Upishi na Maandalizi ya Milo yenye Afya

Mapishi ya Boga La Nazi

Vipimo

Boga la kiasi – nusu yake

Tui zito la nazi 1 ½ gilasi

Sukari ½ kikombe

Hiliki ½ kijiko cha chai

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Menya boga kisha katakata vipande vya kiasi.
Weka katika sufuri tia maji kiasi ya kuchemshia na kuwiva bila ya kubakia maji mengi.
Changanya tui na sukari na hiliki kisha mimina juu ya boga wacha katika moto dakika chache tu bila ya kufunika.
Epua mimina katika chombo likiwa tayari.

Mapishi ya Chapati za Kusukuma kitaalamu

Mahitaji

Unga wa ngano (plain flour 1/2 of kilo)
Siagi (butter vijiko 2 vya chakula)
Yai (egg 1)
Chumvi (1/2 ya kijiko cha chai)
Hiliki (ground cardamon 1/4 ya kijiko cha chai)
Maji ya uvuguvugu (warm water)
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Weka unga wa ngano katika bakuli la kukandia, kisha tia chumvi na hiliki na uchanganye kwanza, baada ya hapo tia siagi na uichanganye vizuri na unga mpaka ipotee. Baada ya hapo tia tena yai na uchanganye vizuri. Mchanganyiko ukishachanganyika vizuri sasa unaweza kutia maji ya uvuguvugu kidogo, kidogo huku ukiwa unauchanganya ili kupata donge. Baada ya hapo anza kukanda hilo donge mpaka mabuje yote yapotee na unga uwe mlaini, ambapo itakuchukua kama dakika 15. Baada ya hapo tawanyisha unga katika madonge ya wastani (yasiwe makubwa sana au madogo sana) Ukimaliza hapo, andaa kibao cha kusukumia chapati kwa kukitia unga kidogo ili chapati isinatie kwenye kibao. Sukuma donge moja la chapati mpaka liwe flat na kisha weka kijiko kimoja cha mafuta na usambaze. ukisha maliza ikunje (roll). Fanya hivyo kwa madonge yote yaliyobakia.
Baada ya hapo andaa chuma cha kuchomea (fry-pan) katika moto wa wastani. Kisha anza kusukuma chapati (ni vizuri ukaanza na zile ulizozikunja mwanzo ili kuzipa nafasi zile za mwisho ziweze kulainika) ukiwa unasukuma hakikisha zinakuwa flat (na zisiwe nene sana au nyembamba sana) Ukishamaliza hapo tia kwenye chuma cha kuchomea. Acha iive upande mmoja then igeuze upande wa pili. Tia mafuta ama kijiko kimoja kikubwa upande wa chini wa chapati na uanze kuukandamiza kwa juu uku ukiwa unaizungusha. fanya hivyo uku ukiwa unaigeuza kuiangalia kwa chini ili isiungue. ikishakuwa ya brown, geuza upande wa pili na urudie hivyohiyvo mpaka chapati iive. Rudia hii process kwa chapati zote zilizobakia.

Siri ya chapati kuwa laini ni kutia siagi au mafuta ya kutosha kipindi unazikanda na pia kuzikanda mpaka unga uwe laini.

Mapishi ya Kachori

Mahitaji

Viazi mbatata (potato 4 vya wastani)
Nyama ya kusaga (mince beef 1 kikombe cha chai)
Kitunguu (onion 1 cha wastani)
Carrot 1
Hoho (green pepper 1/2)
Kitunguu swaum (garlic)
Tangawizi (ginger )
Binzari nyembamba (ground cumin 1/2 kijiko cha chai)
Binzari manjano (turmeric 1/2 kijiko cha chai)
Curry powder 1/2 kijiko cha chai
Limao (lemon 1/2)
Pilipili ya unga (chilli powder 1/2 kijiko cha chai)
Giligilani (coriander kiasi)
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)
Unga wa ngano kiasi

Matayarisho

Katakata vitunguu na hoho katika vipande vidogo vidogo na kisha kwangua carrot na uweke pembeni. Chemsha viazi na chumvi kidogo vikiiva viponde na uviweke pembeni, Baada ya hapo tia nyama limao, chumvi, kitunguu swaum na tangawizi ichemshe mpaka iive na uhakikishe maji yote yamekauka. Kisha Tia binzari zote, pilipili, curry powder, giligilani, vitunguu, hoho na carrot. Pika mchanganyiko huo kwa muda wa dakika 3 na kisha ipua. Baada ya hapo changanya na viazi kisha tengeneza maduara ya kiasi na uyaweke pembeni. Chukua unga wa ngano kiasi na uchanganye na maji kupata uji usiokuwa mzito au mwepesi sana. baada ya hapo chovya madonge katika huo uji na uyachome katika mafuta. Hakikisha zinaiva na kuwa rangi ya brown na hapo zitakuwa tayari kwa kuliwa.Unaweza ukazisevu na chatney yoyote unayopendelea.

Mapishi ya Supu Ya Maboga

Viamba upishi

Blue band vijiko vikubwa 2
Maziwa vikombe 2
Royco kijiko kikubwa 1-2
Pilipili manga (unga) kijiko cha 1
Chumvi kiasi Maji lita 2-3
Boga kipande ½
Viazi mviringo 2
Vitunguu 2
Karoti 2
Nyanya 2

Hatua

• Menya boga, viazi, karoti, nyanya na kwaruza weka kwenya sufuria kubwa.
• Menya, osha na katakata vitunguu kisha ongeza kwenye mboga.
• Ongeza maji na chumvi chemshwa mpaka vilainike.
• Pekecha ikiwa jikoni na moto kidogo
• Ongeza blue band, maziwa royco na pilipili manga ukikoroga kwa dakika 5.
• Onja chumvi na pakua kama supu.
Uwezekano
Tumia siagi badala ya margarine.

Mapishi ya Ndizi Mbichi Za Nyama Ng’ombe

Vipimo

Ndizi mbichi – 10

Nyama – kilo 1

Nazi ya kopo – 1

Chumvi – 1 Kijiko cha chakula

Ndimu – 1

Bizari ya manjano – 1 Kijiko cha chai

Pili pili mbichi – 3

Nyanya (tomatoes) – 2

Kitunguu maji – 1

Kitunguu saumu(thomu/galic) na Tangawizi iliyosagwa – 1 Kijiko cha chakula

Namna ya Kutayarisha Na Kupika

Kata nyama vipande vipande na uisafishe.
Chemsha nyama weka chumvi, thomu, tangawizi na ndimu. Iache iwive.
Kata kata nyanya na kitunguu, kisha mimina kwenye nyama inayochemka, weka na bizari nusu kijiko. Wacha supu iwive kisha weka pembeni. Ukumbusho: Hakikisha supu inakuwa kiasi na si nyingi.
Menya maganda ndizi na uzikate vipande vipande vya kiasi.
Zikoshe ndizi na uziweke ndani ya sufuria.
Weka maji ndani ya sufuria kisha zichemshe ndizi mpaka ziwe laini kidogo.
Zimwage maji ndizi kisha mimina supu na nyama ndani ya ndizi.
Mimina nazi pili pili na bizari nusu kijiko ndani ya ndizi na uziweke kwenye jiko zichemke mpaka zibakie na urojo kiasi. Onja chumvi na uongeze kadri utakavyopenda.
Weka pembeni zipoe.
Pakua ndizi kwenye sahani au bakuli tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Biskuti Za Jam

VIAMBAUPISHI

Unga 2 ½ gilasi

Sukari ¾ gilasi

Samli 1 gilasi

Mayai 2

Baking powder 2 kijiko vya chai

Vanilla 1 ½ kijiko cha chai

Maganda ya chungwa 1

MAPISHI

Tia kwenye machine ya kusagia (blender) mayai, sukari, vanilla, samli na maganda ya chungwa, saga vizuri.
Tia unga kwenye bakuli pamoja na baking powder, mimina vitu ulivyosaga kwenye bakuli, changanya.
Punguza unga uliochanganya kidogo weka pembeni.
Unga uliobakia tia kwenya tray ya kuchomeya, utandaze vizuri, tia jam juu yake.
Chukua la kukwaruzia carrot (grater) ukwaruze unga uliuopunguza juu ya jam.
Choma kwa muda dakika 20 moto wa 180 C.

Acha ipowe kidogo, zikate vipande vya mraba (square) Tayari kwa kula.

Jinsi ya kupika Biskuti Nyembamba (Wafer Bar) Za Chokoleti Na Njugu

MAHITAJI

Wafer Powder/gram wafer (unga wa biskuti uliosagwa wa tayari) – vikombe 2

Maziwa ya Mgando Matamu ya Kopo – 2 vikombe

Nazi iliyokunwa – ½ Kikombe

Chokoleti vipande vipande – 1 Kikombe

Njugu vipande vipande – ½ Kikombe

Siagi – 227 g

MAPISHI

Yeyusha siagi motoni kisha changanya na unga wa wafer acha kidogo motoni
Mimina katika treya unayochomea itandaze vizuri, kisha mimina maziwa juu yake pamoja na njugu vipande , nazi iliyokunwa na vipande vya chokoleti.
Choma (bake) kwenye oveni kwa moto wa 350ºC kwa dakika 20.
Katakata tayari kwa kuliwa

Mapishi ya Half cake (Keki)

Mahitaji

Unga wa ngano (self risen flour) kikombe 1na 1/2
Sukari (sugar) 1/4 kikombe
Barking powder 1/2 kijiko cha chai
Magadi soda (bicarbonate soda) 1 kijiko cha chai
Mafuta 2 vijiko vya chai
Mafuta ya kukaangia
Maji ya uvuguvugu kiasi

Matayarisho

Changanya unga na vitu vyote (kasoro mafuta ya kuchomea) kisha ukande (hakikisha unakuwa mgumu) Baada ya hapo sukuma na ukate shape uipendayo (hakikisha unakata vipande vinene kiasi na sio kama mandazi) Baada ya hapo ziweke sehemu yenye joto na uache ziumuke. Zikisha umuka zikaange katika moto mdogo ili ziive mpaka ndani. Zikisha iva zitoe na uziweke katika kitchen towel ili zichuje mafuta. Ziache zipoe na hapo zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Maini ya kuku

Mahitaji

Maini ya kuku 1/2 kilo
Vitunguu vikubwa 2
Hoho 1
Pilipil 1
Limao 1/2
Swaum/tangawizi 1 kijiko cha chai
Curry powder 1/2 kijiko cha chai
Mafuta ya kupikia

Matayarisho

Safisha maini weka pembeni. Baada ya hapo kaanga vitunguu,swaum na tangawizi pamoja (hakikisha vitunguu visiwe vya brown), kisha tia maini, curry powder, pilipili, chumvi ,hoho na limao kisha changanya vizuri na ufunike. Pika mpaka maini yaive na hakikisha yanakuwa na rojo kidogo. Baada ya hapo ipua na yatakuwa tayari kwa kuliwa na chochote upendacho kama vile chapati, chips, ugali, wali.

Jinsi ya kutengeneza Muhogo Wa Nazi Na Samaki Wa Kukaanga

Mahitaji

Muhogo – 3

Tui La Nazi – 2 vikombe

Chumvi – kiasi

Pilipili mbichi – 2

Mafuta – 1 kijiko moja

Kitunguu maji – 1 kidogo

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Chambua muhogo ukatekate au tumia iliyo tayari.
Chemsha muhogo katika sufuria kwa maji kidogo na chumvi, funika uive muhogo.
Karibu na kukauka maji tia tui, kitunguu maji ulichokatakata na pilipili mbichi.
Unaupika moto mdogo mdogo hadi ukauke tayari kuliwa na samaki au kitoweo chochote kingine

Mapishi ya wali wa Kiafrika Mangaribi

Mahitaji

Mchele (rice vikombe 2 na 1/2)
Vitunguu (onion 2)
Nyanya ya kopo (tin tomato kopo 1)
Tangawizi (ginger paste kijiko 1 cha chakula)
Kitunguu swaum (garlic paste kijiko 1 cha chakula)
Paprika (kijiko 1 na 1/2 cha cha chai)
Pilipil (scotch bonnet pepper 1)
Curry powder (kijiko 1 cha chai)
Maggi cubes 3(unaweza kutumia yenye ladha ya chicken, beef au vegetable. Inategemea unasevu na mchuzi wa aina gani)
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Loweka mchele kwa muda wa dakika 10.Katakata vitunguu kisha weka pembeni, saga pamoja nyanya ya kopo,pilipili, tangawizi na kitunguu swaum kisha weka pembeni. Baada ya hapo kaanga vitunguu vikiiva tia curry powder, maggi cubes, chumvi na paprika na uchanganye vizuri. Kisha tia mchanganyiko wa nyanya na uupike mpaka uive. Baada ya hapo tia mchele na maji na uupike mpaka ukaribie kuiva kisha ugeuze na umalizie kwa kutia njegere na umalizie kuupika mpaka uive. baada ya hapo utakuwa tayari kuseviwa na mboga yoyote kama kuku, nyama, samaki au assorted meat (Mchanganyiko wa utumbo, makongoro na nyama), Hapo mimi nili-save na mchuzi wa kuku wa kienyeji.

Jinsi ya kupika Wali Wa Kichina wa mboga mboga Na Mayai

Viambaupishi

  1. Mchele (Basmati) – 3 vikombe
  2. Mbogamboga za barafu (karot, njegere, spring beans na mahindi) – 1 kikombe
  3. Kuku Kidari – 1 LB (ratili)
  4. Mayai – 2 mayai
  5. Vitunguu (vikubwa) – 2 au 3 vidogo
  6. Pili pili manga – 1 kijiko cha chai
  7. Paprika – 1 kijiko cha chai
  8. Chumvi – Kiasi
  9. Mafuta – 1/3 kikombe cha chai
  10. Kitunguu saumu(thomu/galic) – 1 kijiko cha supu
  11. Tangawizi – 1 kijiko cha chai
  12. Kidonge cha supu – 1
  13. Soy sauce – 2 vijiko vya supu

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika Kuku

Kata kidari cha kuku vipande vidogo vidogo vya kiasi.

Tia mafuta kidogo katika wok (karai ya kichina)

Kisha mtie kuku, thomu, tangawizi, soy sauce, pilipilimanga, paprika chumvi.

Tia mboga za barafu, kidonge cha supu, kaanga kuku na mboga viwive yitu vyote na mchanganyiko ukauke.

Namna Ya Kutayarisha Na kupika Wali

Roweka mchele wa basmati kwa muda wa saa au zaidi.

Halafu chemsha mchele pamoja na chumvi

Wacha uchemke asilimia 70%

Chuja maji na weka kando

Katika sufuria, tia mafuta kidogo tu

Kisha tia mayai mawili ukaange haraka haraka (crumbled egg)

Changanya mchanganyiko wa kuku na mboga

Kisha tia wali changanye vizuri

Rudisha katika moto, funika upikike kidogo hadi uive

Kisha pakua katika sahani na tolea na mayai ya kuchemsha ukipenda.

Upishi na Mafuta ya Zeituni: Faida za Afya na Matumizi ya Mapishi

Upishi na Mafuta ya Zeituni: Faida za Afya na Matumizi ya Mapishi 🍽️

Karibu katika makala hii ambayo itakuletea ufahamu zaidi kuhusu upishi na mafuta ya zeituni, pamoja na faida zake za kiafya na jinsi ya kuyatumia katika mapishi mbalimbali. Kama AckySHINE, ningependa kukushirikisha maarifa haya ili uweze kuboresha afya yako na kufurahia ladha ya vyakula vyenye mafuta ya zeituni.

Mafuta ya zeituni yamekuwa yakitumika kwa muda mrefu katika nchi za Mediterranean kama sehemu muhimu ya lishe yenye afya. Hii ni kutokana na faida zake nyingi za kiafya ikiwemo kulinda moyo, kuimarisha afya ya ngozi, na kuongeza kinga ya mwili.

Hapa chini ni orodha ya faida kumi na tano za afya za mafuta ya zeituni:

  1. Mafuta ya zeituni husaidia kulinda moyo dhidi ya magonjwa ya moyo 🫀
  2. Yanaboresha afya ya ngozi na kuzuia kuzeeka mapema 🌟
  3. Mafuta ya zeituni husaidia kupunguza viwango vya sukari mwilini, hivyo ni nzuri kwa watu wenye ugonjwa wa kisukari 👨‍⚕️
  4. Husaidia katika kupunguza uzito na kudhibiti hamu ya kula 🥗
  5. Ina uwezo wa kuzuia ugonjwa wa saratani 🦀
  6. Mafuta ya zeituni huimarisha mfumo wa kinga na kulinda mwili dhidi ya maradhi 🛡️
  7. Husaidia katika kuzuia ugonjwa wa kiharusi 🧠
  8. Mafuta ya zeituni yana madini ya chuma na vitamini E ambavyo husaidia katika kuboresha afya ya damu 💉
  9. Husaidia katika kudhibiti shinikizo la damu na kuzuia magonjwa ya moyo 💓
  10. Ina mali ya kupambana na uchochezi mwilini, hivyo inaweza kupunguza hatari ya magonjwa ya viungo 🦴
  11. Mafuta ya zeituni husaidia katika uponyaji wa vidonda vya tumbo 🩺
  12. Yanaweza kusaidia katika kupunguza hatari ya kupata ugonjwa wa Alzheimer’s 🧠
  13. Husaidia katika kudhibiti viwango vya cholesterol mwilini 🥚
  14. Mafuta ya zeituni yana mali ya antibakteria na antiviral, hivyo husaidia mwili kupambana na maambukizi 🌡️
  15. Yanaweza kusaidia katika kupunguza maumivu ya viungo na kuimarisha afya ya mifupa na misuli 💪

Kutokana na faida hizi za kiafya, ni muhimu kuyatumia mafuta ya zeituni katika mapishi yako ili kuboresha ladha na afya ya chakula chako. Hapa chini ni mapendekezo yangu ya matumizi ya mafuta ya zeituni katika mapishi mbalimbali:

  1. Changanya mafuta ya zeituni na limau na tumia kama saladi dressing 🥗
  2. Tumia mafuta ya zeituni kwenye sahani za pasta ili kuongeza ladha na afya ya chakula chako 🍝
  3. Pika mboga za majani kwa kutumia mafuta ya zeituni badala ya mafuta ya wanyama 🥬
  4. Tumia mafuta ya zeituni kwenye mchuzi wa supu ili kuongeza ladha na afya ya chakula chako 🍲
  5. Tumia mafuta ya zeituni kwenye pilau au wali ili kuongeza ladha na afya ya chakula chako 🍚
  6. Tumia mafuta ya zeituni kwenye sandwichi badala ya mayonnaise 🥪
  7. Tumia mafuta ya zeituni kwenye kuoka mikate au keki ili kuongeza ladha na afya ya chakula chako 🥐
  8. Tumia mafuta ya zeituni kwenye kuoka samaki ili kuongeza ladha na afya ya chakula chako 🐟
  9. Tumia mafuta ya zeituni kwenye kuandaa vitafunwa kama karanga za zeituni zilizokaangwa 🥜
  10. Changanya mafuta ya zeituni na vikolezo vingine kama vile thyme au basil kwa kuongeza ladha kwenye sahani yako 🌿

Kwa ujumla, mafuta ya zeituni yanaweza kubadilisha na kuimarisha afya yako kwa njia nyingi. Kama AckySHINE, natoa ushauri kuwa unatumie mafuta ya zeituni katika mapishi yako ili kufurahia ladha nzuri na faida za kiafya.

Je, umewahi kutumia mafuta ya zeituni katika mapishi yako? Ni mapishi gani unayopenda kutumia mafuta ya zeituni? Ni faida zipi za kiafya umepata baada ya kuanza kutumia mafuta haya? Nipo hapa kusikiliza na kujadiliana nawe. 😊🌱

Mapishi ya Ugali Kwa Mchuzi Wa Kamba Wa Nazi, Kisamvu Na Kachumbari Ya Papa Mkavu

Vipimo – Ugali

Maji – 4 vikombe kiasi inategemea na unga wenyewe.

Unga wa sembe – 2 vikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Tia maji kiasi katika sufuria, weka motoni, yakipata moto korogea unga wa sembe kiasi na ufanye uji mzito uache uchemke vizuri huku ukikoroga.
Chota kibakuli kimoja cha uji huo weka pembeni kisha mimina unga wote uliobaki upigepige uchanganyike vizuri kwenye uji huo mpaka ushikamane
Punguza moto anza kuusonga taratibu huku ukiongeza ule uji ulioweka pembeni kidogo kidogo mpaka uone sasa umeshikamana vizuri.
Endelea kusonga mpaka ulainike kisha mimina kwenye bakuli au sahani iliyolowanishwa na maji kisha upete pete huku ukiugeuza geuza mpaka ukae shepu nzuri ya duara.Weka tayari kwa kuliwa.

Vipimo – Mchuzi wa kamba wa nazi

Kitunguu – 1

Nyanya – 2

Kamba waliomenywa – 1 Kilo

Pilipili mbichi iliyosagwa – ½ kijiko cha chai

Kitunguu saumu na tangawizi ilivyosagwa – 1 kijiko cha supu

Nazi nzito iliyochujwa – 1 kikombe

Bizari ya mchuzi – ½ kijiko cha chai

Chumvi – Kiasi

Ndimu – Nusu

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Safisha na osha kamba vizuri kisha mtie katika sufuria. Katia kitunguu, nyanya, tia chumvi, pilipili mbichi ya kusaga, thomu na tangawizi, bizari ya mchuzi na ndimu. Tia maji kidogo kiasi acha ichemke.
Watakapoiva na karibu kukauka, mimina tui la nazi taratibu koroga kiasi
Punguza moto aacha ichemke kidogo ukiwa mchuzi tayari.

Vipimo – Kisamvu

Kisamvu – 2 vikombe

Kunde mbichi zilizochemshwa – 1 kikombe

Kitunguu – 1

Nazi nzito iliyochujwa – 1 vikombe

Chumvi – Kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Weka kisamvu katika sufuria, katia kitunguu, tia chumvi, maji kidogo acha kichemke.
Huku ikichemka mimina kunde mbichi zilizochemshwa acha zipikikie kidogo mpaka kisamvu kikaribie kukauka na kunde kuiva.
Mimina nazi nzito punguza moto acha ichemke kidogo, mimina kwenye bakuli tayari kwa kuliwa.

Vipimo – Kachumbari Ya Papa

Papa mkavu (au nguru) – kipande

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Muoshe papa vizuri atoke mchanga kisha mchome kwenye jiko la mkaa au unaweza kumtia kwenye treya kisha kwenye oven kwa moto wa 350 kwa dakika 15 mpaka 20.
Akikauka mchambue chambue weka kando.
Tengeneza kachumbari, kwa kukata kitunguu, nyanya na pilipili mbichi, tia ndimu na chumvi.
Changanya na papa mkavu uliyemchambu ikiwa tayari.

Mapishi ya Bagia dengu

Mahitaji

Unga wa dengu (gram flour 1/4 kilo)
Kitunguu kilichokatwa (onion 2)
Hoho (green pepper 1/2)
Pilipili iliokatwakatwa (scotch bonnet pepper 1/2)
Barking powder (1/4 ya kijiko cha chai)
Chumvi (salt)
Kitunguu swaum (garlic cloves 2)
Mafuta ya kukaangia (vegetable oil)
Binzari manjano (turmeric 1/4 ya kijiko cha chai)

Matayarisho

Changanya unga, chumvi, binzari, barking powder kwanza kisha weka maji kiasi na vitu vyote vilivyobakia (isipokuwa mafuta) na ukoroge vizuri kuhakikisha unga hauna madonge.Hakikisha unga hauwi mzito wala mwepesi sana. Kisha uache kwa muda wa dakika 20. Baada ya hapo choma bagia katika mafuta. Ukiwa unachoma hakikisha bagia zinakuja juu ya mafuta na hazigandi chini. Ikitokea zinaganda chini hapo itakuwa umekosea kitu. Pika mpaka ziwe za light brown kisha zitowe na uziweke katika kitchen towel ili zikauke mafuta na hapo zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Jinsi ya kuandaa Wali Wa Hudhurungi Na Kabeji

VIPIMO VYA WALI

Mchele wa hudhurungi (brown rice)

na (wild rice kidogo ukipenda)Osha na Roweka – 2 Vikombe

Kitungu maji – 1 Kiasi

Kitunguu saumu – 1 Kijiko cha supu

Bizari ya manjano – 1/2 Kijiko cha chai

Mdalasini nzima – 1 kijiti

Iliki iliyosagwa – 1/4 Kijiko cha chai

Chumvi – Kiasi

Pilipili manga – 1/4 Kijiko cha cha

Mafuta – 2 Vijiko vya supu

Majani ya Bay(bay leaves) – 1

Mbegu ya giligilani iliyoponwa (coriander seeds) – 1 Kijiko cha chai

Supu ya kuku ya vidonge – 1

Maji ya wali – 4 vikombe

NAMNA YA KUTAYARISHA NA KUPIKA

Kaanga kitungu, kabla ya kugeuka rangi tia thomu.
Kisha weka bizari zote na ukaange kidogo.
Tia mchele kisha maji na ufunike upike katika moto mdogo.
Na ikishawiva itakuwa tayari kwa kuliwa na kabeji na kuku wa tanduuri.

VIPIMO VYA KABEJI

Kabeji iliyokatwa katwa – 1/2

Karoti iliyokwaruzwa – 1-2

Pilipili mboga kubwa – 1

Figili mwitu (celery) iliyokatwa – 1 au 2 miche

Kitunguu saumu(thomu/galic) iliyosagwa – 1 Kijiko cha supu

Pilipili mbichi – 1

Kisibiti (caraway seed) – 1/4 Kijiko cha chai

Bizari ya manjano ya unga = 1/2 Kijiko cha chai

Giligani ya unga – 1 Kijiko cha chai

Chumvi – Kiasi

Kitungu maji kilichokatwa -1

Kotmiri – upendavyo

Mafuta ya kukaangia – Kiasi

NAMNA YA KUTAYARISHA NA KUPIKA

Kwenye sufuria kaanga kitungu, figili mwitu kisha tia thomu na pilipili zote.
Halafu tia bizari zote na ukaange kidogo.
Kisha weka kabeji na chumvi, ufunike moto mdogo ilainike kidogo na sio sana
Tia karoti na usiwache motoni sana, kisha zima moto na inyunyizie kotmiri juu.

Mapishi ya Chicken Curry

Leo wapendwa nitaenda kuzungumzia mapishi ya mchuzi wa kuku (chicken curry).

Mahitaji

Kuku mzima
Nyanya kubwa 3
Karoti mbili
Pilipili hoho
Kotmiri
Tangawizi
Kitunguu maji
Kitunguu saumu kidogo
Ndimu
Mafuta ya kupikia
Chumvi (pilipili ukipenda)

Matayarisho

1. Menya vitunguu saumu na tangawizi na uvitwange pamoja.
2. Katakata kuku vipande vidogo kisha ukamulie ndimu na kupaka mchanganyiko wa tangawizi na vitunguu saumu (kiasi tu).
3. Katakata vitunguu maji na pilipili hoho uweke pembeni.
4. Grind (Kwangua) kwenye grater nyanya na karoti pia uweke pembeni.
5.Katakata kotmiri vipande vidogo uweke pembeni.
6. Andaa kikaango na jiko.

Mapishi

1. Bandika kikaango jikoni na mafuta kiasi, yakishachemka weka vitunguu maji na kaanga hadi vimelainika na kuiva (hakikisha haviungui).
2. Weka pilipili hoho na karoti na endelea kukoroga hadi vyote viive na kulainika, Kisha weka chumvi.
3. Sasa weka vipande vya nyama koroga na funikia kwa dakika 3, kisha weka nyanya zako ulizo grind na koroga ili zichanganyike vizuri, vikishachanganyika weka kotmiri na pilipili kama utapenda. Acha vichemke kwa dakika 5. Hakikisha moto sio mkali sana.
4. Angalia kama nyama zimeiva vizuri kisha epua mchuzi wako.
5. Pakua kwenye bakuli na katakata kotmiri uweke kwa juu.
Unaweza kula kwa ugali, wali, ndizi rost au chipsi.

Mapishi mazuri ya Wali Wa Kukaanga Kwa Kidari Cha Kuku

Vipimo vya Wali:

Mchele – 3 vikombe

*Maji ya kupikia – 5 vikombe

*Kidonge cha supu – 1

Samli – 2 vijiko vya supu

Chumvi kiasi

Hiliki – 3 chembe

Bay leaf – 1

Vipimo Vya Kuku

Kidari (chicken breast) – 1Kilo

Kitunguu – 1

Tangawizi mbichi – ½ kipande

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 7 chembe

Pilipili mbichi – 3

Ndimu – 2

Pilipilimanga – 1 kijiko cha chai

Mdalasini – ½ kijiko cha chai

Jira/Cummin ya unga – 1 kijiko cha chai

Maji – ¼ kikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Wali:

Osha na roweka mchele kisha weka sufuria katika moto tia samli ipashe moto.
Tia hiliki, bay leaf, kaanga, kisha tia mchele ukaange kidogo.
Tia maji, chumvi na kidonge cha supu, upike wali kama unavyopika pilau.
*Maji kisia kwa kutegemea mchele ulivyo.
*Unaweza kutumia supu yoyote badala ya kidonge.

Kuku:

Katakata kidari cha kuku vipande vya kiasi, weka katika sufuria, tia ndimu, bizari zote, chumvi.
Katakata kitunguu vipande vidogodogo, pilipili, na kitunguu thomu (chopped), tia katika kuku.
Chuna tangawizi mbichi tia katika kuku. Changanya vitu vyote vizuri.
Tia maji kiasi ¼ kikombe tu kiasi cha kumkaushia kuku. Weka katika moto mpike huku unageuzageuza. Anapokaribia kukauka epua akiwa tayari kuliwa na wali (na saladi upendayo)

MAANA YA MANENO YANAYOTUMIKA KATIKA MASUALA YA LISHE

1. Chakula

ni kitu chochote kinacholiwa au kunywewa na kuupatia mwili virutubishi mbalimbali Chakula huupatia mwili nguvu, kuulinda na kuukinga dhidi ya maradhi mbalimbali .Mfano wa chakula ni ugali, wali, maharagwe, ndizi, viazi, mchicha, nyama, samaki.

2. Lishe

ni mchakato unaohusisha hatua mbalimbali za jinsi mwili unavyokitumia chakula kilicholiwa, hatua hizi ni kuanzia chakula kinapoliwa, jinsi mwili unavyokisaga na kukiyeyusha, umetaboli, na hatimaye virutubishi kufyonzwa na kutumika mwilini.

3. Virutubishi

ni viini vilivyoko kwenye chakula ambavyo vinauwezesha mwili kufanya kazi zake, karibu vyakula vyote huwa na kirutubishi zaidi ya kimoja ila hutofautiana kwa kasi na ubora. Kila kirutubishi kina kazi yake mwilini na mara nyingi hutegemeana ili viweze kufanya kazi yake kwa ufanisi. Hakuna chakula kimoja chenye virutubishi vya aina zote isipokuwa maziwa ya mama kwa miezi sita ya mwanzo ya maisha ya mtoto, ni mhimu kula vyakula vya aina mbalimbali ili kuwezesha mwili kupata virutubishi mchanganyiko vinavyohitajika.

4. Mlo kamili

ni ule ambao hutokana na chakula mchanganyiko kutoka katika makundi yote ya chakula na una virutubishi vyote muhimu kwa ajili ya lishe na afya bora. Mlo huu unapoliwa kwa kiasi cha kutosha kulingana na mahitaji ya mwili angalau mara tatu kwa siku huupatia mwili virutubisho vyote muhimu.

5. Ulaji unaofaa

hutokana na kula chakula mchanganyiko na cha kutosha (mlo kamili) ili kukidhi mahitaji ya mwili. Ulaji unaofaa pia huzingatia matumizi ya kiasi kidogo cha chumvi, mafuta, sukari, ulaji wa nyama nyekundu kwa kiasi kidogo. Ni muhimu kuzingatia ulaji wa mboga mboga, matunda, na vyakula vya jamii ya kunde kwa wingi ili kudumisha uzito wa mwili unaotakiwa na kupunguza magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

6. Nishati- lishe

ni nguvu inayopatikana baada ya virutubishi (kabohaidreti, mafuta) kuvunjwa vunjwa mwilini. Mwili huitumia nguvu hiyo kufanya kazi mbalimbali Kama kulima, kutembea, kupumua, kuziweka seli za mwili katika hali inayotakiwa n.k.

7. Kalori au kilo kalori

ni kipimo kinachotumika kupima nishati -lishe

8. Makapi mlo

ni sehemu ya chakula ambayo mwili hauwezi kuyeyusha lakini ni muhimu katika uyeyushwaji wa chakula. Mfano wa vyakula venye makapi mlo kwa wingi ni mboga za majani, matunda( maembe, machungwa, mapera, machenza, mafenesi, unga usiokobolewa( dona) na vyakula vya jamii ya kunde.

9. Lehemu

ni aina ya mafuta yanayopatikana hasa kwenye vyakula vya asili ya wanyama na pia hutengenezwa mwilini. Lehemu inayotokana na vyakula ikizidi mwilini huleta madhara ya kiafya. Vyakula venye lehemu kwa kiasi kikubwa ni pamoja na maini, figo, mayai, nyama iliyonona kama nundu, nyama ya nguruwe yenye mafuta, mkia wa kondoo, samli, siagi, ngozi ya kuku n.k.

10. Utapiamlo

ni hali ya kupungua au kuzidi kwa baadhi ya virutubishi mwilini ambapo husababisha lishe duni au unene uliozidi.

11. Antioxidants

ni viini ambavyo vina uwezo wa kukinga seli za mwili zisiharibiwe na chembe chembe haribifu (free radicals) ambazo huweza kusababisha saratani. Viini hivyo huungana na chembechembe hizo haribifu na kuzidhibiti ili zisisababishe madhara. Mifano ya antioxidants ni pamoja na beta-carotene, lycopene, vitamin C, E, na A.

Mapishi ya Ugali Kwa Mchuzi Wa Nazi Wa Nyanya Chungu/Mshumaa/Ngogwe Na Bamia, Mboga Ya Matembele Na Samaki Wa Kukaanga

Vipimo Vya Ugali

Unga wa mahindi – 4

Maji – 6 kiasi kutegemea na aina ya unga

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Weka maji katika moto.

Tia unga kidogo katika kibakuli, koroga ufanye uji.

Maji yakichemka tia kwenye maji uwe uji.

Ujii ikiiva punguza kidogo tia unga kidogokidogo na usonge ugali. Ikiwa unga ni mgumu utaongeza maji ya ule uji ulopunguza usonge hadi uive ukiwa tayari.

Vipimo Vya Mchuzi Wa Nazi Kwa Nyanya Chungu/Mshumaa/Ngogwe Na Bamia

Nyanya chungu/mshumaa/Ngogwe – 7

Bamia – 10

Kitunguu maji – 2

Nyanya/tungule – 2

Tui la nazi jepesi – 2 viwili

Tui la nazi zito – 2

Chumvi – kiasi

Ndimu – 2 mbili kamua

Bizari manjano/haldi/turmeric – ½ kijiko cha chai

Pilipili mbuzi – 3

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Katakata kitunguu maji na nyanya vipande vidogodogo sana kisha weka katika sufuria.

Iache ichemke kwa maji yake ya nyanya, ikishachemka tia maji kidogo kama robo kikombe.

Tia nyanya chungu, bamia na koleza ndimu, chumvi.

Iache ichemke. Inapokuwa tayari imeiva tia tui jepesi endelea kuacha katika moto huku unakoroga kidogo kidogo.

Tui jepesi likipungua kiasi chake, tia tui zito, kisha usiachie mkono koroga ikichemka kidog kiasi cha kuiva tui mchuzi tayari.

Vipimo Vya Mboga Ya Matembele

Matembele – 5 mafungu

Mafuta – ¼ kikombe

Kitunguu maji kilokatwakatwa – 1

Nyanya/tungule – 4

Chumvi – 1

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Punguza miche ya matembele kwa kuikata ncha kisha osha majani yake. Acha yachuje maji .
Weka mafuta katika sufuria, kaanga kitunguu maji na nyanya hadi viivie.
Tia mboga, Iache ichemke kwa maji yake hadi iive. Ukiona bado haikuiva tia maji kidogo tu.
Ukipenda unatia ndimu kiasi cha kipande kimoja ukamue .

Samaki Wa Nguru Wa Kukaanga

Samaki Wa Nguru – 4 vipande

Kitunguu saumu(thom/galic) na tangawizi ilosagwa – 1 kijiko cha supu

Pilipili mbichi – 4

Ndimu – 2 kamua

Bizari ya samaki – 1 kijiko cha chai

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Mwoshe samaki kisha mtie kitunguu thomu, tangawizi ilosagwa, chumvi, pilipilimbichi ilosagwa, ndimu na bizari ya samaki.
Mwache akolee viungo kwa muda kidogo.
Makaange katika mafuta hadi aive akiwa tayari.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About