Upishi na Maandalizi ya Milo yenye Afya

Mapishi ya Biriani

Mahitaji

Mchele (rice 1/2 kilo)
Nyama (beef 1/2 kilo)
Vitunguu (onion 2)
Kitunguu swaum (garlic 1 kijiko cha chai)
Tangawizi (ginger 1 kijiko cha chai)
Maziwa mgando (yogurt 1 kikombe cha chai)
Hiliki nzima (cardamon 6)
Amdalasini nzima (cinamon stick 2)
Karafuu nzima (cloves 6)
Pilipili mtama nzima (black pepper 8)
Curry powder 1/2 kijiko cha chai
Binzari manjano (turmaric 1/2 kijiko cha chai)
Binzari nyembamba nzima (cumin 1/4 kijiko cha chai)
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Kaanga vitunguu mpaka viwe vya brown kisha tia nyama na uikaange kwa muda wa dakika 10. baada ya hapo tia tangawizi, kitunguu swaum, hiliki(4), amdalasini (1), karafuu (4), pilipili mtama (5), Curry powder, binzari manjano, binzari nyembamba na chumvi. Kisha koroga. Baada ya hapo tia yogurt na uipike mpaka ikauke kisha tia maji kidogo, funika na upunguze moto na uache ichemke kwa muda wa nusu saa.Baada ya hapo nyama itakuwa imeiva na mchuzi kubakia kidogo.Kwahiyo itatakiwa kuiipua.
Loweka mchele kwa dakika 10. kisha chemsha maji mengi kidogo katika sufuria kubwa. baada ya hapo tia hiliki (2) amdalamsini (1) karafuu(2) pilipili mtama (3) chumvi na mafuta kiasi. acha ichemke kidogo kisha tia mchele.Hakikisha maji yameufunika mchele kabisa na uuache uchemke kwa muda wa dakika 8 tu (kwani hautakiwi kuiva kabisa) kisha uipue na uchuje maji yote katika chujio. baada ya hapo chukua sufuria ya kuokea (baking pot kama unayoiona kweye picha) Kisha weka wali nusu na uusambaze sawia kisha weka mchuzi nyama na mchuzi wake pia utandaze na umalizie kwa kuweka leya ya wali uliobakia. Baada ya hapo ufunike na uweke kwenye oven kwenye moto wa 200°C kwa muda wa nusu saa.na baada ya hapo biriani litakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Wali, mchicha wa nazi na nyama ya kukaanga

Mahitaji

Mchele (rice 1/2 kilo)
Mchicha uliokatwakatwa (spinach mafungu 2)
Nyama (beef 1/2 ya kilo)
Nyanya (tin tomato 1/2 ya tin)
Nyanya chungu ( garden egg 3)
Kitunguu swaum (garlic cloves 3)
Tangawizi (ginger)
Curry powder
Vitunguu (onion 2)
Limao (lemon 1)
Chumvi
Pilipili (scotch bonnet pepper )
Tui la nazi (coconut milk 1 kikombe cha chai)

Matayarisho

Kaanga kitunguu kikishaiva tia nyanya na chumvi. kaanga mpaka nyanya ziive kisha tia nyanya chungu,curry powder na pilipili 1 nzima, baada ya hapo tia mchicha na uuchanganye vizuri kwa kuugeuzageuza. Mchicha ukishanywea tia tui la nazi na uache lichemke mpaka liive na hapo mchicha utakuwa tayari.
Safisha nyama kisha iweke kwenye sufuria na utie chumvi, tangawizi, limao na kitunguu swaum. Ichemshe mpaka itakapoiva na kuwa laini. Baada ya hapo weka sufuria jikoni na mafuta kidogo yakisha pata moto tia vitunguu na nyama na uvikaange pamoja, kisha tia curry powder na ukaange mpaka nyama na viunguu vya brown. na hapo nyama itakuwa imeiva. Malizia kwa kupika wali kwa kuchemsha maji kisha tia mafuta, chumvi na mchele na upike mpaka uive. Baada ya hapo chakula kitakuwa tayari kwa kuseviwa.

Mapishi ya Wali maharage,mchuzi wa samaki na spinach

Mahitaji

Mchele (rice 1/2 kilo)
Maharage yaliyochemshwa (boiled red kidney beans 1 kikombe cha chai)
Samaki waliokaangwa ( 2 fried fish)
Nyanya ya kopo (tin tomato 1/2 ya tin)
Vitunguu vilivyokatwa (onion 2)
Kitunguu swaum (garlic 3 cloves)
Tangawizi (ginger kiasi)
Limao (lemon 1/2)
Chumvi (salt)
Pilipili (scotch bonnet pepper 2)
Mafuta (vegetable oil)
Spinach
Tui la nazi (coconut milk 1 kikombe cha chai)

Matayarisho

Saga nyanya, kitunguu, tangawizi na kitunguu swaum pamoja. Tia kwenye sufuria na upike mpaka maji yakauke kisha tia curry powder, mafuta na chumvi na upike tena mpaka mchanganyiko uive kisha tia samaki na limao na maji kiasi na uache uchemke kiasi. Na hapo mchizi utakuwa tayari.
Osha na uzikate spinach kisha kaanga kitunguu na mafuta kiasi (hakikisha visiwe vya brown kisha tia spinach na chumvi. zipike kwa muda wa dakika 3-4 na hapo zitakuwa tayari zimeshaiva.
Wali: Chemsha maji kiasi kisha tia, chumvi, pilipili nzima(isikatwe) mafuta na tui la nazi. Baada ya hapo koroga na utie mchele na maharage na ufunike uache uchemke mpaka maji yakauke. Kisha geuza na ufunike tena na uuache mpaka uive. Baada ya hapo chakula chako kitakuwa tayari kwa kuseviwa.

Mapishi ya Viazi, samaki na asparagus

Mahitaji

Viazi (potato 1/2 kilo)
Samaki (fish 2)
Asparagus 8
Kitunguu kilichokatwa (chopped onion 1)
Kitunguu swaum kilichosagwa (garlic 4 cloves)
Tangawizi iliyosagwa kiasi (ginger paste)
Limao (lemon 1)
Giligilani iliyokatwakatwa (chopped coriander)
Curry powder (kijiko 1 cha chai)
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Safisha samaki na kisha uwamarinate na kitunguu swaum, tangawizi, limao na chumvi kwa muda wa nusu saa. Baada ya hapo wakaange na usiwakaushe sana kisha waweke pembeni. Chukua fry-pan kisha tia mafuta kidogo sana (kama 1/2 kijiko cha chai) kisha tia vitunguu maji na uvikaange kwa muda wa dakika 2 (kwani havitakiwi kuiva kabisa) kisha waweke samaki na uwachanganye na hivyo vitunguu. Kisha baada ya hapo tia giligilani iliyokatwa, kamulia limao na tia chumvi kidogo kisha geuzageuza ili kuchanganya vitu vyote na kisha ipua. Baada ya hapo menya na ukate viazi katika vipande vya wastani, na kisha uvichemshe kidogo na visiive kabisa. Baada ya hapo weka sufuria jikoni kwenye moto wa wastani na utie mafuta kidogo (kama vijiko 2 vya chakula) na kisha tia viazi na uanze kuvipika kwa kuvigeuzageuza mpaka viive na kuwa rangi ya brown kisha tia chumvi kidogo, curry powder na giligilani iliyokatwa.Vipike kwa muda wa dakika mbili kisha viipue. Na baada ya hapo malizia kwa kupika asparagus. Kwanza zioshe kisha zikate kati. Baada ya hapo weka mafuta kidogo kama 1/2 kijiko katika fry-pan yakisha pata moto tia kitunguu swaum, asparagus na chumvi.Zipike kwa kuzigeuzageuza kwa muda wa dakika 5 na hapo zitakuwa zimeshaiva na tayari kwa kuliwa pamoja na samaki na viazi. Unaweza kuvisevu kwa ketchup.

Mapishi ya Pilau ya nyama ya ng’ombe na kachumbari

Mahitaji

Mchele (rice vikombe 3)
Nyama ya ng’ombe (beef 1/2 kilo)
Viazi mbatata (potato 3)
Vitunguu maji (onions 3)
Kitunguu swaum (garlic cloves 4)
Tangawizi iliyosagwa (ginger kiasi)
Hiliki nzima (cardamon 4)
Karafuu (clove 4)
Pilipili mtama (blackpepper 4)
Amdalasini (cirnamon stick 1)
Binzari nyembamba nzima(cumin seeds 1/2 ya kijiko cha chai)
Binzari nyembamba ya kusaga (ground cumin 1 kijiko cha chai)
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)
Nyanya (fresh tomato 3)
Limao (lemon 1)
Pilipili (chilli 1)
Hoho (green pepper)

Matayarisho

Chemsha nyama na chumvi na nusu ya limao mpaka iive kisha weka pembeni. Baada ya hapo andaa vitu vya pilau kwa kuloweka mchele kwenye maji kwa muda wa dakika 10.Menya na kukatakata vitunguu na viazi kisha weka pembeni na pia chemsha maji ya moto na uweke pembeni. Baada ya hapo weka sufuri jikoni na tia mafuta kiasi . Yakisha pata moto tia vitunguu na uvikaange mpaka viwe vya rangi ya kahawia na kisha uitie nyama na ikaange mpaka ipate rangi ya bown pia. Baada ya hapo tia kitunguu swaum na tangawizi na uikoroge vizuri kisha iache ikaangike kwa muda wa dakika 2 kisha tia spice ambazo ni Binzari nyembamba ya unga, hiliki,karafuu, amdalasini na pilipili mtama na viazi. Baada ya hapo unatakiwa ugeuze geuze mpaka mchanganyiko uchanganyike vizuri kisha tia mchele na ugeuzege mpaka uchanganyike na viungo. Baada ya hapo tia chumvi na maji ya kutosha na ukoroge vizuri kisha funika na uache uchemke katika moto wa wastani. Maji yakikaribia kukauka tia binzari nyembamba nzima na ufunike uache mpaka maji yakauke kabisa. maji yakisha kauka ugeuze na ufunike tena na uuache mpaka uive.
Baada ya hapo andaa kachumbali kwa kukatakata vitunguu katika bakuli na kisha tia chumvi kwa ajili ya kuondoa ukali wa vitunguu. Baada ya hapo vioshe mpaka chumvi yote iishe. osha nyanya, Pilipili, hoho na kisha katakata slice nyembamba na uchanganye na vitunguu. Baada ya hapo tia chumvi, kamulia limao na uchanganye zote pamoja. Baada ya hapo chakula kitakuwa tayari kwa kuliwa.

Shopping Cart