Author name: DIN - Melkisedeck Leon Shine

Rozari ya Malaika Mkuu Mikaeli

Rozari ya Malaika Mkuu Mikaeli ni sala nzuri sana ya kumheshimu huyu Malaika Mkuu pamoja na makundi yote tisa ya Malaika. Kuendana na jinsi tunavyofunuliwa katika Maandiko Matakatifu, makundi haya tofauti tofauti ya Malaika hujipanga kuanzia karibu sana na Kiti cha Enzi alipo Mwenyezi Mungu, kwenda chini tulipo sisi wanadamu. Makundi hayo kuanzia juu kwenda chini ni Maserafi, Makerubi, Wenye Enzi, Watawala, Wenye Nguvu, Wenye Mamlaka, Wakuu, Malaika Wakuu na Malaika.

Asili ya Rozari hii ni maono aliyopata Mtumishi wa Mungu Antonia d’Astonac, ambaye alitokewa na Malaika Mkuu Mikaeli aliyemfundisha sala za Rozari hii kwa kumwelekeza kuwa anataka aheshimiwe kwa salamu tisa kufuatana na makundi tisa ya Malaika.

Mtakatifu Mikaeli Malaika Mkuu aliahidi kuwa yeyote anayefanya ibada hii kwa heshima, akaribiapo Meza Takatifu, atasindikizwa na Malaika tisa, mmoja kutoka kila kundi la Malaika. Zaidi ya hayo, kwa kusali rozari hii, aliahidi msaada wa daima, na kwamba Malaika watamsaidia mwenye kuisali duniani na kumtoa toharani akifariki, yeye pamoja na jamaa zake.

ROZARI YA MALAIKA MKUU MIKAELI

Ee Mungu unielekezee msaada, Ee Bwana unisaidie hima!
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo na sasa na siku zote, na milele. Amina.

Sali Baba Yetu (mara nne) kwa heshima ya Malaika Wakuu, Mtakatifu Mikaeli, Mtakatifu Gabriel, Mtakatifu Rafaeli na Malaika Mlinzi.

1. Kwa heshima ya Malaika Mkuu Mtakatifu Mikaeli; Baba Yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, ufalme wako ufike, utakalo lifanyike duniani kama mbinguni, utupe leo mkate wetu wa kila siku, utusamehe makosa yetu, kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea. Usitutie katika kishawishi, lakini utuopoe maovuni. Amina
2. Kwa heshima ya Malaika Mkuu Mtakatifu Gabrieli; Baba Yetu, …..
3. Kwa heshima ya Malaika Mkuu Mtakatifu Rafaeli; Baba Yetu, …..
4. Kwa heshima ya Malaika Wangu Mlinzi; Baba Yetu, ……

Sali Baba Yetu moja na Salamu Maria tatu baada ya kila salamu katika tisa zifuatazo kwa heshima ya Makundi Tisa ya Malaika

Baba Yetu (mara moja, – tazama hapo juu)

Salamu Maria
Salamu Maria umejaa neema, Bwana yu nawe, umebarikiwa kuliko wanawake wote, na Yesu Mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Maria Mtakatifu, Mama wa Mungu, utuombee sisi wakosefu, sasa na saa ya kufa kwetu, Amina.

1. Kwa maombezi ya Mtakatifu Mikaeli na ya kundi la Serafin, Bwana awashe mioyoni mwetu moto wa mapendo kamili. Amina.
Baba Yetu (mara moja), Salamu Maria (mara tatu)

2. Kwa maombezi ya Mtakatifu Mikaeli na ya Kundi la Kerubin, Bwana atuwezeshe kuacha njia mbaya na kuenenda katika njia ya ukamilifu wa kiKristo. Amina.
Baba Yetu (mara moja), Salamu Maria (mara tatu)

3. Kwa maombezi ya Mtakatifu Mikaeli na ya Kundi la Wenye Enzi, Bwana atujalie roho ya unyofu na unyenyekevu wa kweli. Amina
Baba Yetu (mara moja), Salamu Maria (mara tatu)

4. Kwa maombezi ya Mtakatifu Mikaeli na ya Kundi la Watawala, Bwana atujalie neema ya kushinda maasi yetu na tamaa mbaya. Amina
Baba Yetu (mara moja), Salamu Maria (mara tatu)

5. Kwa maombezi ya Mtakatifu Mikaeli na ya Kundi la Wenye Nguvu, Bwana atukinge na vishawishi na mitego ya shetani. Amina
Baba Yetu (mara moja), Salamu Maria (mara tatu)

6. Kwa maombezi ya Mtakatifu Mikaeli na ya Kundi la Wenye Mamlaka, Bwana atukinge na mwovu wala tusianguke vishawishini. Amina
Baba Yetu (mara moja), Salamu Maria (mara tatu)

7. Kwa maombezi ya Mtakatifu Mikaeli na ya Kundi la Wakuu, Bwana atujalie kuwa na roho ya utii wa kweli. Amina
Baba Yetu (mara moja), Salamu Maria (mara tatu)

8. Kwa maombezi ya Mtakatifu Mikaeli na ya Kundi la Malaika Wakuu, Bwana atudumishe katika imani na katika kazi zote njema ili tujaliwe utukufu wa Milele. Amina.
Baba Yetu (mara moja), Salamu Maria (mara tatu)

9. Kwa maombezi ya Mtakatifu Mikaeli na ya Kundi la Malaika, Bwana atujalie ulinzi wao duniani hapa na baadaye watuongoze kwenye furaha za Mbinguni. Amina.
Baba Yetu (mara moja), Salamu Maria (mara tatu)

SALA MBELE YA KITI CHA ENZI CHA MUNGU

Sali Atukuzwe 7 kwa heshima ya Malaika 7 wateule ujipatie neema ya kuepa dhambi mbaya saba na kutujaza mapaji saba ya Roho Mtakatifu.

TUOMBE
Ee Mungu Mwenyezi wa milele, kwa wema na huruma yako ya ajabu, umetaka watu wako waokoke, ukamweka Malaika Mkuu Mikaeli kuwa Mkuu wa Kanisa lako, Utukinge na adui zetu, wasitusmbue saa ya kufa kwetu, bali tuongozwe naye kwenye utukufu wako Mkuu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana Wetu Yesu Kristo. Amina.

Utuombee Ee Mtukufu Mtakatifu Mikaeli Mkuu wa Kanisa la Yesu Kristo, tujaliwe ahadi za Kristo. Amina.

SALA KWA MTAKATIFU MIKAELI MALAIKA MKUU

Mtakatifu Mikaeli Malaika Mkuu, utulinde katika vita, uwe kinga yetu katika maovu na maoteo ya shetani, Mungu amtiishe, tunaomba sana, nawe Mkuu wa Majeshi ya Mbinguni kwa nguvu ya Mungu uwaangushe motoni shetani na pepo wabaya wengine wote, wanaozunguka duniani, ili kuzipoteza roho za watu.
Amina.

SALA KWA MALAIKA WAKO MLINZI

Malaika wa Mungu Mlinzi wangu mpenzi,
Ambaye upendo wake unanifanya niwepo hapa,
Uwe nami leo hii,
Kuniangaza na kunilinda,
Kunitawala na kuniongoza.
Amina.

SALA NYINGINE KWA MALAIKA WAKO MLINZI

Ee Malaika wangu Mlinzi, uliyewekwa na Mungu Mwema, naomba unilinde katika hatari zote za roho na za mwili. Amina

Sali mara kwa mara unapokumbuka, hasa asubuhi uamkapo na usiku kabla ya kulala, Atukuzwe mara saba, kwa heshima ya Malaika wako Mlinzi.

Mambo yanayowazuia Waumini na Watumishi wa Mungu Kufikia Ukamilifu na Utakatifu

Leo nimekuandalia Tafakari kuhusu Mambo yanayowazuia Waumini na watumishi wa Mungu Kuishi Kitakatifu na kufikia Ukamilifu. Mambo haya yanaweza yakaonekana sio dhambi au makosa kwa mtu lakini ni vikwazo kwa mtu kufikia Ukamilifu hasa anaposhindwa kuyajua na kuyaepuka. Wengi wanajiona kwamba wako salama lakini kumbe wako katika dhambi.

Mambo hayo ni kama ifuatavyo;

1. MAJIVUNO

Hii ni hali ya kujiona wa thamani sana, wakipekee na unayestahili sana.

Tofauti ya MAJIVUNO na pointi ya pili hapo chini (UMIMI) ni kwamba MAJIVUNO ni kujiona wa thamani lakini huku unatambua Yupo Mungu anayekuzidi. UMIMI ni kujiona kama Sawa na Mungu.

Kwa yale unayoyafanya: Kujiona kwamba wewe ni wa thamani na kipekee sana kwa yale uliyowahi kufanya, unayoyafanya na unayoweza kufanya. (I did, I do, I will do.)
Kwa vile Ulivyo: Kujiona kuwa wewe ni wa kipekee kwa vile ulivyo. Kusahau kuwa Vile ulivyo na vile ulivyonavyo Umepewa Bure na Mungu.
Kwa vile unavyofanyiwa: Kujiona kuwa wewe ni wa kipekee kulingana na wengine wanavyokuona na vile wanavyokufanyia.

Tafakari na ushauri kuhusu Majivuno
Unavyosoma kuwa majivuno ni hali ya kujiona wa thamani sana, wakipekee na unayestahili sana, unaweza ukafikiri sio kosa wala dhambi kujiona hivyo. Lakini makosa yanakuja kwa yale unayoyafanya kwa Majivuno hayo na kujisikia huko.
Majivuno yanakuwa dhambi pale tunapotenda kwa Majivuno na kujiona. Pale tunaposahau kwamba Upekee wetu sio kwamba tulistahili bali ni kwa Neema tuu. Tunakosea pale tunapoanza kuzarau wengine wale wasio kama sisi.

Unaweza ukafikiri kwamba hauna Majivuno lakini miongoni mwa dalili za Majivuno ni kama ifuatavyo;
1. Zarau
2. Kushindwa Kujishusha
3. Kujigamba/ Kujisifu
4. Kupenda upendeleo
5. Kujiona wa Tofauti
Ukiona kuna wakati una dalili kama hizi ujue tayari Majivuno yanajipandikiza ndani yako. Ninaposema Majivuno ni dhambi namaanisha kuwa matokeo/ matendo yanayotokana na dalili/ sifa hizi ndiyo dhambi.

Mambo ya kuzingatia kushinda Majivuno
Unyenyekevu… Unyenyekevu… Unyenyekevu ndio dawa ya Majivuno.
Utaweza kushinda majivuno kwa Kujishusha na kujiona sawa na wengine.

Unaweza ukashinda Majivuno kwa Kutambua kuwa Vile ulivyo, yale unayoweza kufanya na vile unavyofanyiwa ni Baraka za Mungu tuu. Haimaanishi kuwa umestahili sana kuwa hivyo.

Utashinda majivuno unapotambua kuwa hata wale unaowaona wako chini yako wangeweza kuwa kama wewe tuu. Ni maisha na Mipango ya Mungu ndio iliyofanya ukawa hivyo. Haimaanishi kwamba ni juhudi yako wewe. Wapo wenye Juhudi kuliko wewe lakini wapo chini yako.

2. UMIMI

Kujiona kuwa wewe ni wewe na wewe ni wa kipekee na unastahili kuliko wengine.

Tofauti kubwa na pointi ya kwanza hapo juu ni kwamba UMIMI ni Zaidi ya MAJIVUNO. Ni kujiona Hakuna wa Zaidi yako na wewe unahadhi sawa karibu na Mungu. Yaani, Mungu yupo lakini Mimi Pia nipo.

Kwa cheo, kipawa au mamlaka yako: Kujiona kwa cheo, kipawa au Mamlaka yako hakuna anayekuzidi, Mara nyingine kufikiri kwamba hata Mungu mwenyewe hawezi kukuondolea/ kukupinga. Ni kufikiri kwamba hakuna anayeweza kupinga maamuzi yako na hakuna wa kuamua Juu/ Zaidi yako.
Kwa unayoyafanya: Kuona kwamba kwa yale unayoyafanya hakuna kama wewe. Hakuna anayeweza kufanya kama wewe.
Kwa unayofanyiwa: Kuona kwamba hakuna anayestahili kufanyiwa kama wewe.

Kwamba Unaweza kufanya chochote: Kudhani kwamba unaweza kufanya chochote kile kwa sababu wewe ni wewe.

Tafakari na ushauri kuhusu UMIMI

Ninapoongelea Umimi siwalengi wenye mamlaka Makubwa ya juu tuu, Nalenga pia mtu mmoja mmoja kwa sababu kila mtu anayo mamlaka na Mwili na Utu wake. Unayo kipawa cha utu wako, uwanaume wako, uwanawake wako, Uzima wako. Vile vile Mamlaka ya Familia yako, jumuiya, ukoo n.k. Unamamlaka ya mwili wako na kwa hiyo kwa mwili huo usiutumie kwa uovu kwa sababu tuu umepewa mwili huo.

Kwa hiyo basi, ninapoongelea UMIMI naanzia chini kabisa kwenye Mamlaka na Mwili wako na Utu wako mpaka kwenye ngazi za jamii Kama Vyeo vya Kijamii na Kiinjili.

Unaweza ukadhani kwamba UMIMI sio makosa lakini makosa yanazaliwa pale unapotenda kwa kufuata umimi wako (Vile ulivyo). Dhambi inakuja pale Kwa sababu ya mamlaka yako unapoamua mambo kwa sababu unajua hakuna wa kukupinga. Kwa sababu ya uwezo wako wa kufanya mambo kufanya vitu kwa ubaya kwa sababu tuu unajua hakuna anayekuzidi/ anayeweza kufanya kama wewe/ anayeweza kukuzuia.

Dhambi inatokana na Kujiona kwako kuwa hakuna anayekuzidi kunakupelekea kushawishika kufanya mambo mengine ili kudhihirisha kuwa hakuna anayekuzidi kweli. Hasa kwa uonevu na ubabe.

UMIMI unaanza kuzaa dhambi pale mtu anapomsahau Mungu wake aliyemuumba na Kumpa huo UMIMI (Kumfanya vile alivyo). Unaposahau kuwa yupo Mungu aliyekupa hayo mamlaka, kipaji, kipawa na cheo ndipo unapoweza kuanza kukosea kwa UMIMI.

Mambo ya kuzingatia kushinda UMIMI
Kushinda UMIMI inahitaji unyenyekevu wa kujitambua kuwa Mamlaka, Kipaji, Kipawa au cheo chako Umepewa na Mungu na Unatakiwa Ukitumie kwa Mapenzi ya Mungu.
Ukitaka kuushinda UMIMI unapaswa kutambua kwamba yote yana Mwisho.

Vile vile unatakiwa ujue kuwa Ipo siku utatolea hesabu kwa kile ulichopewa. Ipo siku utaulizwa kwamba Umefanya nini na Mamlaka, Kipaji, Kipawa au cheo chako. Ndio maana wenye hekima wanaogopa sana kuwa na Mamlaka, Kipaji, Kipawa au cheo kwa sababu wanajua kuwa wanayo kazi kubwa kuliko wale wasiokuwa nacho.

Ukitambua kwamba unawajibika kwa vile ulivyo, basi ujitahidi kutenda kwa kumpendeza Mungu.
KUMBUKA Vile ulivyo inaweza kuwa njia rahisi ya kuufikia Ukamilifu na Utakatifu au inaweza ikawa Mtego kwako kwa kufikia Ukamilifu na Utakatifu. Ni wewe tuu kuamua Unaishije kwa Vile Ulivyo.

3. HASIRA, UKOROFI NA CHUKI

Hasira: Kukasirika haraka kwa kukosa uvumilivu na kutokutambua kuwa unapoishi na binadamu wengine ni lazima/ kawaida kukwazika. Watu hawawezi kufanya yote unayoyataka.
Ukorofi: Kuwa mbabe na kuweka vizuizi na masharti ya kiukorofi, pamoja na kufanya vitendo vya ukorofi na ukaidi kwa walio chini yako na hata walio juu yako.
Chuki: Kuwa na kinyongo na uchungu na watu wengine ambapo matokeo yake ni kufanyiana vitendo vya kikatili huku ukiwaza kuwa ni halali yako.

Tafakari na ushauri kuhusu Hasira, Ukorofi na chuki
Hasira, Ukorofi na chuki ni mambo ambayo mara nyingi yanaweza kuonekana sio dhambi moja kwa moja ila matokeo yake ndio yanaonekana kuwa ni dhambi. Hii ni kwa sababu kwa hali ya kawaida ya binadamu ni kawaida kwa mtu kuwa na Hasira, Ukorofi na chuki lakini vile anavyotenda baada ya kupata hasira au chuki inayopelekea ukorofi ndio inayosababisha mambo haya kuzaa dhambi.

Jambo lililo baya Zaidi ni kwamba dhambi inayotokana na Hasira, Ukorofi na chuki mara nyingi huonekana kama ni halali na haki ya mtu. Kwa Mfano, watu wengi wanaona kuwa ni kawaida kuwa mtu akikukasirisha lazima umfanyizie/ umtendee kitu kibaya. Wengine wanafikiri kuwa mtu anapokukasirisha lazima umuonyeshe ubabe. Na wengine wanaona ni kawaida kabisa kuwa na chuki na kinyongo hasa wanapotendewa visivyo na kuhisi kuwa ni haki yao kuchukia na kuwa na Kinyongo.

Lakini ukweli ni kwamba matendo yote yanayotendwa kwa Hasira, Ukorofi na chuki ni dhambi na makosa mbele ya Mungu. Kushindwa kuzuia Hasira, Ukorofi na chuki ni chanzo kikubwa cha dhambi kwa Wakristu walio wengi hasa Watumishi wa Mungu.

Makosa na dhambi za Hasira, Ukorofi na chuki yanawakoseha Neema za Mungu Watumishi wengi wa Mungu kwa sababu wengi wao hawaoni kama ni dhambi au ni makosa kufanya jambo kwa Hasira, Ukorofi na chuki. Wapo waumini na Watumishi wengi wa Mungu ambao wanaweza kufwatilia kikamilifu matakwa yote ya Imani yao lakini wanalegalega katika Imani yao kwa sababu ya kushindwa kutambua na kujiepusha na makosa na dhambi zitokanazo na Hasira, Ukorofi na chuki.

Mambo ya kuzingatia kushinda Hasira, Ukorofi na chuki
Kushinda Hasira
Ili kushinda hasira ni muhimu kuishi kwa kujua wakati wowote ule yupo mtu anaweza kukukosea.
Ni vizuri kuelewa kua wote wanaokukosea hawakukosei kwa kupenda au kwa kusudi. Ni lazima kutambua Katika maisha kuna mambo mengi yanayoweza yakafanya mtu akukosee au kukukwaza wewe. Huu ndio uhalisia wa Maisha.
Ni vizuri kujua kuwa Hasira ni hali inayoweza kuzimwa ukiamua kuizima na ni hali inayoweza kuwaka sana ukiamua kuiwasha. Sasa ni wewe kuchagua kuizima au kuiwasha.
Muhimu Zaidi kukumbuka ni kwamba Umeitwa Kuishi upendo wa Mungu na wa Jirani kwa maana hii umeitwa kusamehe na kuvumilia wengine huku ukiwaongoza na kuwaelekeza kile kinachotakiwa.

Kushinda Ukorofi
Namna kuu ya kushinda ukorofi ni kuwa mvumilivu. Kuwa mvumilivu na kuweza kuachilia (Kupotezea).
Unaweza kushinda ukorofi kwa Kutambua kuwa sio mara zote ni lazima kushindana na kubishana.
Kushinda Chuki
Kushinda chuki ni ngumu sana hasa unapokuwa tayari na katabia ka kuweka kinyongo au kuona uchungu/ wivu.
Wewe kama Mtumishi wa Mungu unaweza kushinda chuki kwa kujiepusha na tabia ya Kushindana na Kujilinganisha.
Chuki ni tabia au mazoea na kwa sababu hiyo unapotaka kuishinda unatakiwa ujijengee tabia na mazoea ya kinyume chake ambayo ni kujiepusha na mashindano na Kujilinganisha.
Zaidi sana, chuki inaweza kushindwa kwa ukarimu. Unapokua mkarimu unashinda chuki na wivu. Vilevile kwa ukarimu huu unaweza ukazuia chuki ya watu wengine. Utawasaidia wengine wasiwe na chuki na wewe pia, huku na wewe unajizuia na chuki.

MWISHO

Katika mambo yote haya Matatu unaweza ukaona kuwa naongelea Dhambi ya asili ya Binadamu. Dhambi ya Asili ya Binadamu ya Kujiona (PRIDE). Kila binadamu anazaliwa kwa kiasili akiwa na hali ya kujiona (PRIDE). Kila binadamu anazaliwa akiwa anajiona kuwa yeye ni yeye na Hakuna kama yeye.

Hali hii ya kuzaliwa ya kujiona ndio inayopelekea Majivuno, Umimi pamoja na Hasira, Ukorofi na chuki

Kuweza kuushinda kabisa Utu na Ubinadamu wako hapo utakua umeweza kushinda Ile asili yako ya dhambi. Ukiweza kushinda ile asili yako ya dhambi ndio utakuwa umejiepusha na makosa haya.

Tunakosa Utii kwa Mungu tunaposhindwa kupambana na Majivuno, Umimi pamoja na Hasira, Ukorofi na chuki

Mungu ametupa Amri Kuu ya Upendo. Upendo kwake na kwa Binadamu. Lakini amri hii haiwezi kutimizwa kama hatutaweza kushinda kwanza Majivuno, Umimi, Hasira, Ukorofi na Chuki.

Mungu na Akubariki sana kwa Neema zake na akuwezeshe uweze kushinda dhambi na makosa yasiyoonekana kama dhambi, ambayo ndiyo yanayozuia Waumini na watumishi wa Mungu kuufikia Ukamilifu na Utakatifu.

Daima Tunakumbushwa kuungama dhambi zetu hata kama ni ndogo kiasi gani

Kulikuwa na vijana wawili walioamua kwenda kwa padri kumwelezea shida zao.
Basi walipofika kwa yule padre, wakamwambia padre, ” samahani padre tuko hapa mbele yako kwa kuwa tumejisikia kuwa ni wadhambi ha hivyo tunahitaji kuungama.

Basi wakwanza akamwambia padre, ” Mimi dhambi zangu ni kubwa sana hata ninaona aibu kuziungama”, wa pili akamwambia padre, ” sahamani padre mimi nimetenda dhambi ila siyo kubwa sana kama za mwenzangu, bali ni dhambi ndogondogo.” Baada ya kusikia hayo padre aliwaambia basi kila mmoja aende akaokote mawe kadiri ya dhambi alizozitenda na akamletee. Hao vijana walienda kuokota mawe kadiri ya dhambi za kila mmoja wao. Mmoja wao alileta jiwe moja kubwa ambalo alikuja akilivilingisha hadi pale alipokuwepo padre, na mwingine alileta mawe madogomadogo mengi kwenye mfuko. Baada ya padre kuone kuwa walifanya alivyowaagiza, basi aliwaambia kuwa kila mmoja arudishe mawe yake sehemu ile ile alipoyaokota. Yule aliyebeba jiwe kubwa ilikuwa rahisi kujua alipolitoa hivyo alilivilingisha mara moja na kulirudisha mahali pake, wakati yule aliyekuwa na mawe madogomadogo alishindwa kukumbuka mahali alipoyatoa, hivyo akaishia kuhangaika na kumwambia padre kuwa hawezi kumbuka mahali alipotoa kila jiwe, na kwake ni vigumu.

Baada ya hayo padre aliwaambia wote kuwa yule mwenye dhambi kubwa daima ni rahisi kuiungama maana huwa inashika nafasi kubwa katika nafsi yake na inamfanya asiwe na amani daima, kwa hivyo ni rahisi kukumbuka kuiungama dhambi yake, vilevile padre akamgeukia yule mwingine aliyebeba mfuko wa mawe madogomadogo na akamwambia kuwa, jinsi ulivyoshindwa kurudisha hayo mawe katika nafasi yake kila moja, ndivyo ilivyo kwa dhambi ndogondogo ulizotenda. Dhambi zionekanazo kuwa ni ndogo zaweza sahulika na kukufanya utende dhambi nyingine ya kutokukumbuka wajibu wako wa kuungama ukidhani kuwa hujatenda dhambi.

Daima tunakumbushwa kuungama dhambi zetu hata kama ni ndogo au hata kama tumesahau, kwa maana kuna zile dhambi ambazo ni nyepesi na rahisi kusahulika na hivyo kutufanya daima tujihisi kuwa sisi hatuna haja ya kuungama.

Siri za Upendo, Huruma, Rehema na Neema za Mungu

Mungu ni Mwingi wa Rehema, Huruma, Upendo na Neema.

Kadiri siku zinavyozidi kwenda ndiyo na upendo, Huruma, Rehema na Neema za MUNGU zinavyozidi Kuongezeka.


Kadiri Mtu anavyoanguka dhambini na kutubu kweli makosa yake ndivyo na upendo, Huruma, Rehema na Neema za MUNGU zinavyoongezeka katika maisha yake.


Chumvi isipochanganywa na chakula haifai kuliwa, lakini chakula kinakua kitamu kikitiwa chumvi. Vivyo hivyo dhambi bila maondoleo na kitubio cha kweli matokeo ni mauti, lakini kitubio na maondoleo ya dhambi matokeo ni Rehema, Neema na Baraka kutoka kwenye chemichemi ya Huruma Kuu ya Mungu na Upendo wake usio na Mipaka.


Uangukapo dhambini jipe Moyo, Tubu na Ondoa dhambi hiyo. Hii ndio njia ya kuelekea Utakatifu

Mungu ni Mwingi wa Rehema, Huruma, Upendo na Neema

Mungu ni mwingi wa rehema, huruma, upendo na neema. Sifa hizi za Mungu zinatuonyesha jinsi alivyo na moyo wa upendo usio na kikomo kwa wanadamu. Katika hali yoyote tunapopita, Mungu yupo tayari kutupa rehema, huruma, na neema zake.

“Bwana, Bwana Mungu, mwenye huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli.” (Kutoka 34:6)
“Kwa maana rehema zake hazikomi. Ni mpya kila asubuhi; uaminifu wako ni mkuu.” (Maombolezo 3:22-23)
“Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu.” (Waefeso 2:8)

Rehema na Neema za Mungu Zinaongezeka

Kadiri siku zinavyozidi kwenda ndiyo na upendo, huruma, rehema na neema za Mungu zinavyozidi kuongezeka. Hii inaonyesha uaminifu wa Mungu na ahadi zake zisizobadilika. Mungu anapenda watu wake na daima yuko tayari kuonyesha neema na rehema zake, hata tunapokabiliana na changamoto za maisha.

“Lakini Bwana anangojea kuwafadhili, naye atainuka ili kuwaonea huruma, kwa maana Bwana ni Mungu wa hukumu; heri wote wamtarajiayo.” (Isaya 30:18)
“Mungu ni mwaminifu, ambaye kwa njia yake mliitwa kuingia katika ushirika wa Mwana wake Yesu Kristo Bwana wetu.” (1 Wakorintho 1:9)
“Lakini Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda, hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu, alituhisha pamoja na Kristo.” (Waefeso 2:4-5)

Kitubio na Maondoleo ya Dhambi

Kadiri mtu anavyoanguka dhambini na kutubu kweli makosa yake, ndivyo upendo, huruma, rehema na neema za Mungu zinavyoongezeka katika maisha yake. Mungu anapenda kuona toba ya kweli na moyo wa unyenyekevu, na anajibu kwa kutubariki kwa neema zake nyingi.

“Acheni maovu yenu, ambayo mnayafanya mbele za macho yangu; naam, acheni kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema; tafuteni hukumu, msaidieni mwenye kudhulumiwa, mwateteeni yatima, mwateteeni mjane.” (Isaya 1:16-17)
“Tukikiri dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na mwenye haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.” (1 Yohana 1:9)
“Kwa maana nitamsamehe maasi yao, na dhambi zao sitazikumbuka tena.” (Yeremia 31:34)

Maana ya Kitubio na Maondoleo ya Dhambi

Chumvi isipochanganywa na chakula haifai kuliwa, lakini chakula kinakua kitamu kikitiwa chumvi. Vivyo hivyo dhambi bila maondoleo na kitubio cha kweli matokeo ni mauti, lakini kitubio na maondoleo ya dhambi matokeo ni rehema, neema na baraka kutoka kwenye chemichemi ya huruma kuu ya Mungu na upendo wake usio na mipaka. Tunahitaji toba ya kweli ili kupata msamaha wa Mungu na kuweza kufurahia neema zake.

“Njoni, nasi tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu.” (Isaya 1:18)
“Tubuni basi, mkaongoke, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana.” (Matendo 3:19)
“Basi semeni naye Bwana, mrudi kwake, mwambieni, Uondoe maovu yote, upate kupendwa na ulipe mazao ya midomo yetu.” (Hosea 14:2)

Njia ya Kuelekea Utakatifu

Uangukapo dhambini jipe moyo, tubu na ondoa dhambi hiyo. Hii ndio njia ya kuelekea utakatifu. Mungu anatupenda na anataka tuwe watakatifu kama yeye alivyo mtakatifu. Kwa kupitia toba ya kweli na kutafuta msamaha wa Mungu, tunaweza kufikia utakatifu ambao Mungu anatamani tuwe nao.

“Kwa sababu mimi ni Bwana Mungu wenu; jifanyeni watakatifu na kuwa watakatifu, kwa kuwa mimi ni mtakatifu.” (Walawi 11:44)
“Furahini katika Bwana sikuzote; tena nasema, furahini. Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu. Msijisumbue kwa neno lolote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.” (Wafilipi 4:4-7)
“Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.” (1 Petro 1:15-16)

Shopping Cart