Kuna watu wengi sana huwa wanani-challenge ninaposema kwamba ni muhimu sana mtu kuishi katika kusudi la maisha yake. Na moja kati ya hoja zao ni kwamba haya maisha ya sasa mtu akisema aanze kutafuta kusudi la maisha yake atakufa maskini. Hivyo wanaonelea ni bora kufanya chochote kitakachotokea mbele yake ilimradi mwisho wa siku anapata pesa. Yaani anachagua kuwa mtumwa wa Pesa
Kusudi la maisha ya mtu huwa halina ukomo na halibadiliki, kinachobadilika au kufikia ukomo ni malengo ya kuli-ishi kusudi hilo. Kwa hiyo unapopanga malengo yako au unapokuwa na ndoto zako ni lazima uweze kupambanua mwisho wa siku hizo ndoto au hayo malengo yanakwenda kukidhi kiu ya aina gani inayofukuta ndani yako.
Ukifanikiwa kulitambua kusudi la maisha yako na ukafanikiwa kuli-ishi kwa vitendo, ni dhahiri utakuwa maarufu kwenye mazingira yanayohusiana na maisha yako. Mazingira yanayohusiana na maisha yako yapo ndani ya kusudi la maisha yako.
Ni wakati gani mtu anaweza kusema amefanikiwa katika maisha yake? Ni pale ambapo tu mtu anapoweza kutatua tatizo fulani katika jamii; Kugundua uhitaji wa kutimizwa au kukamilishwa kwa jambo fulani katika jamii. Ukiweza kuziba pengo fulani. Ukiweza kupata ufumbuzi wa kukamilishwa kwa hilo jambo kwa faida ya jamii fulani au niseme ukiweza kutatua tatizo hilo hapo unaweza kusema umefanikiwa. Huwezi kutatua tatizo lolote katika jamii kama hujawekeza ndani yako.
Haijalishi ni jambo gani unafanya katika jamii na liko kwenye kiwango kipi ilimradi liko ndani ya mstari wa maisha yako. Kwa mfano, una kamtaji kadogo na unaamua kuanzisha genge la kuuza mahitaji madogo madogo ya nyumbani (hasa jikoni) naamini unakuwa umeanzisha kwa sababu umeona eneo hilo kuna uhitaji wa aina hiyo ya huduma. Wewe unaweza kuwa unafanya tu labda kwa sababu ya shida fulani za maisha lakini wakati huo huo moyo wako unafurahia kile unachokifanya na unajikuta kila siku unabuni mbinu mpya na mikakati wa kuboresha genge lako. Kidogo kidogo unafungua genge lingine sehemu nyingine, na lingine na lingine, nk. Mwishowe unajikuta unatamani kuwa na duka kubwa la vyakula na mahitaji mengine ya kila siku au supermarket. Ukijiona unang’ang’ana kwenye “line” moja ya shughuli (Biashara) basi tambua hilo ndio kusudi lako na ndani yako una zawadi kubwa sana ya kutoka kwa Mungu ya kuhudumia jamii kupitia uuzaji wa mahitaji ya nyumbani.
Lakini ukijiona unatanga tanga leo umefanya shughuli hii kesho umefanya shughuli ile ambazo mwisho wa siku hakuna mahali zinakutana kwa namna yoyote ile japo unapata pesa, basi wewe hujatambua kusudi la maisha yako na usipokuwa makini utakuwa mhangaikaji hadi mwisho.
Ukifanya jambo nje ya kusudi ya maisha yako hutakaa ulifurahie kamwe, litageuka kuwa mateso hata kama linakuingizia pesa nyingi. Unaweza ukawa unafanya kitu nje ya mstari wako wa maisha hata kama kinakulipa mabilioni yaani bado utakuwa kama SAMAKI ALIYETUPWA NJE YA MAJI. Samaki akiwa nje ya maji, zile dakika chache kabla hajafa huwa anahangaika sana na ukimmiminia tone moja la maji kwenye mkia utaona anavyojaribu kutaka kuogelea. Kale katone ka maji kwenye mkia wa samaki akiwa nchi kavu ni sawa na wewe unapokuwa unafanya shughuli nje ya kusudi la maisha yako inyokupa hela nyingi lakini ikatokea katika kuhangaika ukafanya ka-kitu kadogo ambako kako ndani ya kusudi la maisha yako – moyo waku unakuwa na amani sana na unafurahi sana. Lakini unajikuta huendelei kufanya hilo jambo kwa sababu halikuingizii hela nyingi kwa wakati huo ukilinganisha na lile lingine hivyo unaamua kuendelea kuishi nje ya kusudi la maisha yako ili upate mali za nje na kuunyanyasa moyo wako. Maana yake ni kwamba, kama unafanya shughuli inayokuingizia kipato iliyo nje ya kusudi la maisha yako, hutokaa uache kuhangaika kujaribisha vitu vya aina mbalimbali. Kwa sababu moyo wako hautotosheka wa kuridhika – HUWEZI KUKATA KIU YA MAJI KWA KUNYWA SODA AU JUISI JAPOKUWA VYOTE NI VIMIMINIKA. . Ndio sababu huwa napenda kusisitiza sana kupata muda kwa ajili ya maisha yako binafsi, hii inakusaidia kujitambua.
Tatizo wengi hatutaki kuanzia chini, tunapadharau huku chini lakini matajiri wakubwa duniani kama unafuatilia historia za maisha yao na jinsi walivyoanza utagundua kwamba walianza wengine wakiwa hawana kitu kabisa. Ukiwa na nidhamu ya maisha hasa kwa kufuata kanuni za maisha, kanuni za biashara/shughuli unayofanya na kanuni za maisha yako binafsi huwezi kuacha kufanikiwa. Mafanikio ni safari. Umaarufu hauji bila kuwa umefanikiwa kwenye jambo fulani hata kama ni ujinga utapata umaarufu kwa wajinga wenzako.
Mafanikio yanaanza kwa wewe kuweza kujitofautisha na maisha yako ya nyuma. Usiruhusu maisha yako ya nyuma kukuwinda na hivyo kuwa kikwazo cha maisha yako unayoyaendea. Usiishi kwa mazoea ya nyuma. Mafanikio ni pale unapoweza kujitambua na kusimama imara katika kanuni za maisha ulizojiwekea na kujitofautisha na watu wengine wote kwa sababu wewe ni wa tofauti, kila binadamu ni wa tofauti ndio mana kila mtu ana nafsi yake mwenyewe hata mkiwa mapacha mmeunganika viungo vya mwili.
MAFANIKIO YANAANZA NAWEWE
References:
Google ScholarResearchGate
Semantic Scholar
AckySHINE