Makala za Kilimo

Jinsi ya kulima vizuri zao la kabichi

Kichwa cha kabichi kinapofunga vizuri, hutumika kama chakula na huvunwa baada ya kufunga na kukomaa vizuri. Kwa kawaida kabichi hupandwa kwa msimu mmoja, lakini iwapo itakuzwa kwa ajili ya kutoa mbegu hukuzwa zaidi ya msimu mmoja. Endapo inalimwa sehemu yenye maji ya kutosha, inaweza kulimwa msimu wote wa mwaka. Soko lake ni la uhakika katika kipindi chote na ni muhimu kwa afya. Pia, linaweza kutumika kama malisho ya mifugo
Mizizi: Mizizi ya kabichi hutawanyika ardhini vizuri. Kwa kawaida, huenda chini kiasi cha sentimita ishirini (20 sm), na hujitawanya kwa kiasi cha sentimita sabini na tano (75sm).
Shina: Shina la mmea wa kabichi huwa na rangi ya kijani au zambarau. Hii hutegemeana na aina ya kabichi, na kwa kawaida ni fupi.

Aina za kabichi

Kuna aina nyingi za kabichi na zifuatazo ni miongoni mwa aina hizo:
1. Prize drumhead

Aina hii hukomaa katika kipindi cha miezi 3.5
2. F1-High Breed

Aina hii hukomaa katika kipindi cha miezi 2-4
3. Duncan

Aina hii hukomaa katika kipindi cha miezi 3
4. Early Jersey wakefield

Aina hii hukomaa katika kipindi cha miezi 3.5
5. Sugar loaf

Aina hii hukomaa mapema sana, kiasi cha miezi 2.5
6. Glory of enkhuizen

Aina hii hukomaa katika kipindi cha miezi 3.5

Jinsi ya kulima kabichi

Hali ya hewa

Kabichi hustawi vyema katika sehemu yenye hali ya baridi, hali ya joto jingi haifai kwa kabichi kwa kuwa huathiri uotaji na ukuaji wake. Joto jingi pia husababisha kulegea kwa vichwa vilivyofunga. Zao hili hustawi vema katika maeneo yenye mwinuko wa zaidi ya mita 100 toka usawa wa bahari.

Udongo

Zao hili linaweza kustawishwa kwenye udongo wa aina yoyote mradi tu udongo huo usiwe na chumvichumvi nyingi na usiotuhamisha maji. Udongo wa kichanga na ule usio na rutuba ya kutosha husababisha kabichi kukomaa upesi na kuzaa kabichi hafifu zenye vichwa vidogo.

Kitalu cha kabichi

Kitalu ni muhimu katika uzalishji wa zao hili. Ni vema kutengeneza matuta yenye upana wa mita moja, na urefu wowote kulingana na matakwa ya mkulima. Mbolea za samadi na zenye asili ya chokaa zichanganywe vizuri kwenye udongo. Kiasi cha gramu 500 za mbegu huhitajika kwa hekta moja. Katika upandaji kwenye kitalu ni vizuri kutengeneza mistari katika tuta, umbali toka mstari hadi mstari uwe sentimita ishirini (20). Udongo kiasi kidogo utumike katika kufunika mbegu.
Baada ya mbegu kuota ni vizuri kupunguza baadhi ya miche na uwe katika kipimo cha sentimita 2-3 toka mche hadi mche. Hii itasaidia kuwa na miche mifupi na yenye nguvu. Inafaa kunyeshea kitalu mara moja au mbili kwa siku na katika sehemu za joto ni vizuri kuweka kivuli katika matuta. Katika wiki ya tatu, hadi wiki ya nne, ni vyema kuondoa kivuli kidogo kidogo huku ukipunguza unyeshaji. Hali hii itasaidia miche isipate mshtuko wa uhamishaji shambani.

Kuhamisha na kupanda

Hamisha na kupandikiza miche shambani ikiwa na umri wa wiki nne, wakati huo miche ikiwa na majani manne ya mwanzoni na urefu wa kiasi cha sentimita kumi na mbili (12). Wakati wa upandaji, ni vizuri udongo ukashindiliwa kwenye kila mche. Inafaa upandaji ufanyike mara moja, na ni vizuri ukafanyika nyakati za jioni au asubuhi sana, na udongo uwe na unyevu wakati wote.

Nafasi kati ya mmea

Katika mstari hadi mstari inatakiwa iwe sentimita 60-75. Kutoka mmea hadi mmea ni sentimita 30-60. Pia sentimita 75-90 inaweza kutumika kati ya mstari na mstari.

Mbolea

Ni vizuri kuweka kiasi cha viganja 2-3 vya mbolea ya samadi iliyooza vizuri katika kila shimo.

Palizi

Wakati wa palizi ni vizuri mkulima akawa mwangalifu ili asiharibu mizizi. Wakati kabichi inapoanza kufunga hufunika ardhi, hivyo, husaidia kuzuia magugu yasiote, kwa wakati huu hakuna haja ya kupalilia.

Kuvuna:

Kabichi hukomaa katika kipindi cha siku 60-100 tangu kupandwa. Kwa ajili ya kuuza ni vizuri kuvuna wakati vichwa vinapofunga vizuri na huwa na uzito wa kutosha kabichi iangaliwe na kutunzwa baada ya kuvunwa ili isikwaruzwe na kuoza kabla ya kutumiwa. Kwa kawaida hekta moja hutoa mavuno kiasi cha tani 50-80.

Yafahamu Mambo Mbalimbali ya muhimu kuhusu kilimo cha Mazao ya Mboga Mboga kwa Ku-Download Kitabu cha MBINU ZA KILIMO BORA CHA MBOGA

Ni kitabu kinachotoa elimu ya Kilimo Cha Mboga. Kipo katika Mfumo wa PDF (Soft copy).

Kina kurasa 100 na utaalamu wa mazao zaidi ya 10, ambayo ni nyanya, kabichi, bamia, vitunguu maji, vitunguu twaumu, hoho, matikiti, karoti, uyoga na matango. Bila kusahau kilimo cha mboga kama chainizi na mchicha.

Pia utaweza kufahamu mbinu mbalimbali za kilimo cha mboga kama vile kuandaa shamba na kitalu, udhibiti wa wadudu na magonjwa katika mboga, kuvuna na kuhifadhi mboga, vilevile utajifunza kuhusu kilimo cha matone.

Kitabu hiki ni Soft copy [pdf] kwa hiyo unaweza kusoma moja kwa moja kirahisi kabisa hata kwenye simu yako. Utatumiwa Kopi ya kitabu hiki kwenye email yako na utaweza kukihifadhi na kusoma wakati wowote utakaotaka.

Jinsi ya kutengeneza mbolea ya mboji kitaalamu na kwa urahisi

Mbolea ya mboji hutokana na mabaki ya majani na miti. Majani na miti yanapooza hugeuka na kutengeneza virutubisho ambavyo husaidia kurutubisha udongo na kupunguza gharama.

Mboji ikichanganywa kwenye udongo huifanya mimea kustawi na kuwa na afya ya kujikinga na magonjwa yanayoshambulia mimea. Kwa kawaida wadudu waharibifu hutafuta mimea ambayo ni dhaifu. Udongo ambao umeimarishwa kwa mboji huwa na mimea michache dhaifu. Kwa hivyo, siyo rahisi kushambuliwa na wadudu.

Mbolea ya mboji ina madini yanayosaidia kuyeyusha madini mengine yaliyo kwenye udongo na kufanya yapatikane zaidi kwa ajili ya mimea kwa muda mrefu. Vijidudu ambavyo hujilisha kwa njia ya mbolea ya mboji kwa muda mfupi hushikilia udongo pamoja, na kuufanya udongo uwe bora na wenye afya.

Faida nyingine ya mbolea ya mboji ni kwamba mbolea hii hupunguza ama huondoa kabisa utumiaji wa mbolea za chumvichumvi na dawa za kuua wadudu ambazo zinaweza kuwa na madhara kwa afya za watu na udongo, ambazo pia ni gharama sana kununua.

Mahitaji ya kutengenezea mboji

Wakati wa kutengeneza mboji unahitajika kuwa na malighafi za kijani na kahawia.

Malighafi za kijani
Mimea yenye kijani kibichi na ambayo haijachanua inafaa zaidi katika kutengezeza mboji, na iwe imekatwa karibuni. Mabaki ya chakula na matunda pia yanajumuishwa katika kundi la malighafi za kijani.

Malighafi za Kahawia
Kundi la malighafi za kahawia ni pamoja na mimea ambayo imekauka baada ya kukatwa muda mrefu, pamoja na kinyesi cha wanyama wafugwao. Udongo na maji ni sehemu muhimu ya mahitaji kwa ajili ya kutengeneza mboji.

Vitu visivyotakiwa kwenye mboji

  • Mabaki ya mimea ambayo imeambukizwa magonjwa au imeshambuliwa na wadudu haitumiwi kwani inaweza kuwa na mayai ya wadudu na inaweza kuendelea kuzaliana.
  • Mimea yenye tindi kali kama vile migunga na Eucalyptus haifai, ijapokuwa kuna wakati inaweza kutumika kutengeneza mboji maalum kwa ajili ya kuongeza kiwango cha tindi kali kwenye udongo inapohitajika.
  • Magugu sugu kama sangare, mashona nguo na ukoka mgumu hayafai kwa kuwa yatasambaza mbegu za magugu katika shamba lako.
  • Usitumie kinyesi cha wanyama kama mbwa na paka.

Kutengeza mboji

Ili uweze kutengeneza mboji nzuri, unatakiwa kurundika rundo kwa matabaka. Kiwango cha wastani kinachofaa kutengeneza mboji ni chenye urefu wa mita moja, na mita moja upana. Rundo ambalo ni dogo kuliko hili haliwezi kuhifadhi joto la kutosha kuozesha malighafi. Hakuna kikomo cha ukubwa wa biwi la mboji, inategemea na ukubwa wa eneo ulilonalo na unataka mboji kiasi gani. Chakuzingatia ni kuwa lisiwe dogo.

Hatua za kufuata kutengeneza mboji

Hatua ya 1
Ondoa majani yote pamoja na vitu vingine vinavyoweza kuharibu mboji yako, kisha lainisha udongo kiasi cha inchi sita kwa kutumia rato au jembe. Hatua hii inasaidia maji kupenya chini
ya rundo la mkusanyiko wa kutengenezea mboji.

Hatua ya 2
Weka tabaka la kwanza kubwa kuliko matabaka mengine. Unaweza kutumia majani makavu, mabuwa ya mahindi na matawi madogo madogo ya miti. Vitu hivi pia ni vizuri kwa rundo la mboji na hurahisisha umwagiliaji maji. Weka rundo la tabaka la kwanza la mabuwa ya mahindi vijiti na matawi madogomadogo ili liwe tabaka lenye inchi sita kwa mita moja kila upande.

Hatua ya 3

Tengeneza tabaka la pili lenye ukubwa wa inchi mbili na malighafi za kijani. Kumbuka kwamba: Tabaka liwe jemjembamba kuliko tabaka la kwanza. Kama una mabaki ya chakula ongeza kwenye tabaka hili.

Hatua ya 4

Weka Tabaka la tatu la udongo lililochanganywa na mbolea au majivu. Tabaka hili liwe jembamba, kama unene wa robo inchi. Unahitaji kutumia kiasi kidogo tu cha mbolea kufunika sehemu ndogo tu katikati ya rundo la mboji kama vile futi moja kwa futi moja. Ni muhimu kutotumia mbolea nyingi kwenye rundo la katikati. Kama unatumia majivu, kiasi kidogo tu kitumiwe katikati ya rundo la mboji. Ukishaweka mbolea katikati, unaweza kuizungushia udongo kufunika tabaka la kwanza.

Hatua ya 5

Ongeza maji ya kutosha kila wakati kwenye rundo la mboji ili liwe na unyevunyevu, lakini yasiwe mengi kiasi cha kutota. Kumbuka, rundo la mboji liwe na unyevunyevu mfano wa sponji iliyowekwa kwenye maji na kukamuliwa.

Hatua ya 6

Kwa kufuata hatua zilizotangulia, kama unataka kuongeza matabaka, rudia kama ulivyofanya mwanzo. Tabaka la majani makavu, ya rangi ya kahawia lenye inchi mbili, likifuatiwa na tabaka la kijani la inchi mbili, likifuatiwa na tabaka jembamba la udongo uliochanganywa na mbolea au majivu au vyote. Endelea kuweka matabaka haya mpaka matabaka yako yawe na urefu wa futi tatu au nne kwenda juu.

Hatua ya mwisho

Weka tabaka la juu mwisho lenye majani makavu ya kikahawia lenye unene wa inchi tatu. Hii husaidia kuhifadhi harufu ambayo wakati mwingine hutokea wakati wa uozaji. Hii pia husaidia kufukuza wanyama ambao huvutiwa na kutaka kuona kuna nini kwenye rundo la mboji.

Baada ya muda Rundo la mboji litakapokuwa tayari, utabakiwa na mboji ambayo itaonekana kama udongo mweusi ulio na mbolea nzuri.

Matumizi ya mbolea ya Mboji

Chukua mboji ambayo ni tayari yani iliyo na udingo mweusi wenye mbolea nzuri na utandaza tabaka jembamba kwenye mazao yako na mimea itastawi, kunawiri vizuri na kutoa mazao bora.

Yafahamu Mambo Mbalimbali ya muhimu kuhusu kilimo cha Mazao ya Mboga Mboga kwa Ku-Download Kitabu cha MBINU ZA KILIMO BORA CHA MBOGA

Ni kitabu kinachotoa elimu ya Kilimo Cha Mboga. Kipo katika Mfumo wa PDF (Soft copy).

Kina kurasa 100 na utaalamu wa mazao zaidi ya 10, ambayo ni nyanya, kabichi, bamia, vitunguu maji, vitunguu twaumu, hoho, matikiti, karoti, uyoga na matango. Bila kusahau kilimo cha mboga kama chainizi na mchicha.

Pia utaweza kufahamu mbinu mbalimbali za kilimo cha mboga kama vile kuandaa shamba na kitalu, udhibiti wa wadudu na magonjwa katika mboga, kuvuna na kuhifadhi mboga, vilevile utajifunza kuhusu kilimo cha matone.

Kitabu hiki ni Soft copy [pdf] kwa hiyo unaweza kusoma moja kwa moja kirahisi kabisa hata kwenye simu yako. Utatumiwa Kopi ya kitabu hiki kwenye email yako na utaweza kukihifadhi na kusoma wakati wowote utakaotaka.

Jinsi ya kutengeneza mbolea ya maji ya kunyunyiza kwenye majani

Mbolea ya kunyunyiza ni nzuri kwani inasaidia kuupa mmea virutubisho moja kwa moja kupitia kwenye majani au shina ambapo ndipo chakula kinahitajika.

Faida za mbolea ya maji ni pamoja na kuongezeka kwa kiwango cha mavuno, uwezo wa mimea kukabiliana na wadudu pamoja na magonjwa, kuvumilia ukame, na kuongeza ubora wa mazao.

Jinsi ya kuandaa mbolea ya maji kwa kutumia samadi

Mbolea ya maji hutengenezwa kwa kuchukua kiroba kilichojazwa samadi, aina mbalimbali ya mimea yenye virutubisho na inayoaminika kuwa dawa ya mimea. Kiroba hicho kinafungwa kwenye kijiti, na kutumbukiza kwa kuning’inia kwenye pipa lililojazwa maji.

Kiroba hicho ni lazima kichukue kati ya kilo 30-50 za samadi pamoja na aina nyingine za mimea kwa maji lita 200 (tazama mchoro). Unaweza kushika upande mmoja wa mti na kunyanyua na kushusha kila baada ya siku tano ili kuchanganya na kuharakisha kutolewa kwa virutubisho zaidi.

Kwa kawaida mchanganyiko huo unakuwa na harufu kali sana maana Nitrojeni nyingi inayopatikana hugeuka kuwa Amonia. Ni vizuri kufunika pipa ili kuzuia kuyeyuka kwa nitrojeni. Harufu ikishaisha, ujue mbolea yako ipo tayari kwa matumizi.

Ongeza maji na utingishe vizuri kabla ya kutumia. Nyunyizia mimea yako kila wiki mpaka utakapoona mabadiliko.

Jinsi ya kutengeneza mbolea ya maji kwa kutumia mimea peke yake (Majani fresh)

Mbolea hii hutengezwa kwa kuchukua majani mabichi na kuyakatakata na kisha kuyachanganya na maji kidogo.

Baada ya kuchanganya na maji unaacha kwa siku tatu au nne ambapo utatikisa mchanganyiko wako kila siku.

Baadae utatikisa na kuchanganya na maji na kunyunyiza shambani.

Vilevile Unaweza kutumia mbolea ya majani ambayo itakuwa kama dawa ya kuulia wadudu, kwa kutumia aina ya mimea kama vile mivule, mibangi mwitu, majani ya minyanya, mwarobaini, mashona nguo, pamoja na vitunguu saumu. Aina hii ya mimea inasaidia sana katika kuzuia magonjwa, wadudu na kutoa virutubisho muhimu kwa mimea vinavyosaidia mkulima kupata mazao bora bila gharama ya ziada ya kununua virutubisho.

Vigezo vya kunyunyiza mbolea ya maji

Ili upate matokeo mazuri wakati wa kunyunyiza mbolea ya maji unatakiwa kufuata vigezo vifuatavyo:
• Inashauriwa kutumia mbolea iliyochanganywa vizuri ili kuepukana na kuunguza mimea.
• Acha maji utakayotumia kuchanganyia mbolea yako nje katika pipa lililowazi usiku kucha, hii inasaidia kutoa madini hatarishi, na kufanya mchanganyiko wenye faida kwa mimea.
• Unatakiwa kutingisha vizuri mbolea yako ya maji kabla ya kunyunyiza. Chembechembe ndogo ambazo hazikuyeyuka zinaweza kuziba mdomo wa bomba la kunyunyizia.
• Matokeo mazuri yanaweza kupatikana endapo mbolea imechanganywa vizuri na kunyunyiziwa wakati hakuna upepo.
• Unatakiwa kunyunyizia mbolea wakati wa asubuhi au jioni wakati hakuna joto na upepo ukiwa umepungua.

Angalizo
Kabla ya kunyunyiza dawa au mbolea uliyoitengeneza mwenyewe shambani nyunyiza kwenye eneo dogo au mimea michache kwanza ili uone kama inaunguza au haiunguzi. Kumbuka kuwa mchanganyiko mwingine ukiwa cream au ukikolea sana unaweza kuchoma. Kwa hiyo kuepuka hili nyunyiza mahali padogo kwanza.

Mambo 6 muhimu ya kuzingatia kupata udongo bora mzuri shambani

1. Usiuchoshe sana udongo

Udongo ni kiungo muhimu sana katika uzalishaji wa mazao. Ni mfumo wa uhai kwa mimea. Kwa hiyo, mkulima ni lazima alenge katika kutunza uhai wa udongo na kuepuka usumbufu kwa uhai wa udongo.
Sababu muhimu za kulima/kutifua udongo ni:
• Hulainisha udongo ili kuruhusu mizizi ya mimea kupenya kwa urahisi.
• Kutifua kunaboresha uwezekano wa kupenya kwa nitrogen na oxygen kutoka kwenye hewa.

• Kunawawezesha viumbe hai waliopo kwenye udongo kufanya kazi zao ipasavyo.
• Kunasaidia Kuandaa sehemu ya kuwekea mbegu.
• Kutifua kunauongeza uwezekano wa maji kupenya kwenye udongo na kupunguza uyeyukaji wa maji.
• Kuchanganya mabaki ya mimea na samadi kwenye udongo

2. Acha udongo upumue

Kama ilivyo kwa binadamu, viumbe hai wanahitajika kwa udongo wenye rutuba, pia mimea inahitajika kwa ajili ya binadamu kupata hewa safi ya oxygen. Kuchanganya matandazo,na mboji kwenye udongo ni muhimu sana ili kuboresha mzunguko wa hewa. Viumbe hai wadogo wadogo, wadudu, minyoo, na wanyama wengineo wanapenyeza hewa kwenye udongo.

3. Weka Matandazo kwenye udongo

Huu ni utaratibu wa kufunika udongo kwa kutumia mabaki ya mimea, kwa mfano, matawi madogo madogo ya miti, majani, mabaki ya mimea ya mazao, magugu na kadhalika. Hata hivyo inahitajika nguvu kazi kwa ajili ya kutawanya matandazo.

Matandazo yanazuia mmomonyoko wa ardhi unaotokana na maji na upepo, yanasaidia ardhi kunyonya maji ya mvua, kutunza unyevu unyevu kwenye udongo kwa kuzuia myeyuko wa maji ardhini.

Matandazo yanapo oza hutoa virutubisho vinavyoboresha na kuongeza rutuba kwenye udongo, mbali na hilo pia hubadilika kuwa udongo mweusi wenye rutuba zaidi. Kama kuna uhitaji wa kuharakisha kuoza kwa matandazo ili kuongeza rutuba kwenye ardhi kwa haraka, kinyesi cha ng’ombe kinaweza kuwekwa na kutandazwa juu ya matandazo, hii husaidia kuongeza virutubisho vya nitrogen.

Matandazo yana faida nyingi sana kwenye ardhi, lakini pia yanaweza kusababisha madhara. Mabaki ya mboga za majani yasitumike kama matandazo kwani yanaweza kusababisha wadudu na magonjwa kwa mimea. Viumbe hatari kama bangu (stem borers) wa shina wanaweza kuishi kwenye mabaki ya mimea.

Mabaki ya mimea iliyokuwa imeathiriwa na magonjwa ya virusi au fangasi yasitumike kama matandazo kuepuka uwezekano wa magonjwa hayo kuambukizwa kwa mazao yatakayopandwa msimu utakaofuata. Kilimo cha mzunguko ni njia bora kuepuka athari hiyo.

4. Panda mazao kwa mzunguko

Kupanda mazao kwa mzunguko ina maana ya kuwa na aina mbalimbali ya mazao katika eneo moja kwa msimu.

Kwa mfano, kama shamba lako umepanda mahindi na maharagwe kwa kipindi cha mwaka mmoja, mkulima anaweza kubadili mzunguko kwa kupanda aina nyingine ya mazao katika eneo hilo kwa mwaka unaofuata.

Mimea iliyo mizuri zaidi katika kilimo cha mzunguko ni pamoja na jamii ya kunde, au malisho kama sesbania ambayo husaidia kuongeza rutuba kwenye udongo.

5. Lisha udongo

Udongo unatakiwa ulishwe ili uwe na virutubisho. Hii ni kazi muhimu sana kwa kila mkulima. Mkulima anaweza Kuulisha udongo kwa kutumia samadi na mboji. Kumbuka udongo uliotumika sana bila virutubisho, umekufa, hauwezi kuzalisha.

6. Kuwa makini na maji

Maji ni mazuri shambani, lakini maji yakizidi ni hatari. Maji yakizidi shambani yanaweza kusababisha mmomonyoko wa udongo. Mmomonyoko wa udongo ni tishio na baa hatarishi kwa rutuba kwenye udongo. Mmomonyoko unaondoa tabaka la juu la udongo, sehemu ambayo ndiyo yenye rutuba zaidi.

Kupanda mimea kwa matuta (kontua) hupunguza kasi ya maji. Baada ya miaka kadhaa, nyasi zinazopandwa zinazopandwa kwenye matuta ya kontua husaidia kuunganisha na kusawazisha sehemu iliyotengwa, kwa kuwa udongo unaomomonyolewa hukusanyika katika sehemu iliyozuiwa na kuunganishwa kwa matuta.

Kwenye mwinuko mkali, kuta au mashimo, ndiyo njia pekee inayoweza kuzuia mmomonyoko wa udongo. Changanya na mimea kama matete, inasaidia kuzuia mmomonyoko na pia kutoa malisho kwa mifugo.

Mbali na matandazo (tazama hatua ya 3) mimea inayotambaa ni mbinu nyingine nzuri zaidi inayoweza kuzuia mmomonyoko wa ardhi. Matone ya maji hufikia ardhi yakiwa na nguvu kidogo sana hivyo kuepuka kumomonyoa ardhi, kwa kuwa yanakuwa tayari hayana nguvu ya kutiririka kwa kasi. Pia mimea inayotambaa hutumika kama kivuli kwa udongo. Mmea wowote unaofunika udongo na kuongeza rutuba unaweza kutumika.

Mfano maharage na mimea mingine ya jamii ya kunde, ambayo ina virutubisho vya nitrogen kwa wingi. Mimea inayopendekezwa ni ile ya jamii ya kunde. Inastahimili ukame, inatoa virutubisho vya naitrojeni, inatoa chakula, na pia inaweza kutumika kama chakula cha mifugo kilicho na protini nyingi. Kwa kuongezea inaweza pia kukabiliana na wadudu waharibifu.

Matumizi ya mihogo kama dawa ya kuzuia wadudu kwenye mimea

Muhogo Inazuia Minyoo na vidukari.

Hatua za Kutayarisha dawa

  • Toa maji ya matunda kwa kuponda mizizi;
  • Pima k i w a n g o kimoja cha maji ya m a t u n d a sawa na maji ya kawaida (1:1).
  • Nyunyiza haraka ukitumia lita nne kwa mita moja za mraba, inasemekana kuwa na athari kubwa.
  • Subiri kwa siku ishirini kabla ya kupanda.

Angalizo: Tafuta ushauri wa mtaalamu wa kilimo kabla ya kutumia dawa yoyote ya asili

Shopping Cart