Dondoo za Mapishi na Lishe

Mapishi ya Wali maharage,mchuzi wa samaki na spinach

Mahitaji

Mchele (rice 1/2 kilo)
Maharage yaliyochemshwa (boiled red kidney beans 1 kikombe cha chai)
Samaki waliokaangwa ( 2 fried fish)
Nyanya ya kopo (tin tomato 1/2 ya tin)
Vitunguu vilivyokatwa (onion 2)
Kitunguu swaum (garlic 3 cloves)
Tangawizi (ginger kiasi)
Limao (lemon 1/2)
Chumvi (salt)
Pilipili (scotch bonnet pepper 2)
Mafuta (vegetable oil)
Spinach
Tui la nazi (coconut milk 1 kikombe cha chai)

Matayarisho

Saga nyanya, kitunguu, tangawizi na kitunguu swaum pamoja. Tia kwenye sufuria na upike mpaka maji yakauke kisha tia curry powder, mafuta na chumvi na upike tena mpaka mchanganyiko uive kisha tia samaki na limao na maji kiasi na uache uchemke kiasi. Na hapo mchizi utakuwa tayari.
Osha na uzikate spinach kisha kaanga kitunguu na mafuta kiasi (hakikisha visiwe vya brown kisha tia spinach na chumvi. zipike kwa muda wa dakika 3-4 na hapo zitakuwa tayari zimeshaiva.
Wali: Chemsha maji kiasi kisha tia, chumvi, pilipili nzima(isikatwe) mafuta na tui la nazi. Baada ya hapo koroga na utie mchele na maharage na ufunike uache uchemke mpaka maji yakauke. Kisha geuza na ufunike tena na uuache mpaka uive. Baada ya hapo chakula chako kitakuwa tayari kwa kuseviwa.

Mapishi ya Viazi, samaki na asparagus

Mahitaji

Viazi (potato 1/2 kilo)
Samaki (fish 2)
Asparagus 8
Kitunguu kilichokatwa (chopped onion 1)
Kitunguu swaum kilichosagwa (garlic 4 cloves)
Tangawizi iliyosagwa kiasi (ginger paste)
Limao (lemon 1)
Giligilani iliyokatwakatwa (chopped coriander)
Curry powder (kijiko 1 cha chai)
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Safisha samaki na kisha uwamarinate na kitunguu swaum, tangawizi, limao na chumvi kwa muda wa nusu saa. Baada ya hapo wakaange na usiwakaushe sana kisha waweke pembeni. Chukua fry-pan kisha tia mafuta kidogo sana (kama 1/2 kijiko cha chai) kisha tia vitunguu maji na uvikaange kwa muda wa dakika 2 (kwani havitakiwi kuiva kabisa) kisha waweke samaki na uwachanganye na hivyo vitunguu. Kisha baada ya hapo tia giligilani iliyokatwa, kamulia limao na tia chumvi kidogo kisha geuzageuza ili kuchanganya vitu vyote na kisha ipua. Baada ya hapo menya na ukate viazi katika vipande vya wastani, na kisha uvichemshe kidogo na visiive kabisa. Baada ya hapo weka sufuria jikoni kwenye moto wa wastani na utie mafuta kidogo (kama vijiko 2 vya chakula) na kisha tia viazi na uanze kuvipika kwa kuvigeuzageuza mpaka viive na kuwa rangi ya brown kisha tia chumvi kidogo, curry powder na giligilani iliyokatwa.Vipike kwa muda wa dakika mbili kisha viipue. Na baada ya hapo malizia kwa kupika asparagus. Kwanza zioshe kisha zikate kati. Baada ya hapo weka mafuta kidogo kama 1/2 kijiko katika fry-pan yakisha pata moto tia kitunguu swaum, asparagus na chumvi.Zipike kwa kuzigeuzageuza kwa muda wa dakika 5 na hapo zitakuwa zimeshaiva na tayari kwa kuliwa pamoja na samaki na viazi. Unaweza kuvisevu kwa ketchup.

Mapishi ya Pilau ya nyama ya ng’ombe na kachumbari

Mahitaji

Mchele (rice vikombe 3)
Nyama ya ng’ombe (beef 1/2 kilo)
Viazi mbatata (potato 3)
Vitunguu maji (onions 3)
Kitunguu swaum (garlic cloves 4)
Tangawizi iliyosagwa (ginger kiasi)
Hiliki nzima (cardamon 4)
Karafuu (clove 4)
Pilipili mtama (blackpepper 4)
Amdalasini (cirnamon stick 1)
Binzari nyembamba nzima(cumin seeds 1/2 ya kijiko cha chai)
Binzari nyembamba ya kusaga (ground cumin 1 kijiko cha chai)
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)
Nyanya (fresh tomato 3)
Limao (lemon 1)
Pilipili (chilli 1)
Hoho (green pepper)

Matayarisho

Chemsha nyama na chumvi na nusu ya limao mpaka iive kisha weka pembeni. Baada ya hapo andaa vitu vya pilau kwa kuloweka mchele kwenye maji kwa muda wa dakika 10.Menya na kukatakata vitunguu na viazi kisha weka pembeni na pia chemsha maji ya moto na uweke pembeni. Baada ya hapo weka sufuri jikoni na tia mafuta kiasi . Yakisha pata moto tia vitunguu na uvikaange mpaka viwe vya rangi ya kahawia na kisha uitie nyama na ikaange mpaka ipate rangi ya bown pia. Baada ya hapo tia kitunguu swaum na tangawizi na uikoroge vizuri kisha iache ikaangike kwa muda wa dakika 2 kisha tia spice ambazo ni Binzari nyembamba ya unga, hiliki,karafuu, amdalasini na pilipili mtama na viazi. Baada ya hapo unatakiwa ugeuze geuze mpaka mchanganyiko uchanganyike vizuri kisha tia mchele na ugeuzege mpaka uchanganyike na viungo. Baada ya hapo tia chumvi na maji ya kutosha na ukoroge vizuri kisha funika na uache uchemke katika moto wa wastani. Maji yakikaribia kukauka tia binzari nyembamba nzima na ufunike uache mpaka maji yakauke kabisa. maji yakisha kauka ugeuze na ufunike tena na uuache mpaka uive.
Baada ya hapo andaa kachumbali kwa kukatakata vitunguu katika bakuli na kisha tia chumvi kwa ajili ya kuondoa ukali wa vitunguu. Baada ya hapo vioshe mpaka chumvi yote iishe. osha nyanya, Pilipili, hoho na kisha katakata slice nyembamba na uchanganye na vitunguu. Baada ya hapo tia chumvi, kamulia limao na uchanganye zote pamoja. Baada ya hapo chakula kitakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Ndizi na samaki

Mahitaji

Ndizi laini (Matoke 6)
Viazi mbatata (potato 3)
Samaki wabichi wa wastani ( Fresh tilapia 2)
Kitunguu swaum (garlic 6 cloves)
Tangawizi (fresh ground ginger vijiko 2 vya chai)
Nyanya ya kopo (tin tomato 1/2 kopo)
Vitunguu (onion 1)
Pilipili (chilli 1 nzima)
Chumvi (salt to your taste)
Mafuta (vegetable oil)
Limao (lemon 1/2)
Curry powder (1/2 kijiko cha chai)

Matayarisho

Safisha samaki kisha wakate vipande vitatu. Wakaushe maji kisha wamarinate na kitunguu swaum,tangawizi, chumvi, na limao kwa muda wa masaa 2. baada ya hapo waoke kwenye oven kwa muda wa dakika 30. baada ya hapo andaa ndizi na viazi kwa kuzimenya na kuziosha kisha ziweke pembeni. Kisha katakata vitunguu maji, Tangawizi, vitunguu swaum na nyanya kisha vitie kwenye blenda na usage mpaka mchanganyiko usagike vizuri. Baada ya hapo tia mchanganyiko katika sufuria na ubandike jikoni, acha uchemke mpaka maji yote yakauke. Maji yakisha kauka punguza moto na utie mafuta, curry powder, pilipili na chumvi. Kaangiza mpaka mchanganyiko uive na baada ya hapo tia viazi na maji kiasi na uache viazi vichemke mpaka vikaribie kuiva kisha tia ndizi na samaki na ufunike. Pika mpaka ndizi na viazi viive. Baada ya hapo chakula kitakuwa tayari kwa kuseviwa.

Mapishi ya Ugali, dagaa (wabichi) na matembele

Mahitaji

Dagaa wabichi (Fresh anchovies packet 1)
Unga wa ugali (corn meal flour 1/4 kilo) (unaweza kutumia unga wa choice uipendayo)
Matembele ya kukaushwa (dried sweet potato leaves, handful)
Nyanya ya kopo (tin tomato 1)
Kitunguu maji (onion 2)
Limao (lemon 1/4)
Pilipili mbuzi nzima bila kukata (scotch bonnet pepper1, do not chop)
Chumvi (salt 1/2 ya kijiko cha chai)
Mafuta (vegetable oil)
Hoho (green pepper 1)
Kitunguu swaum (garlic 5 cloves)
Tangawizi (ginger 1 kijiko cha chai)
Binzari ya curry (Curry powder 1/2 kijiko cha chai)

Matayarisho

Safisha dagaa kwa kutoa vichwa na utumbo kisha waoshe na uwakaushe na kitchen towel na uwaweke pembeni. Baada ya hapo katakata, vitunguu na hoho kisha weka pembeni. Baada ya hapo weka sufuria jikoni na utie mafuta yakisha pata moto tia dagaa na uwakaange mpaka wawe wa brown, kisha tia kitunguu swaum,curry powder na tangawizi, kaanga kidogo kisha malizia kwa kutia vitunguu maji, hoho,pilipili,chumvi na ukamulie limao. Kaanga kwa muda wa dakika 3-4 na hakikisha vitunguu na hoho haviivi sana na hapo dagaa watakuwa tayari.

Baada ya hapo yaoshe na uyaloweka matembele (kama ni makavu) kwa muda wa dakika 15, Kisha yatoe na uyaweke kwenye sufuria pamoja na kitunguu, nyanya, chumvi ,kamulia limao kidogo, pilipili na maji kiasi. acha matembele yachemke kwa muda wa dakika 20 na uhakikishe yameiva kwa kuwa laini. Baada ya hapo yapike mpaka maji yote yakauke na mafuta yatok na hapo matembele yatakuwa tayari.

Ukisha maliza kupika dagaa na matembele andaa chungu cha ugali. Kwanza unatakiwa kuchemsha maji ya moto, kisha koroga pembeni unga kiasi katika maji ya baridi na utie kwenye maji yanayochemka, Fanya kama unatengeneza uji, uji wa ugali ukishachemka tia unga na uanze kuusonga mpaka ugali uive. Ukisha iva pakua na usevu na mboga tayari kwa kuliwa.

Shopping Cart