Baini Siri za Kuwa na Afya Bora na Utimamu

Vyakula vinavyoongoza kuongeza akili kwenye ubongo

BILA shaka ubongo ni miongoni mwa viungo muhimu vya binadamu lakini ni watu wachache sana wanaoutilia maanani. Ubongo ndiyo kiungo kinachohusika na utendaji kazi wote wa mwili na ndiyo unaowezesha mwili kuishi maisha ya furaha au karaha.

Hata hivyo, wakati mwingine utendaji kazi wa mwili unaweza kuwa siyo mzuri kutokana na sababu mbalimbali zinazoathiri ubongo, mojawapo ikiwa ni kukosekana kwa lishe bora na staili ya maisha inayotakiwa kuimarisha ufanisi wa ubongo.

Chakula ni moja ya sababu za msingi kabisa za kuimarisha ufanisi wa ubongo na kuzuia magonjwa mengine ya akili. Lakini kwa bahati mbaya watu wengi hawajui wale vyakula gani kwa lengo la kujenga akili na kuimarisha ubongo.
Ifuatayo ni orodha ya vyakula ambavyo vinaongoza kwa kuimarisha utendaji kazi mzuri wa ubongo:

MAFUTA YA SAMAKI

Mafuta ya samaki ni muhimu kwa ubongo na mfumo wa fahamu. Ulaji wa samaki wenye minofu kama samoni (salmon) na dagaa, utaweza kupata faida hizo kwa sababu aina hii ya samaki ina kiasi kingi cha mafuta ya Omega 3 ambayo huimarisha utendaji kazi na mawasiliano kati ya ubongo na seli za mwili moja kwa moja.

PILIPILI KALI

Pilipili kali nayo huwa ni chakula kikubwa cha ubongo kwa sababu ina kiwango kingi cha Vitamin C ambayo huhitajika zaidi kwenye ubongo, pilipili inaaminika kuwa na kiwango kingi cha vitamin hiyo kuliko hata machungwa.

MBEGU ZA MABOGA

Mbegu za maboga zina kiwango kingi cha madini ya ‘Zinc’ ambayo husadia kuongeza kumbukumbu (memory). Kuna njia nyingi za kula mbegu za maboga, moja wapo ni kuzikaanga na kula kama
karanga, ukila kiasi cha kiganja kimoja kwa siku, inakuwa poa.

NYANYA

Nyanya ni muhimu sana kwa sababu huzuia magonjwa ya ubongo (brain disease) kutokana na kuwa na kirutubisho aina ya ‘Lycopene’ chenye uwezo wa kuzuia magonjwa nyemelezi yanayoweza kutokea. Hivyo ulaji wa nyanya utakusaidia kukupa kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali, yakiwemo ya akili.

BROKOLI

Brokoli ni mboga ya majani aina fulani kama maua ya maboga, ambayo nayo inafaida sana kwenye ubongo, ina vitamin K, C na inatoa kinga ya mwili. Vitamin K inahusika moja kwa moja na utendaji kazi mzuri wa ubongo na husaidia kuzuia magonjwa yatokanayo na uzee.

KARANGA

Aina zote za karanga zina vitamin E, ambayo huzuia tatizo la upotevu wa kumbukumbu na pia zina mafuta yenye afya yanayohitajika mwilini.

MAYAI

Mwisho ni mayai ya kuku, ambayo yana kirutubisho aina ya Choline. Kirutubisho hiki huzalishwa mwilini kwa kiwango kidogo tu, hivyo kwa kula mayai (ya kienyeji) utaweza kuongeza kiwango cha kirutubisho hicho mwilini kwa kiwango kikubwa na hivyo kuimarisha afya ya ubongo.

Utajuaje kama una upungufu wa maji mwilini? Dalili ni hizi

Upungufu wa maji ni pale mwili unapopoteza kiasi kingi cha maji kwa njia mbalimbali, ikiwemo jasho na mkojo, mwili hupungukiwa maji na hivyo mtu huyo huambiwa ana upungufu wa maji. Tunaelezwa kuwa karibu theluthi mbili ya miili yetu imejaa maji.

Ili mwili uweze kufanya kazi yake vizuri, kiwango cha maji mwilini hakipaswi kupungua hata kidogo, hivyo kila mtu ana wajibu wa kunywa maji ya kutosha kila siku ili kulinda kiwago chake cha maji kisipungue na kinapopungua ndipo hapo mwili huanza kuonesha dalili za kukaukiwa maji (dehydration).

Zifutazo ndizo dalili za upungufu wa maji mwilini;

Dalili za upungufu wa maji kwa mtoto.

Kwa kawaida, dalili za upungufu wa maji mwilini hujitokeza zaidi kwa watoto wadogo kuliko watu wazima au wazee. Dalili za upungufu wa maji mwilini kwa watoto huweza kusabababishwa ama na kuharisha, kutapika, kutokunywa maji au vimiminika vingine vya kutosha.

Mtoto mwenye dalili za upungufu wa maji huweza kuonesha dalili zifutazo:

  1. Kukojoa mara chache sana
  2. Mdomo na ulimi kukauka
  3. Mtoto kulia mara kwa mara na anapolia machozi hayatoki.
  4. Mtoto kutokuwa mchangamfu
  5. Macho, tumbo au mashavu kubonyea

Dalili za upungufu wa maji kwa wazee.

Dalili za upungufu wa maji kwa wazee ni tofauti na watu wazima. Wazee wa umri zaidi ya miaka 60 huwa na ngozi iliyosinyaa na hata ukiiminya, hubaki katika hali hiyo kwa muda na unapoikwaruza alama hubaki.
Halikadhalika, wazee hukosa haja ndogo kwa muda mrefu, hupungukiwa uzito kwa kiasi kikubwa na hupatwa na homa.

Dalili za upungufu wa maji kwa wajazito.

Upungufu wa maji mwilini kwa waja wazito ni hatari kwa mama pamoja na mtoto. Dalili zinazoweza kujitokeza kwa waja wazito ni pamoja na:

  1. Kukojoa mkojo wa njano nyeusi
  2. Kuumwa na kichwa.
  3. Mwili kukosa nguvu.
  4. Kichefuchefu na kutapika.
  5. Kukaukwa na mdomo.

Ili kujiepusha na matatizo ya upungufu wa maji na hatimaye kujikuta unakumbwa na dalili kadhaa zilizoelezewa hapo, ambazo ziko pia kwa watu wazima wengine, ni kuwa na mazoea ya kunywa maji ya kutosha kila siku. Hata utakapozidiwa na kukimbizwa hospitali, hakuna dawa nyingine utakayopewa zaidi ya maji (re-hydrating solution) . Kwa nini usubiri hali hiyo ikutokee wakati unaweza kuizuia kwa kunywa maji tu?

Hivyo wito wetu kwako kuendelea kunywa maji mengi ya kutosha kadri uwezavyo hii itakusaidia sana kwa namna moja ama nyingine kuwa na afya bora

Mambo ya Muhimu kuyajua kuhusu maumivu ya Korodani

Kuna wakati mwanaume huweza kupata maumivu ya korodani, ambapo inawezekana ikawa ni maumivu kwa korodani moja au zote mbili.

Maumivu hayo yanaweza kutokea endapo korodani zitakuwa zimeumizwa au kupata maambukizi.

Aidha, maambukizi hayo huweza kuwa makali na ya muda mfupi au makali kwa muda fulani halafu yanapoa yenyewe, lakini pia huweza kuwa ni maumivu ambayo siyo makali ila ni ya muda mrefu na yanayomnyima raha mhusika.

Mbali na hayo, pia maumivu ya korodani huweza kuwa makali kiasi kwamba yatahitajika matibabu ya dharura mfano korodani inavimba kama jipu kubwa, ikiambatana na maumivu makali na homa, tatizo hili kitaalam huitwa ‘Fournier’s gangrene’.

Kuna wakati mhusika anaweza kupata maumivu ya korodani mara inapotokea korodani ikajinyonga yenyewe na kusababisha mhusika kupata maumivu makali ya ghafla yanayoelekea hadi tumboni.

Kimsingi maumivu ya korodani huchangiwa na vyanzo mbalimbali, lakini maumivu sugu ni yale yanayochukua takribani zaidi ya miezi mitatu.

Vilevile maumivu hayo yanaweza kusababishwa na maambukizi katika korodani na kusababisha magonjwa kama Epididymits, Prostatis na Orchitis ambayo yote ni maradhi ya viungo vya uzazi vya mwanaume na husababisha ugumba.

Pia korodani inaweza kuwa na vivimbe kwa ndani, pembeni au juu ya kokwa au kuizunguka. Uvimbe au vivimbe hivi vinaweza kuwa na mishipa ya damu iliyojikunja humo, kujaa maji isivyo kawaida, hivyo kuchangia mbegu za kiume kujikusanya na kushindwa kutoka na mengine ya kitaalam ambayo pia tutakuja kuyaona.

Mambo ya Msingi kuyajua kuhusu Ugonjwa wa Kipindupindu

Mojawapo kati ya magonjwa yanayohusishwa na umaskini na uchafu wa kupindukia ni ugonjwa wa Kipindupindu. Inaripotiwa kuwa Kipingupindu ni miongoni mwa magonjwa ambayo huathiri jamii maskini zaidi kwa kiasi kikubwa hasa hasa kwenye nchi zinazoendelea, kiasi kwamba Shirika la Afya Duniani (WHO) limeuweka ugonjwa huu kama mojawapo ya viashiria vya maendeleo ya jamii husika.

Kwanini nchi zinazoendelea ndizo zinazokumbwa na ugonjwa huu?

Moja wapo ya changamoto zinazokabili nchi zinazoendelea ni jamii kutokuwa na uhakika wa kupata Maji safi na salama, pamoja na kutokuwa na mazingira safi kwa ujumla. Ndio maana mpaka leo nchi zinazoendelea ndizo zinazokumbwa na mlipuko wa kipundupindu au huwa katika hatari ya mlipuko wa ugonjwa huo.

Kipindupindu husababishwa na nini?

Ugonjwa huu hutokana na maambukizi katika utumbo mdogo wa binadamu uletwao na vimelea vya bacteria vijulikanavyo kitaalamu kama Vibrio cholerae.

Jinsi unavyoweza kuambukizwa

Kwa kawaida vimelea hawa hupendelea kuishi katika kinyesi cha binadamu. Mtu anaweza kuambukizwa ugonjwa huu kwa kunywa maji ama chakula kilichochafuliwa na kinyesi chenye vimelea hivi vya kipindupindu.

Mara baada kula chakula au kunywa maji yaliyochafuliwa, baadhi ya vimelea hivi huuwawa kwa tindikali iliyopo kwenye tumbo (stomach) pindi chakula au maji haya yanapoingia tumboni. Hata hivyo baadhi ya vimelea hawa hufanikiwa kukwepa ukali wa hii tindikali na hivyo kuendelea kuishi.

Vimelea waliofanikiwa kuepukali tindikali ya tumbo la binadamu, hujongea kwenda kwenye ukuta wa utumbo mdogo kwa kutumia ‘maumbo’ maalum yaliyo kwenye miili ya ambayo huwawezesha kusafiri ama kwa kitaalamu huitwa flagella. Wawapo kwenye ukuta wa utumbo mdogo Vibrio cholerae hutoa sumu iitwayo CTX au CT (cholera Toxin) ambayo husababisha mtu kuharisha choo chenye majimaji, papo hapo kuendelea kutoa kizazi kingine cha vimelea hao nje kwa njia ya haja kubwa.

Iwapo choo hicho cha mtu aliyeambukizwa kipindupindu kitachanganyika na chanzo cha maji au chakula, watu wengine huambikzwa kirahisi. Hali kadhalika iwapo ni kwenye choo ambacho hakipo kwenye mazingira ya usafi kuna hatari ya choo cha mwambukizwa kuchanganyika na chanzo cha maji au chakula na hivyo kupelekea watu wengi zaidi kuambukizwa ugonjwa huu.

Dalili za kipindupindu ni zipi?

Dalili za mwanzo kabisa za kipindupindu ni

• Kuanza Kuharisha ghafla choo chenye majimaji (ambacho rangi yake ni kama maji ya mchele) na chenye harufu mbaya kama shombo ya samaki.
• Kutapika

Aidha mgonjwa wa kipindupindu huonesha dalili zakupungukiwa maji mwilini kama vile

• ngozi huwa kavu,
• midomo kukauka,
• mgonjwa kuhisi kiu kikali,
• machozi kutoweza kutoka,
• kupata mkojo kidogo sana,
• Kuishiwa nguvu na kujisikia mchovu sana.
• Macho kutumbukia ndani hasa kwa watoto.

Vipimo vya utambuzi wa Kipindupindu

Kwa kawaida kipindupindu huweza kugunduliwa na kutambuliwa kwa kutumia dalili. Hata hivyo ili kuthibitisha kuwa mlipuko uliotokea ni kweli kipindupindu, vipimo vifuatavyo huweza kufanyika;

Kupima damu kwa ajili ya kuotesha vimelea vya kipindupindu maabara.
Kuchunguza choo kwa kutumia darubini (dark field microscope) ambapo vimelea hivi vya V. cholerae huweza kuonekana. Vile vile choo hiki hutumika kuotesha vimelea vya v. cholerae kwa ajili ya utambuzi zaidi.

Tiba ya Kipindupindu

Lengo kuu katika kutibu kipindupindu ni kurejesha maji na madini ambayo mgonjwa wa kipindupindu hupoteza kwa wingi baada ya kuharisha na kutapika.

Njia kuu zitumikazo katika kumrejeshea mgonjwa wa kipindupindu maji na madini aliyopoteza ni kwa kumpatia maji maalum yenye madini hayo kwa njia ya mdomo, yaani kwa kumpa anywe au kwa njia ya mshipa wa damu ambayo kitaalamu huitwa intravenously (i.v).

ORS
Pamoja na ORS hiyo ambayo imetengenezwa na kuwekwa kwenye paketi tayari kwa matumizi, Shirika la afya duniani (WHO) limetoa pia mwongozo wa kutengeneza maji yenye madini yanayohitajika mwilini (oral rehydration fluid) ambao ni rahisi na usio na gharama.
ORS ya kutengeneza nyumbani kwa kadiri ya muongozo huo huitaji kuchanganya na
• Lita moja ya maji safi na salama,
• Changanya na vijiko vidogo vinane vya sukari, kisha
• Ongeza na kijiko kidogo kimoja cha chumvi
• Aidha, unaweza kuongeza nusu glasi ya juice ya machungwa au nusu ya ndizi (tunda) lilipondwapondwa kwa kila lita, ili kuongeza madini ya potassium na pia kuboresha ladha.

Kwa wagonjwa wenye hali mbaya na wale wasioweza kunywa wenyewe, hupewa maji yenye madini mbambali kwa njia ya mshipa wa damu. Maji haya huitwa kitaalamu kama Ringer’s Lactate.

Mwongozo wa kufuata katika kutibu kipindupindu

Baada wa mgonjwa kuwasili katika kituo cha afya, hupimwa kiwango cha upungufu wa maji kilichopo mwilini.

Kisha muhudumu wa afya husahihisha upungufu wowote wa maji utakaonekana kwa awamu mbili. Kwanza kwa kati ya masaa 4-6 ya kwanza tangu kuwasili kituoni na kuendelea mpaka hali ya kuishiwa kwa maji mwilini itakapoonekana imekwisha.

Mhudumu wa afya hutakiwa kurekodi kwenye cheti maalum kiasi cha maji anayokunywa mgonjwa na kiasi cha mojo anachokojoa.

Njia ya mshipa hutumika pale tu, hali ya mgonjwa inapokuwa mbaya sana au pale ambapo mgonjwa hawezi kunywa chochote mwenyewe. Aidha kiasi cha maji kitolewacho kwa njia hii ya mshipa wa damu hwa ni kati ya 50-100 mL kwa kilo za uzito wa mgonjwa kwa saa.

Baada ya hapo, mgonjwa huendelea kupewa ORS anywe kwa kiwango cha 800 mpaka lita moja kwa saa.

Matumizi ya dawa katika kutibu kipindupindu

Ieleweke kuwa tiba sahihi na makini ya ugonjwa huu wa kipindupindu ni kumrejeshea mgonjwa maji na madini aliyopoteza wakati wa kuharisha na kutapika kwa njia ambazo zimeelezwa hapo juu. Matumizi ya dawa (antibayotiki) husaidia tu kufupisha muda wa kuwatoa wadudu na wala yasitumike kama tiba kuu ya ugonjwa huu.

Baadhi ya dawa ambazo hutumika katika matibabu ya ugonjwa huu ni Azithromycin na Tetracycline.

Jinsi ya kuzuia kipindupindu

Mara kwa mara serikali na taasisi zake zimekuwa zikihimiza watu jinsi ya kujikinga na ugonjwa huu wa kupindupindu. Miongoni mwa njia zinazofaa katika kuzuia milipuko ya ugonjwa huu ni
Upatikanaji wa maji safi na salama, watu hawana budi kuhakikisha kuwa maji ya kunywa yanachemshwa vyema kabla ya kuyanywa. Vile vile wanaweza kutumia chlorine katika maji ambayo huua vimelea hawa wa V. cholerae.

Ni muhimu kunawa mikono baada ya kutoka chooni na kabla ya kula

Tunashauriwa kufunika chakula kikiwa mezani ili nzi wasitue juu yake

Inashauriwa kujenga choo umbali wa angalau mita 30 kutoka chanzo cha maji
Inashauriwa kwa wasafiri watokao nchi zilizoendelea kupata chanjo iitwayo Dukoral, pindi wanaposafiri kwenda nchi zinazoendelea.

Madhara ya kutumia dawa za kuzuia mimba wakati wa hatari

Watu wengi hasa vijana watakuwa wanafahamu dawa ambazo hutumiwa sana kuzuia ujauzito pale ambapo wapenzi wamejamiiana ndani ya siku za hatari. Ninazungumzia dawa za kuzuia mimba sio dawa za kupanga uzazi. Dawa hizi zipo za aina nyingi ambazo zitozitaja hapa siku ya leo. Endapo wawili hawa wanakuwa hawapo tayari kupata mtoto, na wanaona kwamba siku walizojamiiana zitapelekea mwanamke huyo kutunga mimba, basi anaweza kutumia dawa hizi ambazo zinaharibu mazingira au uwezekano wa mimba kutungwa.

Dawa hizi zinaweza kutumika ndani ya saa 72 tangu mwanamke alipojamiina, lakini ikumbukwe kuwa, kadiri unavyozitumia mapema, ndivyo uwezekano wake wa kuzuia mimba unavyozidi kuwa mkubwa.

Licha ya kuwa watu wengi hutumia dawa hizi, ni wachache sana huchukua muda na kutaka kujua madhara yatokanayo na dawa hizo. Kwa ufupi tutaangalia madhara yanayoweza kutokana na dawa hizo. Hii haina maana kwamba, ukiitumia, basi ni lazima madhara haya yote yatakayojadiliwa hapa yakutokee, bali yanaweza kutokea baadhi au yasitokee kabisa.

Dawa hizi husababisha madhara kwa baadhi ya watumiaji. Miongoni mwa madhara ya kawaida ambayo husababisha ni pamoja na kupata maumivu ya tumbo, kuvurugika kwa mfumo wa hedhi, kutapika.

Unapotumia dawa hizi, mfumo wa hedhi katika mwezi unaofuata, hedhi inaweza kuanza mapema zaidi au kwa kuchelewa na damu inayotoka inaweza kuwa nzito ama nyepesi kuliko ilivyo kawaida.

Madhara haya ni ya muda mfupi tu, yanapita. Unapotapika ndani ya saa 3 baada ya kumeza dawa hizi, unashauriwa kuonana na mtaalamu wa afya au umeze tena dawa hizo.

Madhara mengine yanayoweza kutokana na dawa hizi ni maumivu ya kichwa, kuumwa na nyonga, maumivu ya mgongo na misuli.

Unapotumia dawa hizi na kuhisi maumivu makali, unaweza kutumia dawa za kutuliza maumivu. Pia unaweza kula chakula au kitu kingine ili kupunguza maumivu ya tumbo.

Bado hakuna ushahidi wa kitaalamu kuwa matumizi ya dawa hizi yanaweza kusababisha madhara ya muda mrefu kwenye afya ya uzazi ya mtumiaji. Aidha, unashauriwa kutozitumia mara kwa mara.

Shopping Cart