Dondoo za Urembo na Mitindo

Matumizi ya Asali kwenye Urembo wa ngozi na Nywele

Asali hutumika kulainisha Ngozi

Asali ina asili ya kuvuta unyevu kutoka kwenye hewa na kuipa ngozi uwezo wa kuhifadhi unyevu hivyo ni faida kwa mtu mwenye ngozi kavu.

Jinsi ya kuandaa
Chukua asali mbichi kijiko kimoja cha chai kisha paka usoni, kaa nayo kwa dakika 15 hadi 20 kisha safisha uso wako.

Asali katika kusafisha ngozi, kutibu na kuzuia chunusi

Kutokana na uwezo wa asali katika kuua bacteria na kuvuta uchafu katika matundu ya ngozi asali itakusaidia kutatua tatizo la chunusi.

Jinsi ya Kuandaa
Chukua asali mbichi Kijiko kimoja cha chakula changanya na mafuta ya nazi vijiko viwili changanya mchanganyiko uwe mlaini kisha paka usoni huku ukisugua taratibu kwa kufanya kama viduara huku ukiepuka kufikisha machoni. ukimaliza kusugua uso na mchanganyiko wako osha uso wako.

Jinsi ya kuandaa kama kisafisha ngozi, exfoliator
Changanya kijiko kimoja asali na kijiko kimoja baking soda. tumia mchanganyiko huu kusugua ngozi yako. Asali inaongeza lishe na chembe chembe kuzuia madhara yanayotokana na sumu za hewani zinazozeesha ngozi. Baking soda inasaidia kusafisha matundu ya ngozi.

Asali inasaidia ngozi iliyoungua na jua kujirudi na kung’aa.

Jinsi ya kutumia asali katika nywele
Asali inatibu nywele kavu zilizopauka, na kulainisha ngozi kavu ya kichwa na kutibu muwasho kichwani.

Jinsi ya kufanya
Changanya kijiko kikubwa cha asali na maji ya uvuguvugu kisha paka kichwani Acha kwa muda wa saa 1 iwe kama conditioner kisha safisha nywele zako.

Unaweza kuchanganya asali kiasi cha kijiko kimoja mpk viwili katika maji vikombe vitano kisha safishia nywele zako taratibu, yaani yapitishe tu hayo maji kwenye nywele zako ambazo ni safi.

Tahadhari: Asali kwa kiasi kikubwa hupausha weusi wa nywele kutokana na Hydrogen Peroxide inayopatikana ndani ya asali.

Ni vema ukatumia asali mbichi kujihakikishia faida za asali katika mwili wako.
Iwapo unavutiwa na matumizi ya kitu cha asili katika urembo wako unaweza kuongeza kitu hicho katika kitu kingine unachotumia mfano katika steaming yako au scrub unayotumia.

Jinsi ya Kuvaa hereni kwa Mpangilio kuongeza Mvuto wako

HERENI ni pambo linavoliwa masikioni na kwa kiasi kikubwa linachangia kuongeza mvuto na muonekano mzuri. Kuna aina nyingi za hereni katika tamaduni mbalimbali. Zipo ambazo hutengenezwa kwa kutumia vito vya thamani kama vile Dhahabu, Almasi, Shaba au Kopa.

Vilevile zipo ambazo hutengenezwa kwa kutumia malighafi za asili kama vile ubao, vifuu vya nazi, mfupa kioo na shanga ambazo zimekuwa zikivaliwa sana na wanawake wa kimasai. Hereni zilizotengenezwa kwa shanga zimekuwa zikiwavutia watu wengi kuvaa kutokana na nakshi zake za asili.

Mara nyingi uvaaji wa hereni unatakiwa kuzingatia aina ya nguo uliyovaa, hapo unatakiwa kucheza na rangi. Mpangilio wako wa nguo na hereni hata na viatu utakufanya uonekane maridadi muda wote.

Unapotoka kwenda katika shughuli zako, au uwapo nyumbani basi zingatia uvaaji wa hereni na nguo. Uvaaji usiozingatia mpangilio wa rangi na hereni zako huondoa ladha ya urembo na si rahisi kwa mtu mwingine kugundua umependeza.

Licha ya kuwa hapo awali hareni zilikuwa zikivaliwa na wanawake pekee lakini miaka ya hivi karibuni tunaona urembo huu unaanza kuwavutia baadhi ya wanaume hususan vijana wa mjini.

Kutokana na hilo kuna hereni ambazo zimetengenezwa maalum kwa kuvaliwa na wanaume, hizi huwa za kubana na huwa na umbo dogo ukilinganisha zile zinazopendwa kuvaliwa na wanawake.

Angalizo: Epuka kuvaa hereni zaidi ya moja katika tundu la sikio kwani kufanya hivyo kunaweza kupelekea ukubwa wa tundu kuongezeka na hatimaye nyama ya sikio kuchanika. Hereni nzito sana nazo huchangia kutokea kwa tatizo hili.

Jinsi ya kutunza kucha kujiepusha na maradhi shambulizi ya Kucha

Mikono, viganja na vidole ni kati ya sehemu muhimu katika mwili wa msichana. Mikono hutumika kufanya shughuli nyingi za nyumbani, shuleni na sehemu mbalimbali katika maisha kuanzia kutandika kitanda, kupika, kufanya usafi, kuandika, kujiremba pamoja na majukumu mengine mengi.

Mikono isipotunzwa vizuri ni rahisi sana kuharibika, kupoteza mvuto wake wa asili na kuharibu afya ya kucha. Hitaji la urembo wakati mwingine humsukuma msichana katika matumizi ya vipodozi vya kupaka kwenye kucha zake ili kukamilisha urembo wake.

Urembo wa vidole na kucha sio lazima ufanyike katika saluni au kwa wataalamu wa kupamba kucha, msichana anaweza kushughulikia afya na urembo wa vidole na kucha zake kwa gharama nafuu na kwa muda ambao mwenyewe anaona unafaa kufanya hivyo hata akiwa nyumbani.

Hii pia itamsaidia Msichana kuchagua vipodozi salama kwa afya ya kucha zake na mwili kwa ujumla. Ni jambo la muhimu kufahamu kuwa baadhi ya vipodozi vinavyotumika katika urembo wa kucha, vina rangi na sumu zisizofaa kwa afya. Sumu kama vile ‘Formaldehyde na Toluene’ zinazopatikana katika baadhi ya rangi za kucha zina madhara kwa afya ya msichana.

Ni kweli kuwa kucha nzuri huongeza urembo, mvuto na furaha ya msichana lakini pia ni busara kukumbuka kuwa afya ni muhimu kuliko urembo na uzuri. Afya ya mwili na kucha za msichana kwa ujumla hutegemea chakula bora chenye protein, madini na vitamini na siyo rangi na vipodozi.

Upungufu wa vitamini A, B Complex, proteni, madini ya chuma na chokaa (kalishiamu) mwilini husababisha kucha zipoteze afya yake ya asili. Kucha ambazo hazina afya zinaweza kuoza, kukauka, kupinda, kupasuka au kuwa na umbo kama kijiko. Magonjwa ya kuvu (fungus), na baadhi ya dawa za kupunguza makali ya virusi pia huharibu afya ya kucha. Mojawapo ya athari za dawa za kupunguza makali ya VVU aina ya Zidovudine (ZDV) ni kucha kuwa na rangi nyeusi.

Kwa ajili ya afya bora ya kucha msichana anashauriwa kula mboga za majani, maharage, korosho, asali na matunda kwa wingi kila siku. Usafi wa kucha kila siku kwa kuziosha kwa maji ya uvuguvugu na sabuni laini pamoja na brashi ndogo ya mikono huimarisha afya ya kucha. Kucha pia zinaweza kusafishwa kwa maji ya mmea wa mshubiri (Aloevera), kitunguu saumu kilichopondwa pondwa au kitunguu maji kisha viganja na vidole vikaushwe vizuri na kupaka losheni.

Kucha za msichana zinatakiwa zisiwe ndefu ili kuepuka utunzaji wa vimelea vinavyosababisha magonjwa na kurahisisha utunzaji na usafi wa kucha. Kucha ndefu zinaweza kuwa chanzo cha hatari kwa afya ya msichana na familia yake hasa pale msichana anapohusika na uandaaji wa chakula cha familia. Katika familia nyingi, hasa familia za kiafrika wasichana ndio wanaobeba wajibu na majukumu ya kuandaa chakula cha familia.

Kwa afya nzuri ya kucha, msichana anashauriwa kukata kucha zake ili ziwe fupi kadri anavyotaka kwa kutumia ‘nail cutter’ au mkasi mdogo au wembe mpya ambao haujatumiwa na mtu mwingine. Kuchangia nyembe za kukatia kucha si salama kwani kunaweza kuwa njia mojawapo ya kusambaza vimelea vya magonjwa hatari ya kuambukiza kama vile virusi vinavyosababisha UKIMWI na ugonjwa wa homa ya ini.

Ni vizuri kulainisha ncha za kucha baada ya kuzikata kwa kutumia tupa ya kucha (nail file) na kuzisugua kuelekea upande mmoja ili kuepuka kucha zisivunjike au zisisababishe michubuko ya ngozi wakati wa kujikuna. Kusugua kucha kwa kwenda mbele na nyuma kunaweza kusababisha kucha zivunjike kwa urahisi na haraka.

Kwa afya njema ya kucha, msichana pia anashauriwa asifungue pini za barua au kukwangua vocha za simu kwa kutumia kucha. Kucha zisikatwe kwa kutumia meno na zisilowekwe kwenye maji kwa muda mrefu hasa pale maji hayo yanapokuwa na kemikali au sabuni.

Kwa ajili ya afya njema ya kucha za miguuni, ni muhimu kuhakikisha kuwa, viatu kabla ya kuvaliwa vinakuwa vikavu na safi kabisa. Viatu visipotumiwa pia vihifadhiwe sehemu kavu isiyo na vumbi, maji au unyevunyevu ili kuepusha visiwe makazi ya kuvu (fungus)

Namna ya kuvaa vizuri kwa mwanamme upendeze na kuwa mtanashati

Nimeona leo nitoe darasa kidogo kuhusu mavazi sababu na mimi ni kipaumbele changu katika maisha.

1.Epuka kuvaa marangirangi

Wakati unamatch mavazi jitahidi kupunguza idadi ya rangi, rangi 3 tu zinatosha kukutoa bomba.

2. Vaa kulingana na mazingira/sehemu

Mtu mjanja anajua kubadilika kulingana na mazingira, sio kuvaa jezi la Man utd lenye jina la Wazza kwenye sherehe

3. Masharti ya kuchomekea

-Marufuku kuvaa oversize/undersize
-Usivae mlegezo
-Hakikisha singlet haionekani
-Usivae mkanda mrefu
-Usivae makubanzi/sandals

4. Kama umevaa pensi /kaptula.

-Hakikisha unavaa soksi fupi zisizoonekana
-Piga raba au makubanzi/sandals bila soksi
-Haipendezi kuchemekea

5. Usivae shati jeupe kama la mwanafunzi

Shati nyeupe ni nzuri kama unaijulia wakati unanunua hakikisha ina urembo wa aina yoyote ile au ni ya kimtindo sio kuvaa shati la shule

6. Hakikisha una suruali nyeusi

Mwanaume yoyote yule wa kijanja anajua umuhimu wa suruali nyeusi sababu inamatch mashati ya rangi nyingi.

7. Saa

-Kama umevaa jeans/kadet unaruhusiwa kuvaa saa ya aina yoyote
-Kama umevaa suti/suruali ya kitambaa epuka kuvaa saa ya mkanda wa plastic.

8. Miwani

Duh hapa pagumu kidogo lakini cha msingi zingatia muundo wa kichwa chako pamoja na aina ya macho uliyonayo na aina ya pamba ulizovaa pia.Sio umepiga jeans kali,kichwa kama madenge na macho kama bundi kisha unapiga miwani ndogo ya njano,ni

9. Vaa kofia za kijanja

Kofia pia huongeza mvuto,chagua kofia kulingana na aina ya kichwa na mavazi uliyovaa,haipendezi kuvaa suti na kapelo.Kanzu sharti ivaliwe na barakashia ndo utaeleweka la sivyo ni sawa na kuvaa dera tu

10. Mkanda

-Usivae mkanda mrefu km vile umefunga nyoka kiunoni
-Mikanda ya vitambaa au madoidoi inafaa kuvaliwa na jeans/kadeti/kaptula
-Jitahidi mkumatch rangi ya mkanda na viatu kama umevaa nguo za kuchomekea
-Zingatia upana wamkanda na rux za nguo yako

11.Tupia cheni za ukweli

Mikufu ya kiume pia huongeza mvuto
-Kama umevaa nguo za kuchomekea au suti itapendeza ukivaa cheni ndogo ambayo haitokezi nje ya shati
-Kama umepiga pamba za kishua mfano T.shirt na jeans hapa tupia cheni kubwa lakini hata cheni ndogo zinakubali

12.Uvaaji wa Tai

-Vaa kulingana na urefu wako
-Kama wewe mwembamba inapendeza kuvaa tie nyembamba
-Jitahidi kumatch tie na rangi ya shirt/suruali
-Hakikisha tie yako imefungwa vizuri shingoni

13.T.shirt na Jeans

Wanaume wajanja wa mjini hupenda kupiga t shirt na jeans na chini kutupia raba Kali…..Vazi hili lina mvuto wa aina yake hasa likivaliwa kitaani na sehemu za mitoko kama vile kwenye Club za starehe.

14. Vaa viatu kijanja

Hapa pia Kuna changamoto
-Usivaa suruali ya kitambaa na Raba
-Usivae suruali ya kuchomekea na makubanzi
-Ukipiga jeans unaweza kumatch t.shirt/shirt na rangi ya viatu
-Ukivaa suti yakupasa upige kiatu kikali ….ulikosea itakuwa sawa na Toyota Mark X yenye matairi ya Fuso !!!

Mambo ya Msingi kujua kuhusu uvaaji wa Tai

Kuna mambo mengi ya kufanya ili tuwe watu wa kuvutia kila wakati.Mpangilio wa mavazi hufanya mtu kuonekana maridadi.

Kama wewe ni mvaaji wa tai unapovaa unazingatia mambo yapi? Na je unafunga tai yako kwa namna inayokubalika?

Wengine huwa hawafahamu jinsi ya kufunga tai na hivyo kuleta mushkeri wakati wa kuvaa tai na kusababisha tai kukaa upande. Unapoamua kuvaa tai na shati ambalo halijanyooshwa ambalo linakuwa kwenye mikunjo au kuvaa tai na ndala unakuwa umeua maananzima na kulivunjia heshima vazi hili.

Tai ni vazi lawatu walio maridadi kama huwezi kuwa maridadi basi vazi hili halikufai kabisa.
Unapovaa taa unatakiwa kuzingatia aina ya umbo lako kama wewe ni mnene vaa tai inayoendana na mtu mnene na kama wewe ni mwembamba basi vaa tai inayoendana na mtu mwembamba.

Kuna wengine huvaa tai zinazofika magotini na kuwa kichekesho anapopita mtaani
Tai ni vazi ambalo huongeza heshima na hadhi ya mvaaji cha muhimu ni jinsi gani unavaa tai yako na ikiwezekana jaribu kumechisha tai na suruali kwa vile ili tai upendeze ni laima iendane na nguo unayovaa.

Ni vyema ukahakikisha kuwa unakuwa na tai zenye rangi tofauti ambazo zitaendana na nguo unazovaa.

Shopping Cart