MASOMO YA MISA, MACHI 22, 2022: JUMATANO, JUMA LA 3 LA KWARESIMA

Updated at: 2024-05-27 07:09:45 (11 months ago by DIN - Melkisedeck Leon Shine)
Musa aliwaambia makutano: Ee Israeli, zisikilizeni amri na hukumu niwafundishazo, ili mmzitende; mpate kuishi na kuingia na kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wa baba zenu.Angalieni nimewafundisha amri na hukumu, vile vile kama Bwana, Mungu wangu, alivyoniamuru, ili mzitende katika nchi mwmingiayo ili kuimiliki. Zishikeni basi,5 mkazitende, maana hii ndiyo hekima yenu na akili zenu, machoni pa mataifa watakaozisikia⁵ amri hizi zote, nao watasema, Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na akili. Kwa maana liko taifa gani kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama Bwana, Mungu wetu, alivyo, kila tumwitapo? Tena liko taifa gani kubwa, lililo na amri na hukumu zenye haki kama torati hii yote, ninayoiweka mbele yenu leo.
Lakini, jihadhari nafsi yako, ukailinde roho yako kwa bidii, usije ukayasahau mambo yale uliyoyaona kwa macho yako, yakaondoka moyoni mwako siku zote za maisha yako; bali uwajulishe watoto wako na watoto wa watoto wako.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
Msifu Bwana, Ee Yerusalemu.Msifu Bwana, Ee Yerusalemu;
Msifu Mungu wako, Ee Sayuni.Maana ameyakaza mapingo ya malango yako,Amewabariki wanao ndani yako. (K)
Huipeleka amri yake juu ya nchi,Neno lake lapiga mbio sana.
Ndiye atoaye theluji kama sufu,Huimwaga barafu yake kama majivu. (K)
Humhubiri Yakobo neno lake,Na Israeli amri zake na hukumu zake.
Hakulitendea taifa lolote mambo kama hayo,Wala hukumu zake hawakuzijua. (K)
Mbegu neno la Mungu, mpanzi lakini ni Kristu; Yeyote ampataye, ataishi milele.
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Msidhani kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka hata yote yatimie. Basi mtu yeyote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme mbinguni.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Updated at: 2024-05-27 07:09:48 (11 months ago by DIN - Melkisedeck Leon Shine)
Updated at: 2024-05-27 07:09:49 (11 months ago by DIN - Melkisedeck Leon Shine)
Yer. 18-18-20
Waliposema, Njoni na tufanye mashauri juu ya Yeremia; maana sheria haitampotea kuhani, wala shauri halitampotea mwenye hekima, wala neno halitampotea nabii. Njoni, na tumpige kwa ndimi zetu, wala tusiyaangalie maneno yake yoyote.
Niangalie, Ee Bwana, ukasikilize sauti ya wanaoshindana nami. Je! Mabaya yalipwe badala ya mema? Maana wameichimbia nafsi yangu shimo. Kumbuka jinsi nilivyosimama mbele zako, ili nisema mema kwa ajili yao, nikaigeuze ghadhabu yako isiwapate.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
Zab. 31:4-5, 13-15 (K) 16
(K) Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako, Ee Bwana.
Utanitoa katika wavu walionitegea kwa siri,
Maana Wewe ndiwe ngome yangu.
Mikononi mwako naiweka roho yangu;
Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli. (K)
Maana nimesikia masingizio ya wengi;
Hofu ziko pande zote.
Waliposhauriana juu yangu,
Walifanya hila wauondoe uhai wangu. (K)
Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana,
Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu.
Nyakati zangu zimo mikononi mwako;
Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia. (K)
Lk. 8:15
Heri wale walishikao neno la Mungu katika moyo wao mwema na unyofu, na wazaao matunda katika uvumilivu.
Mt. 20:17-28
Yesu alipokuwa akipanda kwenda Yerusalemu aliwachukua wale wanafunzi kumi na wawili faraghani; na njiani akawaambia, Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu; na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa wakuu wa makuhani na waandishi nao watamhukumu afe; kisha watampeleka kwa Mataifa wapate kumdhihaki, na kumpiga mijeledi na kumsulibisha; na siku ya tatu atafufuka.
Ndipo mama yao wana wa Zebedayo akamwendea pamoja na wanawe, akamsujudia, na kumwomba neno. Akamwambia, Wataka nini? Akamwambia, agiza kwamba hawa wanangu wawili waketi mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika ufalme wako. Yesu akajibu akasema, Hamjui mnaloliomba. Je! Mwaweza kunywea kikombe nitakachonywea mimi? Wakamwambia, Twaweza. Akawaambia, Hakika mtakinywa kikombe change; lakini kuketi mkono wangu wa kuume na mkono wangu wa kushoto, sina amri kuwapa, bali watapewa waliowekewa tayari na Baba yangu.
Na wale kumi waliposikia, waliwakasirikia wale ndugu wawili. Lakini Yesu akawaita, akasema, Mwajua ya kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu yeyote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu; na mtu yeyote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumikia na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Updated at: 2024-05-27 07:09:38 (11 months ago by DIN - Melkisedeck Leon Shine)
Palikuwa na mtu mmoja jina lake Yoakimu, akikaa Babeli, naye ameoa mke jina lake Susana binti Helkia, mwanamke mzuri sana na mcha Mungu. Wazee wake nao walikuwa wenye haki, pia wamemfundisha binti yao sawasawa na Torati ya Musa. Basi Yoakimu alikuwa mwungwana tajiri, na karibu na nyumba yake alikuwa na bustani nzuri; hivyo Wayahudi humwendea, maana alikuwa ni mwenye heshima kupita wengineo wote. Mwaka ule ule wakaamriwa wawili miongoni mwa wazee wa watu ili kuamua, watu wa namna ile ambao Bwana aliwanena, ya kama ufisadi ulitoka Babeli kwa wazee waamuzi waliohesabiwa kuwa wanatawala watu. Hao walikuwa wakienda mara nyingi kuzuru kwenye nyumba yake Yoakimu; na wote wenye mashtaka yoyote desturi yao wakawajia huko. Basi watu walipoondoka kwenda zao panapo saa sita, Susana huingia katika bustani ya mumewe ili kutembea. Nao wale wazee humwona kila siku anakwenda kutembea; hata wakawaka tamaa kwa sababu yake. Ndipo walipozipotosha nia zao, wakayageuza upande macho yao wasiweze kutazama mbinguni wala kukumbuka hukumu za haki. Ikawa walipongoja wakati wa kufaa, yeye aliingia bustanini kama ilivyokuwa desturi yake pamoja na wajakazi wawili, naye alitaka kuoga kwa sababu kulikuwa na joto. Wala hapakuwa na mtu yeyote isipokuwa wale wazee wawili, ambao wamejificha wakimvizia. Basi akawaambia wajakazi wake, Nileteeni mafuta na sabuni, mkaifunge milango ya bustani ili nioge . Mara wale wajakazi walipokwishas kutoka, wale wazee wawili waliondoka wakamwendea mbio, wakasema, Tazama, milango ya bustani imefungwa asiweze kutuona mtu yeyote nasi tunakupenda sana; haya! Basi, utukubali na ulale nasi. La! Hutaki tutakushuhudia ya kuwa hapa palikuwapo na kijana pamoja nawe, ndiyo sababu uliwaruhusu wajakazi wako. Basi Susana aliugua akasema, Nimesongwa pande zote, maana nikilitenda hilo ni mauti yangu; nisipolitenda siwezi kuokoka mikononi mwenu. Ni afadhali niangukie katika mikono yenu na kukataa, kuliko kutenda dhambi machoni pa Mungu. Mara Susana akapiga kelele kwa sauti kuu; nao wale wazee wawili wakampigia kelele pia. Kisha mmoja wao akakimbia, akaifungua milango ya bustani. Hivyo watumishi wa nyumbani waliposikia kelele bustanini, wao waliingia kwa kasi kwa mlango wa nyuma ili waone ni nini iliyompata. Lakini wale wazee waliisimulia hadith yao nao watumishi wakaona aibu kabisa, kwa maana Susana hakuchongelewa habari ya namna hiyo wakati wowote.
Ikawa kesho yake watu walipokusanyika kwa Yoakimu mumewe, wale wazee wawili wakaja nao, wamejaa kusudi lao ovu juu ya Susana la kumfisha. Wakasema mbele ya watu, "Mwiteni Susana binti Helkia, mkewe Yoakim, aje hapa". Basi akaenda kuitwa; naye akaja pamoja na baba yake na mama yake, na watoto wake, na jamaa zake wote. Naye huyo Susana alikuwa mwanamke mwenye adabu, mzuri wa uso; basi hao watu wabaya waliamuru afunuliwe uso, maana alifunikwa utaji, ili washibe uzuri wake. Kwa hiyo rafiki zake na wote waliomtazama wakasikitika. Ndipo wale wazee wawili waliposimama katikati ya watu, wakaweka mikono yao juu ya kichwa chake. Naye akatoka machozi, akatazama juu mbinguni, kwa maana moyo wake ulimtumaini Mungu. Wale wazee wakasema, Sisi tulipokuwa tukitembea bustanini peke yetu, huyu aliingia pamoja na wajakazi wawili, wakaifunga milango ya bustani, naye mara akawaruhusu wajakazi. Kisha kukatokea kijana, ambaye amejificha humo, akamwendea akalala naye. Walakini sisi tungaliko pembeni mwa bustani, tuliona ubaya huo, tukamwendea mbio. Hata tukiwa tumewaona pamoja, yule kijana hatukuweza kumkamata, maana alikuwa mwenye nguvu kuliko sisi, akifungua milango akaepuka. Bali huyu tulimkamata, tukauliza yule kijana yu nani, asikubali kutuambia. Hayo basi, tunashuhudu. Basi waliohudhuria wakawasadiki, wakiwa wazee wa watu na waamuzi; hivyo wakahukumu auawe. Mara Susana akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Mungu wa milele, Wewe wajua yaliyositirika, wajua mambo yote yasijekuwako, Wewe wajua ya kwamba wananishuhudia uongo, na tazama, imenipasa kufa; walakini sikufanya mambo kama hayo, ambayo watu hawa wameyabuni juu yangu kwa ukorofi.
Naye Bwana akaisikia sauti yake. Kwa hiyo, alipochukuliwa huyo kwenda kuuawa, Mungu alimchocheleza roho kijana mmoja, jina lake Danieli; naye akapaza sauti akasema, Mimi simo; mimi sina hatia kwa habari ya damu yake mwanamke huyu. Mara wote wakamgeukia, wakasema, Maneno hayo uyasemayo, maana yake nini? Akasimama katikati, akasema, Enyi bani Israeli, mmekuwa wapumbavu, hata kumhukumu binti Israeli bila kuhoji wala kupata hakika ya kweli? Rudini hukumuni; mradi hao wanamshuhudia uongo.
Basi watu wote walirejea kwa haraka, nao wale wazee wakamwambia, Njoo uketi kati yetu, utujulishe habari hiyo, endapo Mungu amekupa wewe heshima yam zee. Hapo Danieli aliwaambia, Watu hawa wawili watengwe, nami nitawahoji. Basi wakiisha kutengwa, akamwita mmoja wao akamwambia, Ewe uliyepata kuwa mzee katika uovu, sasa dhambi zako zimekukalia, ulizozitenda zamani kwa kuhukumu isivyo haki, kumpatiliza asiye na hatia na kumwachilia mwovu; lakini Bwana asema, Asiye na hatia, mwenye haki, usimwue. Haya! Basi, wewe ulimwona kwa macho; useme; Chini ya mti gani ulipowaona wakikaa pamoja? Naye akajibu, Chini ya msandarusi. Danieli akasema, Hakika umesema uongo juu ya kichwa chako mwenyewe; maana sas hivi malaika wa Mungu amepokea hukumu ya Mungu, akukate vipande viwili. akamtenga huyo tena, akaamuru kumleta yule mwingine, akamwambia, Ewe mzao wa Kanaani, wala si wa Yuda, uzuri umekudanganya, na tamaa imeupotosha moyo wako. Hivyo ndivyo ulivyowafanyia binti za Israeli, na kwa hofu walitembea nawe; bali huyu binti Yuda hakuweza kuustahimili uovu wako. Haya! Basi, nawe useme; Chini ya mti gani ulipowaona wakikaa pamoja? Naye akajibu, Chini ya mkwaju. Danieli akamwambia, Hakika wewe nawe umesema uongo juu ya kichwa chako mwenyewe; maana malaika wa Mungu yu tayari, anakungoja mwenye upanga, akukate vipande viwili; ili awaangamize nyote wawili.
Mara hiyo makusanyiko yote wakapaza sauti kwa nguvu, wakamhimidi Mungu awaokoaye wamtumainio. Wakawaondokea wale wazee wawili, kwa maana Danieli ameuhakikisha ushuhuda wao wa uongo hata vinywani mwao wenyewe. Wakawatenda kwa Torati ya Musa kama vile walivyokusudia kwa ukorofi kumfanyia jirani yao; wakawaua; na mwenye damu isiyo na hatia aliokolewa siku ile.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
(K) Nijapopita katika bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami.
Bwana ndiye mchungaji wangu,
Sitapungukiwa na kitu.
Katika malisho ya majani mabichi hunilaza,
Kando ya maji ya utulivu huniongoza. (K)
Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza,
Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
Naam, nijapopita kati aya bonde la uvuli wa mauti
Sitaogopa mabaya; kwa maana Wewe upo pamoja nami,
Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. (K)
Waandaa meza mbele yangu,
Machoni pa watesi wangu.
Umenipaka mafuta kichwani pangu,
Na kikombe change kinafurika. (K)
Hakika wema na fadhili zinanifuata,
Siku zote za maisha yangu,
Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. (K)
Maneno yako, Ee Bwana, ni roho, tena ni uzima, Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
Yesu aliwaambia tena akasema, Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.
Basi Mafarisayo wakamwambia, Wewe unajishuhudia mwenyewe; ushuhuda wako si kweli.
Yesu akajibu, akawaambia, Mimi ningawa ninajishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu ndio kweli; kwa sababu najua nilikotoka na niendako; lakini ninyi hamjui nilikotoka wala niendako. Ninyi mwahukumu kwa kufuata mambo ya mwili; mimi simhukumu mtu. Nami nijapohukumu, hukumu yangu ni kweli; kwa kuwa mimi si peke yangu, bali ni mimi nay eye aliyenipeleka. Tena katika torati yenu imeandikwa kwamba, Ushuhuda wa watu wawili ni kweli. Mimi ndimi ninayejishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenipeleka ananishuhudia.
Basi wakamwambia, Yuko wapi Baba yako? Yesu akajibu, Mimi hamnijui, wala Baba yangu hammjui kama mngalinijijua mimi, mngalimjua na Baba yangu.
Maneno hayo aliyasema alipokuwa akifundisha hekaluni, katika chumba cha hazina; wala hakuna mtu aliyemkamata, kwa sababu saa yake ilikuwa haijaja bado.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Updated at: 2024-05-27 07:09:44 (11 months ago by DIN - Melkisedeck Leon Shine)
MASOMO YA MISA, MACHI 25, 2022
IJUMAA, JUMA LA 3 LA KWARESIMA
Isa. 7:10 – 14
Bwana alisema na Ahazi akinena, Jitakie ishara ya Bwana, Mungu wako; itake katika mahali palipo chini sana, au katika mahali palipo juu sana. Lakini Ahazi akasema, Sitaitaka, wala sitamjaribu Bwana. Naye akasema, Sikilizeni sana, enyi nyumba ya Daudi; Je! Ni neno dogo kwenu kuwachosha wanadamu, hata mkataka kumchosha Mungu wangu pia? Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, Bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
Zab. 40:6 – 10 (K) 7 , 8
(K) Tazama, nimekuja, Ee Bwana, kuyafanya mapenzi yako.
Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo,
Masikio yangu umeyazibua,
Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.
Ndipo niliposema, Tazama nimekuja. (K)
Katika gombo la chuo nimeandikiwa
Kuyafanya mapenzi yako,
Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu;
Naam, sheria yako imo moyoni mwangu. (K)
Nimehubiri habari za haki katika kusanyiko kubwa,
Sikuizuia midomo yangu; Ee Bwana, unajua. (K)
Sikusitiri haki yako moyoni mwangu;
Nimetangaza uaminifu wako na wokovu wako.
Sikuficha fadhili zako wala kweli yako
Katika kusanyiko kubwa. (K)
Ebr. 10:4 – 10
Haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi. Kwa hiyo ajapo ulimwenguni, asema, Dhabihu na toleo hukutaka, Lakini mwili uliniwekea tayari; Sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo; Ndipo niliposema, Tazama nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa) niyafanye mapenzi yako, Mungu.
Hapo juu asemapo, Dhabihu na matoleo na sadaka za kuteketezwa na hizo za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo (zitolewazo kama ilivyoamuru torati), ndipo aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili. Katika mapenzi hayo tumepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu.
Neno la Bwana…
Tumshukuru Mungu.
Yn. 1:14
Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu, nasi tukaona utukufu wake.
Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu. Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema. Bwana yu pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani? Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye ju, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu. Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Updated at: 2024-05-27 07:09:44 (11 months ago by DIN - Melkisedeck Leon Shine)
Naliwaamuru neno hili, nikisema, Sikilizeni sauti yangu, nami nitakuwa Mungu wenu, nanyi mtakuwa watu wangu; mkaende katika njia ile yote nitakayowaamuru, mpate kufanikiwa. Lakini hawakusikiliza, wala kutega sikio lao, bali walikwenda kw amashauri yao wenyewe, na kwa ushupavu wa mioyo yao mibaya, wakaenda nyuma wala si mbele. Tokea siku ile baba zenu walipotoka katika nchi ya Misri hata leo, nimewatuma watumishi wangu wote manabii kwenu ninyi, nikiamka mapema kila siku na kuwatuma. Lakini hawakunisikiliza, wala kutega sikio lao; bali walifanya shingo yao kuwa ngumu; walitenda mabaya kuliko baba zao. Nawe utawaambia maneno hayo yote; lakini hawatakusikiliza; nawe utawaita; lakini hawatakuitikia. Nawe utawaambia, Taifa hili ndilo lisilosikiliza sauti ya Bwana, Mungu wao, wala kupokea mafundisho; uaminifu umepotea, umekatiliwa mbali vinywa vyao.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
(K) Ingekuwa heri leo msikie sauti yake! Msifanye migumu mioyo yenu.
Njoni, tumwimbie Bwana,
Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu.
Tuje mbele zake kwa shukrani,
Tumfanyie shangwe kwa zaburi. (K)
Njoni, tuabudu, tusujudu,
Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba.
Kwa maana ndiye Mungu wetu,
Na sisi tu watu wa malisho yake,
Na kondoo za mkono wake. (K)
Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
Msifanye migumu mioyo yenu;
Kama vile huko Meriba,
Kama siku ya Masa jangwani.
Hapo waliponijaribu baba zenu,
Wakanipima, wakayaona matendo yangu. (K)
Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
Unirudishie furaha ya wokovu wako.
Yesu alikuwa akitoa pepo bubu; ikawa pepo alipotoka, yule bubu akanena, makutano wakastaajabu. Wengine wao wakasema, Atoa pepo kwa Beelzebuli, mkuu wa pepo. Wengine walimjaribu, wakitaka ishara itokayo mbinguni. Naye akajua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme uliofitinika wenyewe kwa wenyewe hufanyika ukiwa; na nyumba juu ya nyumba huanguka. Basi, ikiwa Shetani naye amefitinika juu ya nafsi yake, ufalme wake utasimamaje? Kwa kuwa ninyi mnasema kwamba mimi natoa pepo kwa Beelzebuli, wana wenu je! Huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo, hao ndio watakaowahukumu. Lakini, ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia. Mtu mwenye nguvu aliyejifunga silaha zake, alindapo nyumba yake, vitu vyake vi salama; lakini mtu mwenye nguvu kuliko yeye atakapomwendea na kumshinda, amnyang’anya silaha zake zote alizokuwa akizitegemea, na kuyagawanya mateka yake.
Mtu ambaye si pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutapanya.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Updated at: 2024-05-27 07:09:31 (11 months ago by DIN - Melkisedeck Leon Shine)
Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Atakuja vivyo hivyo mlivyomwona akienda zake mbinguni, Aleluya.
Kitabu kile cha kwanza nalikiandika, Theofilo, katika habari ya mambo yote aliyoanza Yesu kufanya na kufundisha, hata siku ile alipochukuliwa juu, alipokuwa amekwisha kuwaagiza kwa Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua; wale aliowadhihirishia nafsi yake, kwa dalili nyingi, baada ya kuteswa kwake, ya kwamba yu hai, akiwatokea muda wa siku arobaini, na kuyanena mambo yaliyouhusu ufalme wa Mungu. Hata alipokuwa amekutana nao aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali waingoje ahadi ya Baba, ambayo mlisikia habari zake kwangu; ya kwamba Yohane alibatiza kwa maji, bali ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu baada ya siku hizi chache.
Basi walipokutanika, wakamwuliza, wakisema, Je! Bwana, wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli ufalme? Akawaambia, Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe. Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.
Akiisha kusema hayo, walipokuwa wakitazama, akainuliwa, wingu likampokea kutoka machoni pao. Walipokuwa wakikaza macho mbinguni, yeye alipokuwa akienda zake, tazama, watu wawili wakasimama karibu nao, wenye nguo nyeupe, wakasema, Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
(K) Mungu amepaa kwa kelele za shangwe, Bwana kwa sauti ya baragumu. au: Aleluya
Enyi watu wote, pigeni makofi,
Mpigieni Mungu kelele kwa sauti ya shangwe,
Kwa kuwa Bwana Aliye juu, mwenye kuogofya,
Ndiye mfalme mkuu juu ya dunia yote. (K)
Mungu amepaa kwa kelele za shangwe,
Bwana kwa sauti ya baragumu.
Mwimbieni Mungu, naam, imbeni;
Mwimbieni mfalme wetu, naam, imbeni. (K)
Maana Mungu ndiye mfalme wa dunia yote,
Imbeni kwa akili.
Mungu awamiliki mataifa,
Mungu ameketi katika kiti chake kitakatifu. (K)
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo; na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake; aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho; juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
Aleluya, aleluya,
Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, na tazama, mimi nipo pamoja nanyi sikuzote.
Aleluya.
Wale wanafunzi kumi na mmoja walikwenda Galilaya mpaka mlima ule aliowaagiza Yesu. Nao walipomwona, walimsujudia; lakini baadhi yao waliona shaka. Yesu akaja kwao, akasema nao, akawambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi sikuzote, hata ukamilifu wa dahari.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Updated at: 2024-05-27 07:09:21 (11 months ago by DIN - Melkisedeck Leon Shine)
Eliya alifika kunako pango, akalala ndani yake. Na tazama, neno la Bwana likamjia. Akasema, Toka, usimame mlimani mbele za Bwana. Na tazama, Bwana akapita; upepo mwingi wa nguvu ukaipasua milima, ukaivunjavunja miamba mbele za Bwana; lakini Bwana hakuwamo katika upepo ule; na baada ya upepo, tetemeko la nchi; lakini Bwana hakuwamo katika lile tetemeko la nchi: na baada ya tetemeko la nchi kukawa na moto; lakini Bwana hakuwamo katika moto ule; na baada ya moto sauti ndogo, ya utulivu.
Ikawa, Eliya alipoisikia, alijifunika uso wake katika mavazi vake, akatoka, akasimama mlangoni mwa pango.
NENO LA BWANA.......
Nisikie atakavyosema Mungu Bwana,
Maana atawambia watu wake amani.
Hakika wokovu wake u karibu na wamchao,
Utukufu ukae katika nchi yetu.
(K) Ee Bwana, utuonyeshe rehema zako, Utupe wokovu wako.
Fadhili na kweli zimekutana,
Haki na amani zimebusiana.
Kweli imechipuka katika nchi,
Haki imechungulia kutoka mbinguni.
(K) Ee Bwana, utuonyeshe rehema zako, Utupe wokovu wako.
Naam, Bwana atatoa kilicho chema,
Na nchi yetu itatoa mazao yake.
Haki itakwenda mbelc zake,
Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia.
(K) Ee Bwana, utuonyeshe rehema zako, Utupe wokovu wako.
Nasema kweli katika Kristo, sisemi uongo, dhamiri yangu ikinishuhudia katika Roho Mtakatifu, ya kwamba nina huzuni nyingi na maumivu yasiyokoma moyoni mwangu.
Kwa maana ningeweza kuomba mimi mwenyewe niharimishwe na kutengwa na Kristo kwa ajili ya ndugu zangu, jamaa zangu kwa jinsi ya mwili; ambao ni Waisraeli, wenye kule kufanywa wana, na ule utukufu, na maagano, na kupewa torati, na ibada ya Mungu, na ahadi zake; ambao mababu ni wao, na katika hao alitoka Kristo kwa jinsi ya mwili.
Ndiye aliye juu ya mambo yote, Mungu, mwenye kuhimidiwa milele. Amina.
NENO LA BWANA.....
Aleluya, aleluya,
Abarikiwe Mfalme ajaye kwa jina la Bwana;
Aleluya.
Yesu aliwalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng'ambe. wakati yeye alipokuwa akiwaaga makutano. Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake.
Na kile chombo kimekwisha kufika katikati ya bahari, kinataabika sana na mawimbi; maana upepo ulikuwa wa mbisho. Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea. akienda kwa miguu juu ya bahari.
Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni kivuli, wakapiga yowe kwa hofu. Mara Yesu akanena, akawaambia, Jipeni movo; ni mimi; msiogope. Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji. Akasema, Njoo.
Petro akashuka chomboni, akaenda kwa miguu juu ya maji, ili kumwendea Yesu. Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe akisema, Bwana, niokoe.
Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka? Nao walipopanda chomboni, upepo ulikoma. Nao waliokuwamo ndani ya chombo wakamsujudia wakisema, Hakika wewe ni Mwana wa Mungu.
NENO LA BWANA..........
Updated at: 2024-05-27 07:09:47 (11 months ago by DIN - Melkisedeck Leon Shine)
Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, na hawakuweza kusema naye kwa amani.
Ndugu zake wakaenda kuchunga kondoo za baba yao huko Shekemu. Israeli akamwambia Yusufu, Je! Ndugu zako hawachungi kondoo katika Shekemu? Njoo, nikutume kwao.
Basi Yusufu akawafuata ndugu zake akawakuta huko Dothani. Wakamwona toka mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya shuri juu yake ili wamwue. Wakasemezana wao kwa wao, Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja. Haya, twende, tukamwue na kumtupa katika birika mojawapo, nasi tutasema, Mnyama mkali amemla; kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake. Reubeni akasikia akamwokoa katika mikono yao, akasema, Tusimwue. Reubeni akawaambia, Msimwage damu; mtupeni katika birika iliyopo nyikani, wala msimguse; ili apate kumwokoa katika mikono yao, akamrudishe kwa baba yake. Ikawa Yusufu alipofika kwa ndugu zake, wakamvua Yusufu kanzu yake, kanzu ile ndefu aliyoivaa, wakamtwaa wakamtupa katika birika; na hiyo birika ilikuwa tupu, hamna maji. Nao wakakaa kitako kula chakula.
Wakainua macho yao, wakaona, msafara wa Waishmaeli wanakuja wakitoka Gileadi na ngamia zao, wakichukua ubani na zeri na manemane, wakisafiri kuvichukua mpaka Misri. Yuda akawaambia ndugu zake, Kwafaa nini kumwua ndugu yetu, na kuificha damu yake? haya, na tumwuze kwa hawa Waishmaeli, wala mikono yenu isimdhuru, maana yeye ni ndugu yetu, na damu yetu. Ndugu zake wakakubali.
Wakapita wafanyabiashara Wamidiani; basi wakamtoa Yusufu, wakampandisha kumtoa katika birika wakamwuza Yusufu kwa Waishmaeli kwa vipande vya fedha ishirini; nao wakamchukua Yusufu mpaka Misri.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
(K) Zikumbukeni ajabu zake Bwana alizozifanya.
Akaiita njaa iijilie nchi,
Akakiharibu chakula chote walichokitegemea.
Alimpeleka mtu mbele yao,
Yusufu utumwani. (K)
Walimwumiza miguu yake kwa pingu,
Akatiwa katika minyororo ya chuma.
Hata wakati wa kuwadia neno lake,
Ahadi ya Bwana ilimjaribu. (K)
Mfalme alituma watu akamfungua,
Mkuu wa watu akamwachia.
Akamweka kuwa bwana wa nyumba yake,
Na mwenye amri juu ya mali zake zote. (K)
Jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee; Kila mtu amwaminiye huwa na uzima wa milele.
Yesu aliwaambia wakuu wa makuhani na wazee wa watu, Sikilizeni mfano mwingine. Kulikuwa na mtu mwenye nyumba, naye alipanda shamba la mizabibu, akalizungusha ugo, akachimba shimo la shinikizo ndani yake, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. Wakati wa matunda ulipokuwa karibu, akawatuma watumwa wake kwa wale wakulima, wapokee matunda yake. Wale wakulima wakawakamata watumwa wake, huyu wakampiga, na huyu wakamwua, na huyu wakampiga kwa mawe. Akawatuma tena watumwa wengine wengi kuliko wa kwanza, wakawatenda vile vile.
Mwishowe akamtuma mwanawe kwao, akisema, Watamstahi mwanangu. Lakini wale wakulima walipomwona yule mwana, wakasemezana wao kwa wao, Huyu ni mrithi; haya na tumwue, tuutwae urithi wake. Wakamkamata, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua. Basi atakapokuja yule bwana wa shamba la mizabibu, atawatendaje wale wakulima? Wakamwambia, Ataangamiza vibaya wale wabaya; na shamba la mizabibu atawapangisha wakulima wengine, watakaomlipa matunda kwa wakati wake.
Yesu akawaambia, Hamkupata kusoma katika maandiko, Jiwe walilolikataa waashi, hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni; neno hili limetoka kwa Bwana, nalo ni ajabu machoni petu? Kwa sababu hiyo nawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa, linguine lenye kuzaa matunda yake.
Wakuu wa makuhani na Mafarisayo, waliposikia mifano yake, walitambua ya kuwa anawanenea wao. Nao walipotafuta kumkamata waliogopa makutano, kwa maana wao walimwona kuwa nabii.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Updated at: 2024-05-27 07:09:25 (11 months ago by DIN - Melkisedeck Leon Shine)
Musa aliwaambia makutano: Nawe utaikumbuka njia ile yote Bwana, Mungu wako, aliyokuongoza miaka hii arobaini katika jangwa, ili akutweze, kukujaribu, kuyajua yaliyo moyoni mwako, kwamba utashika amri zake, au sivyo. Akakutweza, akakuacha uone njaa, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe wala baba zako hawakuijua; apate kukujulisha ya kuwa mwanadamu haishi kwa mkate tu, bali huishi kwa kila litokalo katika kinywa cha Bwana. Basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau Bwana, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa; aliyekuongoza katika jangwa lile kubwa lenye kitisho, lenye nyoka za moto na nge, nchi ya kiu isiyokuwa na maji; aliyekutolea maji katika mwamba mgumu, aliyekulisha jangwani kwa mana, wasiyoijua baba zako.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
(K) Msifu Bwana, Ee Yerusalemu.
Msifu Bwana, Ee Yerusalemu;
Msifu Mungu wako, Ee Sayuni.
Maana ameyakaza mapingo ya malango yako,
Amewabariki wanao ndani yako. (K)
Ndiye afanyaye amani mipakani mwako,
Akushibishaye kwa unono wa ngano.
Huipeleka amri yake juu ya nchi,
Neno lake lapiga mbio sana. (K)
Humhubiri Yakobo neno lake,
Na Israeli amri zake na hukumu zake.
Hakulitendea taifa lolote mambo kama hayo,
Wala hukumu zake hawakuzijua.
aleluya. (K)
Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, je! Si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo? Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
Aleluya, aleluya,
Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; asema Bwana; mtu akila chakula hiki, ataishi milele.
Aleluya.
Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. Basi Wayahudi walishindana wao kwa wao wakisema, Awezaje mtu huyu kutupa sisi mwili wake ili tuule? Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho. Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi. Hiki ndicho chakula kishukacho kutoka mbinguni; si kama mababa walivyokula, wakafa; bali akilaye chakula hicho ataishi milele.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.