Tafakari za Safari ya Kuelekea Utakatifu

Mungu anapenda kutenda jambo baada ya mtu kumuomba/kusali ili mtu aelewe Ukuu wa Mungu na ili Mungu atukuzwe.

Kwa nini tunasali na Kumuabudu Mungu?

Embu tafakari kwa nini unasali na Kumuabudu Mungu!

Je unasali kwa hofu ya kutokua na uhakika na maisha?

Je unasali kwa sababu ya shida na matatizo katika maisha?

Je unasali kwa kuwa unaona wengine wanasali kwa hiyo unafikiri na wewe lazima usali?

Je unasali kwa kuwa unamwogopa Mungu?

Je unasali na kuabudu kama kutimiza wajibu katika dini au kanisa lako?

Je Unasali kutimiza wajibu kama kiumbe kwa Mungu?

Je unasali kwa kuwa unapenda Kusali?

Je unasali kwa kuwa Unampenda Mungu?

Je unasali kwa kuwa Unampenda Mungu na unaona ni wajibu wako Kusali?

Je unasali kwa kuwa Unampenda Mungu na unaona ni njia ya kujenga mahusiano na Mungu?

Je unasali na Kumuabudu Mungu kwa kuwa unajisikia vibaya kwa kuwa unaona wengine hawasali kwa hiyo unataka kumfariji Mungu kwa sala zako?

Tafakari uko wapi wewe?

Read and Write Comments
Namna pekee ya kuwa na Amani ni kuishi Mapenzi ya Mungu, Kwa njia hii Moyo wako hautafadhaika, hautayumbishwa na hautajuta kwa kuwa utakua upo katika njia ya Mungu na njia ya Mungu haina Majuto kwa kuwa ni njema.

Amani ya Moyoni au Rohoni

Amani ya Moyoni au Rohoni ni hali ya kutokua na wasiwasi na hofu moyoni kuhusu Mambo ya Rohoni na ya kidunia.

Ili kuwa na Amani ya Moyoni unatakiwa uishi kwa kutimiza wajibu wako wa kiroho na kidunia kama inavyotakiwa na kwa uwezo wako wote, Huku ukiwa na Matumaini ya kua kile unachokifanya kitafanikiwa, ni sahihi na umekifanya vizuri.

Uwe na Matumaini na utaipata Amani.

Read and Write Comments

Kujikabidhi Kwa Yesu Kristu Yeye Aliye Mwangaza Wa Maisha

Yesu ni Mwanga na Uovu ni giza

Giza na Mwanga havichangamani. Yesu hakai pamoja na uovu.
Giza haliwezi kuzidi Mwanga. Uovu hauwezi kumzidi Yesu.
Mwanga ukija giza linaondoka. Yesu akija uovu unakwisha.

Yesu Kristu ni mwangaza wa maisha yetu, akiwepo giza lote hutoweka.
Yesu akiwepo hakuna haja ya kufukuza giza bali giza litatoweka Lenyewe.

Unapomkaribisha Yesu katika maisha yako umekaribisha mwanga katika maisha yako na utashinda dhambi na uovu kwa kuwa Yesu aliye mwanga atavifutilia mbali.

Kikubwa ni kumkaribisha Yesu katika maisha yako na kumruhusu atawale Maisha yako na kila kitu katika maisha yako. Ukiweza kuachilia yote kwa Bwana Yesu na kumpa maisha yako basi utashinda uovu/dhambi. Vile unavyojiweka karibu na Yesu ndivyo unavyoshinda dhambi na uovu wote.

Kumkabidhi Yesu Maisha ni Kuamua kuishi kulingana na Mafundisho yake, kuachilia yote katika maongozi yake, kumshirikisha Yesu kwenye kila kitu katika maisha yako na Kuwa mkweli na muwazi mbele ya Yesu katika kila kitu.

Unapomkabidhi Yesu Maisha yako na vyote ulivyonavyo yeye huyatakatifuza na kuyafanya yawe kama yanavyotakiwa kuwa kitakatifu.

Changamoto kubwa kwa Wakristu ni kushindwa kujiweka Mikononi mwa Yesu kwa kuachilia yote na kukabidhi yote kwake. Wengi wanashindwa kufanya hivyo kwa sababu ya ubinafsi na uchu wa kusimama wenyewe. Wengine wanashindwa kwa sababu ya kukosa Imani. Hawana uhakika kwamba wanachokifanya wanakifanya kweli.

Lakini ukiweza kweli kumkabidhi Yesu Maisha yako, kila kitu kinakua sawa na utafanikiwa kwenye kila kitu. Utaanza kuona unashinda uovu na dhambi kulingana na vile unavyojikabidhi na kujiachilia kwa Yesu.

Anza leo kujikabidhi kwa yesu kwa kiasi kile unachoweza. Yesu anaelewa ubinadamu na madhaifu yetu. Atakusaidia. Hata kama kuna wakati unaweza kujikabidhi kwake na kisha unaanguka tena, yeye ni mwenye huruma na ni mwelewa haswa kuhusu hali yako, atakusaidia na kukuwezesha. Weka nia ya kujikabidhi kwake na kisha utaendelea kidogo kidogo mpaka utajikuta umejikabidhi mikononi kwake kabisa.

KUMBUKA: Yesu ni Mwanga na Uovu ni giza, mwanga ukiwepo giza halibaki linaondoka. Hata siku moja Giza haliwezi kuuzidi mwanga

Uwe na Imani basi, Mtumainie Yesu Kristu atakushindia uovu.

Yesu ndiyo dawa ya uovu na dhambi, kila unapoanguka dhambini mkimbilie yeye naye atakusamehe na kukuwezesha kushinda dhambi na uovu. Usichoke, kila siku jaribu na kujaribu mpaka utashinda.

Nami nakuombea kwa Jina Takatifu la Yesu, Akushindie Uovu na dhambi

Read and Write Comments

Vile unavyoweza kuwa DARAJA au KIKWAZO kwa wengine

Kwa namna unayoishi unaweza ukawa daraja au kikwazo cha wengine kuishi maisha ya Amani raha na fanaka.
Unaweza ukawa daraja kwa maana kwamba wewe unaweza kuwa sababu ya wengine kupata Baraka na neema za Mungu.
Unaweza kuwa kikwazo kwa maana kwamba unaweza kuwa wewe ni sababu ya wengine kutokupata Baraka na Neema za Mungu.

Kwa jinsi unavyoishi unaweza ukawa chanzo cha Baraka kwa wengine au chanzo cha matatizo na vikwazo kwa wengine.

Vile unavyoweza kuwa Daraja kwa Wengine

Unaweza kuwa daraja au njia ya wengine kupata neema na Baraka katika maisha yao kulingana na matendo yako mema na Ibada yako kwa Mungu.

Kwa ucha Mungu wako, watu wako unaowapenda sana wanaweza kubarikiwa na kupata neema za Mungu Pamoja na wewe. Wale watu unaochangamana nao watabarikiwa kwa sababu na wewe umebarikiwa.
Kwa mfano wewe kama ni mzazi mcha Mungu unaweza ukawa chanzo cha Baraka na neema kwa watoto wako na kwa mwenzi wako wa ndoa. Vivyo hivyo na kwa watoto, mtoto anaweza kuwa chanzo cha Baraka kwa wazazi wake.

Inawezekana kuna Amani katika familia yako kwa sababu tuu wewe ni miongoni mwa wanafamilia hiyo na hivyo Mungu ameachilia Amani katika familia yako kwa sababu tuu wewe upo pale na wewe ni mcha Mungu.

Unaweza kuona sasa wewe ni chanzo cha Baraka kwa wale watu wako wa karibu. Kwa sababu tuu wewe ni mcha Mungu, na wao wanabarikiwa pamoja na wewe. Mungu anapobariki familia yako na wao pia wanabarikiwa.

Kwa hiyo basi, unapolegalega katika ucha Mungu wako unaweza pia kusababisha kulegalega au kikwazo cha Baraka za wengine.

Vile unavyoweza kuwa Kikwazo kwa Wengine

Unaweza kuwa kikwazo au kizuizi cha wengine kupata neema na Baraka katika maisha yao kulingana na matendo yako mabaya na kukosa kwako kumcha Mungu.

Kwa kuacha kumcha Mungu, watu wako unaowapenda sana wanaweza kukosa kubarikiwa na kukosa neema za Mungu kwa sababu wewe unazuia Baraka hizo. Wale watu unaochangamana nao watakosa Baraka kwa sababu umeandikiwa kutokubarikiwa na wanachanganyikana na asiyestahili kubarikiwa.

Kwa mfano wewe kama ni mzazi asiyemcha Mungu unaweza ukasababisha watoto wako wakashindwa kubarikiwa kwa sababu tuu kwa udhambi wako unazuia Baraka kwa familia yako yote wakiwemo watoto wako. Vivyo hivyo na wazazi wanaweza wakashindwa kubarikiwa kwa sababu watoto wao wanawazuilia Baraka zao.

Inawezekana hakuna Amani katika familia yako kwa sababu tuu wewe ni miongoni mwa wanafamilia hiyo. Kunakosekana Amani katika familia yako kwa sababu tuu wewe upo pale na wewe ni mdhambi/ mtu asiyemcha Mungu.

Unaweza kuona sasa wewe ni chanzo cha kukosekana Baraka kwa wale watu wako wa karibu. Kwa sababu tuu wewe ni mtu asiye mcha Mungu, na wao wanazuiliwa baraka pamoja na wewe. Mungu anapoacha kuibariki familia yako na wao pia wanakosa baraka. Kwa mfano unapokosa Amani na Mafanikio ukae ukijua kuwa wale unaowapenda na wanaokutegemea nao watakosa Amani na hawatanufaika kwa sababu hauna mafanikio.

Mwisho

Wewe ni kama Kiungo cha myororo wa Baraka au laana kwa wale uwapendao hasa familia yako. Ukibarikiwa unabarikiwa pamoja nao, ukilaaniwa unalaaniwa pamoja nao.

Kwa sababu hiyo, mara zote chagua kuishi kwa kumcha Mungu kwa sababu huwezi jua ni wangapi walioko nyuma yako na wanaobarikiwa kwa sababu ya ucha Mungu wako.

Mche Mungu kwa juhudi zote kwa sababu hujui ni wangapi wanaonufaika na ucha Mungu wako. Vilevile jitahidi usiwe mdhambi sana kwa sababu huwezi kujua ni wangapi wanaokosa Baraka za Mungu kwa udhambi wako.

Kumcha Mungu kuna faida kwako na kwa wengine, hasa unaowapenda. Kuto kumcha Mungu ni hasara kwako na kwa wale unaowapenda hasa familia yako

Read and Write Comments
Namna pekee ya kuwa na Amani ni kuishi Mapenzi ya Mungu, Kwa njia hii Moyo wako hautafadhaika, hautayumbishwa na hautajuta kwa kuwa utakua upo katika njia ya Mungu na njia ya Mungu haina Majuto kwa kuwa ni njema.

Safari ya kupata fadhila ya Unyenyekevu

Leo tunatafakari kuhusu safari ya kupata fadhila ya Unyenyekevu,

Fadhila ya Unyenyekevu ni tunda ya Upendo na Uvumilivu kwa hiyo ili kufikia Unyenyekevu yakupasa kuwa na Upendo wa kweli kwa Mungu na Wanadamu huku ukiwa mvumilivu, Mwisho wa yote hayo utapata fadhila ya Unyenyekevu

Mungu ni myenyekevu kwa kuwa anaupendo na Uvumilivu

Ni vigumu kuishi kitakatifu bila Unyenyekevu

Read and Write Comments
Namna pekee ya kuwa na Amani ni kuishi Mapenzi ya Mungu, Kwa njia hii Moyo wako hautafadhaika, hautayumbishwa na hautajuta kwa kuwa utakua upo katika njia ya Mungu na njia ya Mungu haina Majuto kwa kuwa ni njema.

TAFAKARI KUHUSU NAFASI YA MATESO NA SHIDA KATIKA MAISHA

Ni kwa nini tunapata Mateso na shida katika Maisha? Kwa nini Mungu ameruhusu tuteseke?

Mungu hapendi mtu Ateseke lakini ni kwa njia ya ya Mateso mtu anaweza akapimwa IMANI yake, UNYENYEKEVU, UTII na Matumaini yake kwa Mungu.


Mateso na shida katika maisha ni nafasi ya kujifunza na Kuonyesha unyenyekevu, Imani na Matumaini ya mtu.


Mateso yanaweza kuwa malipizi ya dhambi kama adhabu au Majitoleo .


Mtu anaweza kujitesa au kukubali Mateso huku akiyachukulia kama malipizi ya dhambi zake au dhambi za wengine.


Sio rahisi kwa mtu wa kawaida kuweza kukubali au kujitesa kwa ajili ya dhambi hasa kwa dhambi zisizokua zake, Ni watu wachache Wenye fadhila hii. Mfano Watakatifu kama Mt. Faustina aliweza kuchukua Mateso kama malipizi ya dhambi hasa za watu wengine ambapo alikubali magonjwa shida na Kudharauliwa kama malipizi ya dhambi.


Yesu mwenyewe pamoja na Umumgu na Enzi yake alikubali Mateso kama Malipizi ya dhambi za watu na Kama njia ya Kuonyesha Unyenyekevu na Upendo.

Kumbuka, Mateso ni njia ya Kuonyesha unyenyekevu, Upendo na Kujitolea kwa hiyo ni kama malipizi na majitoleo hivyo sio lazima mtu ateseke au Ajitese ili aokolewe au aingie Mbinguni.


Mungu hapendi mtu ateseke ila anakubali Mateso kama njia ya kupima mtu na kumtakatifuza.

Mateso = Malipizi = Majitoleo = Kipimo cha Imani na Matumaini kwa Mungu

KUMBUKA: Ni kwa njia ya Mateso na Kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo sisi tuliokolewa. Mababu wote Kwenye Biblia na Manabii walipitia dhiki na Mateso, Hata mitume nao waliteseka


Sio mara zote Mateso na Shida maana yake ni kuachwa na Mungu au Kuadhibiwa na Mungu, mara nyingine mateso ni majaribu, kipimo cha Imani na njia ya kujivika Utakatifu.


Mungu anakupenda sana, mtumainie yeye. Yote yanapita lakini yeye atasimama milele.

Mungu na Akubariki na kukupa Faraja.
Read and Write Comments

Imani ni cheti cha Kuweza kupata yote

Imani ni kuwa na uhakika hata kwa mambo yasiyoonekana na yasiyowezekana. Ni kujua au kutarajia kwa uhakika kwa mambo ambayo bado hayajawa bayana (wazi) kuwa yapo au yatafanyika.

Kwa Imani Kila Kitu Kinawezekana. Kwa Sala na kwa Matendo.

Yesu Kristu anatufundisha tuwe na Imani kupitia Mfano huu;

18Yesu alipokuwa anarudi mjini asubuhi na mapema, aliona njaa. 19Akauona mtini mmoja kando ya njia, akauendea; lakini aliukuta hauma chochote ila majani matupu. Basi akauambia, “Usizae tena matunda milele!” Papo hapo huo mtini ukanyauka.

20Wanafunzi walipouona walishangaa wakisema, “Kwa nini mtini huu umenyauka ghafla?” 21Yesu akawajibu, “Kweli nawaambieni, kama mkiwa na imani bila kuwa na mashaka, mnaweza si tu kufanya hivyo, bali hata mkiuambia mlima huu: Ng’oka ukajitose baharini, itafanyika hivyo. 22Na mkiwa na imani, chochote mtakachoomba katika sala, mtapata.”
Mathayo 21:18-22

Basi Ili tuweze kuwa na Imani tumuombe Mungu atujalie Imani. Tuombe tujaliwe fadhila ya Imani hasa Tunaposali. Vile vile tumwombe Mungu atujalie Imani katika yale yote tunayoyafanya.

Tuombe hasa Imani isiyokuwa na Mashaka. Mashaka na Kusita sita ndiyo adui mkubwa wa Imani.

Read and Write Comments
Mambo haya yanaweza yakaonekana sio dhambi au makosa kwa mtu lakini ni vikwazo kwa mtu kufikia Ukamilifu anaposhindwa kuyajua na kuyaepuka

Mambo yanayowazuia Waumini na Watumishi wa Mungu Kufikia Ukamilifu na Utakatifu

Leo nimekuandalia Tafakari kuhusu Mambo yanayowazuia Waumini na watumishi wa Mungu Kuishi Kitakatifu na kufikia Ukamilifu. Mambo haya yanaweza yakaonekana sio dhambi au makosa kwa mtu lakini ni vikwazo kwa mtu kufikia Ukamilifu hasa anaposhindwa kuyajua na kuyaepuka. Wengi wanajiona kwamba wako salama lakini kumbe wako katika dhambi.

Mambo hayo ni kama ifuatavyo;

1. MAJIVUNO

Hii ni hali ya kujiona wa thamani sana, wakipekee na unayestahili sana.

Tofauti ya MAJIVUNO na pointi ya pili hapo chini (UMIMI) ni kwamba MAJIVUNO ni kujiona wa thamani lakini huku unatambua Yupo Mungu anayekuzidi. UMIMI ni kujiona kama Sawa na Mungu.

Kwa yale unayoyafanya: Kujiona kwamba wewe ni wa thamani na kipekee sana kwa yale uliyowahi kufanya, unayoyafanya na unayoweza kufanya. (I did, I do, I will do.)
Kwa vile Ulivyo: Kujiona kuwa wewe ni wa kipekee kwa vile ulivyo. Kusahau kuwa Vile ulivyo na vile ulivyonavyo Umepewa Bure na Mungu.
Kwa vile unavyofanyiwa: Kujiona kuwa wewe ni wa kipekee kulingana na wengine wanavyokuona na vile wanavyokufanyia.

Tafakari na ushauri kuhusu Majivuno
Unavyosoma kuwa majivuno ni hali ya kujiona wa thamani sana, wakipekee na unayestahili sana, unaweza ukafikiri sio kosa wala dhambi kujiona hivyo. Lakini makosa yanakuja kwa yale unayoyafanya kwa Majivuno hayo na kujisikia huko.
Majivuno yanakuwa dhambi pale tunapotenda kwa Majivuno na kujiona. Pale tunaposahau kwamba Upekee wetu sio kwamba tulistahili bali ni kwa Neema tuu. Tunakosea pale tunapoanza kuzarau wengine wale wasio kama sisi.

Unaweza ukafikiri kwamba hauna Majivuno lakini miongoni mwa dalili za Majivuno ni kama ifuatavyo;
1. Zarau
2. Kushindwa Kujishusha
3. Kujigamba/ Kujisifu
4. Kupenda upendeleo
5. Kujiona wa Tofauti
Ukiona kuna wakati una dalili kama hizi ujue tayari Majivuno yanajipandikiza ndani yako. Ninaposema Majivuno ni dhambi namaanisha kuwa matokeo/ matendo yanayotokana na dalili/ sifa hizi ndiyo dhambi.

Mambo ya kuzingatia kushinda Majivuno
Unyenyekevu… Unyenyekevu… Unyenyekevu ndio dawa ya Majivuno.
Utaweza kushinda majivuno kwa Kujishusha na kujiona sawa na wengine.

Unaweza ukashinda Majivuno kwa Kutambua kuwa Vile ulivyo, yale unayoweza kufanya na vile unavyofanyiwa ni Baraka za Mungu tuu. Haimaanishi kuwa umestahili sana kuwa hivyo.

Utashinda majivuno unapotambua kuwa hata wale unaowaona wako chini yako wangeweza kuwa kama wewe tuu. Ni maisha na Mipango ya Mungu ndio iliyofanya ukawa hivyo. Haimaanishi kwamba ni juhudi yako wewe. Wapo wenye Juhudi kuliko wewe lakini wapo chini yako.

2. UMIMI

Kujiona kuwa wewe ni wewe na wewe ni wa kipekee na unastahili kuliko wengine.

Tofauti kubwa na pointi ya kwanza hapo juu ni kwamba UMIMI ni Zaidi ya MAJIVUNO. Ni kujiona Hakuna wa Zaidi yako na wewe unahadhi sawa karibu na Mungu. Yaani, Mungu yupo lakini Mimi Pia nipo.

Kwa cheo, kipawa au mamlaka yako: Kujiona kwa cheo, kipawa au Mamlaka yako hakuna anayekuzidi, Mara nyingine kufikiri kwamba hata Mungu mwenyewe hawezi kukuondolea/ kukupinga. Ni kufikiri kwamba hakuna anayeweza kupinga maamuzi yako na hakuna wa kuamua Juu/ Zaidi yako.
Kwa unayoyafanya: Kuona kwamba kwa yale unayoyafanya hakuna kama wewe. Hakuna anayeweza kufanya kama wewe.
Kwa unayofanyiwa: Kuona kwamba hakuna anayestahili kufanyiwa kama wewe.

Kwamba Unaweza kufanya chochote: Kudhani kwamba unaweza kufanya chochote kile kwa sababu wewe ni wewe.

Tafakari na ushauri kuhusu UMIMI

Ninapoongelea Umimi siwalengi wenye mamlaka Makubwa ya juu tuu, Nalenga pia mtu mmoja mmoja kwa sababu kila mtu anayo mamlaka na Mwili na Utu wake. Unayo kipawa cha utu wako, uwanaume wako, uwanawake wako, Uzima wako. Vile vile Mamlaka ya Familia yako, jumuiya, ukoo n.k. Unamamlaka ya mwili wako na kwa hiyo kwa mwili huo usiutumie kwa uovu kwa sababu tuu umepewa mwili huo.

Kwa hiyo basi, ninapoongelea UMIMI naanzia chini kabisa kwenye Mamlaka na Mwili wako na Utu wako mpaka kwenye ngazi za jamii Kama Vyeo vya Kijamii na Kiinjili.

Unaweza ukadhani kwamba UMIMI sio makosa lakini makosa yanazaliwa pale unapotenda kwa kufuata umimi wako (Vile ulivyo). Dhambi inakuja pale Kwa sababu ya mamlaka yako unapoamua mambo kwa sababu unajua hakuna wa kukupinga. Kwa sababu ya uwezo wako wa kufanya mambo kufanya vitu kwa ubaya kwa sababu tuu unajua hakuna anayekuzidi/ anayeweza kufanya kama wewe/ anayeweza kukuzuia.

Dhambi inatokana na Kujiona kwako kuwa hakuna anayekuzidi kunakupelekea kushawishika kufanya mambo mengine ili kudhihirisha kuwa hakuna anayekuzidi kweli. Hasa kwa uonevu na ubabe.

UMIMI unaanza kuzaa dhambi pale mtu anapomsahau Mungu wake aliyemuumba na Kumpa huo UMIMI (Kumfanya vile alivyo). Unaposahau kuwa yupo Mungu aliyekupa hayo mamlaka, kipaji, kipawa na cheo ndipo unapoweza kuanza kukosea kwa UMIMI.

Mambo ya kuzingatia kushinda UMIMI
Kushinda UMIMI inahitaji unyenyekevu wa kujitambua kuwa Mamlaka, Kipaji, Kipawa au cheo chako Umepewa na Mungu na Unatakiwa Ukitumie kwa Mapenzi ya Mungu.
Ukitaka kuushinda UMIMI unapaswa kutambua kwamba yote yana Mwisho.

Vile vile unatakiwa ujue kuwa Ipo siku utatolea hesabu kwa kile ulichopewa. Ipo siku utaulizwa kwamba Umefanya nini na Mamlaka, Kipaji, Kipawa au cheo chako. Ndio maana wenye hekima wanaogopa sana kuwa na Mamlaka, Kipaji, Kipawa au cheo kwa sababu wanajua kuwa wanayo kazi kubwa kuliko wale wasiokuwa nacho.

Ukitambua kwamba unawajibika kwa vile ulivyo, basi ujitahidi kutenda kwa kumpendeza Mungu.
KUMBUKA Vile ulivyo inaweza kuwa njia rahisi ya kuufikia Ukamilifu na Utakatifu au inaweza ikawa Mtego kwako kwa kufikia Ukamilifu na Utakatifu. Ni wewe tuu kuamua Unaishije kwa Vile Ulivyo.

3. HASIRA, UKOROFI NA CHUKI

Hasira: Kukasirika haraka kwa kukosa uvumilivu na kutokutambua kuwa unapoishi na binadamu wengine ni lazima/ kawaida kukwazika. Watu hawawezi kufanya yote unayoyataka.
Ukorofi: Kuwa mbabe na kuweka vizuizi na masharti ya kiukorofi, pamoja na kufanya vitendo vya ukorofi na ukaidi kwa walio chini yako na hata walio juu yako.
Chuki: Kuwa na kinyongo na uchungu na watu wengine ambapo matokeo yake ni kufanyiana vitendo vya kikatili huku ukiwaza kuwa ni halali yako.

Tafakari na ushauri kuhusu Hasira, Ukorofi na chuki
Hasira, Ukorofi na chuki ni mambo ambayo mara nyingi yanaweza kuonekana sio dhambi moja kwa moja ila matokeo yake ndio yanaonekana kuwa ni dhambi. Hii ni kwa sababu kwa hali ya kawaida ya binadamu ni kawaida kwa mtu kuwa na Hasira, Ukorofi na chuki lakini vile anavyotenda baada ya kupata hasira au chuki inayopelekea ukorofi ndio inayosababisha mambo haya kuzaa dhambi.

Jambo lililo baya Zaidi ni kwamba dhambi inayotokana na Hasira, Ukorofi na chuki mara nyingi huonekana kama ni halali na haki ya mtu. Kwa Mfano, watu wengi wanaona kuwa ni kawaida kuwa mtu akikukasirisha lazima umfanyizie/ umtendee kitu kibaya. Wengine wanafikiri kuwa mtu anapokukasirisha lazima umuonyeshe ubabe. Na wengine wanaona ni kawaida kabisa kuwa na chuki na kinyongo hasa wanapotendewa visivyo na kuhisi kuwa ni haki yao kuchukia na kuwa na Kinyongo.

Lakini ukweli ni kwamba matendo yote yanayotendwa kwa Hasira, Ukorofi na chuki ni dhambi na makosa mbele ya Mungu. Kushindwa kuzuia Hasira, Ukorofi na chuki ni chanzo kikubwa cha dhambi kwa Wakristu walio wengi hasa Watumishi wa Mungu.

Makosa na dhambi za Hasira, Ukorofi na chuki yanawakoseha Neema za Mungu Watumishi wengi wa Mungu kwa sababu wengi wao hawaoni kama ni dhambi au ni makosa kufanya jambo kwa Hasira, Ukorofi na chuki. Wapo waumini na Watumishi wengi wa Mungu ambao wanaweza kufwatilia kikamilifu matakwa yote ya Imani yao lakini wanalegalega katika Imani yao kwa sababu ya kushindwa kutambua na kujiepusha na makosa na dhambi zitokanazo na Hasira, Ukorofi na chuki.

Mambo ya kuzingatia kushinda Hasira, Ukorofi na chuki
Kushinda Hasira
Ili kushinda hasira ni muhimu kuishi kwa kujua wakati wowote ule yupo mtu anaweza kukukosea.
Ni vizuri kuelewa kua wote wanaokukosea hawakukosei kwa kupenda au kwa kusudi. Ni lazima kutambua Katika maisha kuna mambo mengi yanayoweza yakafanya mtu akukosee au kukukwaza wewe. Huu ndio uhalisia wa Maisha.
Ni vizuri kujua kuwa Hasira ni hali inayoweza kuzimwa ukiamua kuizima na ni hali inayoweza kuwaka sana ukiamua kuiwasha. Sasa ni wewe kuchagua kuizima au kuiwasha.
Muhimu Zaidi kukumbuka ni kwamba Umeitwa Kuishi upendo wa Mungu na wa Jirani kwa maana hii umeitwa kusamehe na kuvumilia wengine huku ukiwaongoza na kuwaelekeza kile kinachotakiwa.

Kushinda Ukorofi
Namna kuu ya kushinda ukorofi ni kuwa mvumilivu. Kuwa mvumilivu na kuweza kuachilia (Kupotezea).
Unaweza kushinda ukorofi kwa Kutambua kuwa sio mara zote ni lazima kushindana na kubishana.
Kushinda Chuki
Kushinda chuki ni ngumu sana hasa unapokuwa tayari na katabia ka kuweka kinyongo au kuona uchungu/ wivu.
Wewe kama Mtumishi wa Mungu unaweza kushinda chuki kwa kujiepusha na tabia ya Kushindana na Kujilinganisha.
Chuki ni tabia au mazoea na kwa sababu hiyo unapotaka kuishinda unatakiwa ujijengee tabia na mazoea ya kinyume chake ambayo ni kujiepusha na mashindano na Kujilinganisha.
Zaidi sana, chuki inaweza kushindwa kwa ukarimu. Unapokua mkarimu unashinda chuki na wivu. Vilevile kwa ukarimu huu unaweza ukazuia chuki ya watu wengine. Utawasaidia wengine wasiwe na chuki na wewe pia, huku na wewe unajizuia na chuki.

MWISHO

Katika mambo yote haya Matatu unaweza ukaona kuwa naongelea Dhambi ya asili ya Binadamu. Dhambi ya Asili ya Binadamu ya Kujiona (PRIDE). Kila binadamu anazaliwa kwa kiasili akiwa na hali ya kujiona (PRIDE). Kila binadamu anazaliwa akiwa anajiona kuwa yeye ni yeye na Hakuna kama yeye.

Hali hii ya kuzaliwa ya kujiona ndio inayopelekea Majivuno, Umimi pamoja na Hasira, Ukorofi na chuki

Kuweza kuushinda kabisa Utu na Ubinadamu wako hapo utakua umeweza kushinda Ile asili yako ya dhambi. Ukiweza kushinda ile asili yako ya dhambi ndio utakuwa umejiepusha na makosa haya.

Tunakosa Utii kwa Mungu tunaposhindwa kupambana na Majivuno, Umimi pamoja na Hasira, Ukorofi na chuki

Mungu ametupa Amri Kuu ya Upendo. Upendo kwake na kwa Binadamu. Lakini amri hii haiwezi kutimizwa kama hatutaweza kushinda kwanza Majivuno, Umimi, Hasira, Ukorofi na Chuki.

Mungu na Akubariki sana kwa Neema zake na akuwezeshe uweze kushinda dhambi na makosa yasiyoonekana kama dhambi, ambayo ndiyo yanayozuia Waumini na watumishi wa Mungu kuufikia Ukamilifu na Utakatifu.

Read and Write Comments
Shopping Cart