Mambo ya Msingi kufahamu kuhusu Ndoa ya Kikatoliki

Daraja na ndoa ni tofauti na sakramenti nyingine kwa sababu gani?
Daraja na ndoa ni tofauti na sakramenti nyingine kwa sababu hazilengi hasa faida ya mtu anayezipokea, bali huduma zake kwa ajili ya Kanisa na jamii. Daraja inatia uwezo wa Kristo kwa ustawi wa Kanisa, Bibi arusi wake. Ndoa inatia upendo wake mwaminifu kwa ustawi wa familia, kanisa dogo la nyumbani.
“Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe” (Mdo 20:28).
“Hakuna mtu anayeuchukia mwili wake popote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa. Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja. Siri hiyo ni kubwa; ila mimi nanena habari ya Kristo na Kanisa” (Ef 5:29-32).

Kadiri ya mpango wa Muumba, ndoa halisi ina sifa ngapi?
Kadiri ya mpango wa Muumba, ndoa halisi ina sifa tatu: umoja, uimara na utayari wa kuzaa.
“Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke, akasema, ‘Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili mmoja?’ Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe” (Math 19:4-6).
Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, ‘Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha’” (Mwa 1:28).
Mitara, uzinifu, talaka, ushoga na kukataa uzazi ni kinyume cha mpango huo.

Yesu aliweka sakramenti ya ndoa kwa sababu gani?
Yesu aliweka sakramenti ya ndoa kwa sababu ya umuhimu wa familia kwa ustawi wa mume na mke, watoto, jamii na ufalme wa Mungu, na kwa sababu ya uzito wa majukumu yanayohusika.
“Siku ya tatu palikuwa na arusi huko Kana, mji wa Galilaya; naye mama yake Yesu alikuwepo. Yesu naye alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake” (Yoh 2:1-2), akaleta divai bora ya ndoa sakramenti badala ya ndoa ya kimaumbile.
Hivyo ametuandalia neema tuweze kushinda “ugumu wa mioyo” (Math 19:8) unaohatarisha daima uzuri wa mpango wa Mungu kuhusu upendo mwaminifu katika ndoa. “Mungu aliona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana” (Mwa 1:31).

Ndoa ya Wakristo ni sakramenti ya nani?
Ndoa ya Wakristo ni sakramenti ya Yesu na Kanisa lake.
“Njoo huku, nami nitakuonyesha yule Bibi arusi, mke wa Mwanakondoo” (Ufu 21:9).
Wakiwa na ndoa halisi, mume na mke waliobatizwa ni ishara wazi ya hao wanaarusi wawili wasioonekana.
“Kama vile Kanisa limtiivyo Kristo, vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo. Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake” (Ef 5:24-25).
Ndiyo sababu Mkatoliki hawezi kufunga ndoa bila ya kuhusisha Kanisa na kufuata taratibu zake.

Ni zipi Sakramenti za Huduma ya ushirika na utume?
Ni Sakramenti mbili ambazo ni Sakramenti ya Daraja na Sakramenti ya Ndoa

Sakramenti ya ndoa ni nini?
Sakramenti ya ndoa ndio yenye kuwaunganisha wakristo wawili mume namke waliopendana kwa hiari bila shuruti au vitisho au kizuizi kwa kuwapa neema ya kuishi pamoja kitakatifu wakiwalea watoto wao katika utakatifu

Je, ndoa halali yaweza kuvunjwa?
Sakramenti ya ndoa iliyofungwa kihalali hudumu milele kwani Yesu anafundisha kuwa “Alichokiunganisha Mungu mwanadamu asikitenganishe” (Mt 19:6)

Ndoa imewekwa na nani?
Ndoa imewekwa na Mungu mwenyewe na Yesu Kristo ameeinua na kuifanya Sakramenti. (Mwz 2:18; Mt 19:1-12)

Kabla ya kupokea Sakramenti ya Ndoa hutakiwa nini?
Kabla ya kupokea Sakramenti ya Ndoa hutakiwa;
1. Uhuru wa kila mmoja
2. Matangazo ya ndoa
3. Wachumba wawe na nia ya kweli ya kuoana
4. Mafundisho na semina ya ndoa
5. Wasiwe na kizuizi chochote cha ndoa
6. Wasikae suria na wapokee Sakramenti ya Kitubio

Mtu aweza kupokea Sakramenti ya ndoa zaidi ya mara moja?
Ndiyo, mwenzi akifa yule aliyebaki yupo huru kufunga ndoa tena (1Kor 7:39)

Vizuizi vya ndoa ni kitu gani?
Vizuizi vya ndoa ni vile vinavyofanya ndoa isiwe halali tangu mwanzo

Vizuizi vya ndoa ni vipi?
Vizuizi vya ndoa ni;
1. Upungufu wa umri
2. Uhanithi
3. Ndoa awali halali
4. Tofauti za dini au upagani
5. Daraja Takatifu
6. Nadhiri
7. Utekaji au kutumia nguvu
8. Taksiri au Jinai au Mauaji ya mwenzi wa ndoa
9. Uhusiano wa damu
10. Uhusiano wa ndoa
11. Ugoni au uhawara
12. Kuasili mtoto au Uhusiano wa kisheria

Ndoa mchanganyiko maana yake ni nini?
Ndoa mchanganyiko ni ndoa kati ya Mkristo Mkatoliki na Mkristo asiye Mkatoliki

Ndoa ya utofauti wa Imani maana yake ni nini?
Ndoa ya utofauti wa Imani ni ndoa kati ya Mkristo Mkatoliki na mtu ambaye hajabatizwa kwa mfano Mpagani, Mwislamu, Yehova, Mlokole tangu kuzaliwa n.k

Mkristo Mkatoliki awezaje kufunga ndoa mchanganyiko au utofauti wa dini kwa uhalali?
Aweza kufunga ndoa hiyo kwa uhalali baada ya kupata ruhusa maalumu ya Askofu kwa Barua.

Ili Askofu atoe ruhusa ya kufungisha ndoa ya mchanganyiko au dini tofauti kuna Masharti gani?
Ndiyo, Askofu atatoa ruhusa baada ya Mkristo Mkatoliki kuahidi kwamba;
1. Atabaki Imani Katoliki mpaka kufa na isiwe amedanganya
2. Watoto wote watabatizwa na kulelewa katika Kanisa Katoliki
3. Huyo anayefunga naye ndoa akubali bila masharti yoyote

Je, Mchumba Mkatoliki aweza kuiacha Imani yake kwa sababu ya Ndoa?
Hapana, Kwa kuwa Kanisa Katoliki limeasisiwa na Mungu kwa njia ya Yesu Kristo kama la lazima kwa kupata wokovu, wanaokataa kuingia au kuhudumu ndani yake hawawezi kuokolewa.

Kuna kosa gani kama mmoja wapo atakuwa amedanganya ili aruhusiwe kufunga ndoa mseto au mchanganyiko
Kama mmoja amedanganya basi ndoa hiyo ingawa imefungwa haitakuwa halali kabisa mpaka mwisho. Watadumu katika dhambi mpaka kufa au watubu.

Kanisa linatoa ushahuri gani kuhusu ndoa halali au ya mseto?
Kanisa linatambua hatari kubwa kwa Imani linashauri watoto wake wawe na busara kubwa wanapoamua kupendana kwa lengo la kufunga ndoa.

Je, ndoa halali inaweza kuvunjwa?
Hapana, Hakuna yeyote anayeweza kuvunja ndoa halali isipokuwa kifo. (Mt 19:4-6)

Anayevunja ndoa na kuoa au kuolewa anaweza kupokea Sakramenti?
Hapana, Anayevunja maagano ya ndoa na kuoa au kuolewa hawezi kupokea Sakramenti ya Ekaristi wala Kitubio hadi afanye toba na kurekebisha hali hiyo. (Mk 10:11-12)

Ni nani wahudumu wa Sakramenti ya ndoa?
Wahiudumu rasmi wa Sakramenti ya ndoa ni wachumba wenyewe, Padri kama shahidi rasmi wa kanisa. Tena ni lazima ifungwe mbele ya mashahidi wengine wawili.

Watu wa jinsia moja waweza kuoana?
Hapana, watu wa Jinsia moja hawawezi kuoana na wakifanya hinyo wanatenda dhambi kubwa inayomlilia Mungu. (Wal 18:22)
Enjoyed? Drop your Comment Below
OR Chat Live with AckySHINE here
Read and Write Comments
Subscribe
Notify of
guest

1 Comment
Most Voted
Newest Oldest
Inline Feedbacks
View all comments
Shopping Cart