Mbinu za Kilimo na Ufugaji Kukuongezea Mapato

Jinsi ya kutengeneza mbolea ya maji ya kunyunyiza kwenye majani

Mbolea ya kunyunyiza ni nzuri kwani inasaidia kuupa mmea virutubisho moja kwa moja kupitia kwenye majani au shina ambapo ndipo chakula kinahitajika.

Faida za mbolea ya maji ni pamoja na kuongezeka kwa kiwango cha mavuno, uwezo wa mimea kukabiliana na wadudu pamoja na magonjwa, kuvumilia ukame, na kuongeza ubora wa mazao.

Jinsi ya kuandaa mbolea ya maji kwa kutumia samadi

Mbolea ya maji hutengenezwa kwa kuchukua kiroba kilichojazwa samadi, aina mbalimbali ya mimea yenye virutubisho na inayoaminika kuwa dawa ya mimea. Kiroba hicho kinafungwa kwenye kijiti, na kutumbukiza kwa kuning’inia kwenye pipa lililojazwa maji.

Kiroba hicho ni lazima kichukue kati ya kilo 30-50 za samadi pamoja na aina nyingine za mimea kwa maji lita 200 (tazama mchoro). Unaweza kushika upande mmoja wa mti na kunyanyua na kushusha kila baada ya siku tano ili kuchanganya na kuharakisha kutolewa kwa virutubisho zaidi.

Kwa kawaida mchanganyiko huo unakuwa na harufu kali sana maana Nitrojeni nyingi inayopatikana hugeuka kuwa Amonia. Ni vizuri kufunika pipa ili kuzuia kuyeyuka kwa nitrojeni. Harufu ikishaisha, ujue mbolea yako ipo tayari kwa matumizi.

Ongeza maji na utingishe vizuri kabla ya kutumia. Nyunyizia mimea yako kila wiki mpaka utakapoona mabadiliko.

Jinsi ya kutengeneza mbolea ya maji kwa kutumia mimea peke yake (Majani fresh)

Mbolea hii hutengezwa kwa kuchukua majani mabichi na kuyakatakata na kisha kuyachanganya na maji kidogo.

Baada ya kuchanganya na maji unaacha kwa siku tatu au nne ambapo utatikisa mchanganyiko wako kila siku.

Baadae utatikisa na kuchanganya na maji na kunyunyiza shambani.

Vilevile Unaweza kutumia mbolea ya majani ambayo itakuwa kama dawa ya kuulia wadudu, kwa kutumia aina ya mimea kama vile mivule, mibangi mwitu, majani ya minyanya, mwarobaini, mashona nguo, pamoja na vitunguu saumu. Aina hii ya mimea inasaidia sana katika kuzuia magonjwa, wadudu na kutoa virutubisho muhimu kwa mimea vinavyosaidia mkulima kupata mazao bora bila gharama ya ziada ya kununua virutubisho.

Vigezo vya kunyunyiza mbolea ya maji

Ili upate matokeo mazuri wakati wa kunyunyiza mbolea ya maji unatakiwa kufuata vigezo vifuatavyo:
• Inashauriwa kutumia mbolea iliyochanganywa vizuri ili kuepukana na kuunguza mimea.
• Acha maji utakayotumia kuchanganyia mbolea yako nje katika pipa lililowazi usiku kucha, hii inasaidia kutoa madini hatarishi, na kufanya mchanganyiko wenye faida kwa mimea.
• Unatakiwa kutingisha vizuri mbolea yako ya maji kabla ya kunyunyiza. Chembechembe ndogo ambazo hazikuyeyuka zinaweza kuziba mdomo wa bomba la kunyunyizia.
• Matokeo mazuri yanaweza kupatikana endapo mbolea imechanganywa vizuri na kunyunyiziwa wakati hakuna upepo.
• Unatakiwa kunyunyizia mbolea wakati wa asubuhi au jioni wakati hakuna joto na upepo ukiwa umepungua.

Angalizo
Kabla ya kunyunyiza dawa au mbolea uliyoitengeneza mwenyewe shambani nyunyiza kwenye eneo dogo au mimea michache kwanza ili uone kama inaunguza au haiunguzi. Kumbuka kuwa mchanganyiko mwingine ukiwa cream au ukikolea sana unaweza kuchoma. Kwa hiyo kuepuka hili nyunyiza mahali padogo kwanza.

Mbinu za kuzuia magonjwa kwa kuku

Mbinu hizo ni hizi zifuatazo;

Namna ya kufanya Ukaguzi wa mara kwa mara wa banda la kuku kuzuia magonjwa

Ukaguzi wa Kila siku
• Hakikisha unasafisha vyombo vya kulishia na kunyweshea pamoja na viota.
• Ondoa kinyesi kwa kuku.
• Waangalie kuku wako kwa makini ili kujua afya na maendeleo yao. Yaani ili kutambua kama kuna mwenye ugonjwa

Ukaguzi Kwa wiki
• Ondoa matandazo machafu na kuweka mapya ili kuzuia kuzaliana kwa vijidudu vya magonjwa.

Ukaguzi kwaKwa mwezi
• Angalia uwepo wa wadudu na chawa, kisha utibu kama kuna ulazima.

Mambo 8 ya kuzingatia kabla ya kuleta mifugo (kuku, ng’ombe,mbuzi n.k) wapya bandani

Mambo hayo ni haya yafuatayo;
1. Hakikisha unaondoa matandazo yote ndani ya nyumba,
2. Ondoa vyombo vya kulishia na kunyweshea.

3. Ondoa uchafu wote unaoonekana bandani.
4. Safisha banda lote kwa kutumia maji na dawa.
5. Suuza na uache likauke.
6. Puliza dawa ya kuua wadudu.
7. Weka matandazo mapya,
8. Weka viombo vya kulishia na kunyweshea.

Jinsi ya kutunza nyumba ya kuku ili kuzuia magonjwa

1. Nyumba ya kuku iwe safi na kavu muda wote kuzuia ueneaji na kuzaliana kwa vijidudu vya magonjwa

2. Nyumba ya kuku iwe na nafasi za kupitisha hewa ya kutosha ili kuepuka joto na unyevunyevu ambao unachangia uwepo wa magonjwa kwa kuku

3. Hakikisha unaondoa matandazo na takataka zote kwenye banda wakati wote hasa yenye unyevu.

4. Fagia banda na kuhakikisha ni safi wakati wote. Weka matandazo mapya mara kwa mara.
5. Weka sehemu za kutosha kuku kupumzikia.
6. Weka viota vya kutosha.
7. Weka maji sehemu ambayo ni rahisi kusafisha.
8. Hakikisha unaondoa wanyama kama panya na wadudu nyemelezi kwenye sehemu ya malisho ya kuku kwani wao hubeba vimelea vya magonjwa.

Namna ya kutunza kuku na kuwakinga na magonjwa

1. Zingatia chanjo muhimu kwa kuku ili kuzuia magonjwa kama utakavyoshauriwa na mtaalamu wa mifugo.
Chanjo huanza katika wiki ya kwanza (mfano chanjo ya kuzuia sotoka) na inaweza kurudiwa baadaye.

2. Epuka kuweka kuku wengi mahali pamoja.
Ni rahisi magonjwa kuenea kwa haraka kuku wanaporundikana.

3. Kumbuka kutenganisha vifaranga na kuku wakubwa (isipokuwa kutoka kwa mama) kwa sababu vifaranga ni rahisi na wepesi sana kushambuliwa na magonjwa.

4. Hakikisha unaweka mipaka na madaraja ya sehemu za kuku kuzunguka/kucheza.

Namna ya kulisha kuku ili wasipatwe na magonjwa

Safisha vyombo vya kulishia na kunyweshea kila siku. Osha, sugua vizuri, kisha suuza kuondoa utando unaobeba bakteria.

Kuku wanahitaji wapewe chakula cha kutosha na chenye virutubisho vyote. Unaweza kuwaongezea majani, makombo, nafaka, mchanga laini, au maganda ya mayai.

Wapatie kuku maji safi muda wote. Wafugaji wengi wameripoti kuwa na matokeo mazuri baada ya kuchanganya dawa ya kuua vimelea kwenye maji ya kunywa.

Nunua chakula kwa wauzaji wazuri na wanaoaminika ili kuepuka minyoo na sumu hatarishi. Usiwape kuku chakula chochote kinachoonekana kuoza au kunuka uvundo.

Hifadhi chakula cha kuku katika sehemu kavu isiyo na joto na isiwe kwa zaidi ya miezi mitatu ili kuepuka kuharibiwa na fangasi.

Namna ya kukabiliana na Magonjwa ya kuku

Hakikisha unamuona mtaalamu wa mifugo mara uonapo dalili zozote za kuumwa kwa mifugo wako.

Tenga na wapatie tiba au kuwaua na kuteketeza kabisa kuku wagonjwa kuepuka kuenea kwa magonjwa.

Ondoa ndege waliokufa mara moja, uwafukie au kuchoma moto. Usile kuku aliekufa. Baadhi ya magonjwa ya ndege yanaweza kuambukizwa kwa binadamu.

Endapo kuna mlipuko wa ugonjwa katika eneo lako, usiruhusu watu kutembelea banda lako. Watu wanaweza kuleta maambukizi kwa miguu yao katika mabuti, nguo na mikono.

Pia magari yanaweza kuleta madhara kwa mabanda yako kupitia matairi na upakuaji wa mizigo.

Mambo 6 muhimu ya kuzingatia kupata udongo bora mzuri shambani

1. Usiuchoshe sana udongo

Udongo ni kiungo muhimu sana katika uzalishaji wa mazao. Ni mfumo wa uhai kwa mimea. Kwa hiyo, mkulima ni lazima alenge katika kutunza uhai wa udongo na kuepuka usumbufu kwa uhai wa udongo.
Sababu muhimu za kulima/kutifua udongo ni:
• Hulainisha udongo ili kuruhusu mizizi ya mimea kupenya kwa urahisi.
• Kutifua kunaboresha uwezekano wa kupenya kwa nitrogen na oxygen kutoka kwenye hewa.

• Kunawawezesha viumbe hai waliopo kwenye udongo kufanya kazi zao ipasavyo.
• Kunasaidia Kuandaa sehemu ya kuwekea mbegu.
• Kutifua kunauongeza uwezekano wa maji kupenya kwenye udongo na kupunguza uyeyukaji wa maji.
• Kuchanganya mabaki ya mimea na samadi kwenye udongo

2. Acha udongo upumue

Kama ilivyo kwa binadamu, viumbe hai wanahitajika kwa udongo wenye rutuba, pia mimea inahitajika kwa ajili ya binadamu kupata hewa safi ya oxygen. Kuchanganya matandazo,na mboji kwenye udongo ni muhimu sana ili kuboresha mzunguko wa hewa. Viumbe hai wadogo wadogo, wadudu, minyoo, na wanyama wengineo wanapenyeza hewa kwenye udongo.

3. Weka Matandazo kwenye udongo

Huu ni utaratibu wa kufunika udongo kwa kutumia mabaki ya mimea, kwa mfano, matawi madogo madogo ya miti, majani, mabaki ya mimea ya mazao, magugu na kadhalika. Hata hivyo inahitajika nguvu kazi kwa ajili ya kutawanya matandazo.

Matandazo yanazuia mmomonyoko wa ardhi unaotokana na maji na upepo, yanasaidia ardhi kunyonya maji ya mvua, kutunza unyevu unyevu kwenye udongo kwa kuzuia myeyuko wa maji ardhini.

Matandazo yanapo oza hutoa virutubisho vinavyoboresha na kuongeza rutuba kwenye udongo, mbali na hilo pia hubadilika kuwa udongo mweusi wenye rutuba zaidi. Kama kuna uhitaji wa kuharakisha kuoza kwa matandazo ili kuongeza rutuba kwenye ardhi kwa haraka, kinyesi cha ng’ombe kinaweza kuwekwa na kutandazwa juu ya matandazo, hii husaidia kuongeza virutubisho vya nitrogen.

Matandazo yana faida nyingi sana kwenye ardhi, lakini pia yanaweza kusababisha madhara. Mabaki ya mboga za majani yasitumike kama matandazo kwani yanaweza kusababisha wadudu na magonjwa kwa mimea. Viumbe hatari kama bangu (stem borers) wa shina wanaweza kuishi kwenye mabaki ya mimea.

Mabaki ya mimea iliyokuwa imeathiriwa na magonjwa ya virusi au fangasi yasitumike kama matandazo kuepuka uwezekano wa magonjwa hayo kuambukizwa kwa mazao yatakayopandwa msimu utakaofuata. Kilimo cha mzunguko ni njia bora kuepuka athari hiyo.

4. Panda mazao kwa mzunguko

Kupanda mazao kwa mzunguko ina maana ya kuwa na aina mbalimbali ya mazao katika eneo moja kwa msimu.

Kwa mfano, kama shamba lako umepanda mahindi na maharagwe kwa kipindi cha mwaka mmoja, mkulima anaweza kubadili mzunguko kwa kupanda aina nyingine ya mazao katika eneo hilo kwa mwaka unaofuata.

Mimea iliyo mizuri zaidi katika kilimo cha mzunguko ni pamoja na jamii ya kunde, au malisho kama sesbania ambayo husaidia kuongeza rutuba kwenye udongo.

5. Lisha udongo

Udongo unatakiwa ulishwe ili uwe na virutubisho. Hii ni kazi muhimu sana kwa kila mkulima. Mkulima anaweza Kuulisha udongo kwa kutumia samadi na mboji. Kumbuka udongo uliotumika sana bila virutubisho, umekufa, hauwezi kuzalisha.

6. Kuwa makini na maji

Maji ni mazuri shambani, lakini maji yakizidi ni hatari. Maji yakizidi shambani yanaweza kusababisha mmomonyoko wa udongo. Mmomonyoko wa udongo ni tishio na baa hatarishi kwa rutuba kwenye udongo. Mmomonyoko unaondoa tabaka la juu la udongo, sehemu ambayo ndiyo yenye rutuba zaidi.

Kupanda mimea kwa matuta (kontua) hupunguza kasi ya maji. Baada ya miaka kadhaa, nyasi zinazopandwa zinazopandwa kwenye matuta ya kontua husaidia kuunganisha na kusawazisha sehemu iliyotengwa, kwa kuwa udongo unaomomonyolewa hukusanyika katika sehemu iliyozuiwa na kuunganishwa kwa matuta.

Kwenye mwinuko mkali, kuta au mashimo, ndiyo njia pekee inayoweza kuzuia mmomonyoko wa udongo. Changanya na mimea kama matete, inasaidia kuzuia mmomonyoko na pia kutoa malisho kwa mifugo.

Mbali na matandazo (tazama hatua ya 3) mimea inayotambaa ni mbinu nyingine nzuri zaidi inayoweza kuzuia mmomonyoko wa ardhi. Matone ya maji hufikia ardhi yakiwa na nguvu kidogo sana hivyo kuepuka kumomonyoa ardhi, kwa kuwa yanakuwa tayari hayana nguvu ya kutiririka kwa kasi. Pia mimea inayotambaa hutumika kama kivuli kwa udongo. Mmea wowote unaofunika udongo na kuongeza rutuba unaweza kutumika.

Mfano maharage na mimea mingine ya jamii ya kunde, ambayo ina virutubisho vya nitrogen kwa wingi. Mimea inayopendekezwa ni ile ya jamii ya kunde. Inastahimili ukame, inatoa virutubisho vya naitrojeni, inatoa chakula, na pia inaweza kutumika kama chakula cha mifugo kilicho na protini nyingi. Kwa kuongezea inaweza pia kukabiliana na wadudu waharibifu.

Mambo Ya Kuzingatia Kuongeza Utagaji Wa Kuku

Inafahamika kuku kutaga mayai mengi hutokana na aina ya mbegu ya kuku, ila jua kwamba hata aina ya mbegu ya kuku yenye sifa ya kutaga mayai mengi kama haitapewa matunzo mazuri  basi sifa yake ya utagaji itapotea.

Kwa kawaida Tetea anatumia muda wa masaa 24 – 27 (siku moja) kutengeneza yai. Hakuna njia ya kupunguza muda huu (yaani atengeneze mayai miwili katika siku moja). Hiyo ndio asili yake. Njia Nzuri ya kumfanya kuku atage muda mrefu ni kumfanya awe na furaha na afya.

Njia za kuwafanya kuku wawe na furaha na afya:

1. Wape chakula bora chenye virutubisho vya kutosha. Usichakachue chakula chao hawatataga.

2. Viota vyao viwe safi. Safisha viota vyao mara kwa mara ili watage sehemu safi.

3. Wawe na sehemu ya wazi ya kuzunguka zunguka na kuparua parua.

4. Wawekee calcium ya kutosha kwenye chakula chao ili mayai wanayotaga yawe na gamba gumu.

5. Wachunguze mara kwa mara
kama wana dalili za kuumwa, na endapo dalili zipo watibu mara moja.

6. Wapatie maji safi kila siku. Pia safisha vyombo vyao kwa sabuni kila siku.

7. Hakikisha banda lao ni safi muda wote ili kusiwe na wadudu kama viroboto, chawa na papasi. Wadudu hawa huwasumbua kuku na kuwafanya wapunguze kutaga.

8. Hakikisha kuku hawapati msongo/stress, mfano kusiwe na wanyama wa kuwatisha wanaopita au kuingia bandani kwao.

9. Chagua aina ya kuku wanaotaga mayai mengi.

10. Umri wa kuku. Kuku wenye umri wa miezi 6 – 18 wanataga sana. Wakiwa na miezi 19 – 24 wananyonyoka manyoya (Annual Molt), hivyo hupunguza kutaga, na wakianza kutaga tena, wanataga mayai makubwa na machache kuliko mwanzo.

11. Wasihamishwe hamishwe banda. Kuku hutaga vizuri zaidi wakiwa kwenye mazingira waliyoyazoea.

12. Walishe mboga za majani za kutosha.
Kumbuka: Kuku wenye furaha na afya ndio watakaotaga sana kwenye maisha yao.
Note: Wakati mwingine inadhaniwa kwamba Jogoo anaweza kumsaidia Tetea kutaga mayai mengi. Jogoo hawezi kuongeza utagwaji wa mayai, lakini anahitajika kuyarutubisha mayai (kuyafanya yawe na mbegu). Kama kuku wako anataga mayai machache, kuongeza Jogoo hakutamfanya Tetea atage mayai mengi.

Matumizi ya mihogo kama dawa ya kuzuia wadudu kwenye mimea

Muhogo Inazuia Minyoo na vidukari.

Hatua za Kutayarisha dawa

  • Toa maji ya matunda kwa kuponda mizizi;
  • Pima k i w a n g o kimoja cha maji ya m a t u n d a sawa na maji ya kawaida (1:1).
  • Nyunyiza haraka ukitumia lita nne kwa mita moja za mraba, inasemekana kuwa na athari kubwa.
  • Subiri kwa siku ishirini kabla ya kupanda.

Angalizo: Tafuta ushauri wa mtaalamu wa kilimo kabla ya kutumia dawa yoyote ya asili

Shopping Cart