Swala la Mapadri kutooa limeandikwa wapi katika Biblia?

JE,SHERIA YA MAPADRE KUTOOA NA KUISHI USEJA IMEANDIKWA WAPI KATIKA BIBLIA AU IMETUNGWA TU NA PAPA?

Pengine umewahi kuulizwa swali hili wakati fulani.Na jibu lake ni kama ifuayavyo:
Mtu anapouliza kila kitu kimeandikwa wapi katika Biblia ni kudhihirisha kutokuijua au kuielewa vizuri Biblia Takatifu na historia yake.Mtu anapong’ang’ania “nionyeshe kitu fulani kimeandikwa wapi kwenye Biblia”ni kutaka kujiona ya kwamba yeye anaielewa sana Biblia na ameisoma yote kwa hiyo kila kitu kilichopo kwenye Biblia anakifahamu kumbe haijui Biblia bali anakariri Biblia!
Na hili suala la kushupalia swala la kuoa linadhihirisha jinsi gani tulivyo kizazi cha zinaa,ni kama tunadhani kuwa UZIMA upo katika kujamiiana!La hasha.
Paulo anasema “Kwasababu ya zinaa ni bora kuoa na kuolewa”(1Wakorintho 7:2.9) haya sio maneno ya kufurahia na kuchekelea tu maana “YANAWALENGA WALE WALIOSHINDIKANA KATIKA YALE YAPENDEZAYO”(1Wakorintho 7:1.8)sasa ni lazima tujiulize je tumeshindikana kiasi hicho?,hiyo sio sifa!
1Wakorintho 7:1.8
“Basi kwa habari ya mambo yale mliyoandika,ni heri mwanaume asimguse mwanamke,8.Lakini nawaambia wale wasiooa bado na wajane heri wakae kama mimi nilivyo”
Na Paulo Mtume anasema “Ni bora kuoa au kuolewa” lakini hakusema “Ni LAZIMA kuoa au kuolewa”
Suala la kutooa kwa mapadre kadiri ya historia lilianza tangu zamani kabisa mwanzoni mwa milenia ya pili katika mtagusi wa pili wa Laterani mwaka wa 1139 ili waweze kumtumikia Mungu kwa uhuru na bila mawaa wala pasipo vikwazo(1wakorintho 7:32-35)
1wakorintho 7:32-35
“32Lakini nataka msiwe na masumbufu.Yeye asiyeoa hujishughulisha zaidi na mambo ya Bwana ampendezeje Bwana;33.bali yeye aliyeoa hujishughulisha zaidi na mambo ya dunia hii,jinsi atakavyompendeza mkewe.34-Tena iko tofauti kati ya mke na mwanamwali.Yeye asiyeolewa hujishughulisha na mambo ya Bwana ili apate kuwa mtakatifu mwili na Roho.Lakini yeye aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya dunia hii,jinsi atakavyompendezesha mumewe.,35.Nasema hayo niwafaidie ninyi,si kwamba niwategee tanzi,bali kwaajili ya vile vipendezavyo,tena mpate kumhudumia Bwana pasipo kuvutwa na mambo mengine”
Maandiko hayo hapo juu yanajieleza wala sidhani kama yanahitaji kufafanuliwa zaidi ya yanavyojifafanua yenyewe.
Watu wengine wanafikiri kwamba kutooa ni dhambi,kama ni hivyo basi hata Yesu mwenyewe alikosa maana hata yeye mwenyewe hakuoa.
Yesu mwenyewe anafundisha kuhusu ubikira(Mathayo 19:10-12)
Mathayo 19:10-12,
“Wanafunzi wake wakamwambia,kama mambo ya mme na mke yakiwa hivyo ni afadhali kutuooa kabisa.Lakini Yeye akawaambia ‘SI WOTE WAWEZAO KULIPOKEA NENO HILO,ILA TU WALE WALIOJALIWA,maana wako MATOWASHI waliozaliwa katika hali hiyo toka matumboni mwa mama zao;tena wako matowashi waliofanywa na watu kuwa matowashi,tena wako Matowashi WALIOJIFANYA WENYEWE KUWA MATOWASHI KWAAJILI YA UFALME WA MBINGUNI’,awezaye kulipokea neno hili na alipokee”
Yesu mwenyewe analifafanua jambo hili kwa mapana,katika orodha ya matowashi Yesu aliowataja,Mapadre ni Matowashi waliojifanya hivyo kwaajili ya huduma ya kanisa na ufalme wa Mungu.
Tena Yesu anatuambia waziwazi kwamba”sio wote wawezao kulipokea neno hilo”yaani sasa sio wote wawezao kuwa Matowashi(Mapadre)bali ni wale tu waliojaliwa na Mungu neema hiyo.wale wasioweza kuishi upadre huoa na kuwa na familia.Tena Yesu anamalizia kwa kusema “Awezaye kulipokea fundisho hili na alipokee”,kwa maana nyingine ni kusema “Fundisho au Utowashi huu sio wa lazima”anayeweza kuishi maisha hayo basi na ayapokee na yule asiyeweza basi aache!
Vilevile Mitume ili kumfuata Yesu kikamilifu waliyaacha yote waliokuwa nayo ikiwepo familia zao ili wamtumikie Bwana(Mathayo 19:27.29)
Mathayo 19:27.29:
“Ndipo Petro akajibu akamwambia ‘Tazama sisi tumeacha vyote tukakufuata wewe,tutapata nini basi?29.Amini nawaambia,kila mtu aliyeacha nyumba au ndugu wa kiume au wakike,au baba au mama au watoto au mashamba KWAAJILI YA JINA LANGU,atapokea mara mia zaidi na kuurithi uzima wa milele”
katika injili hiyo,Yesu anadhihirisha kwamba aliyeacha hayo yaliotajwa si kwasababu hawezi kuyapata la hasha,bali ameyaacha hayo yote KWAAJILI YA JINA LA YESU atapokea mengi hapa duniani halafu tena ataurithi ufalme wa mbinguni.
Mapadre wameyaacha hayo yote,wameacha nyumba,familia zao na kila kitu SIO KWASABABU HAWANA UWEZO AU HAWAWEZI KUPATA MAMBO HAYO bali WAMEACHA KWASABABU YA KUMTUMIKIA MUNGU KWA KADIRI YA MAANDIKO MATAKATIFU na kwakutaka kwao kuyaishi kimamilifu MASHAURI YA INJILI ikiwepo USEJA.
Maneno ya Paulo na yale ya Yesu mwenyewe kuhusu kumtumikia Mungu bila kuoa sio ya bahati mbaya bali ndiyo njia bora na inayofaa sana na kukubalika mbele ya Mungu.
Kwahiyo unapowaona mapadre hawaoi ujue sababu yake ni hiyo kwamba “Wamejitoa kwaajili ya kulihudumia kanisa”
(Na pia huwa nawashangaa mno watu wanaowapiga vita Mapadre kwamba kwanini hawaoi,najiuliza je,hao Mapadre wamewakataza wao kwamba wasioe?.)..na kama jibu ni hapana,sasa Je,”Pilipili ya shamba usiyoila inakuwashia nini?”
TUMSIFU YESU KRISTO!

Unayopaswa kujua Kuhusu Kipindi cha Majilio

Majilio (pia: Adventi ) ni kipindi cha liturujia ya
madhehebu mbalimbali ya Ukristo (kama vile
Kanisa Katoliki, ya Waorthodoksi , Waanglikana
na Walutheri ) kinatangulia sherehe ya Noeli na
kuanza mwaka wa liturujia. Kinaweza kudumu
kati ya siku 22 na 40.
Jina lake kwa Kilatini ni adventus maana yake
ujio (wa Yesu Kristo ), lakini jina la Kiswahili ni
sahihi zaidi kwa sababu linadokeza kuwa ujio
wa Yesu ni kwa ajili yetu na kuwa alikuja
zamani, anakuja kila siku na atakuja kwa
utukufu mwisho wa dunia.
Maana ya Majilio katika
maisha ya binadamu
Sisi binadamu hatuwezi kuishi daima katika
hali ileile bila ya matazamio. Hasa kijana
anatarajia mambo mapya tena mema. Hivyo
tunajitahidi kuyapata. Asiyetazamia chochote
amevunjika moyo, hana hamu ya kuishi. Lakini
matazamio ya kibinadamu yakimfikia mtu
hayamridhishi moja kwa moja. Kristo tu
anatimiza hamu zote kwa kumkomboa kutoka
unyonge. Majilio yanatukumbusha kila mwaka
matarajio ya kweli na hivyo yanaamsha hamu
ya kuishi kwa bidii ya kiroho.
MAJILIO: Katika Kanisa la Roma.
Katika mwaka wa liturujia ya Kanisa la Roma ,
sherehe ya Noeli inaandaliwa na kipindi cha
Majilio ambacho kina mambo mawili:
kinakumbusha Mwana wa Mungu alivyotujilia
mara ya kwanza, na papo hapo kinatuandaa
kumpokea atakapotujilia tena siku ya mwisho .
Kufuatana na hayo kina sehemu mbili: hadi
tarehe 16 Desemba kinahusu zaidi kurudi kwa
Bwana; siku nane za mwisho kinatuelekeza
moja kwa moja kuadhimisha kuzaliwa kwake.
Urefu wa Majilio unategemea siku
inayoangukia Noeli, kwa kuwa ni lazima yawe
na Jumapili nne. Hivyo basi yanaanza kwa
Masifu ya Jioni ya kwanza ya Jumapili
inayoangukia tarehe 30 Novemba au tarehe ya
jirani zaidi; yanakwisha kabla ya Masifu ya
Jioni ya kwanza ya Noeli.
Kwa jumla ni kipindi cha toba: rangi yenyewe
ni zambarau; haziruhusiwi sherehe za fahari;
ala za muziki na maua vinaweza kutumika
kwa kiasi tu. Masharti hayo yanalegezwa
katika Jumapili ya tatu kwa sababu ya furaha
ya kuona tunakaribia sherehe yenyewe.
Katika kipindi hicho tunaadhimisha tumaini la
Israeli lililotimizwa Yesu alipokuja katika
unyenyekevu wa umbile letu; pia tunangojea
arudi kwa utukufu. Kama alivyotekeleza ahadi
mara ya kwanza, atazitekeleza pia mara ya
pili, ingawa kwake miaka elfu ni kama siku
moja tu. Kati ya majilio hayo mawili, Bwana
anatujilia mfululizo kifumbo katika sakramenti
(hasa ekaristi ) na katika maisha ya kila siku
kwa njia ya matukio na watu (hasa maskini ).
Basi tunapaswa kuwa tayari daima kumpokea
ili siku ya mwisho tukamlaki, naye
atukaribishe kwenye uzima wa milele. Pia
tunapaswa kumuomba aje kutukomboa, yeye
aliye tumaini letu.
Katika safari ya Majilio watu watatu
wanatuongoza tukutane na Yesu:
1. Isaya
nabii wa tumaini, mwenye kipaji cha kutokeza
matazamio ya binadamu na kumhakikishia
atatimiziwa na Mwokozi
. 2. Yohane Mbatizaji ,
mwenye kuhimiza toba kwa kuwa tunapaswa
kupindua maisha yetu ili tukutane vema na
Kristo.
3. Maria , bikira aliyekuwa tayari
kumpokea Masiya kwa upendo na kushirikiana
naye katika kutimiza mpango wa wokovu .
Tukiwafuata hao watatu tunaweza kujipatia
maadili yale yanayotuandaa kumpokea
Mwokozi anapotujilia: ndiyo matunda maalumu
tunayotarajiwa kuyachuma wakati wa Majilio:
1. Kukesha katika imani, sala na kutambua
ishara za Bwana kutujilia katika nafasi yoyote
ya maisha na mwishoni mwa nyakati.
2.Kuongoka kwa kufuata njia nyofu.
3.Kushuhudia furaha inayoletwa na Yesu kwa
kuwa na upole na uvumilivu kwa wenzetu, kwa
tumaini la kuwa bidii zetu zinawahisha ufalme
wa Mungu wenye heri isiyo na mwisho.
4. Kutunza unyenyekevu kwa kufuata mifano ya
maskini wa Injili ambao ndio waliompokea
Mkombozi .
kwa mambo mengi mengine ya dini tembelea
https://ludovicktmedia.blogspot.com/

Mahaba kwa wanawake wa siku hizi

Wanawake wengi siku hizi hawajui au hawataki kuonesha mahaba
Nimefanya kautafiti kangu kadogo nimegundua wanawake wengi siku hizi hawaonyeshi mahaba yani kwa ujumla hawako “Romantic”. Wanawake wengi siku hizi akipata mwanaume anaona amepata mtu wa kumsaidia shida zake kwa hiyo hata akiwa ndani ya mahusiano anafikiria zaidi kutatuliwa shida zake kuliko mahusiano yenyewe.

💞
Wanawake wa siku hizi wengi, kwa mfano umemtoa out kidogo mkapate walau msosi sehemu nzuri, mkianza kula mpaka mnamaliza hakumbuki hata kukulisha kidogo kimahaba. Unakuta anakula msosi kimpango wake utafikiri anakula na kaka yake. Mnatoka kidogo mnatembea unakuta anatembea na wewe utafikiri anatembea na kaka yake; yani unaweza ukamuacha nyuma kidogo au akawa mbele yako anashindwa kujiongeza kupitisha mkono wake kwenye kikwapa chako na kukushika kimahaba.
💞
Wakati mwingine anakuona jasho linakutoka usoni anashindwa hata kukufuta kimahaba anakutazama tu utafikiri wewe ni kinyago cha mpapure. Wakati anakuaga anaondoka utafikiri anamuaga kaka yake hakupigi hata busu. Mwanamke unazungumza nae hakushiki hata ndevu zako kimahaba, mwanamke unakuwa nae hakufunyii massage wala hakukati mara moja moja kucha zako kimahaba.
💞
Wakati mwingine unakuta umekaa nae mwaka mzima kwenye mahusiano lakini hajawahi kukwambia neno “Nakupenda”mpaka wewe uanze kumwambia kwanza.
💞
Wanawake wengi wa siku hizi wanapenda kudekezwa, kubembelezwa na kupewa pesa ndio maana wengi utasikia wakisema “nataka mwanaume Romantic na mwenye pesa” lakini hawajiulizi je, wao ni Romantic? Au sisi wanaume hatuhitaji hayo mahaba ya wanawake?
💞
Asili ya mwanamke ni mfariji mkuu wa mwanaume lakini siku hizi wanawake wengi wamekuwa stress kwa wanaume.
💞
Note: Hakuna mwanaume mbahili kwa mwanamke Romantic.

Yafahamu Mambo Mbalimbali kuhusiana na Wanawake kwa Ku-Download Kitabu cha SIRI ZA MWANAMKE

Kitabu hiki kina topiki Zifuatazo;
1. Mambo anayohitaji mwanamke kutoka kwa Mwanaume
2. Mambo yanayowavutia wanawake kutoka kwa wanaume
3. Mambo wanayoyapenda wanawake wakati wa kufanya mapenzi
4. Dalili za mwanamke kicheche
5. Maswali ya kujiuliza kama mwanamke anakupenda kwa dhati au anakudanganya
6. Tabia za mwanamke anayekupenda lakini hawezi kusema
7. Ishara za mwanamke aliyevutiwa na wewe
8. Dalili za mwanamke anayeelekea kukukubali
9. Mambo ambayo mwanamke hawezi kukwambia
10. Njia za kudumisha na kuamsha mapenzi na mwanamke

Kitabu hiki ni Soft copy [pdf] kwa hiyo unaweza kusoma moja kwa moja kirahisi kabisa hata kwenye simu yako. Utatumiwa Kopi ya kitabu hiki kwenye email yako na utaweza kukihifadhi na kusoma wakati wowote utakaotaka.

Historia Fupi ya Ibada ya Rozari

Katika Kalenda ya Kanisa Katoliki,
huwa mwezi wa tano na mwezi wa kumi
ni miezi ambayo imewekwa kwa ajili ya
Bikira Maria na Mama Kanisa. Hivyo
hiyo miezi huwa inasaliwa rozari.
Wengi waweza kujiuliza kuwa ni kwa
nini ifanyike miezi hiyo? Yafuatayo nimajibu, mwezi wa tano umewekwa kwa
heshima ya Bikira Maria kutokana na
nini kilitokea katika historia hapo
nyuma.
Mnamo Karne ya 16 mwezi
watano kwa miaka yote ulikuwa ni
mwezi ambao sikukuu nyingi za
kiserikali ndo zilikuwa zikifanyika.
Kanisa kwa kutambua hilo nalo
likahidhinisha pia mwezi wa tano uwe
ni mwezi wa Rozari, na kwa makusudi
zaidi Kanisa lililenga kuwa sherehe hizo
ziendane na taratibu za wakristu, ni
kwa msingi huo sherehe hizo ziliendana
na mwezi wa rozari na kutokea hapo
ikahidhinishwa kuwa mwezi wa tano wa
mwaka ni mwezi wa Bikira Maria. Pia
mwezi wa kumi (October) pia ni mwezi
wa Bikira Maria na pia ni mwezi wa
Kusali Rozari kutokana na historia ya
hapo nyuma pia, na ilikuwa kwamba
baada ya ushindi wakristo walioupata
katika vita baina yao na yule aliyeitwa
Lepanto mnamo 7 October, 1571, Papa
wa wakati ule Papa Pius V aliufanya
huo ushindi kuwa ulitokana na
maombezi ya Bikira Maria, na alisema
kuwa rozari ni silaha kubwa hata kuliko
silaha kubwa za kivita. Ni Kwa msingi
huu tunaona kuanzia hapo mwezi wa
kumi ukawa mwezi uliotengwa na
Mama Kanisa kwa Bikira Maria, na pia
ukaitwa mwezi wa Rozari.

HISTORIA YENYEWE

Ni kwamba sala ya Rozari inasemekana
kuanzishwa na Mt. Dominico
aliyezaliwa mnamo mwaka 1170 na
kufariki mwaka 1221 na hiyo sala Mt.
Dominico aliipata kwa njia ya ufunuo
ambapo Bikira Maria alimtokea na
kumwamuru awe anasali rozari. Bikira
Maria alimwamuru mtakatifu Dominico
kusali rozari kwa kipindi hicho iwe
kama silaha yake ili kupambana na
uzushi uliokuwa umeibuka ukipingana
na mafundisho ya Kanisa, na huo
uzushi uliitwa ‘ Albigensia’ hili ni kundi
lilokuwa na imani kuwa Duniani kuna
nguvu nguvu mbili zenye uwiano sawa
lakini hupingana na kupigana moja
baada ya nyingine, nazo nguvu hizo ni
Mungu na Shetani. Hivyo hawa
waliamini kabisa kuwa Mungu na
Shetani wana nguvu sawa ( Dualistic )
waliamini pia kuwa dunia hii imejaa
uovu kwa kuwa iliumbwa na mwovu. Ni
kwa msingi huu Kanisa liliamua
kupambana na hawa wazushi ambao
pia walionekana kupotosha mafundisho
ya Kanisa. Ndipo tunaona Bikira Maria
anamtokea Mtakatifu Dominico na
kumwambia asali rozari ili kupambana
na mafundisho hayo ya kizushi. Ni Papa
Pio V ambaye mnamo mwaka 1569
alihidhinisha rasmi kusali rozari kwa
kanisa nzima na kuhidhinisha rozari
iwe jinsi tunavyoiona sasa. Katika zile
zama za kati, watawa wamonaki
walizoea kusali zaburi 150, na kwa
upande wa waumini walei ambao kwa
kipindi hicho hawakujua kusoma zaburi
iliwabidi wasali sala ya Baba yetu mara
150 baadala ya zaburi 150 na hizo baba
yetu walizisali kwa kuhesabu punje 150
zilizokuwa zimefungwa kwenye kamba
ndefu ambayo kwa lugha ya kitaalamu
iliitwa “ Corona ” au kwa Kiingereza “
Crown ” kadiri ibada kwa Bikira Maria
ilivyoendelea kushamiri mnamo Karne
ya 12, sala kwa Bikira Maria
ilianzishwa na hivyo kuanza kusali
salamu maria 150 baadala ya baba yetu
150.
Salamu Maria 150 hapo baadaye
zilikuja kugawanywa katika makundi/
mafungu na Mtawa mdominica
aliyeitwa Henry Kalkar ( 1328-1408),
ambapo kila tendo la rozari lilikuwa na
mafungu 50 ya salamu Maria ambapo
pia kila fungu liligusia maisha ya Bikira
Maria na Yesu katika historia ya
wokovu wetu. Zaidi ya hapo, mtawa
mwingine wa mdominican aliyeitwa
Alanus de Rupe aliendelea kugawanya
hiyo historia ya matendo ya wokovu
wetu katika matendo ya furaha ,uchungu,
na utukufu kama tunavyoyaona sasa.
(NB Matendo ya mwanga hayo ni ya
majuzi siyo ya wakati ule). Na
nikuanzia hapo Bikira Maria amepewa
nafasi kubwa katika shirika la watawa
wa Dominican. Hivyo utamaduni wa
kusali rozari umeendelea karne hata
karne, mfano Papa Leo XIII (1878-1903)
aliweka msisitizo mkubwa juu ya ibada
ya rozari kwa Bikira Maria. Kuanzia
September 1, 1883 Baba Mtakatifu Leo
XIII aliandika jumla ya barua za
kichungaji 11 zote zikiwa zinaweka
mkazo juu ya rozari. Hivyo rozari ni
sala inayotokana na maandiko
matakatifu( Biblia). Mafumbo ya rozari
yote yanapatikana katika agano jipya
ambapo ndo tunaona matendo ya Bikira
Maria na Yesu Kristo katika wokovu
wetu.
tunakumbushwa uchungu aliopata
Bikira Maria Katika maisha yake hasa
ule utabiri wa Simeoni kwa Bikira
Maria juu ya mateso na kifo cha
mwanae Yesu, Matendo saba ya furaha
kwa Maria ambapo yaananza na
kupashwa habari kwa Bikira Maria na
Malaika wa Bwana, kupalizwa
mbinguni, na matendo ya huruma ya
Bikira Maria kwa wale ambao
wanaendelea kuteseka hapa duniani.

JE, WAKATOLIKI WANABUDU SANAMU?

Mpenzi msomaji, kumekuwa na tuhuma nyingi dhidi ya wakatoliki kwamba wanaabudu sanamu. Je, tuhuma hizo zina ukweli gani? Hilo ndilo swali tunalotaka kujibu leo.
Amri ya kukataza ibada kwa sanamu imewekwa wazi katika Biblia Takatifu, Kutoka 20:4-5, “Usijifanyie sanamu ya miungu wa uongo, au kinyago chochote kilicho mbinguni, katika nchi au majini chini ya dunia. Usiisujudie wala kuitumikia; kwa kuwa mimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu.”
Sheria hiyo inapatikana pia katika Kitabu cha Kumbukumbu la Torati 5:8-9: “Usijifanyie sanamu za miungu za kuchonga, wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Isivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu.”
Ni kutokana na vifungu hivyo vya Maandiko Matakatifu, Waamini wa Kikatoliki wamekuwa wakituhumiwa, kushtakiwa na kushambuliwa na baadhi ya waamini wa madhehebu mengine kwamba wanapingana na maagizo ya Mwenyezi Mungu, yanayokataza ibada kwa sanamu. Tuhuma hizo zinakuwa nzito zaidi, hasa zinapohusishwa na Ibada inayofanywa na Waamini Wakatoliki siku ya Ijumaa Kuu kila mwaka.

KUNA TOFAUTI KATI YA KUABUDU NA KUHESHIMU

Mpenzi msomaji, kuna tofauti kubwa kati ya kuabudu na kuheshimu. Kamusi ya Kiswahili ya Maana na Matumizi, ya mwaka 1993, iliyoandikwa na SALIM K. BAKHRESSA, na kuchapishwa na OXFORD UNIVERSITY PRESS, DAR ES SALAAM, inaeleza kuwa neno “kuabudu” maana yake ni “kuomba au kufanya ibada”; na neno “kuheshimu” maana yake ni “kutukuza, kustahi au kuogopa.”
Katika maana yake ya ndani, anayeabudiwa na mwenye haki ya kuabudiwa ni Mungu peke yake. Hakuna mtu, kiumbe wala kitu chochote kinachopaswa kuabuduiwa na chenye haki ya kuabudiwa. Mtu, kiumbe au kitu hupewa heshima tu, tena ya kiwango maalum. Kwa mfano, Bikira Maria, kwa sababu ya nafasi yake katika kazi ya ukombozi, anapewa heshima ya juu kuliko watakatifu wengine. Watakatifu hao wengine hupewa heshima ya kadiri tu, chini ya heshima ile anayopewa Bikira Maria.

KWA NINI MUNGU PEKE YAKE ANASTAHILI KUABUDIWA?

Tumesema ni Mungu pekee yake, ndiye anayestahili kuabudiwa, kwa sababu ndiye MUUMBA wa vitu vyote, vinavyoonekana na visivyoonekana; ndiye anayevitawala na kuviongoza vitu vyote; ndiye mwenye uwezo juu yetu sisi wanadamu na viumbe vingine vyote; ndiye anayejua yote; ndiye aliye pote kwa ajili yetu; ndiye mwanzo na mwisho wa kila kitu; ndiye mkuu na Bwana wa wote.
Aidha, tunapomwabudu Mungu, tunakiri kwamba ndiye aliyetuumba na “ndani yake yeye sisi tunaishi, tunajimudu na tuko!” (Mdo.17:28). Kwa kufahamu hilo, Wakatoliki hawawezi kumwabudu mtu, kiumbe au kitu chochote, isipokuwa Mungu tu.

MAMBO MAKUU NA MUHIMU KATIKA IBADA YA SANAMU

Ili kufahamu vema kinachofanywa na Wakatoliki ni vema kufuatilia na kutafakari yale wanayoyafundisha na kuyasadiki wao wenyewe, badala ya kuwahukumu kadiri watu wengine wanavyofikiri na kusema. Ukweli ni kwamba hakuna Ibada yoyote ya sanamu katika Kanisa Katoliki. Hilo ni dhahiri kwa sababu ili ibada ya sanamu iwe kweli kuabudu sanamu lazima yawepo mambo makuu na muhimu mawili: Kwanza, NIA KAMILI YA KUABUDU SANAMU INAYOHUSIKA;
Pili, KUWEPO NA IBADA YA DHATI YA KUABUDU SANAMU. Ikitazamwa kwa makini, hayo mambo mawili yanakosekana katika Kanisa Katoliki linapokuja suala la picha na sanamu. Kwa hiyo, Wakatoliki hawaabudu sanamu wala picha. Kama ni hivyo, wakatoliki wanafanya nini na hizo sanamu au picha? Wanaziheshimu tu! Tukumbuke kuwa anayemwabudu mtu, kiumbe au kitu, ni sharti akihesabu na kukisadiki kuwa ndicho kinachomwezesha kuishi, kujimudu na kuwa na uhai wake (Rej. Mdo.17:28).

JE, BINADAMU TUNAHITAJI SANAMU AU PICHA?

NDIYO. Binadamu tunahitaji sananmu au picha, tena ni jadi yetu! Kwa sababu gani tunahitaji picha maishani mwetu? Kwa sababu katika udhaifu wetu, mara nyingi tunaweza kufikiri vema kwa kutumia vielelezo au vichokoo vyenye kuonekana na kugusika. Kwa njia ya vielelezo hivyo, binadamu tunaweza kuyafikia kwa urahisi mambo magumu na mafumbo yaliyo juu ya fikra zetu za kawaida. Ndiyo maana tukiona picha au sanamu ya Yesu au Mama Maria au Watakatifu wengine, akili zetu zinaweza kutafakari mambo matakatifu na kupata picha ya kina cha msamaha wa dhambi na mapendo ya Mungu kwetu wanadamu.

KWA NINI WAKATOLIKI HAWAABUDU SANAMU AU PICHA?

Wakatolikihawaabudu sanamu kwa sababu wanajua kwamba Mungu pekee ndiye anayepaswa kuabudiwa. Kwa hiyo, hawaziabudu sanamu au picha kwa sababu wanajua kwamba hivyo siyo Mungu. Zaidi hayo, wanajua kwamba Mungu mwenyewe amekataza kuziabudu sanamu na picha kwani hazina daraja la Muumba. Mungu amepiga marufuku kuzigeukia na kuzisujudia (Law.19:4). Aidha, wameaswa kuziepuka sanamu na Ibada kwa sanamu – “Watoto wangu, epukaneni na sanamu za miungu!” (1Yoh.5:21). Pia wakatoliki wanajua kuwa sanamu na picha hazina uwezo wowote wa kimungu. “Mungu wetu yuko mbinguni, hufanya yote anayotaka. Miungu yao ni fedha na dhahabu; imetengenezwa na mikono ya wanadamu. Ina vinywa lakini haisemi. Ina macho lakini haioni. Ina masikio lakini haisikii. Ina pua lakini hainusi. … Wote wanaoitengeneza wanafanana nayo, kadhalika na wote wanaoitumainia. Enyi wa nyumba ya Israeli mtumainieni Mwenyezi Mungu, yeye ndiye msaada wenu na ngao yenu” (Zab.115:3-9). Pia kuziabudu sanamu ni jambo la kidunia, ambalo haliwezi kumpeleka mtu peponi (Rej. Isa.45:16; Isa.45:20; Gal.5:20). Kwa hiyo, Wakatoliki wanajua kuwa kuabudu sananmu na picha ni jambo haramu kabisa mbele ya Mungu, Mwumba wao (1Pet.4:3-4).

IBADA YA KWELI YA SANAMU INAKUWAJE?

Ibada ya kweli ya sanamu siyo rahisi hivyo, kama baadhi ya watu wanavyodhani! Ibada ya kweli ya sanamu siyo kitu cha mchezomchezo, kama baadhi ya watu wanavyofikiri na kusema. Ibada ya Sanamu ni suala la kuabudu, na kuabudu siyo suala la kuwa na kitu au kikiheshimu tu, bali ni kwenda mbali zaidi ya hapo! Hivyo kumiliki sanamu au picha, mathalani majumbani au kanisani, hakusemi lolote juu ya uwepo wa ibada ya sanamu kwa wale wanaohusika nazo. Kwa hiyo, ikiwa watu hawazipi sanamu au picha hizo mahali pa Mungu wa kweli, basi hawana hatia yoyote.
Jambo muhimu hapa ni kwamba wamiliki wa sanamu au picha hizo wanaziheshimu tu huku wakijua kuwa wenyewe wanaowakilishwa na sanamu au picha hizo hawapo pale kwa hali halisi. Katika maana hiyo, inakuwa sahihi kabisa kuziheshimu picha za marais, ndugu na marafiki wetu tunaowapenda, ambao hawapo karibu nasi. Picha zao hatuzikejeli wala hatuzibwagi chini na kuzikanyaga au kuzitia vumbi. Hatufanyi hivyo, siyo kwa sababu tunawaabudu watu hao au vitu hivyo, bali kwa sababu tunawapenda na kuwathamini wenyewe katika hali zao halisi.
Kwa mfano ikiwa tuna kitabu cha picha (Album) chumbani, chenye picha 100 za ndugu, rafiki na jamaa zetu, hatusemi tuna miungu 100 tunaowaabudu nyumbani mwetu! Vinginevyo, mambo yangetisha sana majumbani mwetu! Wenye picha hizo hatuwaabudu kamwe, ila tunawapa heshima tu kwa sababu tunawajali na kuwapenda. Kwa nini tusiwape heshima hiyo, ambayo ni kitu cha bure! Ukweli huo pia unahusu Bendera ya Taifa, Wimbo wa Taifa, nk.

JE, MUNGU ANACHUKIA KILA SANAMU NA PICHA?

Mungu hachukii kila sanamu au picha. Hapa inafaa ieleweke vema kwamba Mungu alipopiga marufuku sanamu katika Kitabu cha Kut. 20:3-5 na Kumb. 5:7-10, hakupiga marufuku kila sanamu. Yeye mwenyewe anaonesha kwamba anazichukia sanamu zinazotengenezwa kusudi zichukue nafasi yake tu. Kama sanamu au picha hazihatarishi nafasi yake, hana maneno nazo! Ndiyo maana, basi, baada ya kumwagiza MUSA awaambie watu wasizitengeneze sanamu na kuziabudu kama miungu (Kut.20:4-5), alimwagiza MUSA huyo huyo azitengeneze sanamu zisizokuwa hatari, ambazo hazikupewa daraja la Mungu. Mungu alimwagiza MUSA kutengeneza sanamu katika nafasi mbili:
(i) Musa anaagizwa atengeneze sanamu mbili za Makerubi azibandike kwenye Sanduku la Agano wakifunike kiti chake cha rehema. “Utatengeneza pia mfano wa viumbe hai viwili kwa kufua dhahabu, uwaweke kwenye miisho miwili ya kiti hicho; kiumbe kimoja mwisho mmoja na kiumbe mwingine mwisho mwingine. Waweke viumbe hao kwenye miisho ya hicho kiti, lakini wawe kitu kimoja na hicho kiti. Viumbe hao wataelekeana, mabawa yao yamekunjuka kukifunika kiti cha rehema, nyuso zao zitakielekea kiti hicho” (Kut.25:18-20; Rejea pia Ebr.9:5).
(ii) Mungu alimwagiza pia Musa atengeneze Nyoka wa Shaba kama dawa kwa wale ambao waling’atwa na nyoka wa moto kule Jangwani. Musa alielezwa wazi kwamba wale ambao wangemtazama huyo nyoka wa shaba kwa imani kwa Mungu wa Israeli wangepona. “Ndipo naye Mwenyezi Mungu akamwambia Musa: Tengeneza Nyoka wa shaba, umtundike juu ya mlingoti. Mtu yeyote atakayeumwa na nyoka, akimtazama nyoka huyo wa shaba, atapona. Basi, Musa akatengeneza nyoka wa shaba, akamtundika juu ya mlingoti. Kila mtu aliyeumwa na nyoka alipomtazama huyo nyoka wa shaba, alipona” (Hes. 21:8-9; Rejea pia Yoh.3:14-15).
Basi, Musa alitekeleza maagizo hayo ya Mwenyezi Mungu, naye alifurahia. Kwa maagizo hayo mawili ni dhahiri kwamba Mungu hachukii kila sanamu au picha. Mungu anachukizwa na sanamu zile ambazo zimekusudiwa kuchukua daraja la umungu wake, maana ni yeye tu ndiye anayestahili kuabudiwa. Yule nyoka wa shaba alikuwa dawa kwa wale walioumwa na nyoka wa moto. Watu hao hawakumwabudu nyoka wa shaba, lakini walipona, siyo kwa sababu ya nguvu zake, ila kwa nguvu za mwokozi zilizokuwa nyuma yake. “Kama mtu akiitazama alama hiyo aliponywa, lakini kilichomponya siyo hicho kitu alichokiona, bali wewe uliye Mwokozi wa watu wote” (Hek.16:7).
Hapa ni vifungu vingine vya Maandiko Matakarifu, vinavyoonesha kuwa Mungu hachukii kila sanamu au picha.
1Fal. 7:29 “kulikuwa na sanamu za simba, mafahali na viumbe vyenye mabawa. Sanamu hizo za simba na mafahali zilikuwa, zimefunikwa na kutandikwa mapambo yaliyosokotwa vizuri”.
2Nyak.3:10 “Alitengeneza sanamu mbili za viumbe wenye mabawa kwa mbao, akazifunika kwa dhahabu na kuziweka mahali patakatifu sana”
Ezek.41:17-18 “… kwenye ukumbi palikuwepo na michoro iliyofanana na mitende na picha za viumbe vyenye mabawa. Kila baada ya mtende kulichorwa picha ya kiumbe chenye mabawa kukizunguka chumba chote”.
Yoh. 3:14-15 “Kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka wa shaba kule Jangwani, naye Mwana wa mtu atainuiliwa juu vivyo hivyo, ili kila anayemwamini awe na uhai wa milele.”
Ebr.9:5 “Juu ya hilo sanduku kulikuwa na viumbe wenye mabawa, na mabawa yao yalitanda juu ya mahali ambapo dhambi huondolewa”

UBAYA WA SANAMU AU PICHA UKO WAPI?

Ubaya wa sanamu au picha upo katika kuzipa sanamu au picha daraja la Mungu. Hatari na ubaya wa sanamu au picha vimo katika kitendo cha binadamu kuzipa sanamu au picha hizo daraja la Mwenyezi Mungu. Kama sanamu au picha hazipewi daraja la Mungu, haziwi hatari na wala hazina ubaya wowote mbele ya Mungu. Kwa sababu hiyo, basi, mtu anaweza kuwa na sanamu au picha ndani ya nyumba yake au kanisani, lakini bila kumkasirisha Mungu.
Zaidi ya hayo, Mungu mwenyewe anajua fika kuwa sanamu au picha fulani imepewa daraja lake au siyo. Kwa nini Mungu akasirike pale ambapo sanamu au picha haziingilii daraja na ukuu wake? Mungu mjinga wa aina hiyo hayupo! Mungu wa kweli hawezi kukasirikia picha na sanamu ambazo zinaheshimiwa tu, na wala haziabudiwi. Aidha, Mungu mwenye haki hawezi kumwadhibu na kumtupa Jehanamu mtu ambaye anamiliki picha au sanamu duniani lakini bila kuziabudu, yaani pasipo kuzipa daraja la Mungu.

BIBLIA INAWEZA KUTUSAIDIA KUIELEWA IBADA YA SANAMU?

Jibu ni ndiyo! Biblia inatoa maelezo ya kina na ufafanuzi mzuri juu ya ibada ya sanamu. Tumesema hapo juu kuwa ibada ya sanamu siyo jambo la mzaha au mchezo wa kitoto! Ni suala la kuabudu, na kuabudu siyo tu jambo la kuwa na sanamu au picha na kuiheshimu tu. Ni zaidi ya hapo! Kuna mambo muhimu ambayo lazima sanamu zitendewe, ndipo ihesabike kuwa ni ibada ya sanamu.
a) Tukitaka kujua kama kitendo fulani mbele ya sanamu ni kuabudu au sivyo, kwanza lazima iwepo nia thabiti ya mtu anayehusika katika kitendo hicho kinachofanyika. Ibada inakuwa ya kuabudu sanamu ikiwa mtu anayefanya kitendo hicho anaamini moyoni mwake kwamba hiyo sanamu au picha inayofanyiwa kitendo hicho inachukua daraja na nafasi ya Mwenyezi Mungu. Katika kitendo hicho, mtu anaamini kuwa sanamu au picha hiyo ndiyo inayomwezesha kwenda, kuishi, kujimudu na kuwa na uhai wake hapa duniani.
b) Jambo la pili ni kuangalia kama kitendo hicho kinachofanyika katika ibada hiyo ni Liturujia ya kueleweka/maalum. Baada ya kubaini nia thabiti ya mtendaji, tunaweza kuitambua ibada ya sanamu kwa kuangalia yale yanayofanyika mbele ya sanamu au picha kwa kufuatilia mambo ambayo waabudu sanamu huyafanya. Mambo hayo, ambayo waabudu sanamu wanayafanya tunaweza kuyakusanya kutoka katika Biblia yetu. Agano la Kale linaonesha kuwa Ibada ya Kuabudu Sanamu inajumuisha mambo makuu yafuatayo:
i. Kuzitolea sadaka: za kuteketezwa: Rej. Hos.4:13; nafaka na vyakula 2Fal.5:17.
ii. Kuzitolea ubani kwa heshima kamili: Rej. 1Fal.11:8; Isa. 57:6; Yer.7:18.
iii. Kuzimwagia matambiko: Rejea Isa. 57:6
iv. Kuzitolea zaka ya sehemu ya kumi ya mapato ya mwaka ya mazao ya mashambani: Rejea Hosea 2:8
v. Kuziandika meza mbele yao: Rejea Isa. 65:11
vi. Kuzibusu sanamu kwa kuzisujudia kama viumbe vyenye enzi.
Rejea 1Fal. 19:18; Hos.13:2; Ayu. 31:2.
vii. Kuziinulia sanamu mikono katika kuzisujudia: Rejea Isa.44:20
viii. Kuziangukia sanamu kifudifudi ama kuzipigia magoti kwa kuziabudu: Rejea 1Fal.18:26,28.
ix. Kuzichezea ngoma na wakati mwingine kujikatakata kwa visu kama kitendo cha ibada kwa sanamu: Rejea 1Fal.18:26,28.
Hayo yote yakichunguzwa kwa makini, tutaona wazi kuwa hakuna Ibada ya kuabudu sanamu katika Kanisa Katoliki. Kwa hiyo, shutuma kwamba Wakatoliki wanaabudu sanamu siyo za kweli, hazina msingi, na ni uchochezi wa bure wenye lengo la kuleta mafarakano na magomvi. Jambo hilo ni dhahiri kwa sababu Wakatoliki hawana nia thabiti ya kuabudu sanamu wanapotoa heshima kwa sanamu au picha mbalimbali. Pili, matendo ya kiliturujia yanayofanywa na wakatoliki katika kuheshimu sanamu hayalingani na matendo ya kiliturujia yanayofanywa na waabudu sanamu, kama ilivyoelezwa katika Biblia Takatifu, hususan Agano la Kale. Kifupi, wakatoliki hawana nia thabiti moyoni ya kuziabudu sanamu au picha, tena hawazifanyii liturujia yoyote sanamu au picha walizo nazo majumbani au makanisani.
Ni wapi ambapo Kanisa Katoliki linafanya au kuwafundisha rasmi na kuwahimiza wafuasi wake wafanye matendo hayo tisa ya kiliturujia kwa ajili ya kuabudu sanamu? Hakuna! Kwa hiyo, Wakatoliki hawana hatia yoyote ya kuabudu sanamu mbele ya Mungu. Kama mtu mmoja akifanya hivyo, hilo ni shauri lake binafsi, siyo shauri au utaratibu wa Kanisa lote. Aidha, afanyaye hivyo amepotoka peke yake, kwa sababu hajafundishwa na Kanisa Katoliki afanye hivyo. Hilo ni kweli kwa sababu mambo binafsi, siyo mambo rasmi ya Kanisa lote!
Kwa hiyo, tunaona wazi kwamba Wakatoliki hawaabudu sanamu kamwe, kama inavyodaiwa na baadhi ya waamini wa madhehebu mengine ya kikristo. Wanaotoa shutuma hizo inafaa wajiangalie kwanza wao wenyewe, maana imeandikwa: “… mtu akidhani kwamba kitu fulani ni najisi, basi, kwake huwa najisi” (Rom.14:14).

JE, IJUMAA KUU WAKATOLIKI WANAABUDU NINI?

Je, ni kweli kwamba Siku ya IJUMAA KUU Wakatoliki wanaabudu Sanamu au Mti wa Msalaba? HAPANA! WANAMWABUDU WOKOVU-YESU! Kiini cha utata hapa ni “NINI MAANA YA IBADA YA KUABUDU MSALABA” inayoendeshwa siku ya Ijumaa Kuu? Madhehebu hayo yanayofanywa na Wakatoliki Siku ya IJUMAA KUU siyo Ibada ya Kuabudu Sanamu. Labda hapa ni tatizo la lugha au maneno yanayotumika, ndiyo yanayowachanganya watu! Hilo ni kweli kwa sababu jina la madhehebu yenyewe halisemi wazi kitu gani hasa kinanuiwa kufanywa katika ibada hiyo.
Wengi hawajui nini hasa kinanuiwa kufanyika siku ya Ijumaa Kuu katika “Ibada ya Kuabudu Msalaba” – jina ambalo nimesema halitoi picha halisi ya jambo linalokusudiwa kufanyika. Mtu mwenye akili timamu akijua kitu halisi kinachofanyika siku ya Ijumaa Kuu, hawezi kusema madhehebu hayo ni Ibada ya Sanamu au kuabudu mti. Tatizo hapo ni lugha tu inayotumika katika kuieleza ibada hiyo. Labda jina hilo lichunguzwe upya na wataalamu wetu katika Kanisa na ikiwezekana kulirekebisha ili kuondoa utata kwa baadhi ya watu wenye uelewa mdogo, wenye wanaokwazwa nalo!

NINI HASA KINAFANYIKA SIKU YA IJUMAA KUU?

Wanachofanya Wakatoliki Siku ya Ijumaa Kuu ni KUUHESHIMU MTI WA MSALABA na KUMWABUDU WOKOVU. WOKOVU ni nani? WOKOVU NI YESU KRSITO BWANA WETU. Basi, kinachofanyika siku ya Ijumaa Kuu ni kumwabudu WOKOVU yaani YESU KRISTO, ambaye alitundikwa msalabani. Hivyo ndivyo anavyotangaza Kiongozi wa Ibada hiyo ya Ijumaa Kuu, pale anapotoa mwaliko kwa waamini mara tatu, ili kila muumini ausikie na kuelewa vema: “HUU NDIO MTI WA MSALABA, AMBAO WOKOVU WA DUNIA UMETUNDIKWA JUU YAKE, NJOONI TUUABUDU.” Waamini wanaalikwa kiimani kuuabudu WOKOVU, na hilo ndilo linalofanyika, yaani kuuabudu WOKOVU – YESU KRISTO. Waamini wote wanaalikwa kujongea mbele kwa imani kwenda kumwabudu YESU. Watu wanamwabudu YESU kwa sababu WOKOVU maana yake ni YESU.
Jina YESU ambalo linatokana na Kiebrabia “YESHUA”, maana yake “WOKOVU” (Rej. Mt.1:21;1:25; Lk.1:31). Ikiwa wokovu ni YESU, basi Ijumaa Kuu Wakatoliki hawaabudu sanamu au mti, bali wanamwabudu YESU KRISTO. Kwa sababu hiyo, yote yanayofanyika Siku ya Ijumaa Kuu, yanafanyika kihalali na kwa haki kwa sababu YESU KRISTO, ambaye ni WOKOVU ni MUNGU, na MUNGU peke yake ndiye mwenye haki na anayepaswa kuabudiwa. Ikiwa mkristo hataki kumwabudu YESU KRISTO, aliye Mwana wa Mungu na Mungu kamili, na ambaye ameeleta wokovu, anafanya makosa makubwa!
Basi, nasisitiza kuwa Siku ya Ijumaa Kuu, Wakatoliki hawaabudu sanamu wala mti. Wanamwabudu WOKOVU, yaani YESU KRISTO, Nafsi ya Pili ya MUNGU. Kutomwabudu YESU KRISTO ni sawa na kumkana Mungu, kukana wokovu ulioletwa naye. Basi, tujiepushe na ukanaji Mungu wa aina hiyo. Nawaalika wote Siku ya Ijumaa Kuu tufungue mioyo yetu kwa imani kubwa ili tumwone WOKOVU aliyetundikwa msalabani, apate kuukomboa ulimwengu. Kwa imani, wote tumsujudie YESU ili apate kutukumbuka katika Ufalme wake wa milele.
Hatimaye, niseme kwamba ingawa Mungu ametoa amri ya kukataza sanamu na picha (Kut. 20:4-5; Kumb. 5:6-10), lakini hachukizwi na kila sanamu au picha. Sanamu na picha ambazo hazipewi daraja la Mungu, Yeye hazichukii, kwa sababu hazichukui nafasi yake kama Muumba. Basi, Wakatoliki hawaendi kinyume na Biblia kwa kuziheshimu sanamu na picha zilizoko kwenye majumba yao na makanisani.
Shopping Cart