Baini Siri za Kuwa na Afya Bora na Utimamu

Madhara ya kumlaza mtoto kifudifudi, kumlaza kwa tumbo

Unafahamu nini kuhusu suala la kumlaza mwanao? Maana Mapokeo tuliyo yapokea enzi na enzi ni kuwa ukitaka mtoto wako alale bila kushtuka basi alalie tumbo. Bado watu wengi wanaendelea kufanya hivyo hata sasa hivi unaposoma makala haya.

Je madaktari wanasemaje kuhusu suala hili?

Sayansi inashauri kuwa ni hatari kumlaza mtoto kwa tumbo. Visa kadhaa vya watoto kupoteza maisha vimehusishwa na watoto kulalia tumbo.

Kuanzia mwaka 1992 Madaktari wa watoto nchini Marekani walipendekeza kuwa watoto wachanga walale chali ( walalie Mgongo) ili kuepuka vifo vya ghafla vya watoto. Kifo cha ghafla hutokea pale ambapo mtoto mchanga anakutwa amefariki akiwa usingizini.

Tangu pendekezo hilo la madaktari idadi ya vifo vya ghafla vya watoto imepungua zaidi ya nusu ya vifo vyote vya watoto vinavyotokea wakiwa usingizini.

Ni vizuri kuhakikisha kuwa kila mtu anayekusaidia kulea mtoto anajua jinsi ya kumlaza mtoto chali.

Muhimu

Hata hivyo kuna baadhi ya watoto unaweza kushauriwa na daktari iwapo mwanao usimlaze chali na alalie tumbo.

Madhara ya kubana mkojo muda mrefu

Utakubaliana na mimi kwamba, kitendo cha mtu kubanwa na haja ndogo siyo kitu cha hiyari kwamba sasa mtu anaamua ngoja nibanwe na mkojo, hili ni jambo la asili na ni matokeo ya vyakula, matunda au vinywaji tunavyotumia. Kwa lugha nyingine tumekuwa tukiita kuwa ni wito wa asili au nature’s call.

Yawezekana mtu akawa katika mkutano, safarini, akawa katika mitandao ya kijamii anachati au popote pale akiwa anafanya jambo fulani na kutokana na jambo hilo, mtu akaendelea kujibana na kutokwenda kuyapunguza maji haya kutoka katika kibofu cha mkojo kwa kutoa kipaumbele kwa shughuli anayoifanya kuliko kusikiliza kwanza wito huu wa asili. Mambo haya tunayafanya sana, utasikia, mkojo umenibana kweli, ila ngoja nimalizie hii kazi halafu niende kujisaidia, hivi ndivyo watu wengi wanafanya.

Kutokana na vyakula na vinywaji tunavyotumia, kibofu cha mkojo huanza kujaa mkojo, mkojo unapofikia karibu mililita 50 mpaka 500 mtu huanza kuhisi hitaji la kwenda kukojoa. Kibofu cha mkojo kimezungukwa na vigunduzi asili (Receptors) vinavyopeleka taarifa katika Ubongo kuonyesha kuwa kibofu cha mkojo kimekaribia au kimejaa, baada ya taarifa hizi kufika katika ubongo, ubongo unatoa taarifa katika kibofu cha mkojo ili kiweze kushikilia mkojo huo kwa kuikaza misuli maalumu (Sphincters) mpaka hapo muda wa wewe kwenda kukojoa utakapofika.

Kibofu cha mkojo hufanya kazi kwa mfumo wa kujiendesha wenyewe yaani, automatic, kitendo cha mtu kupuuzia kwenda kukojoa husababisha Ubongo upate usumbufu wa taarifa za kujaa kwa kibofu cha mkojo na kwa kuwa Ubongo nao hutuma taarifa katika kibofu cha mkojo kusema kuwa mkojo uendelee kushikiliwa mpaka muda muafaka utakapofika, itafika kipindi uwezo wa ubongo kutoa taarifa hizi na pia uwezo wa vigunduzi asili (Receptors) vilivyoko katika kibofu cha mkojo kupoteza uwezo wake tena wa kufanya kazi hizo au uwezo kuwa mdogo. Matokeo yake ni mtu siku kweli anahitajika kuvumilia kidogo ili afike sehemu inayostahihi kujisaidia, lakini hawezi tena na kujikuta muda mdogo tu….mtu tayari kaloanisha nguo yake.

Mpenzi msomaji, mtu kujibana na kupuuzia kwenda kukojoa husababisha uwezo wa kibofu cha mkojo kujitawala (control) upotee. Pia kama uwezo wa neva zinazopeleka taarifa kwenye ubongo kuhusu mabadiliko/ujazo wa kibofu cha mkojo zitaharibika, basi misuli maalumu ya kubana mkojo (sphincter) itashindwa kuachia na matokeo yake mtu ataendelea kukaa na mkojo katika kibofu chake kwa muda mwingi zaidi kitu ambacho ni hatari kwa afya yake. Endapo mkojo huu utashindwa kutoka, utatengeneza mazalia ya bakteria na kukusababishia magonjwa ya kibofu (bladder infection). Magonjwa ya kibofu cha mkojo ni pamoja na U.T.I (Urinary Tract Infections), pia huweza kusababisha magonjwa ya figo na mchafuko wa damu, bacteremia.

Kuna hali huwa inajitokeza kwa baadhi ya watu, yawezekana alikuwa kabanwa na mkojo au alikuwa hajahisi kwenda kukojoa, ila akinywa maji au akisikia sauti ya maji yanachuluzika mfano maji yakitoka bombani, basi atahisi kwenda kukojoa.

Mpenzi msomaji, ni vyema tukawa wasikivu pale mtu unapobanwa na mkojo, hii ni kwa ajili ya afya ya kibofu chako cha mkojo lakini pia ni kwa ajili ya afya yako kwa ujumla. Kama unalo tatizo, usisite kuonana na wataalamu wa afya.

Madhara ya kisukari kwa nguvu za kiume

Kulingana na baadhi ya chunguzi zilizofanywa na wanasayansi asilimia 60 – 70 ya wanaume hupoteza nguvu za kiume kutokana na ugonjwa wa kisukari.

Sababu ni ngumu sana kuelewa lakini hutokana na mabadiliko ya mwili ambayo hutokea baada ya mtu kupata kisukari.

Ukiachana na kupata hamu ya kufanya tendo la ndoa mara kwa mara unatakiwa kuwa na mtiririko mzuri wa damu kwenye mishipa ya uume ili uweze kusimamisha uume kwa muda mrefu.

Unahitaji mishipa ya fahamu yenye afya na pia unahitaji homoni za kiume zakutosha.

Ugonjwa wa kisukari husababisha kudhoofu kwa mishipa ya damu, misuli pamoja na mishipa ya fahamu.

Uharibifu huu hupelekea mwanaume kupoteza uwezo wa kusimamisha uume kwa muda mrefu na baadae husababisha kushindwa kusimamisha uume kabisa.

Lakini pia ugonjwa wa kisukari hupelekea maradhi ya moyo na kusababisha matatizo makubwa mwilini.

Madhara ya dawa za kuulia wadudu maarufu kama viwatilifu

Dawa za kuulia wadudu maarufu kama viwatilifu zimetengenezwa kwa lengo la kuangamiza wadudu wanaoharibu mazao au wanaomdhuru binadamu. Hata hivyo kutokana na sababu kuwa lengo la dawa hizi ni kuangamiza, huathiri pia viumbe hai vingine akiwemo binadamu.

Takwimu kutoka shirika la afya duniani WHO zinabainisha kuwa kuna zaidi ya vifo 220,000 vitokanavyo na athari za sumu zilizoko kwenye dawa za kuulia wadudu—viwatilifu.

Ikiwa unataka kuweka afya yako salama, basi karibu nikushirikishe athari 8 kiafya za dawa za kuulia wadudu — viwatilifu.

1. Husababisha saratani.

Watafiti mbalimbali wa maradhi ya saratani wanaeleza kuwa dawa za kuulia wadudu zinachangia kwa kiasi kikubwa kusababisha seli za saratani mara zinapoingia kwenye mwili wa binadamu.

Hatari hii hutokea zaidi pale ambapo mtu anakula vyakula vilivyoathiriwa na sumu za dawa za kuulia wadudu.

2. Huvuruga mfumo wa homoni.

Mwili wa binadamu huzalisha homoni mbalimbali zinazowezesha viungo mbalimbali kufanya kazi vyema.

Dawa za kuulia wadudu zinapoingia mwilini huathiri mfumo wa homoni wa binadamu na kuufanya usifanye kazi vyema.

3. Huathiri mfumo wa uzazi.

Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa matatizo ya uzazi kati ya wanaume na wanawake huchangiwa kwa kiasi kikubwa na athari za dawa za kuulia wadudu.

Inaelezwa kuwa sumu hizi zinapoingia mwilini kupitia matunda au mbogamboga huharibu mfumo wa uzazi na kusababisha ugumba au utasa.

4. Huharibu ubongo.

Madawa ya kuulia wadudu — viwatilifu huathiri pia mfumo wa ubongo hasa kwa watu wanaoyapulizia au kukaa nayo karibu kwa muda mrefu.

Maradhi kama vile Mild Cognitive Dysfunction (MCD) ambayo humfanya mtu ashindwe kutambua vyema maneno, rangi au namba huchangiwa kwa kiasi kikubwa na athari za dawa za kuulia wadudu.

5. Huathiri mama mjamzito na mtoto

Mama mjamzito anatakiwa kuchukua tahadhari nyingi sana wakati wa ujauzito ili kulinda afya yake na mtoto aliyeko tumboni.

Matumizi ya viwatilifu ndani ya nyumba au karibu na makazi kwa lengo la kuua wadudu kama vile mbu, chawa, kunguni, au utitiri kunaweza kumwathiri mama mjamzito na mtoto kwa kiasi kikubwa.

Inaelezwa kuwa sumu hizi zinaweza kusababisha mtoto kuzaliwa bila viungo vyote, kuzaliwa kabla ya wakati au hata kifo.

6. Huharibu viungo muhimu vya mwili

Kumekuwa na taarifa mbalimbali ulimwenguni zikieleza kuwa dawa za kuulia wadudu huharibu viungo muhimu vya mwili kama vile figo na ini.

Utafiti uliofanyika huko India ulibaini kuwa watu wengi waliokufa kutokana na maradhi ya figo waliishi katika mazingira yenye sumu za kuulia wadudu au kula vyakula vyenye mabaki ya sumu hizo.

7. Huathiri mfumo wa upumuaji

Kutokana na watu wengi kutumia dawa za kuulia wadudu bila kuvaa vifaa vya kujikinga, wengi huvuta sumu zilizoko kwenye dawa hizo na kusababisha kuathiri mfumo wa upumuaji hasa mapafu.

Hivyo ili kujikinga na athari hii inashauriwa kuvaa vifaa bora vya kuzuia kuvuta sumu zilizoko kwenye dawa za kuulia wadudu.

8. Huathiri ngozi

Kama ilivyo kwenye swala la kuathiri mfumo wa upumuaji, watumiaji wengi wa dawa za kuulia wadudu hawakingi ngozi zao kwa mavazi au vifaa maalumu vinavyoepusha athari za dawa hizo kwenye ngozi zao.

Ikumbukwe kuwa sumu zilizoko kwenye dawa za kuulia wadudu zinaweza kuingia mwilini kirahisi kupitia ngozi na kusababisha athari nyingi za kiafya.

Naamini umeona jinsi ambavyo dawa za kuulia wadudu — viwatilifu zinavyoweza kuathiri afya ya binadamu ikiwa hazitatumiwa kwa uangalifu na kwa kufuata kanuni muhimu za matumizi yake.

Ikumbukwe kuwa vifo vingi na matatizo mbalimbali ya kiafya hutokana na mwili wa binadamu kukutana na sumu mbalimbali, hivyo ni muhimu kuchukua tahadhari.

Lifahamu tatizo la maumivu chini ya kitovu

Tatizo hili huwakumba watu wengi sana kwenye jamii yetu lakini kwa bahati mbaya watu wengi huchukulia ni jambo la kawaida kitu ambacho baadae hupelekea watu wengi kuingia kwenye matatizo makubwa ya kiafya hasa kwenye mfumo wa uzazi na mfumo wa chakula.

Maumivu Chini Ya Kitovu Hutokea Kama Ifuatavyo:

Yapo yale ya chini ya kitovu katikati, kushoto na kulia. Kwa wanawake maumivu ya kushoto na kulia yapo ya aina mbili. Kuna yale ambayo yanakuwa upande mmoja lakini husambaa kwa urefu wa sentimita mpaka nne na inaweza ikawa upande mmoja au pande zote mbili lakini yapo mengine chini ya kitovu ambayo yanaweza yakawa upande mmoja au pande zote mbili bila kusambaa kwa marefu.

Kuna maumivu mengine chini ya kitovu huwapata wanawake wakati tu wanaposhiriki tendo la ndoa kwa ndani ya uke au chini ya kitovu. Pia yapo ambayo huwapata wanawake wakati wameinama, wakati wa kunyanyua vitu vizito, wakati wa kucheka au kuimba na wakati mwingine wakiwa wamelala kifudifudi.

Maumivu chini ya Kitovu Yanaashiria Matatizo Gani Kwa Wanawake?

Mirija ya uzazi kujaa maji mazito na machafu ambayo huzuia yai kutembea kwenye mirija ya uzazi. Mwanamke ambaye amewahi kuambiwa na daktari kwamba anatakiwa asafishwe kizazi chake/mirija ya uzazi na wakati huo huo anasikia maumivu chini ya kitovu kushoto na kulia au upande mmoja kuna uwezekano akawa na tatizo la mirija ya uzazi kuziba kutokana na kujaa maji machafu.

Kutokukomaa kwa mayai ya uzazi. Hii husababisha vifuko vya mayai ya uzazi kuvimba(ovaritis) na kumletea mwanamke maumivu chini ya kitovu mithili ya kichomi. Mwanamke ambaye anamaumivu chini ya kitovu na wakati huo huo ana matatizo ya hedhi mfano hedhi kukoma au kutokuwa na mpangilio maalum kunauwezekano mkubwa akawa na tatizo la vifuko vyake vya mayai ya uzazi kutokomaza mayai na hivyo mayai kutotoka kwenye vifuko hivyo na kusababisha kuvimba na hatimaye kumsababishia mwanamke maumivu makali mithili ya kichomi.

Kuvimba kwa kuta za mji wa mimba na kuta za mirija ya uzazi (PID/Pelvic Inflamatory Disease). Mwanamke anayesikia maumivu chini ya kitovu katikati na pembeni kwa wakati mmoja na wakati huo huo akawa anatokwa na uchafu mzito mithili ya maziwa mtindi kunauwezekano akawa na PID hasa hasa kama amewahi kukumbwa na tatizo la kuharibika kwa mimba kabla haijafikisha miezi mitano.

Afya mbovu ya kibofu cha mkojo ikiambatana na matatizo ya maambukizi kwenye mfumo mzima wa mkojo (UTI). Maumivu chini ya kitovu yanayohusisha afya mbovu ya kibofu cha mkojo huambatana na mgonjwa kutoa haja ndogo kidogo sana ila mara kwa mara.

Maumivu chini ya kitovu kwa wanaume huashiria nini?

Maumivu chini ya kitovu kwa wanaume huashiria pia tatizo la tezi dume liitwalo Prostatitis yaani kuvimba kwa tezi dume. Maumivu haya hujikita kwenye shina la uume na huashiria tatizo hili hasa kama mwanaume anakwenda haja ndogo mara kwa mara nyakati za usiku na umri ukiwa unaelekea miaka 50 au zaidi.

Dalili nyingine ambatano ni kutoa haja ndogo ambayo ina kasi ndogo sana tofauti na kawaida, ikiambatana na maumivu ya kiuno na mgongo, kuvimba kwa korodani, haja ndogo inayoambatana na usaha na damu, maumivu ya uume wakati wa kufika kileleni, na damu katika maji ya uzazi (semen)
Kwa wanaume, maumivu haya ya chini ya kitovu huashiria pia tatizo ambalo kitaalamu hujulikana kwa jina la Hernia ambapo waswahili tunaita ngiri.

Mwanaume anaposikia maumivu haya ya chini ya kitovu ikiambatana na maumivu ya korodani, korodani moja kupungua na nyingine kukua zaidi au zote mbili kukua au kupotea, ni dalili ya ugonjwa huu ambao huharibu ubora wa uzalishwaji wa mbegu za kiume ambazo zaweza kuzalishwa chache au ambazo hazina kasi ya kutosha kusafiri kwenye via vya uzazi vywa mwanamke na hivyo mwanaume kupoteza uwezo wake wa kutungisha mimba.

Maumivu chini ya kitovu kwa wanaume kama ilivyo kwa wanawake huashiria tatizo la maambukizi katika mfumo wa haja ndogo yaani (Urinary Track Infection/UTI) ambapo dalili zake ni kama zile za mwanamke hapo juu.

Vipimo na tiba vyahitajika mapema bila kuchelewa ili kuepuka madhara makubwa katika mfumo wa uzazi, mkojo na hata wa chakula

Shopping Cart