachilia Amani katika familia yako kwa sababu tuu wewe upo pale na wewe ni mcha Mungu.

Unaweza kuona sasa wewe ni chanzo cha Baraka kwa wale watu wako wa karibu. Kwa sababu tuu wewe ni mcha Mungu, na wao wanabarikiwa pamoja na wewe. Mungu anapobariki familia yako na wao pia wanabarikiwa.

Kwa hiyo basi, unapolegalega katika ucha Mungu wako unaweza pia kusababisha kulegalega au kikwazo cha Baraka za wengine.

Vile unavyoweza kuwa Kikwazo kwa Wengine

Unaweza kuwa kikwazo au kizuizi cha wengine kupata neema na Baraka katika maisha yao kulingana na matendo yako mabaya na kukosa kwako kumcha Mungu.

Kwa kuacha kumcha Mungu, watu wako unaowapenda sana wanaweza kukosa kubarikiwa na kukosa neema za Mungu kwa sababu wewe unazuia Baraka hizo. Wale watu unaochangamana nao watakosa Baraka kwa sababu umeandikiwa kutokubarikiwa na wanachanganyikana na asiyestahili kubarikiwa.

Kwa mfano wewe kama ni mzazi asiyemcha Mungu unaweza ukasababisha watoto wako wakashindwa kubarikiwa kwa sababu tuu kwa udhambi wako unazuia Baraka kwa familia yako yote wakiwemo watoto wako. Vivyo hivyo na wazazi wanaweza wakashindwa kubarikiwa kwa sababu watoto wao wanawazuilia Baraka zao.

Inawezekana hakuna Amani katika familia yako kwa sababu tuu wewe ni miongoni mwa wanafamilia hiyo. Kunakosekana Amani katika familia yako kwa sababu tuu wewe upo pale na wewe ni mdhambi/ mtu asiyemcha Mungu.

Unaweza kuona sasa wewe ni chanzo cha kukosekana Baraka kwa wale watu wako wa karibu. Kwa sababu tuu wewe ni mtu asiye mcha Mungu, na wao wanazuiliwa baraka pamoja na wewe. Mungu anapoacha kuibariki familia yako na wao pia wanakosa baraka. Kwa mfano unapokosa Amani na Mafanikio ukae ukijua kuwa wale unaowapenda na wanaokutegemea nao watakosa Amani na hawatanufaika kwa sababu hauna mafanikio.

Mwisho

Wewe ni kama Kiungo cha myororo wa Baraka au laana kwa wale uwapendao hasa familia yako. Ukibarikiwa unabarikiwa pamoja nao, ukilaaniwa unalaaniwa pamoja nao.

Kwa sababu hiyo, mara zote chagua kuishi kwa kumcha Mungu kwa sababu huwezi jua ni wangapi walioko nyuma yako na wanaobarikiwa kwa sababu ya ucha Mungu wako.

Mche Mungu kwa juhudi zote kwa sababu hujui ni wangapi wanaonufaika na ucha Mungu wako. Vilevile jitahidi usiwe mdhambi sana kwa sababu huwezi kujua ni wangapi wanaokosa Baraka za Mungu kwa udhambi wako.

Kumcha Mungu kuna faida kwako na kwa wengine, hasa unaowapenda. Kuto kumcha Mungu ni hasara kwako na kwa wale unaowapenda hasa familia yako

Tafakari Kuhusu Matumizi Ya Mali

Usiwe Bahili wa kutumia Mali ulizojaliwa na Mungu. Mungu amekupa Mali hizo ili ufurahie maisha uliyonayo ambayo siku moja yana mwisho.

Biblia inatufundisha hivi katika Kitabu cha Hekima ya Yoshua Bin Sira;

3Si sawa kwa mtu mchoyo kuwa tajiri.
Utajiri una maana gani kwa mtu bahili?
4Mtu anayekusanya mali kwa kujinyima mwenyewe,
anawakusanyia watu wengine.
Hao wataiponda mali yake katika anasa.
5Aliye bahili kwake mwenyewe atakuwa mkarimu kwa nani,
kama hafurahii utajiri wake mwenyewe?
6Hakuna mtu bahili kuliko anayejichukia mwenyewe;
ndivyo ubaya wake unavyomlipa yeye mwenyewe.
7Hata kama akitenda wema, hutenda kwa ajali,
na mwishowe hujulisha hali yake duni.
8Mtu mwenye kijicho ni mwovu;
huangalia pembeni na kuwadharau watu.
9Jicho la mchoyo haliridhiki na kile alicho nacho,
na uchoyo huidhoofisha roho.
10Mtu mchoyo ni bahili wa chakula,
haweki chakula mezani pake.
11Mwanangu, tumia vitu vyako kukufurahisha uwezavyo,
na mtolee Bwana tambiko zitakiwazo.
12Kumbuka kwamba kifo hakitakawia,
na kwamba hujatangaziwa kauli ya kuzimu.
13Mtendee rafiki yako mema kabla hujafa;
uwe mkarimu na kumpa kadiri ya uwezo wako.
14Usijinyime siku moja ya furaha,
usiache sehemu yako ya furaha halali ikuponyoke.
15Siku moja utawaachia wengine matunda ya jasho lako;
yote uliyochuma kwa kazi ngumu yatagawanywa kwa kura.
16Wape wengine na kupokea kwao ujifurahishe moyo,
maana mtu hatazamii starehe huko kuzimu.
17Viumbe vyote hai huchakaa kama vazi,
maana kauli ya tangu zama ni: “Lazima mtakufa!”
18Kama vile majani katika mti uliotanda matawi:
Hupukutika yakaanguka na mengine huota,
ndivyo ilivyo kwa binadamu wenye mwili na damu:
Mmoja hufa na mwingine huzaliwa.
19Kila kilichotengenezwa huchakaa na kutoweka,
naye mtengenezaji hutoweka na kazi yake. (Sira 14:3-19)

Unaweza ukajikuta unatafuta Mali katika Maisha yako yote kwa kujinyima na kujikatalia lakini mwisho wa siku Mali ulizotafuta hutozifaidi wewe. Tena hata wale watakaozifaidi wanaweza wakasahau kwamba wewe ndio uliyezitafuta. Na tena wanaweza wakazitumia vibaya.

Inawezekana unajibana masha yako yote kutafuta hela bila hata kula chakula kizuri na kunywa vizuri pamoja na kuishi maisha ya furaha, lakini maisha yako yatakapokuwa yameisha wale utakaowaachia mali hizo wakaziponda na kuzitumia vibaya.

Kwa ubahili na ugumu wa kutumia Mali unaweza ukashindwa kuonyesha upendo wako kwa watoto wako, ndugu na marafiki zako. Ukiwa bahili wa kutumia mali huna nafasi ya kufurahi na wanao, ndugu na marafiki. Wakati maisha yako yatakapokuwa yameisha hao uliowabania kutumia mali zako wataishia kukuona kuwa hukuwapenda japokuwa ulitafuta mali kwa ajili yao na umewaachia mali hizo. Utakaowaachia mali hawatakukumbuka kwa sababu hukuwahi kuishi nao kwa furaha kwa kuwa ulikuwa unabania matumizi ya mali zako.

Kwa sababu ya ubahili unashindwa kutimiza wajibu wako kwa Mungu wako wa kutoa zaka na sadaka pamoja na kusaidia masikini na wahitaji.

Matokeo ya ubahili wa matumizi ya mali ni kukosa yote na kupoteza yote.

ANGALIZO: Sikwambii kwamba utumie mali vibaya bila kujalli Maisha yako ya baadae na maisha ya wale wanaokutegemea. Nakwambia kwamba tumia mali zako kwa staha na kwa kujinufaisha mwenyewe na wale ulionao wakati ungali hai. Usijibane sana kwa kujinyima nafasi ya kufurahia maisha yako na ya wale unaoishi nao.

Ni vizuri kujiwekea akiba ya Maisha ya baadae lakini ni vizuri zaidi kuweka wazi kwamba ni nani atakayemiliki mali zako wakati utakapokuwa haupo. Ukishaamua ni nani atakayemiliki mali zako wakati ukiwa haupo, ni wajibu wako pia kumuandaa na kumlea kwa namna ambayo ungependa aendeleze yale uliyoyaanza ili juhudi zako zisiishie tuu pale unapokua haupo, bali ziendelee hata utakapokuwa haupo.

Maisha ya binadamu ni kama majani ya mti; yanachipua, yanakomaa, yananyauka na mwishowe yanaanguka. Wakati jani linakauka na kuanguka, yapo mengine yanayo anza kujichipua na kukomaa. Jani likianguka, linaachia nafasi yale yanayochomoza na kukomaa.

Tutumie Maisha yetu vizuri, kwa furaha, amani na upendo huku tukiwatengenezea wale watakaokuja baada yetu mahali pema pa kuishi.

Zaidi sana, Tumuombe Mungu atupe hekima na Busara ya kutumia Mali anazotujalia kwa manufaa yetu na manufaa ya wenzetu huku tukimtukuza Mungu.

Tafakari Upendo Mkuu wa Mungu kwa Mwanadamu

Utangulizi

Mungu alimpenda sana binadamu hata akauvaa Mwili wa Binadamu akashuka duniani na kuishi kama Binadamu ili amkomboe Mwanadamu na hata akaamua kufa kwa ajili ya Binadamu kwa malipizi ya dhambi za Binadamu na kwa maondoleo ya dhambi.

Je, ni Kitu gani ambacho Mungu angemfanyia mtu ambacho hajakifanya?

Kweli nakwambia hata kama Yesu angebaki duniani na kuwa hai mpaka leo bado watu wasinge mwamini na wapo ambao wangemchukia na kumfanya adui yao hata kumuwinda.

Ni watu wachache sana duniani wanaouona upendo huu mkuu wa Mungu, wengi hawaoni wala hawataki kuona. Wapo hata wacha Mungu lakini hawaelewi upendo huu.

Upendo Mkuu wa Mungu kwa Mwanadamu: Kwa Nini Yesu Alikuja Duniani?

Mungu alimpenda sana binadamu hata akaamua kuuvaa mwili wa binadamu na kushuka duniani ili amkomboe mwanadamu. Alishuka na kuishi kama binadamu, akakubali kuteseka na kufa kwa ajili ya malipizi ya dhambi za wanadamu. Huu ni upendo mkuu ambao Mungu ametufanyia, na ni muhimu kuelewa kwa kina ukubwa wa tendo hili la ajabu.

Mungu Alishuka na Kuishi Kama Binadamu

Mungu, kwa upendo wake usio na kifani, aliona mateso na maumivu ya wanadamu na akaamua kushuka duniani kama binadamu kupitia Yesu Kristo. Aliacha utukufu wake wa mbinguni na kuja kuishi kati yetu. Yohana 1:14 inasema:

“Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli.” (Yohana 1:14)

Yesu alikuja na kuishi kama binadamu, akakutana na changamoto zote tunazokutana nazo, ili aweze kutuelewa na kutukomboa kikamilifu.

Alikufa kwa Ajili ya Dhambi Zetu

Upendo wa Mungu ulionyeshwa kwa namna ya ajabu pale Yesu alipokubali kuteseka na kufa msalabani kwa ajili ya dhambi zetu. Alibeba mzigo wa dhambi za ulimwengu mzima na kutoa maisha yake kama sadaka takatifu. Warumi 5:8 inasema:

“Lakini Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi.” (Warumi 5:8)

Yesu hakufa kwa ajili ya wenye haki, bali kwa ajili ya wenye dhambi, ili kutupa nafasi ya kupokea msamaha na uzima wa milele.

Je, Ni Kitu Gani Ambacho Mungu Angemfanyia Mtu Ambacho Hajakifanya?

Mungu ametufanyia kila kitu kinachohitajika kwa ajili ya wokovu wetu. Alitoa mwanawe wa pekee, Yesu Kristo, ili afe kwa ajili yetu na kutuondolea dhambi zetu. Ni nini zaidi tunachoweza kumwomba Mungu ambacho hajakifanya? Hakuna upendo mkuu zaidi ya huu ambao Mungu ametufanyia. Kama ilivyoandikwa katika Yohana 15:13:

“Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.” (Yohana 15:13)

Yesu Angekuwa Hai Mpaka Leo, Bado Watu Wasingemwamini

Hata kama Yesu angeendelea kuishi duniani mpaka leo, bado kungekuwa na watu wasiomwamini na kumchukia. Hii ni kwa sababu mioyo ya watu wengi imejaa ugumu na kutokuamini. Yesu mwenyewe alisema katika Yohana 15:18:

“Kama ulimwengu ukiwachukia ninyi, kumbukeni ya kwamba ulinichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi.” (Yohana 15:18)

Hii inaonyesha kwamba kuna watu ambao hata wakiweka wazi upendo wa Mungu, bado watakataa na kumwona Yesu kama adui.

Wengi Hawaoni Upendo Huu Mkuu wa Mungu

Ni watu wachache sana wanaoona na kuthamini upendo huu mkuu wa Mungu. Wengi hawaoni wala hawataki kuona. Wengine ni wacha Mungu lakini hawaelewi kabisa kina cha upendo huu. Hata hivyo, wale wanaoona upendo huu na kuukubali wanapata uzima wa milele na uhusiano wa karibu na Mungu. Yesu alisema katika Yohana 3:16:

“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.” (Yohana 3:16)

Hitimisho

Upendo wa Mungu kwa mwanadamu ni mkubwa sana na umedhihirishwa kwa Yesu Kristo kushuka duniani, kuishi kama binadamu na kufa kwa ajili ya dhambi zetu. Mungu ametufanyia kila kitu kinachohitajika kwa ajili ya wokovu wetu. Ni jukumu letu kutambua na kuthamini upendo huu, na kuishi maisha yanayodhihirisha imani na shukrani zetu kwake. Tunapoona upendo huu wa ajabu, mioyo yetu inapaswa kujazwa na furaha na amani, tukijua kwamba Mungu ametupenda sana na anataka tuwe na uzima wa milele.

Unafahamu kuwa Imani ni Cheti cha Kuweza Kupata Yote?

Utangulizi

Imani ni kuwa na uhakika hata kwa mambo yasiyoonekana na yasiyowezekana. Ni kujua au kutarajia kwa uhakika kwa mambo ambayo bado hayajawa bayana (wazi) kuwa yapo au yatafanyika.

Kwa Imani Kila Kitu Kinawezekana. Kwa Sala na kwa Matendo.

Yesu Kristu anatufundisha tuwe na Imani kupitia Mfano huu;

18Yesu alipokuwa anarudi mjini asubuhi na mapema, aliona njaa. 19Akauona mtini mmoja kando ya njia, akauendea; lakini aliukuta hauma chochote ila majani matupu. Basi akauambia, “Usizae tena matunda milele!” Papo hapo huo mtini ukanyauka.

20Wanafunzi walipouona walishangaa wakisema, “Kwa nini mtini huu umenyauka ghafla?” 21Yesu akawajibu, “Kweli nawaambieni, kama mkiwa na imani bila kuwa na mashaka, mnaweza si tu kufanya hivyo, bali hata mkiuambia mlima huu: Ng’oka ukajitose baharini, itafanyika hivyo. 22Na mkiwa na imani, chochote mtakachoomba katika sala, mtapata.”
Mathayo 21:18-22

Basi Ili tuweze kuwa na Imani tumuombe Mungu atujalie Imani. Tuombe tujaliwe fadhila ya Imani hasa Tunaposali. Vile vile tumwombe Mungu atujalie Imani katika yale yote tunayoyafanya.

Tuombe hasa Imani isiyokuwa na Mashaka. Mashaka na Kusita sita ndiyo adui mkubwa wa Imani.

Imani ni Cheti cha Kuweza Kupata Yote

Imani ni kuwa na uhakika hata kwa mambo yasiyoonekana na yasiyowezekana. Ni kujua au kutarajia kwa uhakika kwa mambo ambayo bado hayajawa bayana kuwa yapo au yatafanyika. Imani ni msingi wa maisha ya Kikristo, na ni muhimu kuelewa jinsi inavyofanya kazi na jinsi inavyoweza kubadilisha maisha yetu. Katika maisha ya kiroho, imani inaweza kulinganishwa na cheti kinachokupa uwezo wa kupokea baraka na neema zote kutoka kwa Mungu. Kama cheti kinavyokupa sifa na uwezo wa kupata kitu, vivyo hivyo, imani inatupa uwezo wa kupokea kutoka kwa Mungu.

Imani ni Cheti cha Kuweza Kupata Yote

Kama vile cheti kinavyothibitisha sifa zako za kupokea kitu fulani, imani yetu inathibitisha sifa zetu mbele za Mungu na kutupa uwezo wa kupokea baraka zake. Bila imani, ni vigumu kupokea kutoka kwa Mungu kwa sababu imani ndio msingi wa uhusiano wetu naye. Waebrania 11:1 inasema:

“Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana.” (Waebrania 11:1)

Imani inatufanya tuwe na matumaini na kuamini kwamba mambo ambayo tunatarajia yatatimia, hata kama hatuyaoni bado kwa macho yetu ya kawaida.

Imani Inafanya Kila Kitu Kinawezekana

Kwa imani, hakuna lisilowezekana. Imani inafanya miujiza iwe sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Kwa sala na matendo, imani yetu inadhihirika na kuwa na nguvu za kutenda mambo makubwa. Yesu Kristo anatufundisha kuwa na imani kupitia mfano huu kutoka Mathayo 21:18-22:

“Yesu alipokuwa anarudi mjini asubuhi na mapema, aliona njaa. Akauona mtini mmoja kando ya njia, akauendea; lakini aliukuta hauna chochote ila majani matupu. Basi akauambia, ‘Usizae tena matunda milele!’ Papo hapo huo mtini ukanyauka. Wanafunzi walipouona walishangaa wakisema, ‘Kwa nini mtini huu umenyauka ghafla?’ Yesu akawajibu, ‘Kweli nawaambieni, kama mkiwa na imani bila kuwa na mashaka, mnaweza si tu kufanya hivyo, bali hata mkiuambia mlima huu: Ng’oka ukajitose baharini, itafanyika hivyo. Na mkiwa na imani, chochote mtakachoomba katika sala, mtapata.'” (Mathayo 21:18-22)

Yesu anatufundisha kuwa na imani thabiti bila mashaka. Anatushawishi kuelewa kwamba kwa imani, tunaweza kufanya mambo makubwa na ya ajabu, hata kuhamisha milima.

Kuomba Imani kutoka kwa Mungu

Ili tuweze kuwa na imani, tunapaswa kumwomba Mungu atujalie imani. Imani ni zawadi kutoka kwa Mungu, na tunahitaji kumwomba atupe fadhila hii tunaposali. Kwa kumwomba Mungu, tunapata nguvu na uhakika wa kuamini bila kusita.

Yakobo 1:6-7 inasema:

“Lakini aombe kwa imani, pasipo shaka yoyote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo na kupeperushwa huku na huku. Mtu kama huyo asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa Bwana.” (Yakobo 1:6-7)

Hii inatukumbusha umuhimu wa kuomba kwa imani isiyokuwa na mashaka. Mashaka na kusita-sita ni adui mkubwa wa imani, na ni lazima tuwe na imani kamili ili tuweze kupokea kutoka kwa Mungu.

Imani Katika Sala na Matendo

Imani yetu inapaswa kudhihirika si tu katika sala zetu bali pia katika matendo yetu ya kila siku. Tunapomwomba Mungu kwa imani, tunapaswa pia kuchukua hatua kwa imani, tukiamini kwamba Mungu atatenda. Yakobo 2:17 inasema:

“Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake.” (Yakobo 2:17)

Imani bila matendo ni imani isiyo na uhai. Tunapomwomba Mungu kwa imani, tunapaswa pia kuwa tayari kuchukua hatua kwa kuamini kwamba Mungu atatenda kupitia juhudi zetu.

Kuomba Imani Thabiti

Tunapomwomba Mungu atujalie imani, ni muhimu tuombe imani thabiti isiyokuwa na mashaka. Yesu alitufundisha kwamba tunaweza kufanya mambo makubwa kama tu tuna imani bila mashaka. Kwa hiyo, tuombe kwa bidii ili tujaliwe na Mungu imani inayoweza kuhamisha milima, imani inayoweza kufanya mambo yasiyowezekana yawezekane.

Mifano Halisi ya Imani katika Biblia

Biblia imejaa mifano ya watu waliojawa na imani na jinsi walivyoweza kupata mambo makubwa kupitia imani yao. Hapa kuna mifano sita ya imani kutoka katika Biblia:

  1. Ibrahimu:
    Ibrahimu alionyesha imani kuu kwa Mungu alipoambiwa kumtoa mwanawe Isaka kama sadaka. Alikuwa tayari kumtii Mungu, akiamini kwamba Mungu anaweza kumfufua Isaka kutoka kwa wafu. Imani yake ilimfanya awe baba wa mataifa mengi. (Waebrania 11:17-19)
  2. Musa:
    Musa alionyesha imani alipowaongoza Waisraeli kutoka utumwani Misri, licha ya changamoto nyingi alizokutana nazo. Aliamini ahadi za Mungu na kuamini kwamba Mungu atawatua kwenye nchi ya ahadi. (Waebrania 11:24-29)
  3. Yoshua na Yeriko:
    Yoshua alionyesha imani alipowaongoza Waisraeli kuzunguka ukuta wa Yeriko kwa siku saba kama alivyoamriwa na Mungu. Siku ya saba, ukuta wa Yeriko ulianguka, na Waisraeli walishinda mji huo. (Yoshua 6:1-20)
  4. Danieli:
    Danieli alionyesha imani kubwa alipoendelea kumwomba Mungu licha ya amri ya mfalme ambayo ilipiga marufuku maombi. Aliwekwa kwenye tundu la simba, lakini Mungu alimlinda na simba hawakumdhuru. (Danieli 6:10-23)
  5. Mwanawake aliotokwa na Damu:
    Mwanamke aliyekuwa akitokwa na damu kwa miaka kumi na miwili alionyesha imani kubwa alipogusa vazi la Yesu akiamini kwamba ataponywa. Imani yake ilimponya mara moja. (Marko 5:25-34)
  6. Petro:
    Petro alionyesha imani alipomwomba Yesu amruhusu kutembea juu ya maji. Alipoanza kutembea juu ya maji kuelekea kwa Yesu, aliona nguvu za Mungu. Ingawa alianza kuzama alipokuwa na mashaka, imani yake ilimfanya aweze kutembea juu ya maji kwa muda. (Mathayo 14:28-31)

Hitimisho

Imani ni cheti cha kuweza kupata yote. Kwa imani, tunaweza kuona mambo makubwa yakitendeka katika maisha yetu. Imani inatufanya tuwe na uhakika wa mambo yasiyoonekana na yasiyowezekana. Tunapaswa kumwomba Mungu atupe imani thabiti, na imani hiyo inapaswa kudhihirika katika sala na matendo yetu ya kila siku. Kwa kumtumaini Mungu bila mashaka, tunaweza kufanya mambo makubwa na ya ajabu, tukijua kwamba kwa imani, kila kitu kinawezekana.

Siri ya Yesu: Mwangaza Wa Maisha

Siri ni hii, Yesu ni Mwanga na Uovu ni giza. Giza na Mwanga havichangamani. Yesu hakai pamoja na uovu. Giza haliwezi kuzidi Mwanga. Uovu hauwezi kumzidi Yesu. Mwanga ukija giza linaondoka. Yesu akija uovu unakwisha.

Kujikabidhi Kwa Yesu Kristu Yeye Aliye Mwangaza Wa Maisha

Yesu ni Mwanga na Uovu ni giza

Giza na Mwanga havichangamani. Yesu hakai pamoja na uovu.
Giza haliwezi kuzidi Mwanga. Uovu hauwezi kumzidi Yesu.
Mwanga ukija giza linaondoka. Yesu akija uovu unakwisha.

Yesu Kristu ni mwangaza wa maisha yetu, akiwepo giza lote hutoweka.
Yesu akiwepo hakuna haja ya kufukuza giza bali giza litatoweka Lenyewe.

Unapomkaribisha Yesu katika maisha yako umekaribisha mwanga katika maisha yako na utashinda dhambi na uovu kwa kuwa Yesu aliye mwanga atavifutilia mbali.

Kikubwa ni kumkaribisha Yesu katika maisha yako na kumruhusu atawale Maisha yako na kila kitu katika maisha yako. Ukiweza kuachilia yote kwa Bwana Yesu na kumpa maisha yako basi utashinda uovu/dhambi. Vile unavyojiweka karibu na Yesu ndivyo unavyoshinda dhambi na uovu wote.

Kumkabidhi Yesu Maisha ni Kuamua kuishi kulingana na Mafundisho yake, kuachilia yote katika maongozi yake, kumshirikisha Yesu kwenye kila kitu katika maisha yako na Kuwa mkweli na muwazi mbele ya Yesu katika kila kitu.

Unapomkabidhi Yesu Maisha yako na vyote ulivyonavyo yeye huyatakatifuza na kuyafanya yawe kama yanavyotakiwa kuwa kitakatifu.

Changamoto kubwa kwa Wakristu ni kushindwa kujiweka Mikononi mwa Yesu kwa kuachilia yote na kukabidhi yote kwake. Wengi wanashindwa kufanya hivyo kwa sababu ya ubinafsi na uchu wa kusimama wenyewe. Wengine wanashindwa kwa sababu ya kukosa Imani. Hawana uhakika kwamba wanachokifanya wanakifanya kweli.

Lakini ukiweza kweli kumkabidhi Yesu Maisha yako, kila kitu kinakua sawa na utafanikiwa kwenye kila kitu. Utaanza kuona unashinda uovu na dhambi kulingana na vile unavyojikabidhi na kujiachilia kwa Yesu.

Anza leo kujikabidhi kwa yesu kwa kiasi kile unachoweza. Yesu anaelewa ubinadamu na madhaifu yetu. Atakusaidia. Hata kama kuna wakati unaweza kujikabidhi kwake na kisha unaanguka tena, yeye ni mwenye huruma na ni mwelewa haswa kuhusu hali yako, atakusaidia na kukuwezesha. Weka nia ya kujikabidhi kwake na kisha utaendelea kidogo kidogo mpaka utajikuta umejikabidhi mikononi kwake kabisa.

KUMBUKA: Yesu ni Mwanga na Uovu ni giza, mwanga ukiwepo giza halibaki linaondoka. Hata siku moja Giza haliwezi kuuzidi mwanga

Uwe na Imani basi, Mtumainie Yesu Kristu atakushindia uovu.

Yesu ndiyo dawa ya uovu na dhambi, kila unapoanguka dhambini mkimbilie yeye naye atakusamehe na kukuwezesha kushinda dhambi na uovu. Usichoke, kila siku jaribu na kujaribu mpaka utashinda.

Nami nakuombea kwa Jina Takatifu la Yesu, Akushindie Uovu na dhambi

Shopping Cart