Je, kuna dawa zozote za kutibu magonjwa ya zinaa?

Magonjwa mengi ya zinaa yana dawa za kutibu, kwa mfano: kisonono, kaswende, klamdia, kankroidi au utando mweupe. Lakini hata hivyo ni lazima upate matibabu mapema. Ukisubiri muda mrefu bila ya kutibiwa, inawezekana kwamba via vya uzazi vikapata madhara ya kudumu, kwa mfano, kuziba kwa mirija ya kupitisha mayai.

Ni muhimu sana kwenda kupimwa mapema, wewe pamoja na mpenzi wako. Kwa sababu ukitibiwa peke yako, wakati mpenzi wako bado anaumwa, atakuambukiza tena mara tu ukijamiiana naye.
Magonjwa mengi ya zinaa yanatibika na kupona kabisa

Inakuaje mwanaume anaonyesha dalili za magonjwa ya zinaa zaidi kuliko mwanamke?

Wanaume mara nyingi huambukizwa sehemu za mrija wa mkojo. Katika sehemu hizi ni rahisi kusikia mwasho au maumivu zaidi kuliko kwenye via vya uzazi vya ndani vya mwanamke. Hasa wakati wa kukojoa, chumvichumvi iliyo kwenye mkojo inagusa vidonda ndani ya mrija. Hivyo, ni rahisi zaidi kwa mwanaume kujua kuwa ameambukizwa.
Vilevile mwanaume akiambukizwa na magonjwa haya, sehemu ya mbele ya njia ya mkojo inashambuliwa na huanza kutoa usaha mzito. Lakini uke wa mwanamke hutoa kemikali ambazo hufanya wadudu kutoweza kushambulia kwa haraka, na dalili hazionekani kwa urahisi. Bahati mbaya, kemikali hizi hazizuii kuingia kwa ugonjwa, lakini dalili huchelewa kuonekana.
Usisahau kwamba kama mwanaume anajitambua kuwa na dalili za kuumwa magonjwa ya zinaa, mpenzi wake pia anatakiwa kwenda kliniki ili apate uchunguzi na tiba.

Magonjwa ya zinaa na dalili zake

Kuna magonjwa mengi tofauti ya zinaa, lakini yale ambayo yameenea sana ni kisonono, kaswende, klamdia, kankroidi, utando mweupe , Virusi vya UKIMWI na UKIMWI. Shida kubwa ya magonjwa mengi ya zinaa ni kwamba dalili zake hazionekani kwa urahisi na kama yasipotibiwa kikamilifu yanaweza kuleta madhara makubwa. Maelezo kuhusu magonjwa ya zinaa yaliyoenea sana ni kama yafuatayo:

Kisonono:

Huchukua muda wa siku 1 hadi 14 tangu kuambukizwa mpaka kuonyesha dalili za kuumwa. Kwa wanawake dalili za kisonono ni maumivu chini ya tumbo ambayo yanaweza kuambatana na homa na kutokwa uchafu ukeni. Wapo wanawake wengine ambao hawaoni dalili zozote. Kwa wanaume dalili ni kutokwa na usaha uumeni na kupata maumivu wakati wa kukojoa. Athari yake kwa mwanamke ni kuziba mirija ya kupitisha mayai na mimba kutunga nje ya mfuko wa uzazi, na vilevile ugumba. Kwa mtoto aliye tumboni mwa mama mjamzito kisonono cha mama yake kinaweza kusababisha upofu. Kwa mwanaume athari yake ni kuziba mirija ya kupitisha mkojo.

The ListPages module does not work recursively.

Kaswende:

Dalili ya kaswende kwa mwanamke ni vidonda sehemu za siri hasa kwenye mashavu ya uke na sehemu ya njia ya haja kubwa, pamoja na sundosundo sehemu ya siri. Kwa mwanaume dalili ni vidonda. Mara nyingi kimoja kwenye kichwa cha uume, kwenye kishina cha uume na kuzunguka njia ya haja kubwa. Pia mwanaume anaweza kupata sundosundo sehemu za siri. Ugonjwa huu husababisha matatizo ya moyo, na kuharibu ubongo na kuzaa watoto walemavu.

Klamdia:

Dalili yake kwa mwanamke mara nyingi siyo rahisi kuonekana. Kwa mwanaume dalili ni kupata maumivu wakati wa kukojoa, na kukojoa mara kwa mara. Athari kwa mwanamke ni kuziba kwa mirija ya kupitisha mayai na mimba kutunga nje ya mfuko wa uzazi. Mimba hizi kuhatarisha maisha ya mama na kuleta ugumba vinaweza kutokea. Kwa mwanaume athari ni kuziba mirija ya kupitisha mbegu na utasa.

The ListPages module does not work recursively.

Kankroidi:

Dalili yake ni vidonda sehemu za siri vinavyokuwa na maumivu makali, maumivu wakati mkojo unapopita kwenye vidonda na kuvimba tezi sehemu za siri. Tezi huweza kupasuka na kutoa uchafu na maumivu makali.

Utando mweupe:

Dalili kwa mwanamke ni kutokwa na uchafu ukeni (kama maziwa yaliyoganda), kuwashwa na kuwa na michubuko sehemu za siri. Kwa mwanaume ni kuwashwa sehemu za siri na kusikia maumivu wakati wa kukojoa. Athari ni maumivu wakati wa kujamiiana.

The ListPages module does not work recursively.

Virusi vya UKIMWI:

Katika hatua ya mwanzo baada ya kuambukizwa hakuna dalili maalum. Hatua hii inaweza kuchukua mpaka miaka kumi. Lakini mara mtu anapoanza kuugua UKIMWI dalili zinakuwa nyingi. Pamoja na kupungua kinga ya mwili, kupungua uzito na kuumwa mara kwa mara. Matokeo ya kuugua UKIMWI baada ya muda fulani ni kifo.

Magonjwa ya zinaa yanavyoenea

Magonjwa ya zinaa husababishwa na vijidudu vya magonjwa na huambukizwa kwa kukutana kimwili na mtu mwenye vijidudu hivyo.
Katika Tanzania magonjwa haya yameenea sana haswa kwa vijana.. Hivyo kama una wasiwasi wewe au mpenzi uliyekutana naye kimwili kuwa na ugonjwa kama huo, muhimu mwende kupimwa. Magonjwa hayo yasipotibiwa kikamilifu yanaweza kuleta madhara makubwa. Magonjwa ya zinaa mara nyingi yanasababisha ugumba.

Nifanyeje kujiepusha na vishawishi vya mpenzi wangu vinavyoweza kunifanya nisitumie kondomu?

Mara nyingine siyo rahisi kujiepusha na vishawishi vya kujamiiana bila kutumia kondomu kutokana na msukumo wa mpenzi wako. Lakini kumbuka kwamba siyo rahisi kumtambua mwenye magonjwa ya zinaa na mara nyingi huwezi kujua kama mpenzi wako hana ugonjwa wowote wa zinaa au hata virusi vya UKIMWI.
Huwezi kufahamu ni watu wangapi ameshajamiiana nao maishani mwake na mpenzi wako vilevile hawezi kufahamu kama wewe umeshajamiiana na mtu mwingine. Kila unapojamiiana kuna uwezekano wa kuambukizwa magonjwa ya zinaa. Kwa hiyo jadiliana na mpenzi wako na mkubaliane juu ya umuhimu wa kutumia kondomu wakati wa kujamiiana kwa nia ya kuwakinga wote wawili. Kama mpenzi wako anakuambia kwamba hana ugonjwa kama huo, mwambie kwamba hana uhakika wa kufahamu kutokuwa na virusi vya UKIMWI bila kupimwa damu. Na kama mmoja kati yenu hajapimwa, basi uwezekano wa kuwa na virusi upo. Usikubali kushawishiwa kutotumia kondomu, kwa sababu inaweza kuhatarisha maisha yako.
Matumizi ya kondomu inazuia ujauzito ambao wewe bado hauko tayari kuwa nao

Je, mwanamke anajisikiaje akijamiiana na mwanaume aliyevaa kondomu au aliye “peku”?

Hatuwezi kusema mwanamke husikia raha gani akijamiiana na mwanaume aliyevaa kondomu au na mwanaume asiyevaa kondomu. Kila mtu ana upendeleo wake, lakini jambo la msingi katika kujamiiana ni hisia, hali ya kuelewana katika mapenzi na kiwango cha msisimko.
Wanawake wengine wanapendelea kujamiiana na mwanaume aliyevaa kondomu, kwa sababu hofu ya kupata mimba au kuambukizwa magonjwa ya zinaa haipo. Wanawake wengine wanapendelea kujamiiana bila kondomu. Lakini, pamoja na hatari ya kupata mimba, siku hizi kujamiiana bila kondomu kuna hatari ya kuambukizana magonjwa ya zinaa na hasa Virusi vya UKIMWI na UKIMWI. Kwa hiyo ni vizuri zaidi kutomwamini mtu yeyote mpaka mpimwe kliniki wote wawili kuwa ni wazima wa afya na kuendelea kuwa waaminifu wote wawili.

Mafuta kwenye kondomu

Mafuta yanayowekwa kwenye pakiti ya kondomu ni mafuta maalum na yana kazi ya kuhifadhi kondomu mpaka siku yake ya kutumiwa. Bila mafuta haya kondomu isingekuwa imara, ingekauka na isingekuwa nyumbufu vya kutosha. Vilevile mafuta hayo yanalainisha mpira ili kurahisisha uvaaji na matumizi yake. Kwa watu wengi, mafuta haya hayawaletei matatizo yoyote. Watu wachache sana ambao ngozi yao ni nyepesi kuathirika wanapata matatizo ya kuwasha baada ya kutumia kondomu.

Muwasho huwa sio wa kudumu. Watu wa namna hii wanashauriwa kunawa na sabuni ya kawaida baada ya kujamiiana.
Kuna uvumi kwamba mafuta haya yaliyomo ndani ya pakiti ya kondomu yana virusi vya UKIMWI. Hii siyo kweli, mafuta hayo yanawekwa kwa ajili ya kuhakikisha uimara wa kondomu tu.

Je, mbegu za kiume zinaweza kupita kwenye kondomu?

Hapana, mbegu za kiume haziwezi kupita kwenye kondomu. Kondomu zimetengenezwa ili kuzuia mbegu za kiume kufikia ukeni wakati wa kujamiiana. Kwa sababu shahawa haziwezi kupita kwenye kondomu, kondomu ni njia nzuri ya kuzuia mimba pamoja na maambukizi ya magonjwa ya zinaa pamoja na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.

Watu wengine wanasema kwamba kuna mashimo madogo kwenye kondomu yanayorahisisha mbegu pamoja na vijidudu vya magonjwa ya zinaa kupita. Huu ni uongo. Ukitaka kuwa na uhakika kwamba kondomu mpya haina mashimo, chukua kondomu moja na ijaze maji ya kawaida. Utaona kwamba maji hayapiti kwenye kondomu kabisa. Baada ya kujaribisha itupe kondomu ndani ya choo cha shimo au ichome moto, lakini usiitumie wakati wa kujamiiana

Kupasuka kwa kondomu

Kupasuka kwa kondomu mara nyingi kunasababishwa na kondomu kutowekwa vizuri uumeni. Ni muhimu sana kutoa hewa ndani ya kondomu wakati wa kuvalisha uume. Kwa sababu ile hewa ndani ya kondomu inaweza ikasababisha kondomu kupasuka wakati wa kujamiiana.
Vilevile siyo vizuri kupaka mafuta kama vaselini juu ya kondomu ili kurahisisha kitendo cha kuingiliana. Mafuta kama vaseline yanadhoofisha uimara wa kondomu na yanarahisisha kondomu kupasuka. Mafuta haya yanayowekwa kwenye pakiti ya kondomu yanahifadhi uimara wa kondomu, na ni aina maalumu ya mafuta.
Ni muhimu kukumbuka kwamba mwanaume akivaa kondomu vizuri jinsi tulivyoeleza awali, uwezekano wa kondomu kupasuka ni mdogo sana.

Ukubwa wa kondomu

Kuna aina kondomu za ukubwa mbalimbali. Kwa wastani ukubwa wa kondomu unafaa kwa wanaume watu wazima karibu wote na vijana balehe waliokomaa. Mara chache sana, kondomu ni ndogo kwa wanaume fulani, lakini wakati mwingine wanaume wanaringa tu kuwa na uume mkubwa au wanatumia kisingizio tu kwa sababu hawataki kutumia kondomu.
Kwa upande wa vijana, balehe kondomu zinaweza kuwa ndogo ukilinganisha na ukubwa wa uume wao. Kwa vijana, ambao uume bado mdogo, ni vizuri zaidi wangeacha kujamiiana badala yake watumie njia nyingine za kumaliza hamu ya kutaka kujamiiana kama vile kukumbatiana na kubusu.

Jinsi ya kutumia kondomu ya kike

Kondomu ya kike inafahamika kwa jina la „care“ na “Lady Peteta”. Hapa Tanzania hazipatikani sehemu zote na bei yake ni kubwa kidogo.
Kondomu ya kike huingizwa ukeni kabla ya kujamiiana. Kama unatumia kondomu ya kike, chana kwa uangalifu pembezoni mwa pakiti. Kondomu ina pete mbili za plastiki na uwazi upande wa juu. Pete moja imelegea ni ndogo na iko kwa ndani, upande usio na uwazi. Pete ya pili ni kubwa zaidi, imeshikiliwa na iko upande wa tundu. Shikilia kondomu upande uliozibwa na minya pete ya ndani kwa dole gumba na kidole cha pili na cha kati. Mara nyingine inaweza ikakuponyoka, (kuteleza) lakini endelea kujaribu hadi umeiminya vizuri. Tafuta mkao mzuri na ingiza kondomu ya kike. Huku bado unaminya kwa vidole vyako iongoze kondomu ndani ya uke wako. Ukiiachia pete ya ndani itashikilia kondomu ndani ya uke. Sasa ingiza kidole chako kwenye kondomu, sukuma pete mpaka inapogota kwenye mlango wa uzazi.
Kondomu ya kike inaweza kuvaliwa saa kadhaa kabla ya kufanya ngono na pia inaweza kuvuliwa baada ya muda wa kufanyika ngono kupita. Ili kuhakikisha kuwa uume umeingia sehemu husika, msaidie mwenzi wako kuongoza uume kuingia kwenye uke ili usipenye pembeni.
Baada ya kujamiiana, vua kondomu kwa uangalifu. Tupa kondomu iliyotumika kwenye choo cha shimo au uichome. Usitupe kondomu iliyotumika ovyo.
Kama ilivyo kwa kondomu ya kiume, kondomu ya kike itatumika kwa mafanikio zaidi pale ambapo wahusikia wanakuwa na makubaliano na maelewano juu ya matumizi yake.

Jinsi ya kutumia Kondomu

Wakati wa kutumia kondomu ya kiume ni muhimu kufuata hatua zifuatazo. Hakikisha kwamba pakiti inayoihifadhi haijapasuka na kwamba tarehe ya kuisha muda wake haijafika.
Uume ukishadinda, fungua pakiti kwa uangalifu. Minya sehemu ya juu kutoa hewa ndani ya kondomu wakati wa kuvalisha uume, ili kuzuia kupasuka kwa kondomu wakati wa kujamiiana. Visha uume kondomu taratibu mpaka uufunike wote. Ukiwa na uhakika kwamba kondomu imevishwa inavyotakiwa, unaweza kukutana kimwili na mwanamke.
Wakati wa kutoa uume kutoka ukeni, uwe mwangalifu kwamba kondomu bado ipo sehemu inayopaswa kuwa. Baada ya kutoa uume kutoka ukeni, vua kondomu kwa uangalifu uume ukiwa bado umedinda, ili kuepuka shahawa zisimwagikie ukeni. Tupa kondomu iliyotumika kwenye choo cha shimo au uichome. Usitupe kondomu iliyotumika ovyo. Pia usitupe kondomu iliyotumika kwenye vyoo vya kisasa yaani vya kuflashi na maji.
Ukinunua “salama kondomu“ ndani ya pakiti, kuna maelekezo kuhusu matumizi ya kondom. Unapotaka kutumia kondom wakati wa kujamiiana, ni vizuri ukajaribisha kwanza ukiwa peke yako ili kuzoea jinsi ya kuitumia.

Njia ya kuzuia mimba inayofaa kwa kijana anayeanza kujamiiana

Kila njia ya kuzuia mimba ina faida na hasara zake. Kwa mfano faida ya vidonge ni kwamba kama mwanamke atavimeza kila siku, hakuna haja ya kufanya chochote wakati wa kujamiiana. Matatizo ya vidonge ni kwamba mwanamke anahitaji kufikiria kuvinywa kila siku. Kondomu, kwa mfano ina faida kwamba pamoja na mimba inazuia magonjwa ya zinaa, lakini kasoro yake ni kwamba unahitaji kuivaa wakati wa kujamiiana.
Hakika, ushauri wa sasa ni kuwa kondomu ndiyo njia bora zaidi kwani ni njia pekee inayozuia kwa pamoja mimba zisizotarajiwa na maambukizi ya magonjwa yatokananyo na kujamiiana.

Je, ni lazima kumeza vidonge vya kuzuia mimba siku zote, hata zile siku nisipojamiiana?

Ndiyo, vidonge vya kuzuia mimba ni lazima vimezwe kila siku hata kama hufanyi ngono siku hiyo. Kuna aina ya vidonge vya kuzuia mimba inayokuja katika pakiti yenye vidonge 21 na kuna inayokuja katika pakiti ya vidonge 28. Iwapo utapewa ile ya vidonge 21 utapumzika kunywa siku 7 katika mwezi. Iwapo utapewa ile ya vidonge 28, itabidi kumeza kidonge kimoja kila siku, hata siku za hedhi. Ili kuhakikisha vidonge vya kuzuia mimba vinafanya kazi sawasawa, mwulize yule aliyekushauri kutumia vidonge hivyo jinsi ya kuvimeza.
Kama mwanamke akisahau kunywa kidonge hata kama ni siku moja kuna uwezekano wa kupata mimba. Anaposahau kumeza vidonge, ni vizuri zaidi watumie kondom wakati wa kujamiiana kwa kuhakikisha kutopata mimba. Hii inahusika vilevile kama mwanamke ameharisha au ametapika katika kipindi cha saa 4 tangu ameze vidonge. Kama mwanamke anashindwa kukumbuka kunywa vidonge mara kwa mara, ni vizuri zaidi apate ushauri kutoka kwenye kliniki ya uzazi wa mpango kutumia njia nyingine ya kuzuia mimba.

Je, baada ya kutumia vidonge au sindano kwa muda mrefu, mwamamke akiacha kuzitumia hizo njia ataweza kupata mimba tena?

Vidonge na sindano zinazuia mimba kwa kuzuia yai lisipevuke. Akitumia njia hizi za kuzuia mimba, mwanamke anaona hedhi yake kama kawaida, lakini hakuna yai linalokuwa limepevuka kwa ajili ya kurutubishwa.
Mara mwanamke akiacha kutumia vidonge, mayai hupevuka tena ndani ya kokwa na mwanamke huweza kupata mimba. Mwanamke aliyetumia sindano, anaweza akachukua muda kiasi kurudia hali yake ya uzazi. Kwa wanawake wengine inachukua miezi 12.
Muhimu ni kukumbuka kwamba sindano na vidonge siyo njia za kudumu za kuzuia mimba, hata kama itachukua muda fulani kurudia hali ya kawaida ya uzazi

Vidonge vya kuzuia mimba vinasababisha vidonda vya tumbo?

Wanawake wengine wanapata vidonda vya tumbo, lakini haya hayana uhusiano na vidonge vya kuzuia mimba. Vyanzo vya vidonda vya tumbo mara nyingi ni maambukizi yatokanayo na msongo wa mawazo, kula vyakula vyenye mafuta mengi na viungo vingi, au kuwa na historia ya ugonjwa huu katika familia. Baadhi ya dawa huathiri tumbo kama vile asprini na ndiyo maana sio kila mtu anashauriwa kuzitumia. Vidonge vya kuzuia mimba havisababishi vidonda vya tumbo.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About