Sidebar with Floating Button
Vichekesho vya AckySHINE
AckyShine

Ifahamu Saratani ya Tezi Dume, chanzo, Dalili, Uchunguzi na Tiba

Featured Image

Tezi Dume ni nini?





Tezi dume (prostate), ni tezi iliyo kwenye kizazi cha mwanaume inayozalisha maji maji yanayobeba manii/shahawa. Inaizunguka urethra, mrija unaotoa mkojo kwenye kibofu kwenda nje. Tezi dume ya kila mwanaume huongezeka ukubwa kadri umri unavyoongezeka. Kadri tezi inapokua na kuongezeka ukubwa,inaweza kukandamiza urethra na kusababisha matatizo ya kibofu na matatizo ya kukojoa. Tezi dume inapoongezeka ukubwa huitwa ”benign prostatic hyperplasia” kwa kifupi ”BPH”. Hii sio saratani, na haiongezi hatari ya kupata saratani ya tezi dume.




Saratani ya tezi dume inashika nafasi ya tatu kwa kusababisha vifo vinavyotokana na kansa kwa wanaume duniani. Pia ni chanzo kikuu cha vifo vinavyosababishwa na saratani kwa wanaume wenye umri wa miaka 70 na kuendelea. Hata hivyo, satarani ya tezi dume kwa sasa inawapata sana wanaume kuanzia miaka 25. Lakini kabla ya kuendelea mbele hebu kwanza tujue tezi dume ni zipi.


Kama tulivyosema neno saratani ni jina la gonjwa ambalo hutokea wakati chembe chembe za uhai au seli katika sehemu fulani ya mwili zinapoanza kukua bila kufuata utaratibu wa mfumo wa mwili na kutengeneza vijiuvimbe vidogo vidogo. Kwa kawaida seli huwa zinajigawa, kupevuka na baadaye kufa kwa kufuata taratibu za mfumo wa mwili. Lakini seli za saratani hazifuati mfumo huo. Badala ya kufa, zenyewe huishi muda mrefu kuliko chembe chembe za kawaida na wakati huo huo huendelea kutengeneza seli nyingine na kuwa uvimbe wa saratani au tumour.
Tezi dume linapatikana katika mwili wa mamalia dume tu na pale seli katika kiungo hicho zinapoanza kukua bila kufuata utaratibu wa mfumo wa mwili hapo ndipo mtu hupata saratani ya tezi dume. Ugonjwa huu pia hujulikana kama saratani ya kibofu cha mkojo. Saratani ya tezi dume huwapata wanaume tu na hasa wenye umri wa takribani miaka 50 na kuendelea. Kutokana na tafiti mbali mbali, saratani hii imethibitika kushika nafasi ya pili, ukiachia mbali saratani ya mapafu kwa kusababisha vifo vya wanaume wenye umri wa takribani miaka 50 na kuendelea.
Tafiti za Chama cha Saratani cha Marekani (ACS) na cha Afrika Kusini (CANSA) zimebaini kuwa, mwanaume mmoja kati ya sita hupata saratani ya tezi dume katika uhai wake. Kutokana na takwimu za mwaka 2010 za dunia nzima, malaria iliua watu laki tano, kifua kikuu watu milioni 2.1, Ukimwi watu milioni 1.8 na saratani watu milioni 9.9. Kwa mujibu wa takwimu hizo, idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na ugonjwa wa saratani ni kubwa ikilinganishwa na ya magonjwa mengine. Dk Emmanuel Kandusi ambaye ni miongoni mwa waathirika wa saratani hiyo, na mwanzilishi wa kampeni ya kuangamiza saratani ya tezi dume nchini Tanzania ya '50 Plus Campaign' anasema kuwa, ugonjwa huu ukitambuliwa mapema huweza kutibika kwa urahisi. Ameongeza kuwa, kutokana na ugonjwa huo kuwa hatari nchini, ifikapo mwaka 2020 unatarajiwa kuua watu milioni 20.


VIHATARISHI VYA TEZI DUME


Kuna vihatarishi vingi vinavyochangia mwanamume kupata saratani ya tezi dume. Vifuatavyo ni baadhi yake:-


👉🏿Kwanza kabisa ni umri. Nafasi ya kupata saratani ya tezi dume huongezeka sana hasa ukifikia umri wa karibu miaka 50 na kuendelea.


👉🏿Nasaba ni kihatarishi kingine ambapo wanaume wenye historia ya tatizo hili kwenye familia zao, yaani wale ambao mmoja wa ndugu zao wamewahi kuugua ugonjwa huu huwa katika hatarini ya kupata kansa hiyo kutokana na kurithi jeni za ugonjwa huo.


👉🏿Suala jingine ni lishe ambapo wanaume wanaopenda kula nyama au (red meat) na walaji wa chakula chenye kiasi kikubwa cha mafuta hasa ya wanyama huwa katika hatari kubwa ya kupata saratani ya tezi dume.


Vilevile wataalamu wanatumbia kuwa, wanaume wasiopenda kufanya mazoezi, wanene na wenye upungufu wa virutubisho vya Vitamin E pia wako kwenye hatari zaidi ya kupata saratani ya kibofu cha mkojo.
Wanaume wengine walio katika hatari kubwa ya kupata saratani ya tezi dume ni pamoja na wale wenye asili ya Afrika (Weusi) ikilinganishwa na wazungu, wakulima wanaotumia aina fulani ya mbolea za kemikali, wanaofanya kazi katika viwanda vya kutengeneza matairi na wachimbaji madini, hususan aina ya cadmium.


DALILI ZA TEZI DUME


Hayo yote yakiwa ni tisa, kumi ni je, dalili za saratani ya tezi dume ni zipi?Katika hatua zake za awali, dalili za saratani ya tezi dume hazitofautiani na zile za kuvimba kwa tezi dume au BPH.
Dalili hizo ni pamoja na,


1) Kupata shida wakati wa kuanza kukojoa.


2) Kutiririka kwa mkojo baada ya kumaliza kukojoa.


3) Kukojoa mkojo wenye mtiririko dhaifu.


4) Kukojoa mara kwa mara hasa nyakati za usiku.


5) Kujikakamua wakati wa kukojoa na kushindwa kumaliza mkojo wote


6) kutoa mkojo uliochanganyika na damu.
Pamoja na kueleza dalili hizo watu wanapashwa kutambua kuwa, mwanaume anapoanza kuona na kuhisi baadhi ya dalili hizo, anapaswa kujua kuwa, seli za saratani katika tezi dume lake huwa zina umri wa takribani miaka saba na kuendelea.
Iwapo saratani imesambaa mwilini kiasi cha kuhusisha sehemu nyigine za mwili, mgonjwa anaweza kuwa na maumivu makali ya mifupa katika maeneo ya nyonga, mapajani na kiunoni.
Aidha mgonjwa huwa na dalili nyingine zinazoweza kumpata mgonjwa mwingine yeyote wa saratani kama vile kupungua uzito, kuhisi kichefuchefu, uchovu, kizunguzungu na kadhalika.


UCHUNGUZI WA TEZI DUME


Wanaume wanashauriwa kufanyiwa uchunguzi wa saratani ya kibofu cha mkojo au prostate cancer kwa kuwa imegundulika kuwa wanaume wengi wakiziona na kuzihisi dalili hizo huona soni kwenda kumwona daktari na kufanyiwa uchunguzi.
Baadhi ya watu huzihusisha na magonjwa ya zinaa au na dhana potofu za kishirikina. Wapo wanaokwenda mbali zaidi hata kuuita ugonjwa huo kuwa ni wa walawiti huku wengine wakiurahisisha kwa kuuita kuwa ni ugonjwa wa utu uzima kana kwamba saratani ya tezi dume ni jambo la kawaida kwa watu wazee.
Mambo kama hayo hupelekea wanaume wengi kujinyanyapaa wenyewe na hata wengine kujitibu kwa uficho au kwa kutumia waganga wababaishaji mpaka pale mambo yanapokuwa yamewazidi ndipo hupelekwa mahospitalini na mara nyingine huwa wamechelewa na kupoteza maisha yao bure kwa ugonjwa ambao ungeweza kutibiwa mapema.
Kwa ajili hiyo tunatoa wito kwa wanaume kutoona soni na kuwa na tabia ya kufanyiwa uchunguzi wa afya kwa ujumla, na hasa tezi dume angalau mara moja kwa mwaka.
Kuna vipimo viwili ambavyo daktari anaweza kumpima mwanaume ikiwa ni hatua ya kwanza ya kugundua ugonjwa huo. Vipimo hivyo vya kwanza ni "Digital Rectal Exam (DRE)" na cha pili ni "Prostate Specific Antigen (PSA)". DRE pamoja na PSA huonesha uwepo wa tatizo kwenye tezi dume, lakini vipimo hivi havina uwezo wa kutofautisha iwapo tatizo hilo linamaanisha saratani au uvimbe katika tezi dume. Hivyo basi, ili kuweza kutofautisha kati ya magonjwa hayo mawili, kipimo kiitwacho Prostate biopsy hufanywa. Baada ya vipimo hivyo kama vitaashiria saratani ya tezi dume basi daktari anaweza kuamuru vipimo vingine ili kuthibitisha uwepo wa ugonjwa huo kama vile transrectal ultrasound au prostate needle biopsy.


MATIBABU YA TEZI DUME


Kuna njia kadhaa za matibabu ya saratani ya tezi dume. Hata hivyo uamuzi wa njia gani itumike unategemea ushauri na maoni ya daktari kulingana na hatua ya ugonjwa ulipofikia na umri wa mgonjwa husika. Katika hatua za awali za ugonjwa, daktari anaweza kushauri mgonjwa atibiwe kwa kufanyiwa upasuaji na tiba ya mionzi.
Hii ni katika hali ambayo kwa wagonjwa wazee, daktari anaweza kushauri mgonjwa kuwa chini ya uangalizi tu bila kufanyiwa upasuaji au bila kupatiwa tiba ya mionzi.


Matumizi ya dawa


Alpha 1-blockers kama vile doxazosin, prazosin, tamsulosin, terazosin, na alfuzosin ni dawa zilizo kwenye kundi la dawa zinazotumika kutibu shinikizo la juu la damu. Dawa hizi hulegeza misuli ya shingo ya kibofu na tezi dume. Hii huruhusu mkojo kutoka kwa urahisi. Watu wengi wanatumia dawa ya Alpha 1-blockers, na husaidia sana kupunguza dalili zao.


Finasteride na dutasteride  ni dawa zinazopunguza kiwango cha homoni zinazotengenezwa na tezi dume,hupunguza ukubwa wa  tezi dume, huongeza kiwango cha mtiririko wa mkojo, na kupunguza dalili zinazotokana na ukubwa wa tezi dume kuongezeka. Inaweza kuchukua miezi 3 hadi 6 kabla ya kuona mabadiliko makubwa katika dalili zako. Kutumia finasteride na dutasteride kunaweza kuwa na athari kama vile, kupungua kwa nguvu za kiume na hata kuwa hanithi.


Daktari anaweza kuagiza upewe dawa za antibiotiki ili kutibu kuvimba kwa tezi dume (prostatitis), mara nyingi prostatitis huambatana na kuongezeka kwa ukubwa wa tezi dume.


Upasuaji


Upasuaji wa tezi dume unaweza kupendekezwa  iwapo :



  • Unajikojolea/ unashindwa kuzuia mkojo

  • Unakojoa mkojo wenye damu mara kwa mara

  • Unashindwa kukojoa mkojo wote,(Mkojo unabaki kwenye kibofu hata baada ya kukojoa)

  • Maambukizi ya mara kwa mara kwenye njia ya mkojo

  • Kushindwa kwa figo kufanya kazi

  • Mawe kwenye kibofu


Uchaguzi wa aina maalum ya upasuaji, mara nyingi hutegemea ukali wa dalili ,ukubwa na umbo la tezi dume.



  • Transurethral resection of the prostate (TURP): Hii ni aina ya upasuaji inayopendelewa zaidi kutibu ugonjwa wa tezi dume. TURP hufanyika kwa kuingiza kifaa chenye kamera kupitia kwenye uume na kisha kukata na kuondoa tezi dume kipande baada ya kipande.

  • Transurethral incision of the prostate (TUIP): Upasuaji huu unafanana kidogo na TURP, na hufanyika kwa wanaume walio na tezi dume isiyo kubwa sana. Kwa kawaida upasuaji hufanyika na kisha mgonjwa huruhusiwa kwenda nyumbani (hakuna kulazwa). Kama ilivyo kwa TURP, kifaa chenye kamera huungizwa kupitia kwenye uume mpaka kuifikia tezi dume. Kisha, badala ya  kukatakata na kuiondoa, daktari hufanya mkato mdogo kupanua urethra ili kuruhusu mkojo kupita.

  • Simple Prostatectomy : Mgonjwa hupewa dawa ya nusu kaputi na kisha daktari hupasua tumbo (chini ya kitovu) ili kuifikia tezi dume. Sehemu ya ndani ya tezi dume huondolewa . sehemu ya nje huachwa . Huu ni utaratibu unaochukua muda mrefu, mgonjwa huhitajika kulazwa hospitalini kwa siku 5 hadi 10.



Iwapo saratani imesambaa na kuathiri sehemu nyingine za mwili, matibabu yake yanaweza kujumuisha upasuaji wa kuondoa korodani, matumizi ya dawa za kupunguza kiwango cha homoni ya testosterone katika damu au hormonal therapy, au matumizi ya kemikali za kuua seli za saratani (chemotherapy).


Tukumbuke kuwa, saratani ya tezi dume ni ugonjwa wa kawaida kama yalivyo magonjwa mengine na uchunguzi na matibabu ya mapema huweza kuokoa maisha ya waathirika wengi wa ugonjwa huo.

AckySHINE Solutions

Comments

Please Join AckySHINE to Participate in Discussion.

No comments yet. Be the first to share your thoughts!

Related Posts

Mbinu 11 za kufuata ili uweze kuacha pombe

Mbinu 11 za kufuata ili uweze kuacha pombe

Pombe ni kinywaji kinachotumiwa na watu wengi pasipo hata kufahamu athari zake. Pombe ina athari ... Read More

Vyakula visivyotakiwa kipindi cha ujauzito

Vyakula visivyotakiwa kipindi cha ujauzito

Ili mtoto azaliwe akiwa na afya njema pamoja na akili timamu, akiwa tumboni lazima alishwe lishe ... Read More

Vyakula vinavyofaa kuliwa katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani

Vyakula vinavyofaa kuliwa katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani

Vyakula vinavyofaa kuliwa wakati huu wa mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni vingi, leo tutaan... Read More

Dondoo Muhimu kuhusu ugonjwa wa kisukari

Dondoo Muhimu kuhusu ugonjwa wa kisukari

Wapendwa, napenda kushirikiana na nyinyi kujuzana hili nililolisikia kupitia channel ten leo asub... Read More

Matumizi ya tunda la shelisheli kama dawa ya ngozi

Matumizi ya tunda la shelisheli kama dawa ya ngozi

Shelisheli lililokomaa huwa na uzito wa hadi kilo 6, ambapo mshelisheli unaweza kukua kwa urefu w... Read More

Dalili za kuharibika kwa Mimba

Dalili za kuharibika kwa Mimba

Kuna sababu nyingi zinazoweza kusababisha mama mjamzito mimba yake kuharibika. Sababu kuu huwa ni... Read More

Sababu za magonjwa ya figo na jinsi ya kuondokana na janga la magonjwa ya Figo

Sababu za magonjwa ya figo na jinsi ya kuondokana na janga la magonjwa ya Figo

1.Usichelewe kwenda HAJA. Kutunza mkojo kweye kibofu chako kwa muda mrefu ni wazo ... Read More
Jinsi ya kutibu chunusi kwa kutumia Uwatu (Fenugreek)

Jinsi ya kutibu chunusi kwa kutumia Uwatu (Fenugreek)

Uwatu ni dawa nyingine ya asili inayotumika kutibu chunusi. Uwatu unaondoa sumu na maambukizi mba... Read More

Mambo ya Msingi kujua kuhusu rangi ya mkojo wako

Mambo ya Msingi kujua kuhusu rangi ya mkojo wako

Je unafahamu ya kwamba rangi ya mkoja inakupa matokea sahihi kuhusu afya yako? Kama jibu ni hapan... Read More

Chanzo, dalili, aina na matibabu ya ugonjwa wa kifafa

Chanzo, dalili, aina na matibabu ya ugonjwa wa kifafa

Huu ni ugonjwa ambao unasabababishwa na seli zilizopo katika mishipa ya fahamu zilizopo kwenye ubong... Read More
Faida za kula mayai asubuhi

Faida za kula mayai asubuhi

Mayai ni kitu kilichozoeleka na kinachopatikana kwa gharama nafuu. Kutokana na kuzoeleka huku wat... Read More

Ulaji mzuri hupunguza uwezekano wa kupata shinikizo la chini la damu

Ulaji mzuri hupunguza uwezekano wa kupata shinikizo la chini la damu

Ni mhimu kula mlo kamili kila siku. Kula lishe duni kunaweza kupelekea kuzalishwa kwa damu isiyo ... Read More