Ujana na Makuzi | Mapenzi na Ngono Salama

Kwa nini Albino hawapewi kazi kwa mtazamo kwamba hawawezi kazi?

Watu wengi katika jamii hawana uelewa unaotosheleza kuhusu
ulemavu wa ngozi na ulemavu wa macho wa Albino.
Hii ndiyo sababu mara nyingi jamii inawatenga ikiamini kuwa
inawalinda ili wasipatwe na madhara ya ziada. Wanaweza
vilevile kuwatenga hata kwa kuwazuia kufanya kazi ambazo
wanazimudu bila sababu za msingi au bila kusikiliza maoni yao.
Watu wanapaswa kuzingatia mapungufu walio nayo Albino na
kuwapa kazi kwa kuzingatia uwezo walionao. Kwa mfano kufanya
kazi katika jua kwa muda mrefu ni jambo lisilofaa au kumtaka
Albino asome kwa muda mrefu inaweza kumshinda. Ni muhimu
pia kwa mtu anayeishi na ualbino kujielewa, kujitambua na

kukubaliana na hali hii kwa kuchagua kazi ambazo zitaendana
na mapungufu hayo au kukabiliana na hali yenyewe.

Kwa nini Albino tunaonekana kama mzigo katika familia zetu?

Watu wanaohitaji kupewa uangalizi maalumu wanaweza
kuonekana ni mzigo kwa kuwa wanaweza wakawa wanaomba
kupewa mahitaji au msaada maalumu tofauti na watu wengine
wa kawaida. Wazazi na wanafamilia wengine wanaweza
kuchukizwa na matamshi wanaotoa watu wengine pamoja na
kulazimika kuvumilia utani na matusi. Ndugu wanapaswa kujua
kwa nini ndugu yao Albino ni tofauti na kwa nini anahitaji
uangalizi maalumu.
Familia ndiyo msingi wa kumwezesha mtoto Albino kujitambua
na kukubali hali aliyo nayo. Familia inayoweza kumkubali mtoto
wao Albino inaneemeka na kuwa yenye furaha kwa sababu
mtoto Albino anakuwa kiungo maalumu katika familia, yaani
inaipa familia hali ya kuwa na nguvu yao iliyoungana.

Kwa nini jamii inatuchukia sisi Albino?

Siyo watu wote katika jamii wanawachukia au kuwatenga Albino.
Wazazi, ndugu zenu, rafiki zenu wanawapenda na kuwajali. Ni
jambo la kawaida kwa watu wa aina fulani kuwakataa au kuwakwepa
wale ambao wanaonekana tofauti na wao. Kwa mfano, katika jamii
ya watu weupe ni kawaida kuwakwepa au kuwakataa wale wenye
rangi nyeusi na hivyo ndivyo ilivyo pia kwa jamii ya watu weusi
kuwakataa au kuwakwepa watu weupe.
Jamii ya watu weusi huwaogopa, na hivyo huwakwepa Albino
kwa kuwa hawajui kilichotokea mpaka wakawa hivyo. Hali hiyo
inaimarishwa na uvumi potofu unaosambazwa kuwa ukimgusa
Albino unaweza ukageuka rangi ukawa mweupe au ukiwa na mimba
na ukamcheka au ukakutana na Albino, utazaa Albino. Ukweli ni
kwamba uvumi huu ni potofu na ni upuuzi mtupu. Ualbino ni hali
inayorithiwa na si ya kuambukizwa. Hakuna sababu ya kumuogopa
Albino. Mtazamo hasi wa jamii unaweza kubadilishwa endapo watu
watakuwa na ufahamu zaidi kuhusu ualbino na wanapowafahamu
watu wa aina hii vizuri zaidi kwamba ni watu wakarimu na wenye
urafiki. Na wewe unaweza ukachangia katika kuendeleza uelewa
huu kama utashiriki na watu kwa urafiki na kwa uwazi.

Albino anaathirikaje na unyanyapaa na ubaguzi katika jamii?

Watu wengi huwaona Albino kama watu tofauti na watu wengine
na kuwakwepa, wanaweza hata kubadili upande wa barabara
ili wasikutane nao au kukaa karibu nao katika daladala. Wengi
wanaamini katika uongo na uvumi unaosambazwa. Jamii inawatenga
katika matukio mengi na kwa hiyo kuimarisha uvumi usiyo na
usahihi uliopo kuhusu Albino. Hii inapelekea kunyanyapaliwa,
kubagulliwa na kuwekwa pembeni. Mbaya zaidi, ni kuwa ubaguzi
huu huchangia katika kushuka kujithamini kwa kijana Albino.
Akisha kuwa hajithamini ni vigumu kukubalika au kupata kazi. Kwa
hiyo, ubaguzi unaleta mzunguko wa madhara kwa Albino. Hitaji
muhimu kwa binadamu ni kupendwa, kukubalika na kutunzwa.
Kwani ualbino unatokea katika familia bila kutarajiwa. Kuwepo kwa
ualbino katika familia kunaweza kuwa kichocheo cha kukubalika
na kupendwa miongoni mwa ndugu, wazazi, mababu na mabibi.
Changamoto kubwa iliyopo Tanzania ni kupambana na unyanyapaa
na ubaguzi na kugombea haki sawa kwa ajili ya Albino.

Kuna fikra kuwa Albino ni watu wa kawaida je, kisayansi hii ni kweli?

Hii ni kweli kabisa. Watu wanaoishi na ualbino ni watu wa
kawaida kama binadamu wengine wote na wanaweza kuwa
wa aina tofauti kama binadamu wengine. Wanaweza kuwa
wadogo au warefu, wanene au wembamba, warembo au wasio
warembo, wenye vipaji au wa wastani. Wanaweza kuwa na
uthubutu au wenye aibu, wachangamfu au jeuri, wenye tabia ya
ushirikiano au wenye tabia ya uhasama.
Kumbuka kuwa utofauti wao upo tu kwenye muonekano wa ukosefu
wa rangi kwenye ngozi, nywele na macho. Wakati umefika kwa
jamii kujifunza kuwakubali Albino kama binadamu wengine, wenye
hisia, mahitaji, uwezo na wanastahili haki zote za binadamu kama
alivyo mtu mwingine yoyote.

Shopping Cart