Upishi na Maandalizi ya Milo yenye Afya

Mapishi ya Mchuzi wa kambale

Mahitaji

Kambale 2
Nazi kopo 1
Nyanya kopo 1
Vitunguu 2
Curry powder 1 kijiko cha chai
Turmaric 1/2 kijiko cha chai
Binzari nyembamba ya unga 1/2 kijiko cha chai
Swaum/ tangawizi 1 kijiko cha chakula
Giligilani kiasi
Limao 1/2
Chumvi
Olive oil

Matayarisho

Loweka samaki katika maji ya moto kwa muda wa muda wa nusu saa.Baada ya hapo Saga pamoja nyanya, vitunguu, swaum na tangawizi kisha vibandike jikoni na uvipike mpaka maji yote yakauke kisha tia mafuta. Pika mpaka nyanya zitengane na mafuta kisha tia spice zote.Zipike kwa muda mdogo kisha tia tui la nazi, maji kiasi, samaki, pilipili nzima, chumvi na kamulia limao. Pika mpaka tui la nazi litakapoiva na samaki pia wawe wameiva na mchuzi ubakie kiasi. Baada ya hapo ipua kisha tia giligilani iliyokatwa na mchuzi utakuwa tayari kwa kuliwa. Unaweza kuulia kwa chochote kile upendacho. Mi hupendaga kuulia na ugali mlaiiini au na wali pia.

Mapishi ya Firigisi za kuku

Mahitaji

Filigisi (chicken gizzard) 1/2 kilo
Carrot iliyokwanguliwa 1
Nyanya 1/2 kopo
Vitunguu maji 1 kikubwa
Tangawizi/swaum 1 kijiko cha chai
Hoho 1 iliyokatwakatwa
Limao 1/2
Chumvi
Curry powder 1/2 kijiko cha chai
Turmaric 1/2 kijiko cha chai
Chilli powder 1/4 kijiko cha chai
Mafuta
Chopped coriander

Matayarisho

Safisha filigisi kisha zikate vipande vidogo vidogo.Zichemshe pamoja na chumvi, limao na nusu ya tangawizi na swaum mpaka ziive (hakikisha unabakiza supu kidogo). Baada ya hapo kaanga vitunguu mpaka viwe vya brown kisha tia tangawizi na swaum iliyobakia na kaanga kidogo kisha tia nyanya. Zipike mpaka ziive kisha tia spice zote pamoja na chilli. Zipike kidogo kisha tia filigisi (bila supu kwanza) Zichanganye vizuri na uzipike kidogo. Baada ya hapo tia carrot na hoho na supu iliyobakia. Vipike pamoja mpaka viive na supu ibakie kidogo sana. Malizia kwa kutia coriander na uipue na hapo firigisi zako zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Maini ya ng’ombe

Mahitaji

Maini (Cow liver) 1/4 kilo
Vitunguu (chopped onion) 2
Nyanya (chopped tomato) 1
Kitunguu swaum/tangawizi (ginger /garlic paste) 1 kijiko cha chai
Mafuta ya kupikia
Chumvi
Coriander
Curry powder 1 kijiko cha chai
Limao (lemon) 1/4
Pilipili (scotch bonnet ) 1

Matayarisho

Safisha maini na ukate vipande vidogovidogo na uweke pembeni. Baada ya hapo kaanga vitunguu kidogo(visiwe vya brown) kisha tia ginger/ garlic paste,carry powder kaanga kidogo kisha tia nyanya. Kaanga nyanya mpaka zitoe mafuta kisha tia chumvi, pilipili na vimaji kidogo. Acha vichemke kidogo kisha tia maini na uyapike mpaka yaive. Malizia kwa kukamulia limao na kutia coriander kisha ipua na hapo yatakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Mlenda wa bamia na nyanya chungu

Mahitaji

Bamia (okra) 20
Nyanya chungu (garden eggs) 5
Magadi soda (Bicabonate soda) 1/4 ya kijiko cha chai
Nyanya (fresh tomato) 1
Chumvi (salt) kidogo
Pilipili 1/4

Matayarisho

Osha bamia, nyanya chungu na nyanya kisha vikatekate katika vipande vidogovidogo. Baada ya hapo vitie kwenye sufuria na vitu vyote vilivyobakia na kisha tia maji kidogo.Chemsha mpaka bamia na nyanya chungu ziive na vimaji vibakie kidogo sana. Baada ya hapo ziponde na mwiko kidogo kisha zikoroge na uipue na mlenda utakuwa tayari kwa kuliwa na ugali.

Mapishi ya Dagaa wa nazi, nyanya chungu na bamia

Mahitaji

Dagaa waliokaushwa (dried anchovy 2 kikombe cha chai)
Bamia (okra 5)
Nyanya chungu (garden egg 5)
Tui la nazi (coconut milk 1 kikombe cha chai)
Nyanya (fresh tomato 2)
Kitunguu (onion 1)
Curry powder 1/2 ya kijiko cha chai
Turmeric powder 1/2 kijiko cha chai
Limao (lemon 1/2)
Chumvi (salt kiasi)
Pilipili (scotch bonnet 1)
Mafuta (veg oil)

Matayarisho

Safisha dagaa na uwaweke pembeni. Baada ya hapo kaanga vitunguu vikianza kuwa vya brown tia dagaa wakaange kidogo kisha tia chumvi, pilipili, curry powder, turmeric, bamia na nyanya chungu, koroga vizuri mpaka mchanganyiko wote uchanganyike vizuri kisha tia nyanya na ufunike. Pika mpaka nyanya iive kisha kamulia limao,na pia hakikisha nyanya chungu na bamia zimeiva kidogo(usiache mpaka ziive sana manake zitavurugika pindi utakapotia tui la nazi) kisha malizia kwa kutia tui la nazi na uache lichemke mpaka rojo ibakie kidogo. Hakikisha nyanya chungu na bamia zimeiva ndo uipue. Na hapo dagaa wako watakuwa tayari kwa kuliwa na wali au ugali.

Shopping Cart