Usiyumbishwe na kila upepo wa mafundisho

FROM FR TITUS AMIGU
Siku moja, miaka kama 14 hivi iliyopita, nilimzingua mchungaji wa kikanisa fulani. Alinijia mbio na kuniambia, “Ati… Kadinali wenu amesema kuwa pombe sio dhambi! Kwanini usihame huko? Angalia sasa, hata kiongozi wenu wa juu wa Kanisa amekosea kwa kusema pombe sio dhambi.”
Basi mimi nikamjibu huyo mzee kama ifuatavyo;
Je kisu ni dhambi? Mzee akajibu, “hapana!” Je sumu ya panya? Mzee akajibu tena, “hapana”. Nikampa changamoto hii; Je, kama mtu akimdunga mwenzake kisu na kumuua, hapo dhambi ni kisu au kuua? Au mtu afanyaye kujiua kwa kumeza sumu ya panya, je basi ndio tuseme kuwa sumu ya panya ni dhambi? Mzee akajibu, hapana.
Nikamkumbusha maneno ya Yesu kuwa kitu kimuingiacho mtu hakiwezi kumtia unajisi.
Nikamwambia, “Kanisa lako ni kanisa la walevi.” Mzee akatumbua macho, “… hee… kijana wewe?…” Nikamweleza;
Wengi kama si wote, wa wafuasi katika kanisa lenu ni walevi. Wanatamani kunywa na kulewa, lakini wewe kama mchungaji umewazuia kwa sheria, tena sheria kali yenye vitisho na kuwatia hofu. Umeweka mikono yako machoni pao na kuwaambia kuna shimo mbele, hivyo umewafanya vipofu zaidi. Kila mwanamume amtazamaye mwanamke kwa tamaa amekwisha kuzini naye moyoni , na vivyo hivyo, kila atamaniye ulevi amekwisha kulewa moyoni ; hata kama asipoonja pombe, ni mlevi tu.
Nikazidi kumweleza kuwa mimi niliimarishwa (Kipaimara) kwa kuwekewa mikono na Askofu, nikaombewa ujazo wa Roho Mtakatifu. Kunywa ama kutokunywa nafanya si kwa amri, bali kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu. Sheria ya usionje, usiguse hainihusu, maana mimi ni mtu huru katika Roho. Kwa hiyo siwezi kujiunga na kanisa la walevi, ambao badala ya kumtii Mungu, wanaitii hofu iliyopandwa ndani yao.
Yule mzee akasema, hapo umenijibu vema kijana, lakini mbona ninyi Wakatoliki mnawaomba wafu, kama Bikira Maria? Nikamjibu,;
Sisi Wakatoliki ni Kanisa lililo katika ushirika wa Watakatifu. Yesu aliwaambia Masadukayo kuwa Bwana ni Mungu wa walio hai, Ibrahimu, Isaka, na Yakobo. Ndio maana pale mlimani Yesu alipogeuka sura aliongea na Musa na Eliya walio hai. Katika kikanisa chenu hakuna imani ya kuweza kuongea na Yesu ili muingie katika utukufu wake, na awawezeshe kuongea na Musa na Eliya, Bikira Maria au watakatifu wengine walio hai katika Bwana. Mkifa, mnakufa kama mbwa, na mnakufa kweli kweli. Basi siko tayari kujiunga na kanisa la wafu, tena wasio na imani ya kuona mambo ya rohoni. Japo mnajiita kanisa la kiroho, mambo ya rohoni hamyajui, maana ninyi ni kanisa la wafu.
Yule mzee akazua ghafla safari ya kwenda kunywa chai aliyodai ameitwa na mjukuu wake akanywe, naye faster akasepa.
Je, waijua misingi ya imani yako? Je, unaongozwa na Roho Mtakatifu au na sheria za kidini?
Usiyumbishwe na kila upepo wa mafundisho.
Melkisedeck Leon Shine

Editor: Melkisedeck Leon Shine. About Me | Contact Me | LinkedIn | TikTok | WhatsApp

Read and Write Comments
Shopping Cart